Unauona uso wa Maalim Seif ulivyokunjana? Unaweza kuzisoma hasira zake? Ni baada ya kumsikia Pinda akisema kuwa Zanzibar si nchi!
Maalim Seif Sharif Hamad

“Sasa, mimi hapa natamka kwa mdomo mpana. Natamka asikie Pinda huko aliko, kwamba Zanzibar ilikuwa ni nchi, Zanzibar imekuwa ni nchi, Zanzibar ni nchi mpaka sasa hivi na Zanzibar itaendelea kuwa nchi mpaka yaumul-qiyama. Hapa mimi nimesimama kwenye jukwaa lililo kwenye ardhi ya nchi ya Zanzibar. Sasa kama kuna watu wanaona baya kwa hilo, kama wana uhasidi kwa hilo, watafisidika wao. Zanzibar itakuwepo milele na milele. Walikuwepo maadui wengi tu wa Zanzibar, lakini leo wako wapi? Wamepita. Na kila mbaya wa Zanzibar atakwenda na maji”

Hotuba ya tarehe 16 Julai, 2008 ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), MAALIM SEIF SHARIF HAMAD, kujibu kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwamba Zanzibar si Nchi.

UTANGULIZI

Waheshimiwa Wananchi,

Kwanza, kama kawaida yetu, hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa wazima na kuweza kufika katika mkutano huu, Alhamdulillahir Rabbil Alamyna. Pili, naomba niwashukuru wote waliohusika kwa njia moja ama nyengine kuandaa mkutano huu adhimu. Tatu, naomba niwashukuruni nyote ambao mumeacha shughuli zenu muhimu na mukaja kutusikiliza. Na mwisho tunawashukuru Jeshi la Polisi. Naambiwa tumepeleka barua ya kutoa taarifa ya kufanya mkutano huu na siku hiyo hiyo tukapata majibu. Nasema ahsanteni sana. Tunashukuru.

Kama alivyosema Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu na Mahusiano na Umma (Salim Bimani), huu ni mkutano maalum. Ni mkutano ambao tumeuitisha kufuatia mjadala, ambao hivi sasa katika sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba na hata Bara unaendelea. Ni mjadala uliotokana na kauli ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda.

KAULI YA WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA

Mheshimiwa Pinda, kwa kauli yake mwenyewe katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, alitamka kwamba Zanzibar si nchi. Wazanzibari wengi wamefadhaishwa na kauli hiyo. Kauli hiyo ikazua mijadala mingi – mijadala kwa wananchi, lakini pia katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. La kufurahisha ni kwamba Wawakilishi wa pande zote mbili, wa CCM na CUF, waliitaka serikali ya Zanzibar itoe kauli kwa hilo.

Tulitazamia kwamba mtu anayelingana na Mizengo Pinda, angelisimama akatoa kauli kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Tulitazamia Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha angetoa kauli. Kwa sababu anazozielwa mwenyewe, aliamua kuufyata. Badala yake, mwanasheria mkuu wa Zanzibar, Mheshimiwa Iddi Pandu Hassan, akatoa kauli. Akasema wazi wazi kwamba Zanzibar ni nchi. Na mimi naamini, Mheshimiwa Iddi Pandu alitoa kauli ile kwa madhumuni ya, kwanza, kuwahakikishia Wazanzibari kuwa nchi yao bado ni nchi, lakini, pili, kumnusuru Mheshimiwa Pinda – kumfunikafunika. Akasema Mheshimiwa Pandu kwamba, Waziri Mkuu aliteleza ulimi, hakukusudia.

Sasa, mimi nilidhani pale Mheshimiwa Iddi Pandu Hassan alimsadia Mheshimiwa Pinda. Lakini bahati (mbaya), siku ya pili yake tu, Mheshimiwa Pinda, katika Bunge lile lile la Jamhuri ya Muungano, akasema: “Hapana. Sikuteleza ulimi.” Akasema wazi wazi kwamba Zanzibar si nchi.

Hiyo ndiyo kauli iliyotolewa na Mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda. Huyu si mtu mdogo. Ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika serikali ya Muungano, yeye ni mtu wa tatu: yuko Rais, yuko Makamo wa Rais, halafu Waziri Mkuu. Ni wa tatu katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kauli yake haiwezi kuwa kauli yake peke yake. Ni kauli ya Serikali ya Muungano wa Tanzania. (Ndio maana) tulitazamia viongozi wazito wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wangelisimama wakasema: “Mheshimiwa Pinda umekosea.” Hawakusema. Hawakusema.

Mheshimiwa Pinda alilosema, atawaomba wanasheria wakuu, yule wa Muungano na yule wa Zanzibar, wakutane waangalie suala hilo. Na halafu, kwa mshangao mkubwa, Mheshimiwa Iddi Pandu Hassan, aliyeonesha ujasiri siku ya mwanzo, naye anasema kakubali. Sasa Mheshimiwa Idd Pandu unakubali nini? Hivi kweli, wewe na mwanasheria mwenzako muna mamlaka ya kuamua mambo haya?

Waheshimiwa hiyo ndiyo hali. Hali ambao imewafadhaisha Wazanzibari. Hali ambayo imewasononesha Wazanzibari. Hali ambayo inawaumiza Wazanzibari. Na ni pahala pao Wazanzibari waumie, kwa sababu hakuna Mzanzibari aliyetazamia kuwa madhumuni ya Mzee Abeid Amani Karume na Mwalimu Julius Nyerere kuunganisha tukawa na Jamhuri ya Muungano, ni kuifuta Zanzibar. Hakuna Mzanzibari aliyetazamia hilo. Kwa hivyo, kwa kauli kama hizo lazima Wazanzibari wapate kiwewe.

KAULI YA CUF – CHAMA CHA WANANCHI

Sasa, mimi hapa natamka kwa mdomo mpana. Natamka asikie Pinda huko aliko, kwamba Zanzibar ilikuwa ni nchi, Zanzibar imekuwa ni nchi, Zanzibar ni nchi mpaka sasa hivi na Zanzibar itaendelea kuwa nchi mpaka yaumul-qiyama (siku ya Kiama). Hapa mimi nimesimama kwenye jukwaa lililo kwenye ardhi ya nchi ya Zanzibar. Sasa kama kuna watu wanaona baya kwa hilo, kama wana uhasidi kwa hilo, watafisidika wao. Zanzibar itakuwepo milele na milele (hata maadui wasipende hilo). Walikuwepo maadui wengi tu wa Zanzibar, lakini leo wako wapi? Wamepita. Na kila mbaya wa Zanzibar atakwenda na maji.

