Matembezi ya amani ya tarehe 26 Mei 2012 yaliyofanywa na Jumuiya ya Uamsho na ambayo baadaye Polisi waliyatafsiri kuwa ni maandamano haramu na kuyatumilia kuwakamata viongozi kadhaa wa Jumuiya hiyo na kusababisha machafuko yaliyofuatia baadaye.
Matembezi ya amani ya tarehe 26 Mei 2012 yaliyofanywa na Jumuiya ya Uamsho na ambayo baadaye Polisi waliyatafsiri kuwa ni maandamano haramu na kuyatumilia kuwakamata viongozi kadhaa wa Jumuiya hiyo na kusababisha machafuko yaliyofuatia baadaye.

“Tukiangalia  historia ya Muungano  wa  Tanganyika na Zanzibar, kwa kwelit utagunduwa Muungano huu ulikuwa wa  watu wawili – J. K. Nyerere na Mzee  Abeid Amani  Karume  na tunaweza kuuita  Muungano wa  viongozi wa kisiasa katika Zanzibar na Tanganyika. Na kibaya zaidi, hata wanasharia wakuu hawakushirikishwa  na, kwa bahati mbaya, hata hiyo  inayoiywa HATI ASILI  ya  Muungano haijulikani na yoyote. Na hili limethibitika katika Kesi Na. 20/2005 iliyofunguliwa na Wazanzibari 10 katika Mahakama Kuu ya Zanzibar ya kudai hati asili ya Muungano dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, ambaye aliithibitishia Mahakama hiyo kwamba ofisi yake haikuwa na kukumbukumbu ya hati hiyo.”

Barua ya wazi kutoka kwa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (JUMIKI) kwa viongozi wa vyama vya siasa, Serikali na Wazanzibari wote kuhusu kauli ya Zanzibar si nchi, 14 Agosti, 2008

Kila sifa njema anastahiki M/Mungu, Rehma na amani zimuendee Mtume (SAW) na ahli zake na Masahaba na walio wema katika Uislamu.

Suala la Zanzibar ni nchi au si nchi limegonga takriban nyoyo za Wanzanzibari wote. Kwa sababu hiyo, Jumuiya ya UAMSHO imeonelea kuwa ni wakati muafaka sasa kushikamana na Wazanzibari wote ili kuinusuru Zanzibar.

Kwanza, hatuna budi kujikumbusha Zanzibar ya asili ilivyokuwa. Tunapozungumzia Zanzibar, ni muhimu tuelewe kwamba Zanzibar hiyo ya asili siyo ya leo ya visiwa viwili vya Unguja na Pemba peke yake, bali ni  ile Zanzibar ya kale ambayo ilitanda katika mwambao wote wa Afrika Mashariki na kuanzia kaskazini (Somalia) mpaka kusini (Ruvuma) vikiwemo ndani yake visiwa na tawala na miji yote ile kama Mogadishu, Merka, Barawa, Kismayuu, Pate, Lamu, Malindi, Mombasa, (Mvita), Tanga, Bagamoyo, Pangani, Unguja, Pemba, Tumbatu, Kilwa, Mafia, Sofala na sehemu nyingi nyengine za mwambao wote huo na kuingia Bara mpaka Kongo. Nchi yote hiyo ikijulikana kwa jina la Dawlat Zinjibar yaani dola ya Zanzibar (Zanzibar Empire).

Tunaweza kusema kwamba Zanzibar imeibiwa na kudhulumiwa nchi zake zote zile ambazo zilitanda Afrika Mashariki kote. Waasisi wa wizi huo na dhulma hizo ni Waingereza na Wajarumani wakiwashirikisha Wazungu wenziwao kama vile Wafaransa, Wataliana, Wadachi na wengineo. Njama hizo zinaendelea hadi hivi leo, kwa sababu shabaha yao ya mwisho ni kuung’owa Uislamu kabisa katika Afrika Mashariki. Na njia pekee katika kutekeleza hayo, ni kuvifisidi na kuvidhibiti visiwa vya Zanzibar, Unguja na Pemba, ambavyo ni shina la Uislamu katika Afrika Mashariki. Kwa kuelewa haya, ndio tutafahamu kwa nini Zanzibar ikadhibitiwa na Tanganyika na kuambiwa si nchi.

Tukiangalia  historia ya Muungano  wa  Tanganyika na Zanzibar, kwa kwelit utagunduwa Muungano huu ulikuwa wa  watu wawili – J. K. Nyerere na Mzee  Abeid Amani  Karume  na tunaweza kuuita  Muungano wa  viongozi wa kisiasa katika Zanzibar na Tanganyika. Na kibaya zaidi, hata wanasharia wakuu hawakushirikishwa  na, kwa bahati mbaya, hata hiyo  inayoiywa HATI ASILI  ya  Muungano haijulikani na yoyote. Na hili limethibitika katika Kesi Na. 20/2005 iliyofunguliwa na Wazanzibari 10 katika Mahakama Kuu ya Zanzibar ya kudai hati asili ya Muungano dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, ambaye aliithibitishia Mahakama hiyo kwamba ofisi yake haikuwa na kukumbukumbu ya hati hiyo. Hili linatia wasiwasi wa Muungano huu.

