Rais Jakaya Kikwete. Ni wazi suala la Zanzibar limemuelemea na sasa anatakiwa asimame hadharani kuitambua hadhi ya Zanzibar kwenye Muungano. Ataweza?
Rais Jakaya Kikwete

“…kuanzia sasa kauli yoyote itakayotolewa na  kiongozi yoyote ndani na nje ya Bunge, itakayoashiria kuwa Zanzibar  si nchi, na kuiona haina mamlaka itahisabika kuwa ni ishara ya kuvunja Muungano,na kuigeuza Zanzibar  kuwa ni Iraq ya pili na itaonesha dhamira ya wazi ya Tanganyika kutaka  kuitawala  Zanzibar  kijeshi. Mhe. Rais, Wazanzibari wanasubiri kwa hamu kauli yako ili utudhibitishie Zanzibar  ni nchi na si venginevyo.”

Barua ya wazi ya Taasisi za Kiislamu za Zanzibar kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 20/08/2008

Kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu, Rehma na Amani zimuendee Mtume (SAW), ahli zake na maswahaba zake na kila afanyae wema.

Mhe. Rais, Tokea kusikika kauli ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mheshimiwa Mizengo Pinda ya kusema kuwa “Zanzibar si nchi” katika kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kinachoendelea Dodoma,   kuna mshituko mkubwa kwa  Wazanzibari, ambao asilimia 99 ni Waislamu na imedhihiri wazi nia mbaya ya Muungano huu  pale zilipounganishwa Zanzibar na Tanganyika.

Mhe. Rais, Kwa heshima tunakuomba ufahamu kuwa Wazanzibari wanaamini kuwa Zanzibar ni raslimali yao waliyopewa na Mwenyezi Mungu. Hivyo hawako tayari kuona raslimali hiyo inapotea na kumuona kiongozi au mtu yoyote anaibeza au kuidharau.

Mhe. Rais, Zanzibar haikuwa mali ya TANU, ASP, wala CCM au CUF, kwa hivyo maamuzi ya Zanzibar yataamuliwa na Wanzanzibari wenyewe na wala sio Dodoma.

Mhe. Rais, Matatizo ya Muungano na kasoro zilizopo ni za muda mrefu sana, na kwa bahati mbaya katika muda wote wa uhai wa Muungano, haikuonekana nia nzuri ya kuzitatua,  jambo ambalo limesababisha kero nyingi kwa Wanzanzibari na kupelekea kudhulumika. Kwa hivyo, hivi sasa ni lazima pande zote mbili za Muungano ziwepo zilizozaa Muungano huu, yaani Tanganyika na Zanzibar, ili kutafakari tena  namna ya Muungano mpya.

Aidha kwa sasa, kutokana na hali ilivyo, Wazanzibari  hawako tayari tena kuendelea na Muungano wenye sura hii, kwani unahatarisha uhai wa Zanzibar. Kwa maana hiyo umefika wakati wa kuukana Muungano, kama alivyosema Mwalimu Nyerere, kwenye makala yaliyochapishwa katika gazeti la Observer la Uingereza Aprili 20, 1968:

“Iwapo umma wa Zanzibar, bila ya ushawishi kutoka nje, na kwa sababu zao wenyewe, wataona kuwa Muungano una hasara kwa uhai wao, sitowapiga mabomu kuwalazimisha….Muungano utakuwa hauna tena sababu ya kuendelea iwapo washiriki wake wataamua kuukana.”

Mhe. Rais, Kutokana na mtiririko wa hoja zinazoendelea katika suala hili, sisi Waislamu wa Zanzibar ambao ndio wamiliki wa Zanzibar, tunaipongeza kwa dhati serikali yetu ya Zanzibar na kuunga mkono kauli ya SMZ kupitia viongozi wake wakuu. Aidha sisi Waislamu tupo pamoja na viongozi wetu, na Wazanzibari wote bila kujali itikadi ya vyama vyao katika jambo hili hadi Zanzibar huru ipatikane. Tuko tayari kuilinda kwa hali yoyote pamoja na viongozi wetu wote na wakati wowote.

Mhe. Rais, kuanzia sasa kauli yoyote itakayotolewa na  kiongozi yoyote ndani na nje ya Bunge, itakayoashiria kuwa Zanzibar  si nchi, na kuiona haina mamlaka itahisabika kuwa ni ishara ya kuvunja Muungano,na kuigeuza Zanzibar  kuwa ni Iraq ya pili na itaonesha dhamira ya wazi ya Tanganyika kutaka  kuitawala  Zanzibar  kijeshi.

Mhe. Rais, Wazanzibari wanasubiri kwa hamu kauli yako ili utudhibitishie Zanzibar  ni nchi na si venginevyo.

Mwenyezi Mungu ibariki Zanzibar na watu wake.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.