Na Ali Nabwa
Na Ali Nabwa

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni mrithi halali wa Serikali ya Jamhuri ya Zanzibar, ambayo mwaka 1964 ilitia saini Mkataba, yaani, Makubaliano ya Muungano. Mshiriki mwengine wa mkataba huu ni Serikali ya Tanganyika. Kwa maelezo ya Makubaliano hayo, Jamhuri ya shirikisho yenye mamlaka kamili (Sovereign Federal Republic) ya mfumo wa Serikali tatu (triangular) ilianzishwa….”

Katiba ya muda ya Tanzania haikupitishwa na Bunge. Isitoshe, baina ya 1965 na 1976 imerekebishwa kwa njia zisizo halali mara kadhaa, yakiongezwa mambo ya muungano kutoka 11 hadi 16. Baada kutungwa katiba ya kudumu mwaka 1977, mambo ya Muungano yaliongezeka kufikia 23, lengo ya yote ikiwa ni kubana uhuru wa Zanzibar. Si ajabu basi kwamba Rais Salmin Amour, katika mahojiano na gazeti moja la Kenya, alisema Zanzibar inatambua mambo 11 tu kama ndio ya Muungano.

Hata Profesa Issa Shivji wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema katika  maandishi yake ya (Constitution of United Republic (Katiba ya Jamhuri ya Muungano) kwamba “ikiwa marekebisho ya Mambo ya Muungano yatachukuliwa kama ni halali, uhuru wa Zanzibar utakuwa bufuru tupu.”

Lakini pigo kabisa kwa Makubaliano ya Muungano lilikuja mwaka 1994. Kifungu cha III (b) cha Mkataba (Makubaliano) kinasema: “….ofisi za Makamu wa Rais wawili, ambapo mmoja wao (akiwa ni mtu ambaye kwa kawaida anaishi Zainzibar) atakuwa mkuu wa utawala uliotajwa kabla katika na kwa Zanzibar, na ndiye atakayekuwa msaidizi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika utekelezaji wa shughuli za uwongozi kuhusiana na Zanzibar.”

Hii ilimhakikishia Rais wa Zanzibar nafasi ya kudumu katika Serikali ya Muungano kama mmoja wa Makamu wa Rais wawili. Sasa Rais wa Zanzibar anachukuliwa kama waziri wa kawaida tu, na huu ni uvunjaji mkubwa wa Makubaliano ya Muungano.

Kwa kweli hicho kinachoitwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ina ubovu mwingi ikiwa ni pamoja na:

  • Nia ya kukwepa kwa makusudi kuonyesha kuwepo kwa ‘Tanganyika’ kama dola huru
  • Kuingiza kifungu kinachosema kwamba kutakua na Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano. Haya ni makosa kisheria, kwa vile Tanganyika na Zanzibar kila mmoja na mfumo wake wa sheria ambao si jambo la Muungano, lakini imefanywa kusudi ili Mwanasheria Mkuu wa Tanganyika awe na sauti juu ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kwa mambo yote ya Muungano. Na hivyo ndivyo ilivyo leo.
  • Hakuna pahala yanatajwa matumizi ya Serikali ya Tanganyika au angalau matumizi kwa mambo yasiyo ya Muungano kuhusiana na ‘Tanzania Bara’. Badala yake, Katiba imeingiza vifungu 133 mpaka 144 ambavyo vinahusika na Mambo ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano na ambavyo vinaashiria  kuwepo kwa Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano.

Kwa ufupi, kwa hivyo, Katiba ya 1977 ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania imeelezea wazi kuwapo kwa Serikali ya Zanzibar. Pia kuna Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambayo ina madaraka ya kushughulikia mambo yote ndani ya kwa Jamhuri ya Muungano na kwamba yote mengine ndani ya na kwa Tanzania Bara.

Dhamana hizi mbili kwa Serikali ya Muungano zimeleta mtafaruku na suitafaham kubwa. Hii ni pamoja na mgawanyo wa mapato, Mahkama ya Katiba, Mahkama ya Rufaa kwa Tanzania, Orodha ya Mambo ya Muungano na Mwenendo wa Mabaraza ya Sheria.

Kuna mfuko mkuu kwa Jamhuri ya Muungano, kwa mfano, ambao unaingiza mapato yote au pesa zote kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Mungano. Tafsiri safi na isiyo na mashaka inaonyesha kwamba mfuko huu unapaswa kutumiwa kwa mambo ya Muungano tu, kama yalivyoorodheshwa  katika Nyongeza ya Kwanza (First Schedule) ya Katiba.