Pengine Mheshimiwa Waziri Mkuu anasikia tu neno Zanzibar. Hajui umuhimu wa Zanzibar, hajui Zanzibar ni nini. Sasa, leo nataka nichukuwe muda mfupi sana kumueleza Mheshimiwa Pinda na wenzake wenye mawazo kama yake, na pia kutoa darasa kwa sisi wenyewe hapa. Sawa sawa?

HADHI NA UTUKUFU WA ZANZIBAR

Waheshimiwa,

Umaarufu wa Zanzibar, utukufu wa Zanzibar, uzito wa Zanzibar, hasa katika maeneo ya Afrika Mashariki na Kati na katika Bahari ya Hindi, na katika nchi za Ghuba, haulingani na udogo wa Zanzibar. Ukiiona, Zanzibar ni nchi ndogo, watu milioni moja tu, lakini umaarufu wake, umuhimu wake, uzito wake ni mkubwa sana. Mkubwa sana kabisa. Tunamuomba Mheshimiwa Pinda alitambuwe hilo. Na pengine, ni kutokana na mambo hayo ndiyo mahasidi wa Zanzibar wanataka kuifuta. Yaguju (haiwezekani).

Kwa taarifa yenu, niwaambie, vitabu mbali mbali vimeitaja Zanzibar kwa majina tafauti kuanzia miaka 500 kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo au Nabii Issa. Tunavyoambiwa, kwa kufuata kalenda tulizonazo, ni kwamba tangu kuzaliwa kwa Nabii Issa hadi sasa ni miaka takriban 2008. Sasa, miaka 500 kabla ya hapo, Zanzibar tayari ishaandikwa katika vitabu. Yaani miaka 2508 nyuma, Zanzibar tayari inajuilikana katika ulimwengu wa historia. Wakati huo hakuna Kenya, hakuna Tanganyika, hakuna Malawi, hakuna chochote, lakini iko Zanzibar.

Hivi karibuni, katika Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza imepatikana ramani iliyochorwa katika karne ya 11; na katika ramani hiyo visiwa vya Zanzibar, Unguja na Pemba, vimo na makao makuu yake yalikuwa ni Unguja Ukuu, hapa Zanzibar. Hakuna Tanganyika, hakuna Malawi, hakuna Msumbiji, lakini Zanzibar.

Wakati huo, na kwa kipindi kilichoendelea, Zanzibar ikitawaliwa na falme za kienyeji katika sehemu mbali mbali. Kuna watu wa Tumbatu walikuwa na falme yao, mwisho wakaja wakamalizia kwa Mwana wa Mwana. Pemba walikuwa na falme zao wakamalizia kwa Mkama Ndume. Kwa hivyo, kulikuwa na falme mbali mbali za wenyeji wa visiwa hivi.

Ilipofika mwanzo wa karne ya 16, mwaka 1500, akatokea Mwinyi Mkuu. Yeye akawa ndiye symbol (alama) ya utawala wa kienyeji katika Zanzibar, na makao makuu yake yalikuwa Dunga; na Mwinyi Mkuu wa mwisho alifariki mwaka 1877.

Vile vile, katika mwanzo mwa karne hiyo ya 16, katika mwaka 1503, Zanzibar ikapata msukosuko mkubwa wa kwanza. Wareno waliivamia, wakaingia, wakaikalia Zanzibar. Walienda kupiga Unguja Ukuu. Utawala wa Kireno ulikuwa ni utawala wa kuwadhalilisha wananchi. Na msidhani kwamba Zanzibar, kwa wakati huo, mababu wa mababu zenu walivumilia hilo. Hapana. Walipambana. Walipambana, wakashindwa. Mateso yakawa makubwa, wakakusanyana watu kutoka sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba, wakasema: “Jamani, huyu atatumaliza. Tufanyeje?” Wakasema: “Tumesikia katika nchi za Ghuba, kuna nchi ambayo imepambana na Mreno na imeshinda. Oman. Kwa nini hatuendi tukawaambia waje watusaidie?” Wakakubaliana, wakatafuta jahazi, wakapeleka ujumbe kwenda kuomba msaada wa kuja kumuondoa Mreno. Wakaja, wakapambana na Mreno akashindwa. Sisi, kule kwetu kuna kisiwa tunakiita Mtambwe Mkuu. Mpaka leo kuna alama za mapambano hayo baina ya wananchi wa pale na Mreno.

Kwa hivyo, walipoona wananchi wa Zanzibar mambo yamekuwa makubwa wakasema tutafute msaada. Wakaja Waomani wakapambana na Wareno, Wareno wakaondoka. Wakaingia wao (Waomani). Na ndiyo kawaida: kama umetafuta mtu akusadie, mukishashinda, basi na yeye anakaa pale pale. Kwa hivyo na wao wakakaa.

Sultan Said bin Sultan (mtawala wa Oman wa wakati huo) akasema: “Hebu nikakuone huko Zanzibar.” Akaja mwaka 1828. Akapapenda, kwa hivyo akaamua kuwa: “Hapa ni pahala pazuri kuwa makao makuu ya utawala wangu mpaka Oman.” Kwa hivyo, katika mwaka 1832, akayafanya makao makuu ya utawala kuwa hapa Zanzibar. Alikuwa anatawala Zanzibar na anatawala Oman kutokea hapa.

ZANZIBAR KAMA DOLA HURU

Na hapo ndiyo Zanzibar ilipotambulika kama dola huru. Mataifa makubwa ya magharibi yakafungua mahusiano ya kibalozi na Zanzibar. Marekani, kwa mfano, katika mwaka 1837 wakafungua ubalozi wao hapa. Wakafuatiliwa na Waingereza ambao walifungua katika mwaka 1841. Wakafuatilia na Wafaransa ambao walifungua ubalozi mwaka 1844. Wakafuatiliwa na Wajerumani katika mwaka 1847.

