Na George Maziku

"Zanzibar ni nchi"
Ali Juma Shamhuna, Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni wa Zanzibar:

“Viongozi wa sasa wa serikali na CCM visiwani Zanzibar wako imara na hawawezi kutishwa wala kudhibitiwa. Na hili linathibitishwa na kauli ya Shamhuna kwamba: “Nani wa kuwadhibiti wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika suala hili? Enzi za vitisho na kutaka kudhibitiana zimepitwa na wakati…Nyakati hizi ni za uwazi na ukweli na zenye kufuata misingi ya utawala bora na demokrasia, hazipaswi kuwekewa vikwazo vya vitisho.” Misimamo thabiti na ya wazi ya wajumbe wa Baraza la wawakilishi ambayo wameionyesha kuhusu suala hili wakati wa mjadala wa bajeti ya SMZ unaoendelea sasa visiwani humo ni uthibitisho mwingine wa hali halisi ya mambo. Kuna wengine walifikia hata kula kiapo barazani kuwa wapo tayari kufa kwa kutetea hadhi ya Zanzibar kuwa ni nchi na taifa huru sambamba na Tanzania!”

MJADALA kuhusu hoja ya hadhi ya Zanzibar kama ni nchi au la, unazidi kupamba moto, na ni dhahiri kuwa hoja hii imewagawa Watanzania katika pande mbili. Wapo wanaoitaja Zanzibar kama nchi na dola kamili, na wapo wanaosema Zanzibar si nchi bali ni sehemu ya Tanzania, lakini bila kutuambia ni mkoa au wilaya ya Tanzania.

Hoja ya Zanzibar ni nchi au la ilianzia katika Bunge baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda, mara mbili kwa nyakati tofauti kusimama na kusisitiza kuwa Zanzibar si nchi bali ni sehemu ya Tanzania, majibu yaliyoibua mjadala na mvutano mkali kwa Watanzania wa kada mbalimbali.

Viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kimsingi wanaunga mkono matamshi ya Pinda huku wenzao wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanampinga. Kupitia kwa Naibu Waziri Kiongozi Ali Juma Shamhuna, SMZ imesema: “Zanzibar itaendelea kuwa nchi hadi mwisho wa dunia…Na suala hili tuachiwe Wazanzibari wenyewe tulitolee maamuzi yetu, na huo ndio ukweli.”
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande wao wamegawanyika, ambapo baadhi hususan wale wanaotoka Zanzibar wanampinga Pinda huku baadhi yao hususan wanaotoka Tanganyika wakimuunga mkono.

Kwa upande wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wote bila kujali tofauti zao za kiitikadi, wanampinga Pinda. Kwa wananchi, karibu Wazanzibari wote bila kujali tofauti zao za siasa za vyama wanampinga vikali Pinda, huku wenzao wa Tanganyika wakiwa wamegawanyika, baadhi wakimuunga mkono na wengine kumpinga.

Kwa upande wa vyama vya siasa, kama kawaida yake chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa mpiga debe wake mwenye kiherehere, Tambwe Hiza kilitoa tamko la kuunga mkono matamshi ya Pinda, huku vyama vya upinzani hususan Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kina ushawishi mkubwa visiwani Zanzibar, vikimpinga waziri mkuu.

Kwa ufupi hali ya kisiasa juu ya hoja hii ni mbaya sana, pengine kuliko ilivyowahi kutokea wakati wowote kabla. Nakubaliana na maoni ya mwanasiasa maarufu visiwani Zanzibar, Mohammed Raza kwamba upepo wa suala hili safari hii ni tofauti kabisa na mtafaruku wa siasa za Zanzibar wa mwaka 1984 uliobatizwa jina la ‘kuchafuka kwa hali ya siasa’, ambao ulisuluhishwa kibabe kwa kulazimishwa kujiuzulu nyadhifa zote kwa aliyekuwa rais wa visiwa hivyo, Aboud Jumbe.

