Rais Jakaya Kikwete. Jibu lake kwa hadhi ya Zanzibar halijakidhi haja wala kujenga hoja. Anatakiwa aitishe mjadala wa kitaifa kuujadili Muundo wa Muungano, kwani ndio tatizo
Rais Jakaya Kikwete

Katika makala hii iliyoandikwa katika gazeti la Tanzania Daima la Septemba 3, 2008, Edward Kinabo anahoji kwamba agizo la Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwamba suala na hadhi ya Zanzibar liamuliwe na wanasheria wa pande mbili za Muungano au na vikao vya juu vya CCM halina mashiko ya kimantiki, maana tatizo hili ni la kitaifa si la kiserikali wala kichama. Badala yake anaungana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kudai mjadala mpana juu ya muundo mwengine wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

WIKI chache zilizopita, mjadala uliokuwa umefungwa kwa muda, ulifunguka tena. Zamu hii ufunguo uliotumika ni mjadala wa Bunge juu ya hotuba ya Wizara ya Sheria na Katiba, iliyowasilishwa na Waziri Mathias Chikawe.

Rais Kikwete naye katika hotuba yake akajaribu kutoa kauli za kuzima mjadala huu lakini kama ilivyoripotiwa na gazeti hili juzi na jana ni kwamba “JK amegonga mwamba.” Ameshindwa kuwaridhisha Wazanzibari kuhusu hadhi ya Zanzibar. Kimsingi, kugonga mwamba kwa Rais Kikwete kunatokana na azima ya serikali yake kutaka kujibu hoja zinazotolewa badala ya haja inayotakiwa.

Huu ni mjadala juu ya hadhi ya Zanzibar kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Mada ya mjadala huu ni kwamba ‘Zanzibar ni nchi kamili inayojitegemea au ni sehemu tu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar?’ Katika mada hii kuna pande kuu mbili za hoja, moja ni ile inayosema kuwa Zanzibar ni nchi na nyingine ni ile inayosema Zanzibar si nchi, bali ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.

Serikali ya Kikwete inataka kujibu hoja hizi kupitia wanasheria wakuu wa Zanzibar na wale wa Muungano kama alivyosema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (mchokonozi wa hoja hii) bungeni. Wanataka kutazama hoja, wanasahau kuwa ipo haja ambayo haiwezi kutimizwa kwa kujibu kuwa Zanzibar ni nchi au si nchi.

Niweke wazi kuwa pamoja na kuambiwa tusubiri matokeo ya wanasheria hao, tayari Kikwete katika hotuba yake ameshatuchanganya zaidi. Kwanza, alisema kuwa tunapozungumzia suala hili kwa mtazamo wa kimataifa basi nchi ni moja tu, nayo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini tunapozumngumza wenyewe humu ndani, basi nchi ni mbili, nazo ni Tanganyika na Zanzibar.

Hapo aliibua mjadala mwingine wa hadhi ya Tanganyika, sina hakika kama alitaka iwe hivyo au pengine umakini wake ulipungua! Hapa tunaweza kujiuliza, iko wapi Tanganyika? Tanganyika ina hadhi katika serikali ya muungano? Ingawa alitoa jibu alilofikiri kuwa litafurahisha pande zote mbili zinazopingana, hakufanikiwa.

Kibaya zaidi, baada ya kutupa jibu ambalo sidhani kuwa wanasheria wake watampinga, bado anatutaka tuendelee kusubiri matokeo ya wanasheria hao kuhusu hadhi ya Zanzibar. Hii si sawa, naamini tunapoteza muda! Matokeo yake, Wazanzibari wameripotiwa kuwa wanaendelea kumpinga. Maandamano ya kumpongeza huko Unguja yalikwama na kuvunjwa kwa sababu zisizojulikana. Vipeperushi vimeanza kuenezwa kusisitiza kuwa Zanzibar ni nchi. Hii inazidi kutuashiria kuwa hata uchambuzi wa wanasheria nao pia utagonga mwamba. Hautakidhi kile kinachotakiwa.

