*Na Dk. Yussuf Salim

Sheikh Abeid Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar. Ni kweli aliyasalimisha mamlaka ya Zanzibar katika kiwango cha kuifanya isiwe nchi?

“Iweje leo nchi na dola linalotegemea misaada ya kutoka nje kwa asili mia 40-60%, lisiloweza kujimudu wenyewe, litake kuitawala nchi nyengine, wakati nchi na dola lenyewe likichechemea? Kibri hichi kinatoka wapi? Kwa tafsiri yangu, hakitoki kwengine ila ni kutokana na upungufu taaluma  ya mambo na kutojuwa hasa nini kiini na makusudi ya Muungano au labda kuficha siri zenyewe.”

Kwa heshma na taadhima naomba kudurusu tafsiri ya Prof. Issa Shivji kuhusu mjadala wa Zanzibar ni nchi au dola. Kwanza natanguliza shukurani zangu nyingi na za dhati kwa uchambuzi wa jumla na makhsusan wa mara kwa mara wa Prof. Shivji kuhusu tafrija za Muungano dhidi na kuhusu Zanzibar.

Mimi ni mmoja kati ya waliofaidika sana na taaluma hii, ingawa baadhi ya nyakati hushindwa kukubaliana na Profesa katika vipengele fulani kama vile katika kitabu chake cha karibuni, Pan-Africanism or Pragmatism? Lessons from Tanganyika and Zanzibar Union, juu ya jinsi Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Kwanza wa Tanganyika, alivyomlaghai na kumhadaa Mzee Abeid Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar, katika uundaji wa Muungano. Hadaa hiyo ndiyo leo inayotuletea suitafaham katika kulitafsiri suala la nguvu za serikali ya Muungano na ya Tanganyika katika Muungano na kutawaliwa au kudhibitiwa kwa serikali na nchi ya Zanzibar.

Katika kitabu chake hicho mwanana, Prof. Shivji, kwa mfano, ananukuu kwamba Abdurahman Mohammed Babu na Khamis Ameir walishuhudia kuzungumzwa na kupitishwa suala la Muungano kabla haujatiwa sahihi katika Baraza la Mapinduzi (BLM). Hii ni kauli muhimu katika kulijadili suala la jinsi Zanzibar ilivyobururwa kwenye Muungano. Sitaendelea kuzungumzia suala hili zaidi ya kwamba kuna kanda kadhaa za video ambamo Babu anakanusha kauli hiyo, vile vile kauli hiyo inakanushwa na Ameir mwenyewe. Wengine katika BLM, kwa wakati huo, vile vile hawathibitishi. Kwa ufupi, hakuna anayethibitisha tamko hilo.

Nina hakika kwamba Prof. Shivji ni gwiji la hali ya juu na kila mara uchambuzi wake huwa wa viwango vya juu, lakini hata naye mara nyengine ama huegemea sana upande mmoja tu wa sheria (katiba) au wa siasa ikitegemewa vile vile kuwa ni wapi habari zinazohusika kazipata. Lakini, kwa vile wengi wetu huwa tunategemea utaalamu wake, lingekuwa jambo la maana kama tukizidi kupiga mbizi na kuyapigia darubini kwa yale anayojaribu kutuelimisha. Kwa sababu hiyo, ndiyo nimeona kwa unyeyekevu niombe kutokubaliana na Prof. Shivji pale anapotafsiri kwamba Zanzibar ni dola na sio nchi au kumaanisha kwamba nchi inaweza kuwa dola na dola kuwa nchi.

Tumeshuhudia uliwenguni madola tofauti. Kuweko kwa madola huko India, Nigeria, Umarekani, Usovieti, Yugoslavia pamoja na kukuweko kwa Muungano kama wa UAR, Sene-Gambia, peke yake, kunaoyesha kwamba mbali ya kuwa dola linaweza kutafsirika tofauti katika hali, nyakati na sehemu tofauti, bado dola pekee haliwezi kuwa nchi.