Hii inatokana na ukweli kwamba mazingira ya kisiasa nchini wakati huu ni tofauti mno na ya miaka ya 1970 na 1980. Ubabe katika kushughulikia migogoro ya kisiasa uliotumiwa na aliyekuwa rais wa Tanzania na mwenyekiti wa CCM wakati huo, Baba wa Taifa hayati Julius K. Nyerere, leo hii hauwezi kufanikiwa.

Viongozi wa sasa wa serikali na CCM visiwani Zanzibar wako imara na hawawezi kutishwa wala kudhibitiwa. Na hili linathibitishwa na kauli ya Shamhuna kwamba: “Nani wa kuwadhibiti wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika suala hili? Enzi za vitisho na kutaka kudhibitiana zimepitwa na wakati…Nyakati hizi ni za uwazi na ukweli na zenye kufuata misingi ya utawala bora na demokrasia, hazipaswi kuwekewa vikwazo vya vitisho.”

Misimamo thabiti na ya wazi ya wajumbe wa Baraza la wawakilishi ambayo wameionyesha kuhusu suala hili wakati wa mjadala wa bajeti ya SMZ unaoendelea sasa visiwani humo ni uthibitisho mwingine wa hali halisi ya mambo. Kuna wengine walifikia hata kula kiapo barazani kuwa wapo tayari kufa kwa kutetea hadhi ya Zanzibar kuwa ni nchi na taifa huru sambamba na Tanzania!

Pamoja na ukweli kwamba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Aman Abeid Karume hajatoa kauli bayana kuelezea msimamo wake binafsi na wa serikali yake, lakini nashawishika kuamini kuwa kauli ya Shamhuna ndiyo msimamo wa Karume binafsi na SMZ kwa ujumla. Mtu anayedhani Shamhuna aliropoka na alikuwa akiwasilisha tamaa zake binafsi, atakuwa anajipotosha mwenyewe.

Hili linathibitishwa na kauli ya mwanasheria mkuu wa SMZ aliyoitoa barazani kabla ya kauli ya Shamhuna, kwamba Zanzibar ni nchi. Bila shaka mwanasheria mkuu hakutoa kauli hiyo kwa matamanio yake, bali alikuwa akiwasilisha msimamo wa mkuu wake wa kazi, Rais Karume, na uongozi mzima wa SMZ na CCM Zanzibar kwa ujumla.

Na katika kuthibitisha zaidi msimamo wa Rais Karume juu ya hoja hii ni kwamba, kwa mtu yeyote anayefuatilia siasa za Zanzibar hususan kuhusu Muungano na hadhi ya Zanzibar ndani ya Muungano, atakubaliana nami kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Karume, kumekuwepo mageuzi mengi yanayoimarisha hadhi ya Zanzibar kama nchi na taifa huru.

Ni katika kipindi hiki ambapo tumeshuhudia Zanzibar ikizindua rasmi bendera yake kama nchi na taifa huru, ambayo inapepea katika ofisi zote za umma visiwani humo, katika majengo ya Baraza la Wawakilishi na kwenye ofisi zinazotumiwa na SMZ nje ya visiwa hivyo.

Pia ni wakati huu ambapo tumeshuhudia nguvu kubwa ya SMZ ikielekezwa katika kuimarisha vikosi vya SMZ na kuvifanya vibadilike kuwa majeshi kamili ya ulinzi. Hayo yote hayafanyiki kwa bahati mbaya, bali ni mpango maalum wa kuimarisha mamlaka ya Zanzibar kama nchi na taifa huru lenye dola yake.

Kwa hiyo, bila kujali Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar zinasema nini, viongozi na wananchi wa Zanzibar kwa ujumla wanaamini na kusimamia imani yao kwamba Zanzibar ni nchi na taifa huru. Na katika hili hakuna wa kuwatisha wala kuwadhibiti. Anayetaka kupima nguvu za upepo ajaribu kuuzuia aone atakavyosombwa na kutupwa mbali kama karatasi.