Katika wakati huo, hakukuwa na nchi yoyote katika Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, iliyokuwa inajuilikana kama ni dola na yenye mahusiano na nchi nyengine isipokuwa Zanzibar. Halafu leo mtu aje aseme kuwa Zanzibar si nchi, we! Huko Dodoma, kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano, ambako Mheshimiwa Pinda kasimama kusema, ilikuwa ni katikati ya Dola ya Zanzibar wakati huo. Dola ya Zanzibar ilianza tangu Zanzibar kwenyewe mpaka Kongo. Kuanzia Kaskazini, Kismayuu (Somalia ya sasa), mpaka Kusini, Sofala (Msumbiji ya sasa), ilikuwa Dola ya Zanzibar. Vijana hiyo ndiyo historia yenu. Ndiyo Zanzibar yenu.

Baada ya hapo, Zanzibar ikajitangaza, ikaimarika. Ikawa ni kituo muhimu cha kibiashara, kituo muhimu cha kisiasa, kituo muhimu cha uchumi, katika Afrika Mashariki na Kati na katika Bahari ya Hindi.

KINYANG’ANYIRO NA KUGAWIWA KWA ZANZIBAR

Katika miaka 1880, Wazungu wakaanza kutafuta makoloni, ikafuatiwa na kinyang’anyiro cha kugawana Afrika, suala ambalo sitaki niliseme kwa undani. Lakini baada ya kukaa kule Berlin (Ujarumani) mwaka 1884, wakakubaliana kwamba hii Dola ya Zanzibar waikate. Sehemu ambayo sasa inajuilikana kama Kenya wakapewa Waingereza. Sehemu inayojuilikana kama Tanganyika wakapewa Wajarumani. Zanzibar ikabakishwa na Ukanda wa Pwani, maili 10 kwenda ndani, kuanzia Kenya mpaka Msumbiji, na visiwa vyenyewe vya Zanzibar.

Wajarumani waliopewa Tanganyika wakaununua Mwambao wa Tanganyika kutoka Sultan wa Zanzibar. Mwambao wa Kenya umebaki kuwa ni sehemu ya Zanzibar mpaka Zanzibar ilipopata uhuru mwaka 1963. Ndiyo, Mombasa na sehemu yote ya pwani ilikuwa ni sehemu ya Zanzibar mpaka Zanzibar inapata uhuru, lakini katika mazungumzo ya kutafuta Uhuru huko Lancaster House (Uingereza), wakakubaliana baina ya Mfalme wa Zanzibar na serikali yake pamoja na serikali ya Uingereza na serikali mpya ya Kenya kwamba, ule mwambao wa Kenya urejeshwe Kenya. Na hakukuwa na malipo yoyote, wakarejeshewa tu. Kwa hivyo, waheshimiwa, hiyo ndiyo Zanzibar.

UHURU NA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

Zanzibar tukapata uhuru kutoka kwa Mwingereza tarehe 10 Disemba, 1963. Kulikuwa na mgawanyiko: kuna wengine walioutambua uhuru ule, wengine hawakuutambua, lakini (ukweli ni kuwa) kutoka makucha ya ukoloni wa Kiingereza, Zanzibar ilipata uhuru tarehe 10 Disemba, 1963. Na kwa sababu ni nchi huru, tarehe 16 Disemba 1963, Zanzibar ikajiunga kama mwanachama rasmi wa Umoja wa Mataifa. Tukawa na kiti chetu katika Umoja wa Mataifa. Januari 12, 1964 yakatokea Mapinduzi. Lakini Mapinduzi yanafanyika, Mzee Karume anafanya Mapinduzi, yeye ni kiongozi wa dola huru ya Zanzibar. Ana mwakilishi wake wa kudumu katika Umoja wa Mataifa.

MAZINGIRA YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR, APRILI 1964

Aprili 1964, ikatangazwa Zanzibar na Tanganyika zimeungana. Sasa hapa nizungumze kidogo mazingira ya Muungano huu. Kwanza, Mwalimu Nyerere inaonekana, kwa mujibu wa nyaraka za kihistoria, alijenga chuki ya binafsi dhidi ya Zanzibar. Sijui walimfanya nini Wazanzibari? Na anathibitisha kwa kauli yake mwenyewe. Kwa mfano, mwaka 1961 akizungumza na mwandishi wa habari, anasema waziwazi kwamba: “Ningekuwa na uwezo, ningehakikisha visiwa hivi vya Unguja na Pemba navitupa huko katikati ya mkondo.” Na huyu mwandishi kaandika hayo mwenyewe (Nyerere) yuko hai, hakupata kukanusha hata siku moja. Hayo yameandikwa na kuchapishwa kwenye kitabu, na Mwalimu kakisoma kitabu, wala hakupata kukanusha hata siku moja. Basi kama unafika hadi unasema visiwa vizima ungekuwa na uwezo ungevichukuwa na kuvisukuma huko, unavipenda hivyo?

Sasa, sijui chuki hii ilitoka wapi. Mwaka 1985 akihutubia, Mwalimu Nyerere anasema, wakati wa mazungumzo ya uhuru wa Kenya, alimwambia waziri wa makoloni wa Uingereza wa wakati huo, akiitwa Duncan Sands: “Ikiwa mumekubali nyie Waingereza kumlipa Sultan wa Zanzibar fedha ili mwambao wa Kenya urudi Kenya, kwa nini nyinyi hamufanyi hivyo hivyo kumlipa Sultan wa Zanzibar na Zanzibar ikawa sehemu ya Tanganyika?”

Kwa hivyo, Zanzibar ilikuwa inamchanganya kabisa huyu mzee (Nyerere). Sasa, kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kuitupa huko, Waingereza hawakumkubalia kuwa wamuuzie, kwa hivyo baada ya Mapinduzi ukapatikana mwanya, akasema sasa hapa ndio pahala pa kuikamata Zanzibar.

