Na Ally Saleh
Na Ally Saleh

Zilikuwa zimebaki saa 48 tu kabla Zanzibar kuingia katika historia. Historia ambayo tumeiona katika nchi nyingi ambazo zilikuwa zikipita katika mawimbi ya Muungano au umoja au muundo wa nchi zao. Siku ya Agosti 4, 2008 ingeingia katika historia ya Zanzibar, lakini hilo halikutokea na ndio mantiki na hoja ya kuandika makala hii. Pengine ingefanana kama Disemba 10, 1963 au Janauri 12, 1964 au hata April 26, 1964.

Kwamba fursa imepotea na watakuwa ni Wazanzibari wenyewe wa kujilaumu kuwa ilifikia saa 48 tu kuweka sawa khatma yao lakini wakarudi nyuma. Wamerudi nyuma kama mbwa aliyekutana na chatu, mikia yao wameikunja, kama naweza kutumia msemo huo.

Kwamba ilifika hatua kuwa lazima uamuzi ufanywe na vyombo vya kutunga sheria vikafanya uamuzi kama huo ambao umeweza ama kujinasua kutoka mfumo wa Muungano uliokuwa umewachosha wananchi au ambao haukuwa ukienda kabisa na matakwa ya wananchi.

Ilikuwa ni fikra ya wengi kuwa kusema mtu mmoja mmoja, au muwakilishi mmoja mmoja au mwanasiasa mmoja mmoja au chama kimoja hakungekuwa na athari itakiwayo katika jambo hili….ila sauti ya Baraza la Wawakilishi ilihitajika.

Kulikuwa na sauti moja katika hili. Vyama vya CUF na CCM kupitia wajumbe wake wa Baraza la Wawakilishi waliafikiana kabisa kwamba hoja binafsi kuhusu suala la Zanzibar ni nchi au si nchi. Ilibakia saa 48 tu kabla ya umoja wa Wazanzibari kudhihirika kupitia wajumbe wote wa CUF na CCM katika Baraza la Wawakilishi.

Bendera ya Zanzibar, moja wa alama zinazoonesha kwamba Zanzibar ni nchi kama ilivyopitishwa na Baraza la Wawakilishi. Ni bahati mbaya kwamba Spika Kificho aliling'oa meno Baraza hilo hilo mara hii likashindwa kujadili hoja binafsi na kutoa azimio la Zanzibar ni nchi.
Bendera ya Zanzibar, mojawapo ya alama zinazoonesha unchi wa Zanzibar ni nchi, kama ilivyopitishwa na Baraza la Wawakilishi. Ni bahati mbaya kwamba Spika Pandu Kificho 'aliling'oa meno' Baraza hilo hilo mara hii hata likashindwa kujadili hoja binafsi na kutoa azimio la Zanzibar ni nchi, azimio ambalo lingemaanisha mengi kwa khatima ya Zanzibar na watu wake.

Hilo la kukubaliana lilikuwa ni la umuhimu mkubwa katika mambo machache vyama hivi vyenye upinzani mkali kukubali kufanya kitu kwa pamoja kwa sababu ya kuumizwa na Uzanzibari wao na kupokwa hadhi ya nchi yao.

Makubaliano ya kuwa na hoja moja yalitokana na kwamba kwa wiki tatu kulikuwa na mvutano katika Baraza la Wawakilishi baada ya wajumbe wawili kutaka kutoa hoja ya kupinga matamshi ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda, aliyoitoa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Kwa upande wa CUF alikuwa ni kiranja wao Abubakar Khamis Bakari ambaye aliwasilisha rasmi nia yake ya kutoa hoja binafsi lakini mara taarifa zikazuka kuwa mwakilishi wa CCM, Salmin Awadh nae anataka kufanya hivyo hivyo.

Spika Pandu Ameir Kificho aliikataa hoja ya Khamis kwa sababu mbili. Kwanza ni kuwa kulikuwa na hoja nyengine inayofanana na hiyo kutoka kwa Awadh lakini pili ni kuwa alikuwa na wasi wasi na hilo kwa vile tayari kulikuwa na maelekezo ya Waziri Mkuu Pinda kuwa kazi hiyo waachiwe wanasheria wa Serikali ya Zanzibar na wale wa Serikali ya Muungano.