Halafu mimi nawashangaa sana hawa watu wenye kiherehere cha kusimama mbele huku mabega yakiwa juu na kunadi eti Zanzibar si nchi! Hivi lugha hii maana yake nini? Watu hawa wanataka kutueleza nini hasa? Kama Zanzibar si nchi, mbona hawatuambii hadhi yake? Ni mkoa au wilaya? Mbona hawatuambii kuhusu hadhi ya rais wa visiwa hivyo? Ni Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya?

Mimi nadhani mtu anayesema kuwa Zanzibar si nchi anajidanganya mwenyewe, wala kweli haimo ndani yake. Anajua anasema uongo na anadhani Watanzania wote ni wajinga kiasi cha kukubaliana na uongo wake. Mtu wa aina hii anadhani Watanzania wa leo ni wale wale wa miaka ya 1961 na 1980, ambao wanakubaliana na kila hoja na hawathubutu kuhoji hata kama watagundua kuwa msemaji anadanganya.

Bila kujali Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo iko juu ya katiba zote nchini, inasema nini, Zanzibar ni nchi na taifa huru lenye dola kamili. Sisemi haya kwa matamanio binafsi na sijarukwa na akili. Nayasema haya kwa kuzingatia ukweli halisi wa mambo yalivyo na ninayo mifano kadhaa hai kuthibitisha kauli yangu.

Zanzibar ni nchi kwa sababu ina bendera yake ya taifa, ina wimbo wake wa taifa, ina mhuri wake wa taifa na ina nembo yake ya taifa. Pia Zanzibar ina majeshi yake (Vikosi vya Ulinzi vya SMZ) ambayo yapo chini ya rais wa visiwa hivyo.
Aidha, Zanzibar ni nchi kwa sababu ina mipaka yake inayotambulika na kuheshimika kimataifa.

Uthibitisho wa hili ni kwamba, kila kiongozi wa nje anapoingia hapa nchini (Tanganyika-Dar es Salaam) hupokelewa na Rais wa Tanzania (Tanganyika) na kupigiwa mizinga 21. Lakini kiongozi huyo huyo akiingia ndani ya mipaka ya Zanzibar hupokelewa na rais wa visiwa hivyo kama mkuu wa nchi na hupewa heshima ya kupigiwa mizinga 21 kama utambulisho kuwa ameingia nchi nyingine.

Hata wakati rais wa Zanzibar anapofanya ziara za kikazi nchi za nje, hupokelewa huko na wakuu au viongozi wengine waandamizi wa nchi anazotembelea, na hupewa heshima zote za mkuu wa nchi. Hutandikiwa zulia jekundu na kupewa heshima ya kukagua gwaride la kijeshi kama heshima kwake binafsi na nchi yake.

Rais wa Zanzibar huteua ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wa kuongoza Brigedi ya jeshi hilo ya Zanzibar na sharti awe Mzanzibari, na pia huteua ofisa wa Jeshi la Polisi ili kuwa kamishina wa polisi Zanzibar, na sharti awe Mzanzibari. Kwa kufanya kazi hii, anatofautiana vipi na rais wa Tanzania anyewateua mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama (CDF) na mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) akiwa amiri jeshi mkuu? Kwa kuzingatia hilo, tutakuwa tunakosea tukisema kuwa rais wa Zanzibar naye ni amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama visiwani Zanzibar?