Na taarifa ni kwamba Mzee Abeid Amani Karume alikuwa mgumu sana, mgumu sana, mpaka alipotishiwa, akaambiwa: “Kama hutaki Muungano, basi naondosha askari wangu!” Kwa sababu baada ya Mapinduzi, askari kutoka Bara waliletwa kuja kusaidia ulinzi. Wakati ule Serikali ya Mapinduzi ni mpya, haina jeshi, haina chochote. Na (Mzee Karume) anaambiwa: “Sisi tukiondoa askari wetu, hawa muliowapindua watarudi kukupindueni nyinyi.” Kwa hivyo, Mzee Karume akakubali shingo upande kwa pressure (shinikizo) za aina hiyo.

Lakini ukimuacha Karume, kipindi hiki kilikuwa kikijuilikana kama wakati wa Vita Baridi, Cold War. Mataifa ya Mashariki, wakiongozwa na Urusi na Uchina, na mataifa ya Magharibi, wakiongozwa na Marekani na Uingereza, walikuwa na mpambano na kila mmoja akitafuta kudhibiti sehemu mbali mbali duniani. Sasa, baada ya Mapinduzi, hawa wa Magharibi (Waingereza, Wafaransa na Wamarekani) walikataa kuitambua Serikali ya Mapinduzi. Warusi, Wachina, Wajerumani Mashariki haraka wakaitambua serikali na, kwa hivyo, wakawa na ushawishi mkubwa katika Zanzibar.

Na kwa yale Mapinduzi, hasa zile hatua za haraka za kimapinduzi zilizochukuliwa, kama land reform (ugawaji wa ardhi), Wamarekani wakasema: “Kama tukilegea, basi Zanzibar itakuwa Cuba ya Afrika Mashariki. Na ikiwa Cuba ya Afrika Mashariki, maana yake hatuna influence (ushawishi).” Wakakumbuka usemi kwamba ukipiga tarumbeta Zanzibar, watu walioko mpaka maziwa makuu wanadimka (wanacheza). Yaani unapiga tarumbeta hapa, lakini watu walioko Lake Victoria huko, Lake Tanganyika huko, wanadimka kwa tarumbeta ya Zanzibar.

Kwa hivyo, wakasema: “Lazima tuingilie hapa.” Na wao wakaweka shinikizo kubwa kwa Nyerere, shinikizo kubwa kwa Karume, kwamba wafanye Muungano huu, kwa kuamini kwamba wataidhibiti Zanzibar. Hayo ndiyo mazingira ya Muungano huu.

Kwa hivyo, Wazanzibari wakaingia kwenye Muungano, lakini Mzee Karume, nina hakika, asingekubali hata siku moja kuambiwa kuwa Zanzibar si nchi. Ni Mzee Karume huyu huyu, Karume original, nimemsikia kwa masikio yangu anatwambia pale Maisara kwenye mkutano wa hadhara: “Vijana musishughulike na Muungano. Muungano ni kama koti, likikubana unalivua.” Na hawa, Sauti ya Unguja, kama watakwenda katika archives (maktaba) na kama hawajafuta, wataziona kaseti hizo, lakini Karume kasema hivyo. Halafu leo uje umwambie kuwa Zanzibar si nchi! Huko aliko, nina hakika, anatikisika.

NJAMA ZA MUUNGANO DHIDI YA ZANZIBAR

Kwa hivyo, waheshimiwa, mimi nina hakika Karume alikuwa katika Muungano kwa nia njema kabisa. Wakati ule kuimarisha Pan-Africanism (umoja wa Afrika). Lakini sidhani kama mwenzake alikuwa na nia njema kama yake, maana baada tu ya Muungano, visa vya kuhakikisha kuwa Zanzibar inamalizwa, vikaanza.

Kwanza, angalieni, walivyokubaliana maraisi wawili ni kwamba Mambo ya Muungano ni 11 tu, sasa yahisabu! Yashafika 23, na kama utachambua kwa undani, kwa kweli, ni 32. Na kila ukisema unalifanya jambo ni la Muungano, unaipokonya Zanzibar madaraka yake. Ndio maana yake.

Lakini, sheria zilizotungwa na Baraza la Kutunga Sheria la Zanzibar, zinapaswa kama ni kufutwa zifutwe na Baraza la Zanzibar, ila kuna sheria kadhaa wa kadha zilizofutwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano. Hawana mamlaka hayo.

Moja ni ile waliyokuwa wakiita Exchange Control Decree, ambayo waliifuta 1965. Mamlaka hayo waliyapata wapi? Kuna masuala mazima ya vipi Benki Kuu hii ilivyoanzishwa na upi mchango wa Zanzibar. Benki hii imetokana na fedha zilizotoka katika East African Currency Board, ambayo Zanzibar ilikuwa ni mwanachama. Baada ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya wakati huo kuvunjwa, wakaamua rasilimali na fedha zigaiwe. Kenya wakapewa zao, Uganda zao na Tanzania wakapewa zao. Lakini Watanganyika wakajifanya wao ndio Wazanzibari, zile za Zanzibar wakazichukuwa wao. Wakazifanya ni zao.

Vikao vya bodi, vya East African Currency Board, baada ya Aprili 1964, ikifanywa hila ili wajumbe wa Zanzibar wasiende. Wakifichwa. Kwa hivyo, ukichukuwa fedha zilizoanzisha Benki Kuu ya Tanzania, mtaji wa Zanzibar ni asilimia 11.2. Lakini leo, tunaambiwa kuwa ati tunalipwa gawio la asilimia 4.5, na hizo hazilipwi kwa wakati.

Kwa hivyo, waheshimiwa, wenzetu hawa walikuwa na dhamira nyengine. Lakini nyundo kubwa zaidi ni pale Wazanzibari tulipkubali chama cha Afro-Shirazi kife. Tulikosa taasisi ya kisiasa kutusemea Wazanzibari. Tukakutana hapo Amani, tukaimba: “Baba Afro tunakuaga wee, sio kama umetukosa wee!”

