Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda. Hoja yake ya Kikatiba kwamba Zanzibar si nchi imekosa mashiko ya kisheria, kwani Mkataba wa Muungano ambao uko juu ya Katiba unaitambua Zanzibar kama nchi. Wazanzibari wanasimamia Mkataba wa Muungano na sio Katiba ya Muungano katika kutetea udola, unchi na utaifa wa Zanzibar

“Nionavyo mimi kusema kuwa Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya kuwa na jina la eneo hilo kiutawala ni utata katika hiyo Katiba ya Muungano na ndio mwanzo wa kuanza mazungumzo kuhusu suala hilo. Na hata hivyo mbona Zanzibar ikiwa ni Kanda au ikiwa ni Mkoa ina mambo ambayo hayako katika Kanda nyengine na Mikoa mengine iliyopo nchini Tanzania?”

*Makala ya mwandishi mkongwe wa Zanzibar, Ally Saleh, katika gazeti la Mwananchi, 30 Julai, 2008.

Kwa mara nyingine tena niko katika ulingo wangu wa makala ambapo kazi yangu kubwa ni kuchambua hali ya kisiasa inayojitokeza Zanzibar kila wiki. Na kwa wiki tatu mfululizo sasa suala kubwa ni moja tu.

Suala hilo ni lile linalotakana na matamshi ya Waziri Mku wa Tanzania, Mizengo Pinda aliyesema kuwa Zanzibar si nchi, lakini bila ya kuendelea kutoa maelezo mengine yoyote zaidi ya kusema kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania Zanzibar inatambulikana kuwa ni sehemu ya Tanzania.

Ila mpaka sasa si Pinda wala si mwengine yoyote aliyekwenda mbali ya hapo. Ni sawa, tuseme mathalan Zanzibar si nchi sasa ni kitu gani? Ni kanda kama kanda za Kaskazini, Kusini, Nyanda au nyenginezo? Au ni mkoa kama Manyara, Mtwara au Pwani?

Nionavyo mimi kusema kuwa Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya kuwa na jina la eneo hilo kiutawala ni utata katika hiyo Katiba ya Muungano na ndio mwanzo wa kuanza mazungumzo kuhusu suala hilo.

Na hata hivyo mbona Zanzibar ikiwa ni Kanda au ikiwa ni Mkoa ina mambo ambayo hayako katika Kanda nyengine na Mikoa mengine iliyopo nchini Tanzania?

Jee hii haifanyi Zanzibar kuwa na hadhi tofauti na Kanda au Mikoa hiyo? Bila ya shaka iko tofatui na kwa hivyo kwa nini kuna tofauti hiyo? Ni ya bahati mbaya au ya kukusudiwa?

Kama ni ya kukusudiwa athari yake ni ipi katika upana wa nchi ya Tanzania na kama ni ya bahati mbaya taathira yake ni ipi mbele ya macho ya nchi ya Tanzania?

Zanzibar imeungana na Tanganyika mwaka 1964 na Kanda ya Ziwa haikuungana na Zanzibar sawa na Mkoa mfano wa Tanga, jee Zanzibar itaweza kuwa sawa na Kanda ya Ziwa au Mkoa wa Tanga? Na kama kuna tofauti ni kwa nini ipo tofauti hiyo?

Jee kuna bahati mbaya au makusudio kabisa kuiachia Zanzibar kuwa na vyombo vya dola yaani Mahakama, Utawala na Baraza la Kutunga Sheria yaani Baraza la Wawakilishi? Na kwa kuwa na vyombo hivyo vya dola si Zanzibar imekuwa tofauti na Mkoa wa Shinyanga au Kanda ya Kaskazini?

Zanzibar imeruhusika kabisa kikatiba kuwa na alama zake za kidola. Ina Adam na Hawa, ina wimbo wa Taifa, ina bendera yake na ina Vikosi vyake? Kwa nini vitu vyote hivi vikaruhusiwa kuwepo?

Jee hii ni bahati mbaya tena au ni kitu kilichokusudiwa? Kama ni bahati mbaya mbona Rais wa Muungano anapokuja Zanzibar anapigiwa wimbo wa taifa wa Zanzibar na anasimama mbele ya bendera ya Zanzibar na anakagua Vikosi vya Zanzibar?

Rais wa Tanzania kwa kufanya hivyo hakuwa kwa hivyo akitambua kuwepo kwa mamlaka kiasi fulani ya Zanzibar na kwa hivyo kujua kuwa Zanzibar sio tu ina serikali yake kwa maana ya viongozi, lakini pia ni nchi ndani ya mfumo wa Tanzania ?

Katiba ya Zanzibar inasema wazi juu ya maeneo ya Zanzibar kwamba ni mipaka ile ile iliyokuwa imeunda Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kabla Muungano wa 1964. Na hii kwa fikra zangu ni uhakika wa kulinda mipaka ya Zanzibar kwamba haitazidi wala haitapunguzwa?

