Na Ali Nabwa, Juni 12, 2002
Marehemu Ali Nabwa

Kwa namna alivyoonekana na alivyojijenga, Mwalimu Julius Nyerere hakufikiriwa kwamba angeliweza kutumiliwa kulinda maslahi ya mataifa ya kibeberu dhidi ya nchi changa za Kiafrika, ambazo mwenyewe alitaka iaminike kwamba anazitetea na kwamba yeye  ni muumini mkubwa wa Pan-Africanism (dhana inayopingana kabisa na Imperialism). Lakini, katika makala hii iliyochapishwa kwa mara ya mwanzo Juni 12, 2002, katika gazeti la Dira Zanzibar, Ali Nabwa (ambaye sasa ni marehemu), anahoji kwa ushahidi kamili kwamba Nyerere alitumiliwa na Uingereza kuipokonya Zanzibar fedha zake baada Mapinduzi na Muungano wa 1964

Tumeona madai kwamba hapakuwa na mazungumzo ya maana baina ya pande mbili za Muuungano zilizodaiwa kuwa sawa kuhusu Marekebisho ya Kumi na Moja ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Yaliyofichuka ni kwamba, kuna mkataba wa upande mmoja (unequal treaty). Matokeo ya uchunguzi wangu ni ya kushangaza kuliko hadithi za James Bond. Mambo matatu yamejitokeza: mosi, wakati Zanzibar iliingia katika Makubaliano ya Muungano kama Dola huru inayojiamulia yenyewe khatima yake, Tanganyika ilikuwa kama karagosi anayechezeshwa na mkono wa London. Pili, maadili yaliwekwa pembeni na mwito ulikuwa ni kuikaba roho Zanzibar kwa vyovyote vile. Tatu, lengo kuu lilikuwa kuifanya Zanzibar mkoa wa Tanganyika.

Tuchukue mfano mmoja: uanachama wa Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki. Nimebahatika kuona nyaraka za zaidi ya miaka arubaini iliyopita ambazo zinajieleza zenyewe. Kwa kuzingatia kwamba zaidi ya miongo mitatu ishapita, barua hizi zilizoko Crown Agency London si siri tena (declassified).Tunahisi Watanzania wa pande zote mbili wana haki ya kujua yaliyopita nyuma, ili waweze kuangalia upya mahusiano yao na kuimarisha  Muungano kwa kurekebisha kasoro tunazozieleza humu na nyengine nyingi.

Wakati wa ukoloni zile nchi zilizojulikana kama East African Territories, Kenya, Uganda, Tanganyika, Zanzibar, Somalia na Aden, zilikusanywa pamoja katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, East African Currency Board (EACB). Baada ya uhuru, Aden na Somalia zilikwenda njia zao, lakini nchi zilizobakia ziliendelea na mpango huu wa pamoja wa sarafu na fedha.

Kadhia inaanza na barua ya Juni 1, 1964 kutoka kwa H.R Hirst wa EACB kwenda kwa Waziri wa Fedha wa Tanzania, J.D Namfua. Katika kifungu cha tatu, barua inasema: “Suala la iwapo Zanzibar inastahiki kuwakilishwa pekee katika Bodi ni muhimu sana na nitashukuru nikipata ushauri wako kama kutakuwa na mwakilishi kutoka  Zanzibar katika mkutano ujao…”

Kabla Namfua kujibu, J.B.Loynes, anamuandikia Hirst kutoka Hertfordshire, Uingereza akisema: “Punde hivi nimemuandikia Hinchey kwamba isipokuwa kama kuna kauli madhubuti kutoka Dar es Salaam inayothibitisha kuhudhuria kwa Zanzibar (na tusiwe sisi tunaozua suala hilo), haitokuwa sawa kwa Bodi kumualika mwakilishi kutoka Zanzibar kwa sasa. Kusema kweli, italeta fadhaa (embarrassment) kuona wale wenye nia ya kujitenga huko Visiwani wanapewa kichwa.”

Lakini kulikuwa na kauli madhubuti kutoka Dar es Salaam. Namfua alimuandikia Hirst Juni 9, 1964 kusema “Nimeagizwa kutamka kwamba kwa mujibu wa Katiba ya muda inayoongoza Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar, katika vikao vya siku za mbele vya Bodi utaendelea kwa utaratibu ule ule kama ilivyokuwa kabla ya Muungano. Makubaliano ya Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar hayahamishi moja kwa moja (does not specifically transfer) mambo ya sarafu kuingia katika Serikali ya Muungano na mpaka  yatakapofanywa mabadiliko kama itakavyokubaliwa, uanachama wa Bodi ya Sarafu unabaki kama ulivyo.” Msimamo huu ulisambazwa na Sekretarieti ya Bodi katika barua ya pamoja (circular) ya Juni 19, 1964 kwa Hazina za Uganda, Kenya na Aden.