Ndiyo, tukakosa sasa taasisi ya kisiasa ya kuisemea Zanzibar. Leo ni ndoto tu za “tutarejesha chama chetu.” Ndoto tu! Hasa wakati ule wa chama kimoja, ambapo chama kilikuwa supreme, chenye maamuzi ya mwisho, ndio Zanzibar hapo ikawa alhamdulillah (shukrani kwa Mwenyezi Mungu, Zanzibar imekwisha). Maana, hata mkiwa kwenye serikali mkifanya maamuzi hayatakiwi na chama, basi mnaambiwa hiyo siyo sera ya chama. Inabidi hapo uufyate tena, siyo sera ya chama. Na wenzetu hawakuishia hapo.

JITIHADA ZA CUF KUINUSURU ZANZIBAR DHIDI YA NJAMA ZA MUUNGANO

Kuhusu Vyama vya Siasa kuwa vya Kitaifa

Niseme kwamba tangu kufa kwa Afro-Shirazi, Zanzibar ilikosa mtetezi, mpaka ilipoundwa CUF. Na (kwa hakika) CUF ilianza kazi kabla hakijakuwa chama. Hawa walipotaka kuanzisha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, walikubaliana na wakaamua kwamba vyama hivi viwe vya kitaifa, yaani walilifanya suala la siasa kuwa la Muungano. Mpaka 1992, suala la siasa si la Muungano, lakini kijanja wakasema vyama vyote viwe vya Muungano. Wakati huo CUF hakijazaliwa, lakini mzee wa CUF, Kamahuru, ikatoka wazi wazi kusema: “Tunapinga! Hiyo itaua uhuru wa Zanzibar.”

Lakini angalia, Mzanzibari mwenzetu, mzee wangu ninayemuheshimu sana, Mzee Ali Hassan Mwinyi, mwenyewe kwa kauli yake anasema: “Tumefanya maamuzi haya ya vyama viwe vya kitaifa, kwa sababu tunataka tuwazuie wapinzani Zanzibar wasiunde vyama vyao.” Kumbe lengo sio kulinda maslahi ya Zanzibar, bali ni kuhakikisha kuwa wapinzani wa Zanzibar, ambao walijua they are very strong (wana nguvu sana), tuwatie kamba. Na tumeshuhudia migogoro iliyokuwa ikifanywa na akina Mapalala, Nyaruba na wengine. Kumbe zote zile zilikuwa ni kututia kamba, lakini CUF ime-stabilize, kimekuwa chama imara, baada ya kumpata Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti wetu. Kwa sababu Lipumba ni mzalendo, anaijua vizuri historia ya Zanzibar, anashirikiana na Wazanzibari. Na wao walishituka sana kusikia Lipumba anaingia CUF. Ndiyo, keshakuja!

Kwa hivyo, nasema Kamahuru ilifanya kazi hiyo kabla ya CUF kuundwa. 1992, Januari (vyama vingi) vikaruhusiwa, tukaunda CUF yetu.

Kuhusu Zanzibar na OIC

Mwaka 1993, chini ya uraisi wa Dk. Salmin Amour, wakaamua Zanzibar ijiunge na Jumuiya ya Kiislam (OIC). Na wakaruhusiwa kujiunga. Kumbe Mwalimu Nyerere hilo linamuuma. Akasimama kidete kuhakikisha Zanzibar inajitoa. Rafiki yangu, ndugu yangu Salmin akajikakamua sana mpaka akawaambia: “Musitikise kibiriti!”

Na japo kama sisi hatukushauriwa, mambo yote yalifanywa siri siri, lakini kwa sababu tulijuwa ni kwa maslahi ya Zanzibar, tulitoka hadharani kuunga mkono kwamba ni haki yetu kujiunga na Jumuiya. After all (baada ya yote), katika Mambo ya Muungano inasemwa wazi wazi kwamba suala la Muungano ni Mambo ya Nje. Mambo ya Mashirikiano ya Kimataifa si ya Muungano.

Sasa, Nyerere alipotaka kulimeza hili, akaunda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ili kutunyima ule uhuru wetu. Sisi tukasimama kidete kusema: “We have the right (tuna haki).” Yakatiwa mambo ya kidini. Kwani kama ni suala la Uislam, (mbona) Msumbiji wamejiunga na OIC, na kule Waislam ni chini ya asilimia 12, Uganda wamejiunga na OIC, Waislam hawafiki asilimia 30?

Tunazuiwa sisi, ambao Waislam ni asilimia 98, kwa sababu Bwana Mkubwa hataki tu. Kwa sababu Zanzibar itanufaika tu. Ikafa. Tukaambiwa lugha za kibabaishaji, za kilaghai: “Zanzibar itajitoa kuipisha Tanzania.” Haya, tangu 1993 mpaka leo 2005, miaka 15 imepita, mbona hatujasikia hata kama Tanzania imeomba? Basi, ulikuwa ni uhasidi tu. Waliona Zanzibar itanufaika, basi. Jambo la ajabu sana. Muungano gani huu, ambao mwenzako hataki unufaike?

(Hapa hadhara inajibu: Koti!!!)

Koti, enh!? Basi kama Karume original hakuweza, Karume afanye. Avue koti. (Makofi).

Mwaka huo 1993, kwa sababu hiyo ya kupinga mambo haya ya Zanzibar kujiunga na OIC, likazuka kundi la wabunge waliojiita G55, waliodai Tangayika yao. Kwamba kuwe na serikali ya Tanganyika kama vile kulivyokuwa na serikali ya Zanzibar. Na lilikuwa kundi lenye nguvu. Wakapeleka hoja kwenye Bunge, ikapitishwa kwamba Tanganyika iwe na serikali yake. Wakati huo rais ni mzee wangu, Mzee Mwinyi. Nyerere, hana madaraka yoyote, si kiongozi, si raisi, si mwenyekiti wa chama, lakini akasema: “Sitaki, hilo haliwi!”

Kwa nini? Likiwa, Zanzibar itapata nguvu, na ile azma ya kuimeza itakuwa haifanikiwi tena. Kwa hivyo, akapinga kwa nguvu zote mpaka akatunga kitabu Tanzania, Tanzania we! (Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania). Na kwa maelezo yake katika kitabu hicho, anasema sera ya CCM ni serikali mbili. Kufanya serikali tatu ni kurudi nyuma, afadhali tutoke kwenye mbili twende kwenye moja. Hayo ni maendeleo.