Nchi hizi zote zimeonyesha kuwa na mifumo na tafsiri tofauti ya madola. Japokuwa yote hayo huitwa madola ndani ya nchi zinazohusika, lakini hayatambuliki kuwa nchi ndani ya madola. Kwa hivyo, dola lina mfumo wa mpito ikitegemea na hali ya siasa au serikali ya wakati fulani katika nchi inayo- au zinazohusika. India imetuonyesha mfano wa kumeguka kwa Pakistan na hatimaye Bangladesh, ingawa iliashiriwa kuwa kama ni dola moja, ya Kashmir bado hayajesha. India imebaki kama nchi na si kama dola tu ingawa imemeguka.

Tutakumbuka pia jinsi dola la Biafra lilivyotaka kujimega na kuungwa mkono na takribani Nyerere peke yake. Biafra haikuwa nchi ingawa tulilazimishwa tuamini hivyo kwa sababu na lengo la kiini macho. Hilo la Biafra lilikuwa dola sio nchi, kwani nchi ni Nigeria. Tumeona mmung’unyiko wa umoja wa nchi za Sovieti, ambazo kila moja likitambuliwa kama dola la Soviet kwa wakati huo, na sasa zimebaki kila nchi na yake kwa sababu ziliunganishwa pasi na umaumbile wa ki-nchi.

Ni kisheria na kisiasa, hasa za kimabavu, ndizo mbinu zinazotumika nyakati fulani kulazimisha nchi kuwa dola au jimbo na kwa vile si kimaumbile tunaona kwamba mfumo wa kisiasa ukibadilika nchi huishia kupata uhuru wao kwa kupitia njia za kidemokrasia. Kwa desturi za kimaumbile ni nchi ndiyo yenye dola au madola, na si kinyume cha hivyo, yaani hakuna dola zikazaa nchi.

Uhusiano baina ya nchi na dola ni sawa sawa na ule wa roho na maisha ya mtu. Bila ya roho hakuna maisha, na bila ya nchi hakuna dola. Zanzibar ni ina dola, taifa, serikali, mamlaka na utawala wake wenyewe. Yote haya hayawezekani kuwepo kama hapana nchi. Hakuwezi kuwa na dola hewa kama hakuna nchi.

Zanzibar ilibaki kuwa nchi chini ya utawala wa Kiingereza bila ya kujali kwamba kwa wakati huo huo ilikuwa ni koloni, na kwa wakati huo huo ilikuwa mama wa Jumuia ya Madola. Kuna nchi zilizobaki chini ya mamlaka ya malkia wa Uingereza kwenye Jumuia ya Madola na nyengine kujitambua kama jamhuri huru. Jumuia ya Madola haikuwa wala haitambuliki kama nchi moja, bali ni madola yanayowakilisha nchi huru au chini ya ukoloni. Nchi ikibaki katika Jumuia hiyo inabaki kama nchi na ikijitoa inabaki kama nchi bila ya kujali kuwa dola ndani ya Jumuia hiyo. Kama ulivyo Muungano wa Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar, kila moja ni nchi yenye dola lake linaloweza kuamua kuwa na uhuru wa kubaki au kutoka katika Muungano au jumuia hiyo.

Katika utangulizi wa kijitabu changu, Zanzibar Dola, Taifa na Nchi Huru, 1994, nimeandiaka yafuatayo: “Kwa mujib wa historia ya kale ya enzi zetu, kuambatana na maandishi ya Perpulus of the Erythrean Sea, Claudiius Ptolemy, Edris, Chronicles of Kilwa, n.k., Zanzibar (Menouthias Island) ikijulikana kama nchi iliyokuwa ikitambulika na kufanya biashara na Mashariki ya Kati, Mashariki ya Mbali zikiwemo Bara Hindi, Uchina na Japan, pamoja na nchi kubwa kama Marekani tokea enzi za kale.

