Na Salma Said, Zanzibar

Viongozi wa Wakuu wa Vyama vya Kisiasa Zanzibar ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakivutana wamekutana katika Baraza la Eie El Fitri wiki hii na kuzungumza lugha moja ya kuwataka wananchi kudumisha amani na maelewano katika jamii ili kusaidia mustakabali wa Taifa.

Viongozi  ni Rais wa Zanzibar, Alhajj Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Alhajj Maalim Seif Shariff Hamad ambao kwa nyakati tofauti wamesema ipo haja ya kuutumia mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa ni somo kubwa kwa waumini la kuwafundisha umoja na mshikamano miongoni mwao kwa maslahi ya nchi na watu wake.

Akituhubia katika Baraza la Eid El Fitri lililofanyika Hoteli ya Bwawani, Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume amewataka wananchi kupitia sikukuu hiyo kutathimini kwa dhati malezi mema, tabia nzuri na mafunzo yote ya kheri ambayo wameyapata katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Amesema ni vyema kutumia siku hiyo ya Eid El Fitri kutia nia ya kuendeleza mema na kuwa ni misingi bora ya maisha miongoni mwa hayo ni kutilia mkazo umoja na mshikamano wa kuendeleza kustahamiliana na kuvumiliana, kukuza upendo katika jamii moja.

“Ni jambo la kufurahisha sana kwamba wakati wa kufunga watu wote walikuwa watulivu, wastahamilivu na wenye kusaidiana, huu ni utamaduni ambao ni vyema kuuendeleza. Sote kwa pamoja tujenge tabia ya kuleta umoja, kusaidiana na kushirikiana kati ya watu” amesisitiza Rais Karume.

Rais Karume pia amesisitiza suala la kuheshimu tabia na taratibu za sheria za dini na nchi na zaidi kuendeleza kusaidiana katika shughuli za maisha hasa kwa kuwafikiria wanyonge, wasiojiweza na kujimudu kimaisha ili nao wajihisi Ramadhani imewajengea ufunguzi wa kheri ya maisha na washiriki katika sherehe za Eid El Fitri.

Amewataka wananchi wote kwa pamoja wajenge tabia ya kuleta umoja na kusaidiana na kushirikiana kati ya watu kwa kunukuu aya za Quran Tukufu “Na saidianeni katika wema na ucha Mungu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui” amenukuu.

Rais Karume ameeleza haja ya kuwepo umoja na mshikamano kwa kusema kuwa Taifa lililoongka ni lile lenye wananchi walioshikamana kama jengo moja imara ili wote wasaidiane katika mema huku akiwataka wananchi kuamini njia hiyo ndiyo itakayoweza kunufaisha nchi na watu wake.

Akiunga mkono nasaha hizo Katibu Mkuu wa Chama Ca Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad nje ya Hoteli ya Bwawani wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Baraza la Eid El Fitri lililofanyika Mjini Zanzibar. Amesema ni nafasi adhimu kwa waislamu kutafakari umuhimu wa kukaa pamoja na kushirikiana katika shughuli mbali mbali za kuleta maendeleo katika nchi.

Maalim Seif amesema nchi inakuwa na baraka kutoka kwa Mwenyenzi Mungu iwapo kunakuwa na umoja na mshikamano miongoni mwa jamii na kuwataka wananchi kuutumia mwezi wa Ramadhani kuwa fundisho la kuleta umoja na mshikamano.

Katibu Mkuu huyo amewataka wananchi wote kusahau tofauti zao za kiitikadi na kuweka mbele maslahi ya taifa mbele ili kuilinda nchi yao ambapo kumeanza kujitokeza mambo ya maadui ambao hawaitakii mema Zanzibar na watu wake.

Katibu Mkuu huyo pia amesema ipo haja ya wananchi na viongozi wao kushirikiana kwa kuweka uzalendo mbele na kudumisha mila silka na utamaduni wa kizanzibari amabo umeanza kuonekana kutoweka miongoni mwa jamii kutokana na muingiliano wa watu mbali mbali.

Akizungumzia suala la serikali ya umoja Maalim Seif amesema ipo haja ya kuwepo na serikali ya umoja wa kitaifa ikiwa ni njia moja ya kufikia demokrasia ya kweli katika nchi za kiafrika.

“Sio kudidimiza demokrasia za vyama vingi lakini ni vizuri kuunda serikali za mpito kwa sababu viongozi wetu katika bara la Afrika wengi wamekuwa hawaheshimu demokrasia aktika nchi zao na wamekuwa wakingangania madaraka hata kama wameshindwa kwa kupitia sanduku la kura sasa serikali za aina hiyo hiyo ni kama njia moja ya kufikia kule kwenye demokrasia ya kweli” amesema Maalim Seif wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari

Katibu Mkuu huyo amesema Zanzibar inahitaji umoja na mshikamano kwa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa kwa lengo la kusahau na kuzika tofauti zilizopo ambazo imedumu kwa miongo kadhaa sasa.

Amesema ili kujenga imani na mahusiano mazuri miongoni mwa viongozi wa pande mbili hizo zenye kuvutana ni vyema kukawepo mazingira ya kufanya kazi pamoja kwa kuaminiana na kuondosha ile dhana ya kuweza upande mmoja kulipiza kisasi dhidi ya mwengine ili kutayarisha mazingira mazuri katika uchaguzi mkuu ujao wa 2010.

“Ni kweli Zanzibar inahitaji umoja na mshikamano na ili kuondosha tofauti zilizopo na kusahau yaliopita ipo haja kubwa ya kufanya kazi pamoja kati yetu kwa lengo la kuondosha ile dhana na kuwa mmoja anaweza kulipiza kisasi lakini pia tutakapofanya kazi pamoja tunajenga mazingira mazuri ya kuaminiana hasa katika kipindi hiki kinachokuja cha matayarisho ya uchaguzi mkuu wa 2010” amesisitiza Maalim Seif.

Awali katika sala ya Eid El Fitri Imamu Mkuu wa Masjid Jibril, Sheikh Abrahman Habshi amewataka wananchi kusameheana na kuzika tofauti zao za kiitikadi na kumcha Mwenyenzi Mungu ikiwa ni njia moja kuu ya maelewano.

Sheikh huyo amesema mwezi wa Ramadhan umekwisha lakini sasa wananchi kama walivyoweza kuvumiliana na kusatahamiliana na kusaidiana katika hali zote basi uvumilivu huo uendelee na isiwe unafanyika kwa mwezi wa Ramadhani peke yake kwani Allah anampenda mja wake mwenye kuendeleza mema na ucha Mungu.

Hata hivyo akitoa nasaha zake amewataka waumini wa dini ya kiislamu kushikamana katika njia ya Allah na kujenga umoja na mshikamano wa kweli kwani Mwenyeenzi Mungu amehimiza watu kushikana katika kamba yake na wala wasifarikiane.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.