Angalieni. Huyu si pekee, hata mzee wangu, raisi wangu – kwa sababu alipokuwa rais, mimi nilikuwa Waziri Kiongozi wake – Mzee Mwinyi, naye kasema kauli hiyo hiyo. Kwamba sera ya CCM ni serikali mbili kwenda moja. Kauli iliyorudiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Phillip Mangula. Ikarudiwa na bwana mmoja anaitwa Mwaitambo, hapo Kisonge, kwamba azma ni serikali moja.

Sasa angalieni, waheshimiwa, muone hizi njama. Muone pia ni jinsi gani CUF imekuwa ikisimama na kuomba wenzetu tuungane, lakini badala yake tunachopata ni kejeli. Huambiwa tunataka vyeo, tunataka madaraka.

Kuhusu Mapendekezo ya Tume ya Shelukindo

Waheshimiwa, mwaka 1994 kulikuwa na tume imeundwa ati kuchunguza matatizo ya Muungano na kupendekeza jinsi ya kuyatatua. Mwenyekiti alikuwa mtu mmoja anaitwa Shelukindo. Mambo ya ajabu ni taarifa yao waliyoitoa kwamba matatizo yote, solution (suluhisho) yake ni kuinyang’anya madaraka yake Zanzibar.

Na mimi nilipopewa taarifa, nikatoka hadharani kwenye mkutano nikasema hayo hatuyakubali. Kwa mfano, wakasema suluhisho la tatizo la uhamiaji, basi paspoti iondolewe Zanzibar. Maana hapa ilikuwa ukienda Bara uwe na paspoti, ukija uwe na paspoti. Kwa hivyo, Shelukindo akapendekeza paspoti iondolewe. Matatizo ya kuondolewa kwa paspoti sasa munayajua wenyewe, sitaki kuwaambia.

Katika matatizo ya mambo ya ulinzi, kwa mfano, solution (suluhisho) ya Bwana Shelukindo, KMKM ifutwe kabisa. Matatizo ya kiuchumi, kwa mfano, wanasema viwango vya ushuru baina ya Zanzibar na Bara viwe sawa. Zamani, kabla ya hapo, ilikuwa viwango vya Zanzibar vya ushuru kwa bidhaa zinazoingia nchini vilikuwa chini. Ndio maana bidhaa nyingi zikaletwa Zanzibar na ndio maana serikali ikapata pesa nyingi kuendeshea shughuli zake. Wakasema viwe sawa sawa. Matokeo yake hakuna bidhaa inayokuja Unguja. Lakini sisi tukasimama hadharani kupinga.

Kuhusu Mabadiliko ya 11 ya Katiba ya Muungano

1994 hiyo hiyo, mwezi wa Disemba, ndio unga ukazidi maji. Walipitisha marekebisho ya 11 ya Katiba yaliyomuondolea Rais wa Zanzibar kuwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Suala hili ni la kikatiba, na sio la kikatiba tu, lakini ni katika Makubaliano ya Muungano. Ile wanasema ndio sheria kuu (grand norm), huwezi ukaibadilisha. Msingi wa Muungano wenyewe umejengwa juu ya Makubaliano yale (Articles of the Union). Wenzetu hawakujali hilo. Wakaondoa. Wakamuondolea Rais wa Zanzibar wadhifa wa kuwa moja kwa moja Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Na ile iliwekwa makusudi na waasisi wa Muungano ili kuhakikisha kuwa Zanzibar inawakilishwa na mtu ambaye kachaguliwa na Wazanzibari wenyewe ili awawakilishe. Tukapiga makelele pale Malindi. Ndipo nilipomuomba ndugu yangu, rafiki yangu Salmin Amour: “Tangaza mgogoro wa kikatiba.” Na nikamwambia: “Kama unaogopa, tutakupa wana-CUF laki moja waizunguke Ikulu, tumuone huyo Nyerere apige mabomu hapo!” Tulichoambulia ni kuambiwa: “Aah, balahau kuna itifaki!” Leo ndiyo itifaki hiyo, waheshimiwa.

Kuhusu Mafuta ya Zanzibar

Katika kampeni ya 2000, katika viwanja hivi hivi (vya Kibadamaiti), tulifanya mkutano tuliouita “Kumtoa Paka Guniani.” Na ajenda ilikuwa moja tu: suala la mafuta. Ubaya wao, wakati nazungumza, walipojua ni mafuta, wakazima redio, wakazima kila kitu, eti nisisikike. Nikawaambia, jamani Zanzibar mafuta yapo. Lakini wenzetu wameyatia mafuta katika Muungano, lakini mafuta tu – sio dhahabu, sio almasi, sio chengine chochote. Changu mimi kiwe chetu, chako wewe kiwe ni chako. Nikasema hapa hapa. Nikasulubiwa kwa maneno: “Huyu muongo. Hakuna wee. Mzushi huyu!”

Haya, mie mzushi, lakini sasa wenzetu waliomo kwenye serikali limewakwama, limewakaa hapa (kooni). Na katika hayo marekebisho waliyoyatia ya mafuta, wamesema mafuta na gesi. Wenzetu tangu 2003 wanachimba gesi, inatoka, inazalishwa. Naambiwa wacha kando gharama za uzalishaji, faida washayoitia ndani ya mfuko, ni shilingi bilioni 80. Tuwaulize katika bilioni 80, ngapi zimekuja Zanzibar? Not a single cent (si hata senti moja); na hili ni jambo la Muungano.

Ukiuliza, tena nashukuru kuna wabunge kama yule wa Chwaka ni CCM, lakini kakazana anauliza: “Fedha ziko wapi?” Jibu: “Aa, kuweni na subira. Tushamteua mshauri elekezi atushauri jinsi ya kugawana mapato.” Tena kumbe hawa wabunge wa Zanzibar wakiuliza maswali haya, hawa wajumbe wa Bara wanahamaki kwelikweli. Leo nasikia mmoja kaja juu, kwa nini Wazanzibari wakauliza maswali haya. Ala, wasiposema kwenye Bunge wakaseme wapi?