Lakini Loynes hakuvunjika moyo. Alimuandikia Hirst Septemba 8, 1964 akisema: “Tunaweka wazi kwamba hatuitaki Zanzibar katika kikao chetu kinachofuata na natumai njia zinaweza kupatikana kuwaweka nje. Lile ambalo ningependa kufanya kwa sasa ni kukumbusha juu ya suala hili ili kuhakikisha kwamba hakuna makabrasha yanayovuka bahari hadi tutapokuwa na uhakika wa msimamo wetu.”

Bila ya shaka hawakuweza kufanya hivi kwa njia ya kisheria na yanayofuata yataingia katika historia kama moja ya dhambi kubwa zilizofanywa kwa jina la Dola. Hirst alimuandikia Edwin Mtei, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ya Tanganyika akimpelekea “nakala moja zaidi ya kila waraka …badala ya kuzipeleka moja kwa moja Zanzibar kama ilivyokuwa utaratibu huko nyuma”.

Hata hivyo, katika kuandikiana barua huko kote, Hirst anaonekana kuwa na wasiwasi juu ya uhalali wa yale aliyotakiwa kufanya na wakubwa zake. Katika barua hii anasema: “Tunachukulia kwamba utahudhuria kikao kama mjumbe wa Bodi kwa Jamhuri ya Muungano, lakini bila ya shaka utapenda kufikiria kama nakala za ziada zinafaa zipelekwe Zanzibar kwa taarifa.”

Mgao wa ziada wa fedha za bodi ulifanywa Oktoba 1964 na fungu la Zanzibar hapo, na kuanzia hapo, lilikwenda katika kasha la Tanganyika katika Crown Agency (rejea barua ya W.H. Tweed ya Oktoba 1, 1964). Hata hivyo, kwa vile Bodi ilijua fika inafanya mambo kinyume na sheria, iliendelea kuwa na wasiwasi na ikaamua kuanza kupeleka tena nyaraka Zanzibar kwa barua ya Oktoba 7, 1964.

Tarehe 3 Novemba 1964, Ofisi ya Ofisa wa sarafu Dar es salaam (Tanganyika) ilimuandikia Katibu wa EACB ikitaka kujua ikiwa ofisi hiyo ijulikane kama “Ofisi ya Tanzania ya Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki” na kutahadharisha: “Mabadiliko haya ya jina la Ofisi huenda yakaleta sura kwamba ni dhamana kwa sarafu Zanzibar, na kwa hiyo sina hakika kama ni vyema kubadilishwa.”

Katika majibu yake, Katibu wa EACB alipiga chenga suala hili kwa kusema “kiasi nijuavyo mimi, nchi zinazounda Tanzania zingali zinaitwa Tanganyika na Zanzibar.” Akaongeza: “inaonesha hakuna wasiwasi, kwa hivyo, kwamba Ofisi yako iendelee kuonekana kama Ofisi ya Tanganyika.”

Hata hivyo, sehemu ya dondoo (notes) za Loynes juu ya kikao kisicho rasmi baina yake na Makatibu Wakuu (Fedha) wa Kenya, Tanzania na Uganda kilichofanyika Dar es Salaam Februari 23, 1965, zinaeleza: “Niliwekewa wazi huko nyuma na Mtei, kwamba kikao kamili cha Bodi kitaleta fadhaa (embarrassing) kwa hivi sasa kwa vile haitowezekana kuepuka kuwepo kwa mwakilishi wa Zanzibar.”

Ghilba hii ‘ilihalalishwa’ kwa Toleo la Sheria (Legal Supplement), Mswada (Bill) Na. 43, la Juni 18, 1965, ambapo ilielezwa:“2. Mambo yafuatayo sasa yanatengwa (reserved) kwa Bunge na Serikali ya Jamhuri ya  Muungano na yanatangazwa kuwa mambo ya Muungano …(Currency, coinage and legal tender (including paper money )- mambo yanayohusiana na sarafu na mzunguko wake – na  shughuli za benki, edha za kigeni na udhibiti wa viwango vya kubadilishana fedha, na kifungu kidogo (1) cha kifungu 68 cha Katiba ya Muda hivi sasa kinarekebishwa kwa kuongeza mambo yaliyotajwa kama jambo jipya (new item) (xii) katika tafsiri ya ‘Mambo ya Muungano’.