Kwa nini JK amegonga mwamba kuhusu hadhi ya Zanzibar? Niweke bayana kuwa lengo la makala hii si kujibu kuwa ‘Zanzibar ni nchi au si nchi’ na wala si lengo la makala hii kushabikia mwenendo wa malumbano yanayoendelea.

Ukweli juu ya Zanzibar kuwa nchi au si nchi ni mjadala uliopata wachangiaji wengi, tena wa kada mbalimbali. Yamesemwa mengi, wacha nigusie kidogo hoja za wachangiaji kwa jumla wake. Kwa upande mmoja, kuna waliosema kuwa Zanzibar ni nchi kwa kuwa ina eneo na mipaka yake, watu wake ambao ndio Wazanzibari wenyewe, inayo katiba inayounda serikali ikiwa na rais na baraza la mawaziri, mahakama na chombo cha kutunga sheria na kuwawakilisha wananchi wa nchi hiyo (Baraza la Wawakilishi).

Kwa upande mwingine, wapo waliosema Zanzibar si nchi wakimuunga mkono waziri mkuu. Kwa hawa, nchi ni Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kwa mantiki yao, Zanzibar ni sehemu ya nchi hii. Wakatoa mifano ya Zanzibar kutotambulika kama nchi kwa Umoja wa Mataifa (UN) na kwa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).

Wakanukuu vipengele kadhaa vya katiba na kufanya rejea ya hukumu za kesi mbalimbali za nje na ndani ya nchi hususan ile ya uhaini na kushawishi kile wanachokiamini wao kuwa Zanzibar si nchi.

Kimsingi, ni mjadala uliojikita katika hoja na ubishi. Wapo walioelimisha na walioamua kupotosha. Wapo waliosema wasichokijua na wapo waliojisikia kubishana. Inatosha! Sina sababu ya kuendeleza usahihi au upotoshaji juu ya Zanzibar kuwa nchi au la. Hata nikifanya hivyo, sitakidhi haja ya wahusika wa mjadala huu.

Sitaki kurudia kosa ambalo Kikwete amelifanya na ambalo wanasheria pia wanaelekea kulifanya. Sitaki kuamini kuwa wote wanaolumbana, ndani na nje ya Bunge na Baraza la Wawakilishi ni watu wasiojua kusoma na kuandika hata kushindwa kusoma katiba na sheria kisha kubaini ukweli wa suala hili.

Ndiyo, wanaweza kujitetea kuwa kuelewa sheria na matumizi yake ni jambo gumu linalohitaji ujuzi na uzoefu lakini, sitaki kuamini kuwa eti wahusika wamekosa kabisa wanasheria makini wa kuwasaidia kuelewa hadhi ya Zanzibar. Inawezekana kabisa kwa katiba na sheria zetu kuwa na utata, lakini sitaki kuamini kuwa utata huo ni mkubwa kiasi cha kuibua mjadala mkali kiasi hiki.

Naamini kuwa wengi wanaolumbana wana uwezo wa kuuelewa ukweli. Sidhani kwamba wanahitaji kufahamishwa hilo na wanasheria wa Pinda. Tatizo ni ama wameuelewa ukweli wasioutaka au wanataka wanachokitamani kiwe ukweli wenyewe. Inawezekana pia, wapo wasioridhishwa na maslahi ya ukweli huo, hawa bila shaka haja yao ni kujenga msingi wa kusimamia masilahi hayo au kutaka kuungwa mkono kwa kuwa mstari wa mbele kusimamia ukweli huo! Mwenendo, uzito na mshikamano wa watu wa pande hizi mbili katika mjadala huu, vyote vinaashiria dhahiri kuwa kuna haja ya msingi inayopaswa kutimizwa.

Kwa mantiki hiyo, lengo la makala hii ni kutathmini njia inayotumiwa kutafuta suluhu ya suala husika. Njia hii ni ile iliyotajwa na Waziri Mkuu Pinda na kutajwa tena na Rais Kikwete kwenye hotuba yake bungeni, kwamba wanasheria wakuu wa pande hizi mbili watakaa na kulifanyia kazi suala hili kisha watalitolea ufafanuzi. Kwamba jibu la Zanzibar ni nchi au la, litajibiwa baada ya wataalamu hawa kufanya uchambuzi wa kina wa katiba na sheria.