Awali wengi tulifikiri ilikuwa ni mbinu ya Spika Kificho kuipiga na chini CUF. Kwa maana ya kuwazuia wasipate fursa ya kisiasa na kuitumilia kuwa wao ni watetezi zaidi wa Zanzibar kuliko CCM.

Na baada ya hapo mambo yakabadilika wakati Spika Kificho alipojaribu kupiga marufuku suala hilo lisijadiliwe tena katika Baraza la Wawakilishi lakini wajumbe kwa pamoja wale wa CCM na CUF wakapinga maagizo yake.

Kila aliyenyanyuka wa CUF na CCM alizungumzia suala hilo hilo kwa kutafuta tu njia ya kulipenyeza iwe ni kwenye bajeti ya Wizara ya Afya, Kilimo, Utawala Bora, Maji na mambo yakawa yako kileleni wakati wa bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo.

Kinara wa Wizara huyo, Mwakilishi wa Jimbo la Donge, Ali Juma Shamuhuna akaripuka. Alisema suala lazima lijadiliwe na kumpinga Waziri Mkuu Pinda na zaidi akasema wakati wa kutishana umepita. Zanzibar haitatishwa.

Sisi wachambuzi wa siasa tukaona sauti ya Shamhuna si yake peke yake bali alikuwa anawasilisha na kuwakilisha mtizamo wa Baraza la Mawaziri la Zanzibar ambapo yeye ni mjumbe wake na mtu mwenye wadhifa wa Naibu Waziri Kiongozi.

Hakuna aliyemruka Shamuhuna kwa wiki nzima. Si Spika, si mnadhimu wa CCM ndani ya Baraza Haji Omar Kheir, si Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha na wala si Rais wa Zanzibar Amani Karume. Wengi tukaamini msumari umeingia.

Hapo Julai 31 taarifa zinasema kuwa kulifanyika kikao cha Uongozi cha Baraza la Wawakilishi na kuhudhuriwa na wajumbe wa vyama vyote wanaostahiki kuhudhuria kikao hicho na ajenda kubwa ikawa ni kuhusu hoja binafsi.

Baada ya majadiliano ilikubaliwa kuwa kikao cha Baraza la Wawakilishi kiahirishwe rasmi Jumanne ya Agosti 5 baada ya kumaliza kazi yake ya kupitisha Bajeti ya Serikali ya Zanzibar ya 2008/2009 na wajumbe wa CUF kuonyesha kuiunga mkono.

Na kwa hivyo ikawa ni makubaliano ya Kamati ya Uongozi kuwa ichaguliwe Kamati ya muda itayokuwa na wajumbe wa CCM na CUF watumie siku za mwisho wa wiki Agosti 2 na 3 ili kuandaa hoja hiyo na iweze kuwasilishwa Barazani Jumatatu Agosti 4.

Mchana mchana wa Ijumaa Agosti 1, zikaanza kupatikana fununu kuwa Waziri Kiongozi Nadodha ataahirisha kikao jioni hiyo na sio siku ya Jumanne ya Agosti 5 baada ya kuwasilishwa hoja binafsi Jumatatu ya Agosti 4.

Na kweli jioni ya Agsoti 1 jioni Waziri Kiongozi Nadodha alifika kuahirisha kikao lakini haikuwa kabla ya Spika Kificho kuchukua nafasi yake kuelezea kuwa hoja binafsi haitakuwepo tena. Na huo pia ukawa ndio msimamo wa Waziri Kiongozi Nahodha, ambapo wote wawili walikuwapo katika Kikao cha Julai 31.

CUF walipoona msimamo huo wa Serikali wakaamua kutoka nje ya ukumbi wakati Waziri Kiongozi Nahodha akihutubia kwa nia ya kuahirisha kikao hadi Oktoba 5. Na alisema ni kikao hicho ndipo ambapo patawasilishwa ripoti ya suala la Zanzibar nchi si nchi baada ya wanasheria kukutana.

Kwa fikra zangu, suala la Zanzibar nchi si nchi si la kisheria tu lakini pia lina mzizi mrefu katika siasa na kwa hivyo ni la kisiasa. Tena naamini kuwa ni la kisiasa zaidi hata kuwa ni la kisheria.

