Labda katika hotuba yake ya 21 Agosti 2008 Bungeni, Rais Jakaya Kikwete alikusudia kuumaliza kabisa mjadala wa ikiwa Zanzibar ni nchi au la, lakini kama ambavyo amekuwa akifeli katika mambo mengine yanayohitaji umakini na kusimamisha uongozi (providing leadership), amefeli pia katika hili. Badala yake, Rais Kikwete ameibua mjadala mzito zaidi, ukiwemo wa ikiwa kumbe Tanganyika nayo ni nchi…. Makala hii iliyochukuliwa kutoka mtandao wa ZanziNet inauhakiki mjadala huo.

Akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano, Agosti 21, mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alisema hivi kuhusu hadhi ya Muungano: “Muungano huo ambao ulifikiwa kwa hiari ulisababisha kuzaliwa kwa mamlaka moja ya Tanzania ambayo kimataifa ndiyo inayotambuliwa rasmi kama nchi.”

Hata hivyo alisema, hali hiyo haiwezi kuacha kando ukweli kwamba, katika mazingira ya ndani ya nchi, bado kuna nchi ya Zanzibar ambayo ni sehemu ya Tanzania, na Tanganyika ambayo pia ni sehemu ya Tanzania: “Kwa mambo ya ndani yapo ya nchi ya Zanzibar ambayo ni sehemu ya Tanzania, na ya nchi ya Tanganyika ambayo nayo ni sehemu ya Tanzania,” alifafanua Rais.

Rais alikiri kuwapo kwa tofauti kati ya pande hizi mbili za Muungano (Zanzibar na Tanganyika), akasema: “Tofauti zetu zinazojitokeza zinazungumzika na tuzizungumze.”

Rais Kikwete amekuwa Rais na kiongozi  wa kwanza wa juu kukiri kuwapo kwa nchi ya Zanzibar na nchi ya Tanganyika ndani ya Muungano, jambo ambalo huko nyuma lilichukuliwa kama uhaini na kitendo cha kutaka kuvunja Muungano, wakati kumbe ni kuuimarisha.

Kabla ya hotuba ya Rais Kikwete, wabunge walikuwa wamegawanyika juu ya hadhi ya Muungano, hususani kama Zanzibar ni nchi au la, hoja ambayo ilkuwa imeshupaliwa kwa pamoja na wabunge kutoka Zanzibar bila kujali tofauti zao za kiitikadi na kumfanya Mbunge Lucas Seleli (Nzega) aseme bora Muungano uvunjwe: “Kuvunja Muungano ni jambo baya, lakini kama wanataka kufanya hivyo…tufikie mahali tuamue mambo mawili, kuvunja Muungano, au tuwe na Serikali moja,” alisema.

Naye Hafidh Ali Tahir (Dimani), akinukuu maneno ya hayati Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar na muasisi wa Muungano, alisema: “Muungano ni kama koti, ukiona linakubana ni vema ukaachana nalo.” Alisema Katiba ya Jamhuri imejifunga sana kiasi cha kutoweka wazi kuhusu kipi kinastahili kwa Zanzibar, jambo linalowafanya Wazanzibari waendelee kutatizwa, “Kwa nini tusipewe ile hati ya kuonyesha waasisi waliunganisha mambo gani?” alihoji Tahir.

Naye mbunge wa Mchinga, Mheshimiwa Mudhihir wa Mudhihir, alisema: “Wanaodai mambo (ya Muungano) yameongezwa wanakosea, kwani makubaliano (mkataba) ya Muungano si Biblia au Msahafu ambao hauwezi kubadilishwa.”

Mitazamo hii kinzani ya wabunge, iliyojikita juu ya utata wa muundo wa Muungano wetu ndiyo mitazamo tata vile vile kwa umma wote wa Kitanzania, ambayo bila kuipatia msimamo na ufumbuzi  Muungano wetu utazidi kuyumba.