“Katika maandishi hayo, ambayo ni kati ya maandishi ya zamani kabisa kuhusu Afrika ya Mashariki, hakukutajwa nchi au taifa lilojulikana kama Tanganyika. Hadi Aprili 28, mwaka 1885 ndio tarehe ambayo serikali ya Kijerumani ilipoamua kuzinyakua maili 60,000 za eneo la Mrima. Baada ya hapo ndipo makubaliano baina ya Mngereza na Mjerumani yakafikiwa, Mngereza akachukuwa Hegoland kama kiinua mgongo na Mjerumani  kuchukua eneo la Mrima.

“Unyakuaji wa Wazungu wa Bara la Afrika, ulitokea hususan baada ya Mfalme wa Ubelgiji kuitisha mkutano wa nchi zilizokuwa zikiongoza Ulaya, katika mwaka 1876, huko Brussels, Ubelgiji. Kama tunavyoona muda mrefu kabla ya hapo Zanzibar tayari ilijulikana kama ni nchi wakati Tanganyika kama nchi ilikuwa bado haijazaliwa.”

Inashangaza kuona leo mtu akurupuke na atamke kuwa Zanzibar si nchi wakati Zanzibar ilikuwa nchi kabla hata Tanganyika haijazaliwa. Hali hii sio tu inaonyesha kwa mtu kutoijua historia ya nchi yake mwenyewe, bali wakati huo huo inadhihirika kutoijua kabisa historia ya na umuhimu wa nchi ya Zanzibar katika Afrika ya Mashariki. Hali hii inathibitisha kibri kinachotokana na ukosefu wa kujua na kuheshimu mambo.

Wale ndugu zetu wa Tanganyika wanaosisitiza kuwa Zanzibar si nchi wamegeuka kama matarumbeta yanayopulizwa tu na kutoa sauti na pale yanapowekwa chini sio tu hayatoi sauti, bali hata kujikuna hayawezi. Uongozi wa juu wa nchi sio jambo la maskhara, kuwa na kibri peke yake hakutoshi. Kung’ang’ania kutaka kuimeza Zanzibar kumewafanya ndugu zetu kujitokeza katika ngozi zao halisi na kutupilia mbali zile ngozi zao za kondoo. Hili limewatanabahisha hata wale wengine waliokuwa hawajui nia ya Muungano kuamka na kujua kwamba njama za Muungano hazikuwa za kuimarisha udugu na umoja wa Bara la  Afrika, bali ulikuwa na njama za kikoloni za mkubwa kumtawala na kumkandamiza mdogo.

Iweje leo nchi na dola linalotegemea misaada ya kutoka nje kwa asili mia 40-60%, lisiloweza kujimudu wenyewe, litake kuitawala nchi nyengine, wakati nchi na dola lenyewe likichechemea? Kibri hichi kinatoka wapi? Kwa tafsiri yangu, hakitoki kwengine ila ni kutokana na upungufu taaluma  ya mambo na kutojuwa hasa nini kiini na makusudi ya Muungano au labda kuficha siri zenyewe.

Ndugu zetu wengine wanajiona kama wao ni watawala na Wazanzibari kwao kuwa visonoko, hawa wanakereketesha roho. Inafaa mtu akarejea kitabu cha Amrit Wilson, Uhasidi wa Marekani kwa Mapinduzi ya Zanzibar, apate undani na makusudi ya Muungano kabla mtu hajajitutumua na kujiona bora kushinda Mzazibari.

Inafaa ndugu zetu wanaong’ang’ania kuwa Zanzibar si nchi, wauchunguze kikamilifu uundaji wa Muungano kabla ya kukurupuka na kujitolea matamshi yasiyo na ukweli.

Kwa ufupi, njama za kuunda Muungano zote zina manukato ya kiharamia, tokea alif mpaka wasalaam. Ilikuwaje kitu cha kheri na baraka kifichwe na kufanywa chini kwa chini? Kwa nini wajuwe watu wachache tu walio karibu na na wanaoaminiwa na Nyerere? Kwa nini wawe ni wanasheria wa serikali ya Tanganyika tu huku wanasiasa wa Zanzibar kwa jumla wawe walikuwa hawajui kitu kuhusu makusudi ya kuunda Muungano? Kwa nini hata wanasheria wa Zanzibar wawe hawajui wala hawakushirikishwa katika maandishi, kuithamini au kuipitisha Katiba ya Muungano? Vipi Nyerere amchukue Mzee Karume peke yake, ambae hakuwa na ujuzi wa kisheria, na amfanye ndiye muasisi wa Katiba ya Muungano?