Sasa tunaambiwa huyo mshauri elekezi keshateuliwa na mkataba baina ya serikali mbili upo. Waliosoma mkataba, waheshimiwa, wananambia wamekwenda vifungu vyote, kinachotajwa katika mkataba ni mafuta tu, gesi haikutajwa, na Katiba inasema “Petroleoum and natural gas.” Lakini mkataba una petroleoum tu, gesi imetajwa mwisho kabisa na katika sababu gani? Naambiwa kuna kifungu kinachosema, kwa zile sehemu ambapo pamekuwa na utafiti au uchimbaji basi wananchi hao watalipwa fidia. Basi. Yaani mapato ya Muungano yawalipe watu wa gesi ambao Zanzibar hawanufaiki. Lakini kwamba tugawane mapato ya gesi, haimo kwenye mkataba. Ndugu zetu hao!

VITIMBI VYENGINE VYA MUUNGANO DHIDI YA ZANZIBAR

Zanzibar Kujiunga na FIFA

Jamani, hiyo ndiyo hali. Hao ndugu zetu tumewaambia jambo dogo tu: jamani suala la michezo si suala la Muungano. Katika Orodha ya Muungano, hamuna michezo. Ndio maana tuna ZFA na kule wana TFF. Sasa tunajua kuwa ZFA wamechukua jitihada kutaka kujiunga na Shirika la Mpira Duniani, FIFA, lakini wanaopinga ni nani? Ni ndugu zetu wa damu. Jamani, kama ni Muungano, Uingereza ni muungano wa nchi nne: kuna England, kuna Scotland, kuna Northen Ireland, kuna Wales. Wote hawa ni Muungano wa United Kingdom. Kidunia wanajuilikana United Kingdom, lakini Scotland ni wanachama wa FIFA, Wales ni wanachama wa FIFA, Northern Ireland ni wanachama wa FIFA na England wenyewe ni wanachama wa FIFA. Mbona Uingereza haijadhurika?

Hivyo kweli, kama wenzetu wangekuwa na nia njema na sisi, wakatusaidia kupata uanachama wa FIFA, wao wangepata hasara gani? Isipokuwa ni ile ile tu, kwamba Zanzibar isijuilikane. Hata zile fedha zinazotolewa na FIFA kuendeleza soka katika nchi wanapewa TFF. ZFA wanadai, mpaka Waziri kwenye Bunge anasema: “Hatutoi, hatutoi. Hatuwapi!” Nini? Fedha zikija hapa, zitatumika kuendeleza vijana. Saa hivi soka ni kazi. Ukipata, ukawaendeleza vijana, kwa nini tusitoe akina Maradona, kwa nini tusitoe Ronaldo hapa? Vipaji tunavyo, lakini wenzetu hawataki. Hata nalo hilo, hebu nambieni jamani: tungekuwa sisi wanachama wa FIFA, wao wangepata hasara gani? Wanayo?

Uwakilishi wa Zanzibar katika Wizara za Muungano

Angalia katika wizara nyengine zote za Muungano, uwakilishi wa Zanzibar ukoje. Chukua Foreign Ministry, Mambo ya Nje. Hapa alikuja Waziri akaulizwa, mbona Wazanzibari hawamo, jibu lake: “Enh, hawaombi, hawana uwezo!”

Jamani, ee jamani wee, eti Zanzibar hakuna watu wenye uwezo!? Hao wachache waliochukuliwa wameweka rekodi. Kulikuwa na Balozi Mohammed Mwinyi Mzale kaweka rekodi. Kuna balozi, huyu ambaye sasa ni Naibu Waziri (Mambo ya Nje), mbona kafanya kazi nzuri tu kule? Kina Mheshimiwa Diria, marehemu, walikuwa Wazanzibari wote hao. Hivi kweli hakuna Mzanzibari mwenye uwezo? Hakuna? Nenda katika zile ofisi za kibalozi, angalia wako Wazanzibari wangapi?

Katika safari yangu moja nilikwenda Denmark. Nikenda katika ofisi yao inayoshughulikia mambo ya Fero Islands. Fero Islands nao wana utawala wao kama sisi hivi, lakini kwanza wale jamaa katika balozi zao Denmark, kila pahala kuna uwakilishi wa Fero Islands kupigania maslaha ya Fero Islands. Pili wakanambia, kwa mfano, wao kazi yao kubwa ni uvuvi, sasa ile serikali ya Fero Islands, kama serikali ya Zanzibar, wanayo haki ya kuingia mkataba na jumuiya nyengine kama European Union wao wenyewe, na wakishaingia, Denmark kwao ni kuidhinisha tu, basi. Kwetu lipo hilo? Basi hata hili wenzetu hawalioni?

Kama ni suala la watu hawana uwezo, tulikuwa naye Mzanzibari mmoja mzalendo anaitwa Mohammed Yussuf. Alikuwa ubalozi wa Tanzania, Umoja wa Mataifa. Huyu kijana kajiendeleza, ana uwezo mkubwa sana, lakini akawa anawekewa mkungu asije juu. Anafunikwa asije juu. Mwisho akaona atafute kazi mahala pengine, katika mule mule Umoja wa Mataifa. Akaomba kazi katika Kitengo cha Ukaguzi, Geneva. Hakusaidiwa na serikali; ni mwenyewe tu. Kwa sababu anajuilikana uwezo wake, wakampa. Kafanya wonders kule, kafanya maajabu. Kwa hivyo, sio kweli kwamba hatuna uwezo.

Zanzibar na Jumuiya ya Afrika Mashariki

Afrika Mashariki, jumuiya inayofufuliwa. Waliposema tu kwamba wanafufua Afrika Mashariki, nilimuandikia barua Rais Ali Hassan Mwinyi (wa Tanzania), Rais Daniel arap Moi (wa Kenya) na Rais Yoweri Museveni (wa Uganda) kuwaambia kuwa na Zanzibar iwe mwanachama wa Afrika Mashariki na kopi nikampelekea Dk. Salmin Amour. Lakini, ndiyo hivyo tena. Leo Jumuiya ya Afrika Mashariki inashughulika na mambo 17. Katika mambo 17 hayo, manne tu ndiyo yako chini ya Muungano. Jiulize, haya mambo 13 yanashughulikiwa na nani kama huna Zanzibar?