Inaonekana kila mmoja alikuwa na malengo yake na maslahi yake binafsi na sio kwa maslahi ya wananchi wao, Rais Karume yeye alikuwa anaogopa Mapinduzi  kutoka kwa makomredi  na alikuwa hana budi  kutafuta hifadhi kutoka Tanganyika, na J. K. Nyerere alikuwa na lengo la kuimeza Zanzibar  na kuifuta katika ramani ya Ulimwengu. Haya ni katika mtiririko ule ule wa kutekeleza dhamira ya kuifanya Zanzibar itawaliwe na wageni ili kupeleka siasa inayotakiwa na maaduwi ya kuuangusha Uislamu na kuinuwa Ukiristo.

Wanzanzibari wenye ujuzi na ghera ya nchi yao walilazimika kuondoka Zanzibar kwa kudhihiri ubaguzi na chuki, na badala yake wakaingizwa makazini Watanganyika na kushika nafasi muhimu serikalini ili kurahisisha ule mpango au siasa ya kuanzisha chama kimoja cha siasa katika shabaha ya kuunda serikali moja katika madhumuni ya kuimeza Zanzibar.

Kiasi cha miaka 10 iliyopita kumeanza kupaliliwa chuki za hali ya juu baina ya ndugu wawili – Waunguja na Wapemba. Yote haya ni katika mtiririko ule ule wa kuingiza fitna za chuki na kuwababaisha Wazanzibari wasijijuwe, wasijitambuwe na kupoteza lile lengo la kuidaia Zanzibar uhuru wake wa kweli.

Kwa kadri ya khatuwa hizo zinavyocheleweshwa, ndio pekecho za chini kwa chini zinavyoendelea kuimung’unya Zanzibar kidogo kidogo kama vile mchwa ‘fimbo ya Nabii Suleiman na tahamaki kuporomoka. Na hili ndilo wanalolitaka Wazungu na Wakristo.

Kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Askofu Mkuu Polycarp Pengo hazikutolewa kwa bahati mbaya, ila imedhihiri ile niya yao na paliwahi kusemwa serikali mbili kuelekea moja na kuimaliza Zanzibar.

Mwenyezi Mungu kwa utukufu wake ametudhihirishia nia mbaya ya serikali ya Tanganyika iliyojificha chini ya Muungano na kuamsha ule usingizi mzito ambao S.M.Z ilikuwa imelazwa kwa muda mrefu bila yenyewe kujitambuwa.

Zanzibar kabla ya Muungano ilikuwa na mamlaka yake hata katika maamuzi ya kujiunga na jumuiya za kimataifa. Zanzibar ilikuwa ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa tokea tarehe 16 Disemba, 1963.

Ili kutekeleza azma ya maaduwi ya kutaka kuimeza Zanzibar, Julius Nyerere aliiandama Zanzibar ili isiweze kuwa na uwezo wowote wa kiuamuzi na hata katika kujiunga na jumuiya za kimataifa. Na hayo yalidhihirika pale Zanzibar ilipotumia mamlaka yake kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislam (O.I.C) kwa maslahi ya kiuchumi, na  kwa amri yake (Nyerere) akalazimisha ijitowe.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unaonesha wazi kuwa ulikuwa ni ubabaishaji  na ndio maana ukapelekea kuwepo kasoro nyingi, kasoro ambazo zilipelekea  kutojulikana ni mambo yepi ya Muungano na yepi  si ya Muungano. Na kutokana mzongano serikali zote mbili ilibidi kukutana pamoja na kujadili ‘Kero za Muungano,’ mkutano huo uliofanyika Dar es Salam tarehe 15 Disemba, 2002. Na SMZ iliunda kamati ya wataalamu ili kuishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya njia bora ya kutatua matatizo hayo.

Hii inaonesha wazi hakukuwa na makubaliano yaliyo wazi kuhusu Muungano mwaka 1964 na kama yapo inaonesha yalikufa pamoja na waasisi wa Muungano huo. Tume   mbali mbali ziliundwa ili kutatuwa Kero za Muungano kwa mfano:-

1. Ripoti ya Jaji Nyalali
2. Kamati ya Shellukindo
3. Kamati ya Jaji Bomani
4. Kamati ya Jaji Kisanga, n.k.

Katika Muhtasari wa Ripoti ya Baraza la  Mapinduzi  juu ya Matatizo ya Muungano na Taratibu za Kuyaondowa, itakudhihirika wazi kuwa Muungano huu haukuwa na nia njema kwa Wazanzibari, kwani mapendekezo yaliyomo katika ripoti hiyo iliyotaka baadhi ya mambo kuondolewa katika Muungano, hadi sasa hayajashughulikiwa.