Ipo njia nyingine pia aliyotutangazia Pinda kwamba suala hili litajadiliwa ndani ya chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hii inamhusu zaidi yeye na wenzake ndani ya chama chao. Kwa maana ni njia iliyo nje ya utaifa. Imekumbatiwa na uchama. Hata kama taathira yake itagusa taifa, bado kwa sasa sioni uhalali wa taifa kujihusisha nayo.

Zanzibar na hadhi yake si mali ya CCM. Kwa mantiki hiyo, tutathmini njia inayotuunganisha sote kama taifa katika kushughulikia suala hili, njia ya kisheria. Je, uchambuzi wa kisheria utakidhi haja?

Kabla hatujatathmini hili na hata kupendekeza nini hasa kifanyike katika kumaliza malumbano haya, kuna masuala ya kujiuliza hapa. Kwanza, iwapo baada ya uchambuzi huo wa kisheria jibu litakuwa Zanzibar si nchi bali ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano, je, Wazanzibari wataridhika – hata kama ukweli utaonekana dhahiri kuwa ni huo?

Pili, ‘wataalamu’ wa Pinda wakitujibu kuwa Zanzibar ni nchi je, Wazanzibari wataridhishwa na jibu hilo? Hayataibuka madai mengine kuhusu Zanzibar kuwa nchi? Wabara je, wataridhika iwapo jibu litakuwa Zanzibar ni nchi? Hawatadai Tanganyika yao? Na mbona mjadala bado unaendelea hata baada ya kutoa jibu lililojaribu kuridhisha pande zote? Hapa kuna haja ya msingi inayopaswa kutimizwa. Je, suluhu ya kisheria itakidhi haja hii?

Tukijiuliza haya tunaweza kubaini kuwa kinachotafutwa ni zaidi ya mtu kujua kuwa Zanzibar ni nchi au si nchi. Mjadala huu ni mwanya unaotoa fursa kwa watu kutatua kero zao na wengine kuhakikisha kuwa hakutokei mazingira mapya ya wao kuwa sehemu ya kero hizo.

Naam! Ni kero za miaka mingi – kero za Muungano. Hili linathibitishwa pia na baadhi ya kauli nzito zinazoambatana na hoja za mjadala wenyewe kama ifuatavyo:

Julai 25 mwaka huu, mfanyabiashara maarufu wa Zanzibar, Mohamed Raza, alinukuliwa na Tanzania Daima akisema: “Upepo wa suala la Muungano uliovuma mwaka 1984 ni tofauti na upepo wa safari hii, kwani hauvumiliki kwa Wazanzibari”. Kauli hii inaweza kuwa na maana kadhaa lakini inatupa jibu moja la msingi kuwa kinachotafutwa si jibu la hadhi ya Zanzibar pekee, bali ni suala zima la Muungano ambalo kimsingi haliwezi kutimizwa kwa jibu la Zanzibar ni nchi ama la.

Jana, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, iliripotiwa kuwa amepasua jipu. Alisema Wazanzibari hawaridhishwi na muundo wa sasa wa muungano. Kauli hizi zote zinatuthibitishia kuwa kinachotakiwa si kujibiwa kuwa Zanzibar ni nchi au si nchi bali ni kuondoa kero zote za muungano kwa mapana yake.

Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF), aliwahi kuuliza: “Kipi kiko juu kati ya Katiba na Makubaliano ya Muungano?” Hili halikujibiwa. Spika alikataza kwa kuwa lingejibiwa, basi Bunge lingeweza kurejea tena katika suala ambalo tayari waziri mkuu alishasema linashughulikiwa na wanasheria wakuu wa pande zote mbili.