Aidha, mtu akitaka kujua juu ya hadhi ya rais wa Zanzibar, basi afuatilie mpangilio wa itifaki kwa viongozi wakati wa sherehe za kumbukumbu ya mapinduzi Zanzibar. Wakati wa sherehe hizo rais wa Zanzibar huwa wa mwisho kuingia na wa kwanza kutoka eneo la tukio ambako pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huwepo. Na zaidi wakati wa sherehe hizo rais wa Zanzibar hukagua gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama akishuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano kumpa rais wa Tanzania mamlaka ya kuigawa Tanzania katika mikoa na wilaya na kuteua wakuu wa mikoa na wilaya, lakini hajawahi kutekeleza mamlaka hayo kwa upande wa Zanzibar, na mgawanyo wa mikoa na wilaya uliopo sasa na wakuu wake wamewekwa na waliokuwa marais wa Zanzibar wakati huo.

Kwa hiyo, Mtanzania yeyote anayefuatilia na kufanya uchambuzi makini wa siasa za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, hususan kuhusu Muungano, atakubaliana nami kuwa Zanzibar ni nchi na dola kamili. Na kimsingi hakuna wadhifa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu huyo anayedaiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano hana mamlaka hata chembe juu ya Zanzibar na wala hawezi kumwajibisha kwa namna yoyote rais wa Zanzibar kama atakataa kushirikiana naye au kumdharau.

Katika hali halisi ya mambo, kuna rais wa Tanganyika (rais wa Tanzania) na rais wa Zanzibar, ambao kwa kweli wana madaraka sawa, hakuna bosi wa mwenzake. Na kwa msingi huo ninashawishika kusema kuwa kinachodaiwa kuwa Muungano kati ya nchi hizi mbili hakipo, ila kuna mazingaombwe au kiini macho tu. Kilichopo hapa ni urafiki tu wa viongozi wanasiasa wa CCM. Siku yoyote rais wa Zanzibar anaweza kuamka na kutangaza kuitoa nchi yake katika Muungano na tusiwe na ubavu wa kumwambia wee, acha.

4 thoughts on “Kama Zanzibar si nchi, Karume Mkuu wa Mkoa?”

  1. aa, natumai kwa haya sina la kusema kwani huu ni ukweli mtupu ila kwa wenye itkadi za siasa atasema hii sio kweli ila kwa mtazamo wa kiukweli hii ndo ilivyo.hata rais wa jamhuri akienda zanzibar basi hana malaka kwani rais wa zanzibar ndo mas’uul wa nchi hiyo.HUU NDO UKWELI HALISI.HONGERA KWA KUSEMA UKWELI

  2. asalam aleikum,haya mambo ya zanzibar naona kila tukirabu kujinasua ndivyo wenzetu wa ccm wanavyozidi kukaza kamba kwa nini kwa sababu wanaangalia zaidi maslahi yao binafsi.angalia mtu kama mohammed seif tulitegemea aitetee zanzibar lakini wapi kwa sababu anajua maslahi yake yako zaidi bara kuliko zanzibar.siyeye tu angalia salim ahmeid salim wakati akiwa waziri mkuu alisimamia kwa kila hali zanzibar isiwe na bendera yake wakati akijua fika hiyo bendera isingesaidia chochote lakini alfanya hivyo kujipendekeza kwa nyerere kwa kujua kwamba maslahi yake yako bara,kwa hivyo hizo kelele tunazopiga kila siku ni buretu wakati hao viongozi tunaowachagua wa ccm, ni wanafiki .lakini nahofia kizazi kijacho hakitakubali na hapo matatizo yanayotokea katika sudan huko dafur sina wasiwasi yatatokea hapa kwetu

  3. ndugu yangu khamis hayo matatizo yaliotokea sudan mimi nataka kama sasa hivi yatokee lakini ni bora tukose sote tushachoka, kwa nini wafaidike wachache na wengi tubaki tukiteseka? tumechoka kudhulumiwa, tumechoka kuuliwa, tumechoka kusulubiwa, wazanzibari tuondowe mambo ya itikadi na tuungane kuikomboa nchi yetu.haya maneno sitaki hata kuyasikia sijui tanzania, sijui muungano tumechoka tena tumechoka, tuikomboe nchi yetu kwa manufaa yetu na vizazi vyetu

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.