Kwa sababu Katiba yoyote hutengenezwa kwa kufuata matakwa ya kisiasa. Na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni wanasiasa na ambao wanawakilisha matakwa ya wananchi wao ambao wamewachagua kuwa wawakilishi wao kisiasa na baada pia kisheria.

Fikra za kuahirisha suala hilo hadi Oktoba naamini hazikupata ushauri mzuri. Si ushauri mzuri kwa sababu ningependa nimuulize Waziri Kiongozi Nahodha ni jambo gani zuri lenye maslahi ya Zanzibar ambalo limepata ufumbuzi wa haraka na bila msuguano kutoka Serikali ya Muungano?

La pili, ni vipi Waziri Kiongozi anatarajia Zanzibar iingie katika mjadala huu bila ya kupata hoja na sauti ya pamoja ya wawakilishi wa wananchi wakati Serikali ya Muungano tayari imeshaweka msimamo wake kuwa Zanzibar si nchi?

Waziri Kiongozi Nahodha na chama chake cha CCM wanataka kufanya jambo hili ni la Kiserikali na la kitawala kuliko kuwa ni la nchi na la wananchi kwa ujumla wao?

Wakati akilipiga dana dana hili, jee Waziri Kiongozi Nahodha hajui kuwa kunaweza kuwa na athari kubwa ya kisiasa na kiutawala kwa Serikali ambayo yeye ni mtendaji wake?

Naamini hajasahau kuwa mbali ya hili ya Zanzibar si nchi, kuna hoja nyengine nyingi ambazo zinaning’inia juu ya kichwa chake kama vile Muwafaka, madai ya kuundwa kwa Serikali ya Pemba na madai mengine kemkem juu ya haki za wananchi.

CCM na Serikali ya Zanzibar na yeye Nahodha ajue kuwa wametoa jukwaa kwa Wapinzani kutumia fursa hii. Ni jukwaa ambalo chama chochote kile makini hakitasita kulitumia.

Ni miezi mitatu mema kabisa, ambayo kama CUF wataitumia vyema, wataitia CCM jeraha kubwa la kisiasa ambalo litachukua muda kulitibu na kama litatabika kabisa maana Waswahili walisema kuwa msema mwanzo ndio anaesema.

CCM na Serikali ya Zanzibar hawakupaswa kuliahirisha hili maana kama wanajua hali ilivyo huku nje. Wana-CCM wanaoipenda Zanzibar wanaumia kama wana-CUF wanaoipenda Zanzibar.

Kwa muda tokea kuzuka hili, wananchi wamekuwa wakitaka Rais Karume aonyeshe uongozi na fursa kama hiyo haijatokea. Na sasa hili la Waziri Kiongozi kuipoteza fursa kama hiyo ambapo Baraza la Wawakilishi lingechukua uongozi katika suala hili, litakuwa na athari kubwa sana kisiasa.

Nionavyo mimi, tukio hili ni kama kitanzi kikubwa kwa CCM Zanzibar na SMZ. Ni kitanzi ambacho kamba yake ikisaki ni vigumu mno kutolewa shingoni. Maana kitanzi kikiwa ni cha wananchi tena katika suala la nchi yao, ambayo wanataka kunyang’anywa, kinakuwa kitanzi kikali sana.

Kwa mara nyingine tena, CCM na SMZ wanajilimbikizia mambo yenye athari kisiasa bila ya kuwa na ulazima wa kufanya hivyo kwa sababu tu ya kuogopa kushirikiana na wapinzani, CUF, ilhali wao kama wao hawawezi kusimamia suala la maslahi ya Zanzibar kwa ukamilifu wake hasa inapoingia Serikali ya Muungano na Chama cha Mapinduzi.

Letu ni kusema. Na tumesema na tutaendelea kusema kuwa maslahi na uhai wa Zanzibar unatishiwa na kinachohitajika au kilichohitajika ni kuwa na nguvu za pamoja za Wazanzibari.

Kitakachofanywa chochote dhidi ya hilo ni kujitia kitanzi, na kwa sasa CCM na SMZ inacho shingoni mwake na khatma ya kitanzi hiki itajulikana siasa itapokuwa tayari kutoa hukumu yake. La sivyo, CCM tuione ijivue kitanzi hiki, mapema ikiwezekana. La sivyo, litawakuta lisilowaridhi.

* Makala ya Ally Saleh katika gazeti la Mwananchi, Agosti 6, 2008

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.