Ujambazi wa hali ya juu! Halafu leo mtu anathubutu kusema, bila kupepesa macho, kwamba “Katiba iliyopo inakidhi haja.” Haja ya nani? Basi hii ilitupilia mbali ile rega rega ya Jacob Namfua ambaye alikufa katika ajali ya gari ambayo haikuelezeka uzuri (hadi leo) na nafasi yake ikachukuliwa na Maridhia Amir Jamal.

Kama tulivyokwisha kueleza, Mkataba wa Muungano (Mkataba uliozifunga Dola mbili zinazoungana) ulikuwa na mambo 11 ambayo yalikubaliwa kama mambo ya Muungano. Kwa njia za maajabu yameongezeka kufikia 23 (na ukiyanyambua yanafikia 34).

Hapa tunaona mambo yalivyokuwa yakifanyika na yanavyoendelea kufanyika. Huu ni uonevu dhahir uliofanywa na Nyerere, Jamal na Mtei kwa kuchochewa, kuongozwa na kudhibitiwa na watawala, wakoloni mamboleo. Tunaona jinsi gani watawala hawa walivyowadharau vibaraka wao wakati huo huo walipokuwa wakiwatumia kuibana Zanzibar ambayo ni wazi waliiogopa. Mtei aliandika Disemba 29, 1965, akijigamba kwamba sasa aliweza kuiwakilisha Tanzania nzima, pamoja na Zanzibar. Lakini maskini roho yake, jinsi alivyopiga magoti kujipendekeza, ndivyo walivyomuona, kwa kauli ya Loynes, infradig (kitaka taka tu).

Hirst anahoji kama barua ya Mtei “inakidhi haja”. Loynes pia hakuona kama barua ya Mtei ilikuwa na thamani yoyote. Baada ya kejeli kadhaa, anapendekeza kwa Hirst kufikiria mambo gani yanahitajika kuingizwa na “utamke kwa maneno yako mwenyewe –spell out in your own words- nini ungependa kisemwe. Rasimu inaweza baadae (labda baada ya kuiona mimi) kuoneshwa wakili”.

Aibu ilioje? Serikali ya Dola inayojigamba ni huru inaandikiwa barua na wakoloni wake wa zamani, wao watie saini tu. Uingereza inaiambia Tanganyika “Kandamiza Zanzibar” na Tanganyika inasema: “Hewallah”.

Lakini Loynes na wenzake hawakuwa wapumbavu.Wakijuwa wakati wote kwamba wanayofanya si halali. Hivyo anaongeza katika barua yake ya Januari 6, 1966: “kwa maoni yangu, hili ni suala ambalo ingekuwa vyema pengine kutotumia mawakili wa E.A.C.S.O. (Jumuiya ya Ushirikiano ya Afrika Mashariki) au pengine hata wakili mwengine yeyote wa kiserikali”. Hiki ni kilele cha njama (conspiracy) dhidi ya Zanzibar, ambayo iliingia katika Muungano na Tanganyika kwa nia safi bila kutarajia visu vya mgongoni vya aina hii .

Zikafuata rasimu kwa rasimu za barua iliyokuwa inatakikana kuhalalisha kutolewa kwa Zanzibar nje ya Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (EACB). Loynes alisisitiza kwamba lugha iwe makini kiasi kwamba wao (wapanga njama hizi) wasiweze kutambulika. Katika barua yake ya Januari 17, 1966, Loynes sio tu alionesha dharau ya mwisho kwa Mtei, ambaye anamuelezea kama “Katibu Mkuu (au vyovyote anavyoitwa)”-“Principal Secretary(or whatever they call him)”-na kupendekeza  kwamba  aanze barua yake kwa maneno “Nimeagizwa na Waziri kuandika…”, lakini pia alisema maneno yafuatayo ambayo yanatupa mwangaza: “Kama mtakavyoona katika rasimu ya muda ambayo nimejaribu kuifanya, lazima tuitaje Serikali ya Zanzibar kama (Serikali ya kabla ya Muungano) na SERIKALI YA MKOA YA ZANZIBAR (msisitizo ni wetu) au maneno yoyote muwafaka (kwa maana ya Serikali ya baada ya Muungano).” Kwa tafsiri hii, Serikali ya Zanzibar ilipoteza uhai wake baada ya Muungano. Kilichopo sasa ni ’Serikali ya mkoa’.