Lakini Tanzania Bara haina mfuko mkuu kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano, yanayoihusu yenyewe (Tanzania Bara) tu.  Kinyume chake ni kuwa Zanzibar inao mfuko mkuu wake kwa mambo yasiyohusu Mungano, yanaoihusu Zanzibar tu. Na hicho ni moja katika vilio vya  Wazanzibari, kwamba matumizi  ya Tanzania Bara kwa mambo yasiyo ya Muungano yasigharamiwe na mfuko mkuu wa Jamhuri ya Muungano.

Kwa upande mwengine, kuna Akiba ya Pamoja ya Fedha (Joint Finance Account) ya Jamhuri ya Muungano ambapo zitatiwa fedha kutoka michango ya serikali mbili kwa viwango vitavyowekwa na Tume ya Pamoja ya Fedha (Joint Finance Commssion). Kwa hiyo, kikatiba ni Serikali za Jamhuri ya Muungano na Zanzibar ambazo zina wajibu wa kuchangia huduma na uendelezaji wa Muungano. Lakini Tanzania Bara haichangii kitu na wala haiwajibiki kuchangia kwa mujibu wa Katiba, maana serikali yake haipo.

Ilivyopaswa iwe ni kwamba suala hili la mapato lihusishe Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na serikali ya Tanzania Bara, jambo ambalo linaonyesha haja ya kuwa na serikali tatu. Hapo pasingekua na haja ya Tume ya Pamoja ya Fedha, ambayo, tangu hapo, mfumo wa kuteuliwa kwake unalalamikiwa.

Suala ya Mahkama ya Katiba ni tatizo jengine. Ingawa kuwepo kwa mahkama hiyo kunatajwa katika katiba zote mbili, lakini haisemwi kama hilo ni suala la Muungano. Halafu kuna suala la mahkama hii itasikiliza malamiko baina ya nani na nani? Baina ya Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanzania Bara au baina Serikali ya Zanzibar na Serikali ya  Muungano ambayo Zanzibar ni sehemu yake? Tena, nini nafasi ya Jaji Mkuu wa Tanzania Bara, ambaye pia ndiye mkuu wa Mahkama ya Rufaa isiyomshirikisha Jaji Mkuu wa Zanzibar?

Kufungu 99 (2) (a) cha Katiba ya Zanzibar kinaizuwia Mahkama ya Rufaa kusikiliza rufaa yoyote inayohusu tafsiri ya Katiba ya Zanzibar. Kifungu hiki kinapingana na kifungu 117 (1), (3) na (4) cha Katiba ya Muungano. Mzozo ukizuka baina ya katiba mbili hizi nani wa kuutuliza na kuamua?

Katika kesi ya SMZ v Machano Khamis na wengine 18, Mahkama ya Rufaa iliamua kwamba Zanzibar si dola, kwani, kwa mujibu wa majaji wa rufaa waliohusika, iliyo dola ni Muungano. Ni jambo la kusikitisha kwamba majaji hao hawakuzingatia asili ya Jamhuri ya Muungano na mambo yaliyochangia katika Muungano.

Ilibidi wazungumzie Makubaliano ya Muungano kwanza kabla kuingia kwenye matokeo ya makubaliano hayo. Tanganyika na Zanzibar kila moja ni dola ambayo imeshirikiana na mwenzake kufanya Muungano. Wazanzibari hawawezi kukubali hata siku moja kuwa dola yao imepotea, na hii inaonekana katika malalamiko yaliyozidi kukua tangu utoke uamuzi huo.

Mbili katika moja, ukiongeza moja, ni tatu

Kwa mujibu wa Katiba ya Muungano kuna Serikali ya Zanzibar na Seriali ya Muungano, ambayo pia itashughulikia mambo ya Tanzania Bara ambayo si ya Muungano. Kwa maneno mengine, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ingeshughulikia tawala mbili (two jurisdictions), ya Muungano na ya Tanganyika, wakati Katiba ya Zanzibar inashughulikia utawala mmoja.

Mtu yoyote anayejua hesabu, ataona kuwa kama kuna tawala mbili katika katiba moja na zikiongezewa na utawala mmoja katika katiba nyengine, zinafanya tawala kuwa tatu. Kwa lugha nyepesi, machungwa mawili katika kikapu kimoja na chungwa moja katika kikapu kigine, yamekuwa machungwa matatu, sio mawili tena.

