Naam, Zanzibar ina wenyewe na ndio maana hata wale Afro-Shirazi wazalendo wa Zanzibar walikuwa wa mwanzo kuuliwa.

Zanzibar ina wenyewe na ndio maana hata baada ya kupinduliwa Serikali Huru ya Zanzibar ikawa hata akina Mzee Jumbe, Maalim Seif mpaka kufikia Dk. Salmini, wote walikuja kuchukiwa na Nyerere.

Wazanzibari wazalendo ndio tamaa ya Zanzibar na tishio kwa Tanganyika. Aliposhindwa Nyerere ni kule kuja kuwaondowa madarakani watu wake alipomtumia Mzee Jumbe kulitawanya Baraza la Mapinduzi la wageni kutoka Bara.

Nyerere alifika mahala akawa hana tena support ya Wazanzibari wazalendo na kwa bahati nzuri Mzee Jumbe alikuwa ameshalianzisha Baraza la Wawakilishi. Nyerere alifikiria baada ya muda angeliweza kuwafanya Wazanzibari wote wawe “Waafrika” na kuukanya “Ushirazi”, “Upemba” na maana ya Ushirazi na Upemba katika kuiwekea Zanzibar hadhi yake. Haikuwa.

Sasa tunakoelekea kwenye uchaguzi wa 2010, itabidi CCM ya si Wazalendo wamtafute mtu mwenye sifa za Mzanzibari mzalendo ambaye atachanganyisha sifa za Upemba, Uunguja, na Ubara lakini asiwe na Uzalendo wa kuitetea Zanzibar. Atafutwe kibaraka Mzalendo!

Lengo ni kuwatuliza Wazanzibari ili maamuzi yaendelee yasifanyike Kisiwandui au Mtendeni. Yakafanywe Dodoma kama Sunna ya CCM inavotamka.

Suala: jee, Wazanzibari wazalendo wa CCM wataweza kumchagua kiongozi wao na iwe imetosha na pasikuweko kwenda Dodoma kuchujwa halafu kubarikiwa?

Jee, Wazanzibari wazalendo wa CCM wataweza kuondoa chuki dhidi ya chama cha CUF kwa kuondoa ile fikra kuwa wao ndio wenye kuyalinda Mapinduzi ambayo kwa fikra zao yanapingwa na CUF?

Wanasahau kuwa Mapinduzi yamekuja kumpinduwa Mzanzibari mzalendo, ikiwa alikuwa Afro-Shirazi, ZNP, CCM, au CUF.

Ndugu zetu Wazanzibari wazalendo wa CCM bado hapo hawajapashtukia na pale watakapoufikia muamko huo itakuwa rahisi zaidi kuaminiana na Wazanzibari wazalendo ndani ya CUF. Sasa hapa kuna tatizo la wanasiasa la kutaka kupikuana kisiasa na nani atamzidi nani maarifa/kete.

CUF nao hawana ajenga moja ambao iko simple, clear na consistent. Wanarukia matawi mingi bila ya kuonekana wazi ni mzizi gani ulioukamata mti wa Zanzibar na kipi khasa wanachokitaka. CUF yenye msimamo ulio wazi wenye kufahamika na usiobadilika mara kwa mara utaweza kuwavutia CCM wazalendo kwa urahisi zaidi.

Pia kuna tatizo la wenye kujifanya watetezi wa Zanzibar kwa sababu wanatambuwa kuwa kutofanya hivo itakuwa ni kwenda na maji. Kwa hiyo si kila mwenye kuitetea Zanzibar anafanya hivo kwa maslaha ya Zanzibar. Pana kutetea matumbo kwenye pande zote mbili – CUF na CCM.

Baraza la Wawikilishi wataweza kuliweka sawa suala la Zanzibar kama ni Nchi na Serikali yenye Raisi ile iweze kumchagua kiongozi wake kwa baraka za Wazanzibari wazalendo na bila ya kwenda kubatizwa Dodoma?

Hili ndilo suala (mzizi) wa kuusimamisha mti wa Zanzibar mpaka ijulikane moja wapo nainani anaweza kutoyumba kwenye suala hili na ni nani anaelitumilia kwa kupata faida za kisiasa?

Katika hichi kitendawili cha Zanzibar ni Nchi au si Nchi kuna mambo matatu lazima tuyazingatie:

  1. Unapotaka kuleta maabadiliko ya kikweli ya ilani ya Zanzibar kama ilikuwa nchi, na sasa si nchi kwa sababu Tanganyika imetunyanganya nchi yetu, ni lazima tufahamu kuwa Tanganyika haitotuachilia kuendelea na agenda muhimu kama hiyo. Madam tutaendelea kuidai Zanzibar basi Tanganyika itaendelea kutuletea majeshi kutupinga. Kuamini kinyume ya hivo ni kujidanganya na dawa yake ni Wazanzibari wazalendo kuwa kitu kimoja. Ajenda moja. Muungano yes, lakini Zanzibar iwe ni Nchi yenye kutambulikana NJE, yenye Serikali na Raisi wake ambaye anatambulikana na anaheshimiwa Tanganyika. Kama Bwana hataki tumuwache atupe talaka tatu kama Malaysia ilivoipa Singapore talaka tatu!
  2. Zanzibar itakapofaulu kutakuwa na wachupiaji wa kila aina ambao watajiita wao ndo wakombozi. Kila alohusika katika kuibomoa Zanzibar atashika bendera kuwa miaka yote alikuwa mstari wa mbele katika kugombania kuinusuru Zanzibar. Hivo ndo itakavokuwa na imeshaanza na hapo inatakiwa tuwe haadhir nani ni mkweli na yupi ni mjanja wa kisiasa. Mbwa mwitu watakaovaa ngozi za kondoo watakuwa wengi na tayari wameshatoka mashimoni na wako uwanjani wananusa upepo. Mti na macho!

  3. Lazima tuchukuwe calculated risks. Hilo haliepukiki.

Shuruti la kwanza la yote hayo ni Uhuru, si Uhuru kutoka Tanganyika au wa kuvunja Muungano. Ni Uhuru wa kumpa KILA MZANZIBARI MZALENDO lile shati la “Yusufan” lililomrejeshea macho yenye kuona Nabii Yaaqub.

Nguvu za Tanganyika zinatokana na kuwa wao wako katika sehemu wanatuona na sisi hatuwaoni. Uhuru wa Zanzibar ni kuirejeshea nuru ya macho jamii ilofanywa iwe kipofu kwa makusudi ili wenye kutuona kutoka nyuma ya pazia waendelee na agenda ya kuifanya Zanzibar Nchi Moja, Serikali Moja.

Tutakaplifungua pazia mwenye kuona atageuka kuwa kipofu na kipofu atakuwa anaona. Katika kulifanikisha hili inafaa tukae tujiulize kama wanasiasa ni ufunguo au ni mlango wa jiwe katika kuikomboa Zanzibar?

Eid Mubarak!

Harith

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.