Mwansheria Mkuu wa Zanzibar, Iddi Pandu Hassan. Kauli yake ya kupinga kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ilikuwa madhubuti, lakini ameshindwa kuisimamia

Kwa hivyo inabidi itafutwe njia ya kupatikana ridhaa ya wananchi na hata vipengele vya Articles of Union viwe vinazungumzika. Kwetu sisi Articles of Union ndio Mkataba Mama. Matumaini yetu kwa wanasheria ni kulitambua hili. Tunaelewa jambo hili hupuuzwa hasa na baadhi ya wanasheria wa Bara. Jee tunaweza kuulizia uhalali wa hizo Articles of Union?

Tamko ya Jumuiya ya Wazanzibari, Zanzibar Committee for Democracy, yenye makao yake makuu Copenhagen, Denmark, kuhusu suala la Zanzibar kuwa na kutokuwa nchi

Tamko la Waziri Mkuu wa Serikali ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mizengo Pinda, katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Zanzibar si nchi limewashituwa Wazanzibari wa ndani na nje ya nchi yao, Zanzibar.

Majibu ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mheshimiwa Idi Pandu katika Baraza la Wawakilishi kuisuta kauli hiyo na kuelezea kuwa Waziri Mkuu ameteleza ulimi, yamezusha malumbano na kutoa fursa pana ya kuujadili Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kuonyesha ukakamavu wake Mheshimiwa Pinda hakusita kuirejea tena kauli yake kwa nguvu zaidi kwamba Zanzibar sio nchi. Kama nia yake ilikuwa ni kuweka mambo wazi au ni uchokozi basi vuno alilolipata limemshitua hata kufika kusema wanaomuuliza tena suala hilo hawamtakii mema.

Ili kuuzuia moto usizidi kuwaka, kwa upande wa Zanzibar, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mheshimiwa Pandu Kificho, alitaka wajumbe wasilijadili tena suala hili; na kwa upande mwengine wa Muungano, Spika wa Bunge, Mheshimiwa Samuel Sitta alifuata nyayo za mwenziwe.

Jitihada zao za kuufunga mjadala huu hazijasaidia kitu. Kwani suala hili limekuja kama msumari wa moto kutonesha donda la siku nyingi. Jambo lisilofahamika ni kwa nini Serikali ya Muungano mpaka hivi sasa imekaa kimya bila ya kutoa tamko rasmi?

Ijapokuwa huko mwanzoni alijichomoza Bwana Tambwe Hiza, aliyehama kutoka Chama cha Wananchi, CUF, na sasa akiwa mkuu wa propaganda wa Chama Cha Mapinduzi, CCM, kuamrisha wananchi wasilizungumzie tena suala hilo. Akiwakilisha hisia za Wazanzibari walio wengi waliotoneshwa kwenye donda lao la muda mrefu, Naibu Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Ali Juma Shamhuna, alisema kwa nguvu moja kwamba suala hili haliwezi kunyamazishwa. Isitoshe, aliongeza  kwa ujasiri zaidi kwa kusema  huu si wakati wa kutishana. Matokeo haya ya karibuni yamewashituwa watu wengi mpaka kufikia kujiuliza kuna nini?

Katika mjadala huu, tungependa kuzungumzia kwa ufupi mambo muhimu ya msingi. Tangu kuundwa kwa Muungano, kuna mambo mengi yaliyojitokeza ambayo hayafahamiki. Jambo kubwa muhimu la kukumbukwa ni kwamba Muungano umeundwa bila ya kupatikana ridhaa ya wananchi, kwani hakuna hata mtu mmoja aliyeulizwa mawazo yake. Kuna ushahidi wa kutosha kuonyesha kwamba hata viongozi wa juu walikuwa hawayajui.

Tukitaka kuyafahamu mazingaombwe yaliyopita, inatubidi tutazame hali halisi ilivyokuwa. Tukiachana na yote yale ya “enactment” na “ratification,” taswira nzima ya sakata la Muungano inaonyesha dhahir shahir kwamba ulikuwa ni uamuzi uliochukuliwa na watu wawili, kwa hivyo ni Muungano wa watu wawili tu: Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume.

Nyerere ndie aliyekuwa ameshika mpini. Zaidi ya elimu yake mwenyewe, alizungukwa na wataalamu wa sheria, mmojawapo akiwa Bwana Brown. Dola za Magharibi zikiongozwa na Marekani nazo kwa upande wao ziliupalilia sana Muungano huu katika mazingira ya vita baridi.

Kwa upande wa Zanzibar, hakuna kiongozi wala mwanasheria yeyote mwengine zaidi ya Mzee Abeid Karume aliyehusishwa katika mazungumzo haya. Ukisoma maandishi ya wanazuoni waliofanya utafiti na kutafakari juu ya Muungano, unatikisa kichwa kwa huzuni. Kwa mfano mtu aliyekuwa karibu na aliyekuja  kuchukuwa nafasi ya Mzee Karume, Al Hajj Aboud Jumbe, aliwekwa gizani kwa sababu zisizofahamika.  Hii inaonyesha wazi kwamba ridhaa ya wananchi, tangu mwanzo, haijatafutwa.

Kwa hivyo inabidi itafutwe njia ya kupatikana ridhaa ya wananchi na hata vipengele vya Articles of Union viwe vinazungumzika. Kwetu sisi Articles of Union ndio Mkataba Mama. Matumaini yetu kwa wanasheria ni kulitambua hili. Tunaelewa jambo hili hupuuzwa hasa na baadhi ya wanasheria wa Bara. Jee tunaweza kuulizia uhalali wa hizo Articles of Union?

Ndio, tunaweza. Tayari tumeona ujanja uliotumika katika utengenezaji wa hizo Articles of Union. Tumechezewa foul ya kibeberu. Tunaamini wanasheria pamoja na wanasiasa wanahofu kuzijadilli kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kuwapelekeya kufunguliwa mashitaka ya uhaini. Hili si tishio. Tumeona Rais wa Zanzibar, aliyechaguliwa na Wazanzibari, Al Hajj Aboud Jumbe,  jinsi alivyovuliwa vyeo vyake vyote kufumba na kufumbua.

Tunaelewa mikataba mingi ya Kimataifa katika historia ilikuwa tangu mwanzo si ya usawa. Katika umri wetu huu, tunakumbuka wakati ule serikali ya China ilipotoa tamko kuhusu mikataba iliyofanyika kati yao na Urusi. Ugomvi huu ulipelekea kuzuka mapigano na kurushiana risasi mpakani. Wachina walikuwa hawajakataa ”uhalali” wa hiyo mikataba, lakini walitaka ipitiwe tena kwa sababu Mataifa hayo wakati wa kutia sahihi mikataba hiyo hayajakuwa katika hali ya usawa.

Kama China walivyofanya na Urusi wakati ule inabidi na sisi leo Zanzibar na Tanganyika tutafute njia ya uwiano ya kuujadili upya Muungano. Ikiwa hatujafanya, hivyo basi tutabaki na hii katiba ya viraka inayopelekea Zanzibar kumezwa na kupunguzwa kinyemela mamlaka yake kila siku zikipita.

MUNGU IBARIKI NCHI YA ZANZIBAR NA WATU WAKE

*Zanzibar Committee for Democracy

Gustav Bangsgade 11st, th

2450 Copenhagen

Denmark

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.