Wasomi, kama Profesa Srivastava na Profesa Shivji wanakiri kwamba Makubaliano ya Muungano yaliashiria mfumo wa shirikisho.  Shivji anasema si kweli kwamba Tanganyika haina serikali yake, bali kilichofanyika ni kuingiza uongozi wa serikali (Executive) na sheria (Legislature) katika Jamhuri ya Muungano.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni mrithi halali wa Serikali ya Jamhuri ya Zanzibar, ambayo mwaka 1964 ilitia saini Mkataba, yaani, Makubaliano ya Muungano. Mshiriki mwengine wa mkataba huu ni Serikali ya Tanganyika. Kwa maelezo ya Makubaliano hayo, Jamhuri ya shirikisho yenye mamlaka kamili (Sovereign Federal Republic) ya mfumo wa Serikali tatu (triangular) ilianzishwa. Kutokana na hayo basi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikua chini ya nguvu, taasisi au chombo chochote cha dola. Kwa maana hiyo, Zanzibar ni, na itabaki dola inayojitegemea (Sovereign  state), na itakuwepo kama sehemu nzima (Integral part) ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, kwa mujibu wa maelezo na masharti yaliyowekwa katika Makubaliano ya Muungano baina ya dola ya Zanzibar, yaani, Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika. Tanganyika nayo ipo kama sehemu nzima (integral part) ya Jamhuri ya Mungano, ingawa imeingizwa katika Katiba ya Muungano.

Haya yanajitokeza hata katika Katiba ya 1977, licha ya kasoro zake nyingi. Kwanza, sehemu ya kwanza ya katiba hiyo inasema kua “Tanzania  ni Jamhuri kamili (sovereign) ya Muungano.” Jina rasmi la  jamhuri hii halijapata kuwa Tanzania. Hata sentensi inayosomeka kuwa “Tanzania ni Dola moja” ni uzushi na haimo katika Katiba ya asili ya 1977. Kwanza ilikuwa Jamhuri ya Muungano ya Tanganyika na Zanzibar na baadaye Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Kama tutaendeleza jina sahihi, tutakumbuka asili ya Muungano.

Pili, sehemu ya 2 (1) inataja nchi mbili zilizounda Jamhuri ya Muungano kuwa “Tanzania Bara” na Zanzibar. Hili “Tanzania Bara “ ni jina jipya lilobuniwa kuchukua mahala pa Tanganyika na waliotunga Katiba ya 1977. Lakini lina tafsiri ile ile kama jina la asili la 1964, “Jamhuri ya Muungano ya Tanganyika na Zanzibar.” Ni wazi basi kwamba kuna vitu vitatu kamili, tawala tatu tafauti: Tanganyika, Zanzibar na Jamhuri ya Muungano.

Tatu, sehemu 34 (3) inaeleza kwamba: “Mamlaka (executive authority) ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano kuhusiana na Jamhuri ya Muungano na mambo yote ya Muungano na pia mambo yote mengine kuhusu Tanzania Bara yatakuwa katika mikono ya Rais.” Suali hapa ni kwa nini kubana mamlaka ya Jamhuri ya Muungano katika masuala ya Muungano na yaliyohusu Tanzania Bara tu kama nia ilikua ni kuwa na mfumo wa serikali moja?

Nne, tunaweza kujiuliza nini masuala ya Muungano? Sehemu ya 4 (3) inatuongoza kwenye Nyongeza ya Kwanza ya Katiba. Hapa kuna orodha ya mambo 23 ambayo Tanganyika na (Zanzibar) yamesalimu kwa Jamhuri ya Muungano. Awali kulikua na mambo 11 tu, lakini pole pole yakaongezeka kufikia 23 bila ridhaa ya Wazanzibari. Hii haikubaliki kisheria na ni ukiukwaji wa Makubaliano ya Muungano.

Tukitoka kidogo katika Katiba na kuingia upande wa siasa, tutaona Mzee Abeid Karume hata siku moja hakuonesha dalili ya kutaka kuunganisha vyama vya Afro Shirazi na TANU. Hii ina maana kwamba ASP iliongoza Serikali Zanzibar; TANU iliongoza Serikali Tanganyika, halafu ndio inakuja Serikali ya Muungano, ambayo ingeweza kuongozwa na Muungano wa vyama ambavyo visingelazimika kuwa vyama rafiki kama ASP na TANU.

Aboud Jumbe ndiye aliyevuruga yote haya kwa kuunganisha vyama jambo ambalo limeleta tatizo la Makamu wa Rais hivi karibuni kwa kuwa CCM ndio inayotawala pande zote mbili.

Inakaribia miongo minne sasa tangu uundwe Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kulikua na wakati wa kutosha kurekebisha kasoro zilizopo. Hii haikuwezekana kutokana na ubabe wa Mwalimu Nyerere ambaye aliamua kuwatia shemere Wazanzibari na kuhakikisha Muungano unakwenda kama alivyotaka yeye hata baada ya ‘kuondoka madarakani.’ Lakini sasa si jambo la kuficha kwamba pande zote mbili za Muungano zimechoshwa na unafiki uliopo na zinadai Katiba ya kweli kweli itakayoweka misingi mipya ya ushirikiano na heshima baina ya pande hizo.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.