Hamna.

KOSA LA MSINGI LA WAZANZIBARI

Kwa hivyo, wenzetu wana malengo tafauti. Sasa, tunalosema waheshimiwa – na naomba munisikilize vizuri – kinachogomba ni sisi Wazanzibari tumekubali kugawiwa. Na madamu tumegawiwa, wenzetu wanafanya watakavyo.

Hapa uchaguzi wa 1985 ilipandikizwa fitina makusudi baina yangu mimi na Marehemu Mzee Idrissa (Abdulwakil). Mwalimu Nyerere huyo huyo, akihutubia Pemba anawaambia: “Aah, watu wa Unguja wamezidi tena, basi maraisi wote wanatoka Unguja tu! Tutahakikisha mara inayokuja, Mpemba awe raisi.” Siku hiyo hiyo akaja Unguja, pale Kisiwandui, akawaambia: “Wapemba wataka raisi wao, lakini nyinyi watu wa Unguja ni Idrissa wenu.” Akapanda mbegu ya fitina; na tukaimeza hiyo baadhi yetu.

Imetumiwa: “Seif mbaya, anampinga Idrissa.” Jamani, mimi namshukuru sana marehemu mzee yule (Mzee Idrissa Abdulwakil), maana mwisho alitambua kuwa kwa kweli akipotoshwa. Na mimi, kwa kweli, nimemsamehe fil-dunia wal-akhera (duniani na akhera). Kabisa kabisa. Kwa hivyo, tukatiwa sumu, tukatiwa sumu, tugombane sisi wenyewe kwa wenyewe.

Hapa katika Awamu ya Tatu, moja katika mafanikio yake ni kuwaunganisha Wazanzibari. Wakati ule Wazanzibari tulikuwa wamoja. Ndio maana nchi ilipata maendeleo haraka. Nakumbuka, walifanya ramani ya Tanzania na katika ramani ile Zanzibar ikaoneshwa kama ni mikoa miwili na wilaya tano: yaani mkoa wa Unguja, mkoa wa Pemba; wilaya ya Kaskazini Pemba, Kusini Pemba, wilaya ya Mjini Magharibi, wilaya ya Kusini Unguja na Kaskazini Unguja. Map hiyo, official (rasmi).

Nilipoiona, nikiwa Waziri Kiongozi, nikasema: “Map hii marufuku! Marufuku kabisa.” Na tukafanya fujo kweli, zikaondolewa Tanzania nzima. Hawa wanabonyeza, ukibonyea…..

Nakumbuka wakati ni Waziri Kiongozi tulikuwa na utaratibu wa kusoma bajeti yetu baada ya kushauriana na wao, Muungano. Sisi tukawasilisha bajeti yetu katika Baraza la Wawakilishi, ikapitishwa. Walipokuja wao, wakapunguza thamani ya shilingi. Kwa hivyo, moja kwa moja, bajeti yetu ikawa haina maana. Nilisimama imara katika Baraza. Na wakati huo kumbuka, Waziri Mkuu ni Salim Ahmed Salim – ndugu yangu, mwenzangu, tulokuwa pamoja. Lakini sikumtizama kwamba huyu ni mwenzangu, uzalendo ulikuja zaidi kuliko ubinafsi. Nikasema lazima serikali ya Muungano wafidie gharama zetu na Baraza la Wawakilishi likaniunga mkono.

Sasa, nilifanya yale yote kwa nini? Si kwa kuwa ni hodari, bali kwa sababu Wazanzibari tulikuwa wamoja. Nilijuwa Wazanzibari wote wako pamoja na mimi; kwa hili tunakwenda bega kwa bega. Ndio nguvu zangu. Na ndio maana walipoona tuko strong (madhubuti), wakaanza fitna za kutugawa. Na wengine tukazichukuwa fitna hizi. Zinatudhuru wenyewe.

MSIMAMO WA CUF: WAKATI NI HUU

Sasa umefika wakati Wazanzibari tuungane. Wakati umefika kusahau yaliyopita. Ishayopita si ndwele, tugange ijayo. Tunadhurika sote. Hebu tuungane, tuone.

Kwa hivyo, nitoe wito kwa viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha atumie ukumbi wa Baraza la Wawakilishi kumuhakikishia Pinda na wenzake kwamba Zanzibar ni nchi. Na hata kama kwa uzito wake, Mheshimiwa Karume anao uwezo wakati wowote kuamua kulihutubia Baraza. Aende kwenye Baraza akatie kauli nzito kuhakikisha kwamba Zanzibar ni nchi. Na mimi nina hakika, atoe Nahodha atoe Karume, wana CCM wa Zanzibar watamuunga mkono. Na kwa hili, nawahakikishia CUF wa Zanzibar wote watamuunga mkono. Nawatoe kauli. Waende watoe kauli.

Sasa, msimamo wetu. Kwanza, narudia kusema mara elfu wa elfu, Zanzibar ni nchi, itabaki kuwa nchi.

Pili, ama Mheshimiwa Karume au Mheshimiwa Nahodha, waende kwenye Barza kutoa kauli kusema Zanzibar ni nchi; na kwa sababu atakuwa ni Waziri Kiongozi au Rais kasema hivyo, na huku Pinda kasema si nchi, hapo ni mgogoro. Kwa hivyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itangaze mgogoro wa kikatiba. Halafu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar idai kuundwa kwa Mahakama ya Katiba kwa mujibu wa Kifungu cha 127 cha Katiba ya Muungano.

Ikiwa watashindwa kufanya hivyo, mimi nawaagiza wawakilishi wa CUF wapeleke hoja binafsi ya kudai hayo.

La mwisho kabisa, namwambia Mheshimiwa Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Pinda awaombe radhi Wazanzibari hadharani.

Waheshimiwa wanachama tunakubaliana na hayo?

Mikono juu kama tunakubaliana!

One thought on “Zanzibar ni nchi na itabaki kuwa nchi”

  1. Mchanga wa kujengea tu umekua changamoto kupatikana sasa hiyo hadhi ya zanzibar kuwa nchi mnaitoa wapi

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.