Ukweli ni kuwa kilicho juu ni Makubaliano ya Muungano yaliyozaa Katiba hiyo ya Jamhuri ya Muungano, ambayo ndiyo sheria mama ya muungano huo. Siasa huzaa sheria. Sheria huheshimika, hufuatwa na huwa na nguvu pale inapokidhi haja na matakwa ya watu. Watu huridhiana haja na matakwa yao kwa njia za ushawishi, majadiliano na hatimaye maafikiano. Hii ni siasa. Baada ya siasa hii, ndipo watu huweka sheria za kulinda na kusimamia maafikiano hayo. Hapo ndipo huzaliwa katiba na sheria nyingine.

Kwa mantiki hiyo, kunapotokea tatizo kubwa katika suala ambalo chanzo chake ni maafikiano ya kisiasa, basi tatizo haliwezi kutatuliwa vema kwa kuanzia kwenye sheria. Litatatuliwa kuanzia kwenye siasa iliyosababisha kutengenezwa kwa katiba ama sheria ambazo sasa hazikidhi haja za wahusika.

Kwa mantiki hii ni vyema ikaeleweka kuwa suala la hadhi ya Zanzibar linagusa muktadha mzima wa kero za muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ambalo chanzo chake kilikuwa ni majadiliano na hatimaye makubaliano ya kisiasa kati ya Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume kuwa “sasa tuungane”.

Kwa hiyo, ili kumaliza suala la hadhi ya Zanzibar ni vema Kikwete na wenzie wakakubali ukweli kuwa baada ya miaka 44 ya Muungano huu, sasa kuna haja ya dhati kabisa ya kufanyika kwa mjadala mpya wa kitaifa juu ya Muungano wetu ili kubaini kwa kina upungufu uliopo na kutoa fursa kwa watu wa pande zote ambao hawakuwahi kushirikishwa kuwasilisha haja na matakwa yao yatakayoendana pia na wakati walionao.

Haja hizo mpya ndizo zitakazoboresha ama kujenga makubaliano mapya ya muungano yatakayozaa katiba na sheria mpya za muungano huo. Lakini tukianzia kwenye sheria zilizopo hatutakwama kwa kuwa katiba yenyewe haiakisi haja za wahusika wa muungano huu.

Naungana na Maalim Seif kuwa muundo wetu wa muungano hauwaridhishi Wazanzibari. Kwa mtazamo wangu muundo huu ndio kiini cha kero nyingine zote za muungano. Ni muundo huu ulioitoa Tanganyika katika historia ya dunia na kufanya hadhi ya Zanzibar kuwa kero kwa Wazanzibari. Kipindi chote hiki Muungano huu umedumu kwa serikali kunyamazisha wale wanaoibua kasoro zake au kufanya utatuzi usiomaliza tatizo la msingi.

Naamini kuwa Kikwete na wenzie wanalijua hili, lakini wanalikwepa kwa kuwa sera ya chama chao si kutimiza haja mpya za muungano. Kwa wao muungano wetu wa serikali mbili uko sawa ila una matatizo madogo madogo ya hapa na pale ambayo kurekebishwa kwake hakuhitaji kujadili muundo huu iwapo unakidhi haja au haukidhi haja.

Kikwete na wenzake wanaunga mkono muundo huu kwa kuwa ni sera ya chama chao – CCM. Katika kitabu cha “Uongozi wetu na hatma ya Tanzania”, kilichoandikwa na Mwalimu Nyerere imeelezwa kuwa serikali ilitetea kwa nguvu zote muungano wa serikali mbili na kupinga ule wa serikali tatu kwa hoja kuwa kuunda serikali tatu kungekuwa na gharama kubwa sana za uendeshaji wa nchi.

Pia ilielezwa kuwa serikali tatu zingedhohofisha umoja na mshikamano wa muungano huo. Kuhusu serikali moja, muundo huu unadaiwa kuwa utaimeza nchi ndogo ya Zanzibar kuwa sehemu ya Tanganyika itakayoitwa Tanzania.

Umefika wakati wa Kikwete na wasaidizi wake kukubali kuwa tujadili muundo wa muungano wetu, vinginevyo ataendelea kugonga mwamba.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.