Tuanze na hoja ya Mheshimiwa Seleli, ni dhahiri alitumia hoja ya nguvu badala ya nguvu ya hoja kutoa hisia zake. Ikumbukwe kwamba hoja ya kuwa na Serikali moja ilikataliwa tangu enzi za waasisi wa Muungano kufuatia hoja ya Zanzibar kukataa kumezwa ndani ya tumbo la Tanganyika kubwa. Kwa hiyo, hoja ya Seleli ya kutaka kuvunja Muungano au kuunda Serikali moja haina msingi.

Naye Mudhihir wa Mudhihir, kwa kuwaponda wanaodai kuongezwa kinyemela kwa mambo ya Muungano, anaonyesha uelewa mdogo wa misingi na Makubaliano ya Muungano na utaratibu wa kikatiba unaotakiwa kutumika kuongeza mambo ya Muungano, kama ilivyofafanuliwa vizuri katika Hati ya Muungano (Articles of Union) na Sheria za Muungano (Acts of Union) ambazo lazima ziheshimiwe.

Kauli ya Mheshimiwa Hafidh Tahir (akimnukuu hayati Abeid Karume), kwamba Muungano ni kama koti unaloweza kulivua likikubana, inaonyesha uhiari wa Muungano na jinsi nchi hizi mbili zilizoungana zilivyo na hiari ya kuendeleza au kuuvunja zikipenda, jambo ambalo sote tunakiri ni baya, na Rais amesema wazi kwamba kero za Muungano zinazungumzika.

Kauli ya Tahir juu ya uhiari huo wa Muungano inashabihiana na kauli ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika makala yake kwenye gazeti la “The London Observer” la Aprili 20, 1968 aliposema: “Kama umma wa watu wa Zanzibar, bila ya kurubuniwa kutoka nje, na kwa sababu zao wenyewe, wakaamua kwamba Muungano hauwatendei haki juu ya kuwapo kwao, nisingeweza kuwashurutisha kubakia ndani ya Muungano. Muungano ungekoma kuwapo pale (nchi) wanachama wake zingejitoa.”

Ninakubaliana na hoja ya Tahir, kwamba Katiba ya Jamhuri imejifunga sana kisasi cha mtu kushindwa kuelewa nini kilichokubaliwa kwenye Hati ya Muungano na kwenye Sheria za Muungano ambazo zote hizi (Hati ya Muungano/Sheria ya Muungano) ndizo mhimili na msingi mkuu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, jambo ambalo Mheshimiwa Mudhihir anashindwa kulielewa.

Kuna kila sababu kwa wabunge (na wananchi) kupewa nakala ya mkataba wa Muungano, hoja ambayo imeungwa mkono pia na Profesa Haroub Othman wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakati akizungumza na gazeti la “Taifa Letu” hivi karibuni.

Tumeeleza mara nyingi kwamba uhalali wa Muungano wetu hauhojiki. Wale wanaodai kwamba wananchi waliburuzwa kwenye Muungano (bila ya kura ya maoni) wanajikosesha, kwani Marais wa nchi hizi mbili walikuwa na uhalali, uwezo na mamlaka ya kuingia mkataba wa kimataifa kama huo bila kura ya maoni ya wananchi wa nchi zao.

Nyerere alipata mamlaka hayo chini ya Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika ya 1962, na Karume alifanya hivyo kwa mujibu wa Amri ya Rais (Presidential Decree) ya 1964.

Mtindo wa kura ya maoni (referendum) kwa nchi zinazofuata mfumo wa Sheria wa Uingereza (Common Law System) Tanganyika na Zanzibar zilikuwamo, ulikuwa haujulikani wakati huo; na ulianza kutumika miaka ya 1970 wakati wa mgogoro/sakata la Uingereza kujiunga na Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Ulaya (EEC), sasa Umoja wa Ulaya (EU).

Zipo kumbukumbu kuonyesha kwamba baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, Mwalimu Nyerere alifanya mawasiliano na Rais Abeid Karume mara nyingi kumtaka waingie Muungano wa nchi zao.