Serikali ya Zanzibar ilishauri mambo ambayo yaondolewe katika Muungano kama ifuatavyo:-

1. Mafuta na gesi aasilia
2. Elimu ya Juu
3. Posta
4. Simu
5. Biashara za Nje
6. Kodi ya Mapato
7. Ushuru wa Bidhaa
8. Takwimu
9. Utafiti
10. Ushirikiano wa Kimataifa
11. Leseni za Viwanda
12. Bandari
13. Usafiri wa Anga
14. Polisi
15. Usalama

Pamoja na mengi yalioandikwa katika ripoti hiyo, laiti haya yangalitekelezwa, angalau hadhi na heshima ya Zanzibar ingalikuwapo. Lakini mapendekezo haya yamebakia kwenye vitabu na Serikali ya Tanganyika chini ya kivuli cha Muungano haikuwa tayari kuyashukhulikia mapendekezo hayo ambayo ni matakwa ya Zanzibar.

Wasiwasi na maudhi makubwa waliyoyapata Wazanzibari baada ya kauli ya Waziri Mkuu ni kitendo cha Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, kuzuwia mswada huo kujadiliwa barazani, na kitendo cha jeshi la Polisi kuzuwiya maandamano. Hii ni ishara mbaya ya kuipoteza Zanzibar.

Hivi sasa ipo serikali hapa Zanzibar, lakini tujiulize nini hali ya uchumi wa Zanzibar, na nini hali ya maisha ya watu wa Zanzibar? Hivi sasa Zanzibar na watu wake wameingizwa kila upande kama samaki waliomo uzioni au tandoni – wanazunguka kwa mapana na marefu lakini mwishowe wake wanagonga kila wanapokwenda. Hii ndio hali ya Zanzibar na viongozi wake ilivyo sasa.

Njia ya pekee ya kujitowa katika hali hii ni Wazanzibari wenyewe pamoja na viongozi wao kujiunga pamoja kwa hivi sasa mpaka kung’owa uzio huo (Muungano usio na maslahi kwa Zanzibar) na baadaye waone nini la kufanya. Bila ya hivyo, hali itakuwa ile ile: kunyanga’nywa Wanzanzibari Zanzibar yetu na kuachiwa chuki baina yetu na tukigongana vichwa wenyewe kwa wenyewe. Dini yetu inatuhimiza kuwa pamoja na kuacha chuki baina yetu tupate kuinusuru nchi yetu.

Tusibabaishwe na kuambiwa tuna Serikali na tukaendeleza chuki baina ya Upemba na Uunguja. Hayo yanatiwa makusudi kwa kuwababaisha wanaohusika ili wasahau kwamba Zanzibar imo njiani kumezwa. Aibu ilioje kwa Zanzibar na Wazanzibari waliokuwa wakiongoza Afrika Mashariki katika kila hali, leo wamefikishwa hali hiyo na kufanywa kama roboti.

Ikiwa mabepari wa Uingereza na makomunisti wa Russia, ambao wote walikuwa watu wa aina mbali mbali na mataifa mbalimbali, dini zao mbalimbali, lungha zao mbali mbali na imani ya siasa zao ni tofauti, waliweza katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vya (1939-45) kushirikiana na kupigana  na mafashisti wa Ujarumani na Utaliana bega kwa bega mpaka wakawashinda na baada ya hapo  kila mmoja akaongoza njia yake na sisa yake, kuna ugumu gani au sababu gani iliyo kubwa  na nzito hata Wanzanzibari ambao idadi yao wote labda ni milioni moja, watu wa taifa moja, dini moja, nchi moja, wanaishi pamoja, wanasema lugha moja, wamezaliwa pamoja, wamecheza pamoja, wamekwenda chuoni  na skuli pamoja, na wanakutana  msikitini kutwa mara tano  pamoja, washindwe kuketi pamoja na kushauriana na kukabiliana  kwa rai na moyo mmoja jinsi ya kuinusuru Zanzibar na kujinusuru nafsi zetu katika janga hili la kumezwa?

Tuelewe nini katika hali hii? Ni wazi Watanganyika wametuweza na kututeka akili zetu na kutujaza chuki.

Wito wetu kwa viongozi wa Vyama na Serikali, Wabunge na Wawakilishi wa Zanzibar na Wazanzibari wote tushikamane pamoja, na tuwache tafauti zetu za kisiasa, na tuone Zanzibar katika wakati huu ambapo imepata majaraha makubwa, inahitajia kila la wema na huruma. Lengo la Wazanzibari kwa sasa liwe kujiwinda katika kuwania kufanyiana wema na kusafishiana nyoyo ili kuondowa chuki miongoni mwetu na kuinusuru Zanzibar kumezwa na kuangamizwa. Hii ni kwa maslahi yetu na vizazi vyetu na kurejesha utu wetu, na Zanzibar kurejea katika neema zake na utukufu wake.

Shime Wazanzibari wote waliopo Zanzibar na nje tuikombowe nchi yetu kwa nguvu na umoja wetu hadi Zanzibar iwe huru. Kufa kupona, mapema iwezekanavyo ukombozi wa Zanzibar upatikane.

WABILLAH TAUFIQ

………………………………..

AZZAN KHALID HAMDAN

NAIBU AMIR (JUMIKI)

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.