Tunajuwa kuwa, licha ya Mzee Karume hakuweza hata kupata msaada wa kisiasa wa wanasiasa wenziwe seuze wanasheria. Mzee Karume alitishwa na kudanganywa na kwa vile alikuwa anamuamini sana Nyerere kama kipofu kwa imani yake njema, hakuona wala kutarajia mitego aliyowekewa yeye na Wazanzibari kwa jumla. Alipokuja kutanabahi, mambo yalikwishafika kooni, hakutokeki hakuingiliki, na ndio maana siku zake za mwisho Mzee Karume akaanza kufanya mikiki ya kutaka kujipapatua kujitoa katika Mungano.

Mengi sana yameandikwa kuhusu uharamia wa Katiba ya Muungano na lengo la azma ya kuyanyakuwa madaraka ya Zanzibar. Ni bahati njema kwamba sasa Wazanzibari, karibu wote, wameanza kuyatamka hadharani yale waliyokuwa siku zote wakiyashuku na kuyasemea vibuyuni tu.

Kuna mengi ambayo Mzee Karume aliyashitukia kuhusu uundaji na lengo la Muungano, ambayo hayana kasoro ya zaidi ya kutaka kuimeza Zanzibar. Itakumbukwa jinsi Mzee Karume alivyokasirishwa kwa kupitia nje ya Katiba ya Muungano, na bila ya yeye kama Makamo wa Rais wa Muungano kujulishwa, kwa kuanzishwa kwa cheo cha kuweko Waziri Mkuu ambae kwa wakati huo huo -waziri Mkuu huyo alikuwa atoke Tanganyika.

Kutojulishwa, kutoshauriwa na kupuuzwa kwa Mzee Karume kama Makamo wa Rais na muasisi wa Muungano kulimkasirisha sana na kuzidi kumtambulisha azma halisi za Muungano. Hapo Mzee Karume alijuta kutolisikiliza BLM na mawaidha ya wanasheria walioweka maslahi ya Zanzibar mbele. Alijuta kutolishirikisha BLM katika kulizungumza, kulichambua na kuli- au kutolipitisha suala la Katiba ya Muungano katika Baraza. Alijuta kwa nini asiwashirikishe Wazanzibari katika uamuzi wa kujitia au kujitoa katika Muungano.

Hasira zake hatimae zilimpelekea kutaka kufanya mengi, mengine ya siri na mengine ya dhahiri (soma Zanzibar Dola, Taifa na Nchi Huru). Katika jambo moja wapo  la dhahiri Mzee Karume alitaka kufanya ni kuishitaki Serikali ya Muungano (yaani Nyerere) kwa kwenda  kinyume na Katiba ya Muungano kwa kuanzisha cheo cha Waziri Mkuu wa Serikali kinyume/dhidi hata na hiyo Katiba ya mabugumunya, isiyopitishwa si na  serikali ya au watu wa Zanzibar. Hayo kwa bahati mbaya Mzee Karume, hakuwahi kuyatekeleza. Yaliyomfika tunayajua.

Hicho ni kipengele kimoja tu muhimu kinachodhihirisha upotofu na upungufu wa heshima ya Zanzibar katika Katiba ya Muungano. Mengi ya kificho na ya jua kali yamepenyezwa katika Katiba hiyo kwa namna hii au nyengine ndani au nje ya Katiba ya Muungano katika njama na makusudi ya kuipora Zanzibar madaraka na u-nchi wake.

Mapambano yanaendelea….

*Dk. Yussuf Salim ni Mzanzibari anayeishi Denmark na mwandishi wa kitabu ‘Zanzibar: Dola, Taifa na Nchi Huru.’

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.