Kwa kuanzia, Mwalimu aliwatuma Bibi Titi Mohammed, Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Tanganyika African National Union (TANU) na Naibu Waziri, na Oscar Kambona, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Mambo ya Nje. Karume alimjibu Mwalimu kupitia wajumbe aliowatuma kwamba alihitaji muda zaidi kufikiri juu ya jambo hilo na muda wa kuirekebisha hali ya ndani ya nchi yake. Kabla ya kuondoka Zanzibar, ujumbe huo ulionana na Mabwana Saleh Saaddalah na Kassim Hanga na kuwaomba wamshawishi Karume akubali kuungana. Mwalimu alituma ujumbe wa pili ukiwahusisha Mawaziri Tewa Saidi Tewa na Job Lusinde; na Mei 21, 1964 Karume alikwenda Dar es Salaam kuitika mwaliko wa Mwalimu. Katika ziara hiyo ya saa chache Karume alifuatana na maafisa usalama watatu pekee na kurejea Zanzibar siku hiyo hiyo.

Kinachobishaniwa na wengi sasa si uhalali wala umuhimu wa Muungano, bali ni muundo wa Muungano uliokusudiwa. Dhambi kubwa inayofanywa na viongozi wetu madarakani na kuzua kero nyingi na kubwa ni ile ya kuwanyima wananchi elimu  juu ya msingi wa Muungano na kuhusu kilichokubaliwa, na hivyo kuufanya Muungano uonekane wa viongozi na si wa wananchi.  Na hapa swali linalokita daima bila kupata jibu ni hili: “Ni Muundo gani wa Muungano uliokusudiwa?”

Kwa kutumia hotuba ya Rais Kikwete, tutajaribu, katika makala haya, kuelezea aina ya Muungano uliokusudiwa na kwa nini Mheshimiwa Rais, amethubutu kukiri kwa mara ya kwanza kuwapo hai kwa Tanganyika na Zanzibar ndani ya Muungano wa Tanzania.

Mkataba wa Muungano unaofahamika kama “The Articles of Union” kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ulitiwa sahihi Aprili 22, 1964 na kuridhiwa na Mabunge ya nchi hizo, kabla ya Muungano huo kutangazwa rasmi hapo Aprili 26, 1964.

Tanganyika na Zanzibar hazikuungana kwa mambo yote bali kwa mambo kumi na moja tu, ambayo ni: Katiba ya Muungano huo, Mambo ya nje, Ulinzi, Polisi, Mamlaka kuhusiana na mambo ya hali ya hatari, Uraia, Uhamiaji na Utumishi katika Jamhuri ya Muungano.

Mengine ni mambo ya Kodi, Ushuru wa forodha; Bandari, Usafiri wa anga, Posta na Simu. Kwa mambo yasiyotajwa, mbali na haya kumi na moja, Tanganyika na Zanzibar ziliendelea kusimamia mambo yake ya ndani yasiyo ya Muungano na kujiendesha kama nchi  kwa kutumia Sheria zake za Bunge bila kuingiliwa na Serikali ya Muungano. na Mkataba wa Muungano uko wazi juu ya hilo, kwamba (ibara ya 4) “Sheria za sasa za Tanganyika na za Zanzibar zitaendelea kuwa na nguvu katika nchi hizo.”

Mkataba wa Muungano na Sheria za Muungano zote ziko hai na zenye nguvu mpaka sasa, ingawa zinakiukwa kila mara. Kwa mantiki hii, ni kwamba, kufuatia Muungano wa mambo hayo kumi na moja tu, Serikali ya Muungano ilitakiwa kuwa na Katiba yake wakati Tanganyika na Zanzibar nazo zilitakiwa kila moja kuwa na Katiba yake kuendesha Serikali kwa mambo yasiyo ya Muungano.

Na kuhusu mambo ya nje ya Muungano, Tanganyika na Zanzibar zilipoteza hadhi ya kuitwa nchi nje ya mipaka yake (kimataifa) kwa sababu zilikubaliana kujikabidhi katika duru za kimataifa (mambo ya nje) kwa jina la Muungano wa Tanzania. Vivyo hivyo, zilikubaliana kuvunja majeshi yake, Polisi na mambo ya hali ya hatari ili yashughulikiwe na Serikali ya Muungano. Ni kukiuka makubaliano ya Muungano, kwa Zanzibar sasa kuwa na vikosi vyake vya ulinzi vyenye kuitika kwa Serikali ya Mapinduzi kwa maana suala la ulinzi ni jambo la Muungano.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.