Katibu wa EACB katika dokezo la siri la Januari 21, 1966, alionesha wasiwasi kuhusu pendekezo la kuwakwepa  mawakili  rasmi  na alisititiza kwamba Wakili  wa EACSO atakiwe ushauri wake: “angalau katika hatua ya awali”. Isitoshe alionesha wasiwasi kuhusu tamko la ‘Serikali ya mkoa’ na akasema kwa kumaliza, “Huenda  kukawa na ulazima, nafikiria, kutaja  Serikali ya Zanzibar ‘iliyopita’ na ‘ya sasa’ (au ‘ya baadae’) badala ya kutaja ‘Serikali ya mkoa’.

Ni wazi kwamba Sekretarieti ya EACB hawakufurahia yaliokuwa yanatendeka na kushirikishwa kwao katika uovu huo. Mwenyekiti aliikataa barua ya Tanzania, akisema ingawa haikuwezekana kufanya khati rasmi ya kisheria (!!) “lakini tutashukuru sana iwapo utaonesha kwamba wewe unatosha kusaini kwenye karatasi rasmi ya barua ya Tanzania (a Tanzanian headed letter) barua inayofuata rasmi iliyoambatanishwa hapa”.

Januari 31, 1966, Katibu wa Sheria wa Ofisi ya Sheria ya EACSO anasema, miongoni mwa mengineyo: “Inatilisha wasiwasi kwamba makubaliano ya namna hiyo yanaweza kufanywa bila mabadiliko makubwa katika hadhi (status) ya kisheria ya EACB yenyewe. Ni jambo la kutiliwa mashaka au sadiki ukipenda (dubious) iwapo barua ya Katibu Mkuu inatosha kujenga uwajibikaji wa kisheria.”

Wanagutusha pia kwamba “Serikali ya Zanzibar” (“The Executive for Zanzibar”) ndio maneno yanayotumika katika Katiba na sio ‘Serikali ya mkoa’.

Lakini halali au si halali, inafaa au haifai, ilishaamuliwa kuwa Zanzibar lazima ipokonywe haki zake, na, kwa kuwafunga mdomo wataalamu wa EACSO, Waziri Amir Jamal anafanywa atie saini kwenye karatasi rasmi ya Wizara ya Fedha, Machi 22, 1966.

Hata hivyo, katika barua yake inayozungumzia barua ya Jamal, Hirst anasema: “kwa sababu zisizojulikana, wameingiza maneno yanayotaja kifungu cha (xi) pia: hiki kinahusu bandari, usafiri wa anga, posta na simu, jambo ambalo ni wazi halihusu hapo…kinapaswa kutolewa.”

Katika waraka uliokuwa na kichwa cha maneno ‘Msimamo wa Bodi Kuhusiana na Zanzibar’ uliyotayarishwa kwa ajili ya kikao cha Mei 10, 1966, Hirst anaandika katika nukta ya tano kwamba: “Uanachama wa hivi sasa uliwekwa na Waziri- Secretary of State- (wa Uingereza), lakini ukaendelezwa baada ya uhuru kwa kuhamisha madaraka ya Waziri kuhusiana na Bodi kwa Serikali zinazoshiriki katika Bodi zikiamua kwa kauli moja. Kusema kweli, basi, lazima Serikali zote zinazounda Bodi hii ziidhinishe mabadiliko haya.”

Anachosema Hirst, au Katibu wa EACB, ni kwamba Tanganyika (Tanzania) haiwezi kujipa madaraka ya Zanzibar bila ya wao wenyewe (Zanzibar) kutoa kibali cha dhahir (specific approval).

Kwa maneno mengine, yote yaliyofanyika, kwa matamshi ya uongozi wa EACB, si halali.

Waraka unauliza iwapo:

a) “Bodi inadhani taarifa ya Waziri wa Fedha wa Tanzania inakubalika,” na

b) “Iko tayari kuunga mkono mabadiliko katika uanachama?”

Yaliofuata hapo ni historia na mzozo mmoja mkubwa katika Muungano, ikaingiza suala la nafasi ya Benki ya Tanzania (BoT) na nani anamdai mwenzake katika Muungano huu.

Haya tutayazungumzia wakati mwengine. Limeletwa suala hili hapa kwa lengo maalum la kuonesha kwamba Zanzibar ina haki kabisa kuyakataa mambo (items) yote yaliyo zaidi ya yale 11 katika Makubaliano ya asili ya Muungano (Articles of Union)

Zaidi ni kuthibitisha ile hoja kwamba, upande wa Bara unadhani una haki ya kuamua mambo mazito bila kushauriana na upande wa Visiwa kama vile upande huu ni “Serikali ya Mkoa.”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.