Jee uko Mkoa au Kanda ulioingia kwenye Muungano wa 1964 na ikiwa na utambulisho wa mipaka yake nje ya mipaka iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika kabla ya Muungano wa 1964?

Huu si ukweli kuwa wa kufananishwa na Zanzibar si mkoa wala si kanda bali ni Tangayika kwa ujumla wake kwa kuwa hiyo ndio ilioingia muungano na Zanzibar na kwa hivyo kama kulikuwa na Tanganyika iliyoyayeuka ndani ya Muungano na Zanzibar iliyobaki na mipaka yake na serikali na vyombo vyake vya dola hii si mantiki kuwa Zanzibar ni nchi ndani ya utaratibu wa Muungano?

Mfano mzuri ambao tunaweza kuutumia wa muungano unaoweza kubakisha nchi chini ya mfumo wa muungano ni pale Sudan na Misri zilipoungana au Senegal na Gambia zilipoungana na muungano wa nchi hizo ulipovunjika kila nchi ikachukua nchi yake kwa kuwa kila nchi ilibakisha nchi yake hata kama ziliungana.

Tunachoogopa kukisema wengi wetu na ambacho badhi yetu tunaweza kukisema, ni kuwa Muungano wetu umeundwa kwa neno lisemwalo ‘forever after’ yaani Muungano wa milele na ndio maana watu wakihoji wanaonekana ni wachochezi, wapinga muungano au wamekosa uzalendo.

Na hapa ndipo kosa kubwa lilipofanyika. Na ndipo wengi wakaja na dhana kuwa Muungano huu sio tu wa nchi mbili, bali nchi moja imeyayuka haraka baada ya Muungano na nyengine yake Zanzibar nayo inangepaswa kuyayeyuka na kubaki na nchi moja ya Tanzania.

Waznzibari wamelalamika juzi, jana na hata leo wataendelea kusema kuwa haikuwa ni matakwa yao kwa Tanganyika kuyeyuka ndani ya Muungano, na hilo kuwa limetokea Watanganyika wamlaumu Nyerere na wanaendelea kusema kuwa wao hawakubali Zanzibar yao kuyeyuka ndani ya Muungano.

Na huo ndio msingi wa hoja yangu ya leo. Kwamba Muungano una maeneo kadhaa yenye utata, ila hili la kuwa Zanzibar ni nchi ama si nchi ndio kwa sasa limepata umuhimu mkubwa kwa sasa ni la kisiasa.

Nasema tena kwa maoni yangu inawezekana Katiba inasema kama inavyosema, lakini hayo si matakwa ya Wazanzibari, na kama wadau wakuu katika Muungano huu hawataki kitu kwenye Muungano, ina maana ndio hawataki na Katiba kwa hivyo hairidhi matakwa ya wadau na kwa hivyo ni lazima ibadilishwe.

Haiwezekani baada ya Katiba kutolewa makosa kadhaa, baadhi ya watu wakitoa maoni kama hayo kwa miongo mwili sasa, lakini Serikali ya Tanzania na hata ile ya Zanzibar zikiwa wabishi kama mbogo, sasa leo ndio yanaonekana.

Kwa muda mrefu yamekuwa ni maoni ya wasomi na baadhi ya wanasiasa kuwa lazima kuwe na Mkutano wa Katiba ili kwayo kuzikabili changamoto za kikatiba zilizojitokeza kwa kuwa Muungano unakuwa, lakini Chama cha Mapinduzi imekuwa ikilipinga jambo hilo.

Leo tunaona jinsi viongozi wa CCM wa Tanzania Bara na Zanzibar wakitofautiana na juu ya suala hili hadhi ya Zanzibar katika Muungano na wengine wakidiriki kufuata mstari mmoja na maoni ya Wapinzani, Civic United Front.

Hoja yangu ni kuwa hatuwezi kuendelea kujidangaya na kusema kuwa mambo hayawezi kubadilika kwa kuwa yamesimama Kikatiba wakati Katiba yenyewe ina upungufu wa kila rangi na siku zote tukikataa kufanya mabadiliko ya kina lakini tukichagua kuziba viraka.

Sasa wa Wazanzibari hawajali Katiba anavyoisema au Pinda anasemaje. Na iseme isiemavyo au Pinda aseme asemavyo lakini vifungu vinavyokataa kuwa Zanzibar si nchi haviwezi kusimama kwa uhalali na matakwa ya wananchi.

Zanzibar ikiwa ni sehemu moja kamili ya Muungano, ambao ni wa pande mbili hairidhishwi na wala haitakubali kugeuzwa kuwa ni Kanda wala Mkoa katika Muungano wa Tanzania.

Na kwa hivyo Pinda anapaswa kujua kuwa wakati umefika hivi sasa kuwa kurudi katika kujadili upya Mkataba Mkuu wa Muungano tuanze upya kabisa kama Wazungu wanavyosema “to go back to drawing boards.”

Kama hatujafanya hivyo itakuwa Pinda leo na kesho itakuwa mwengine. Na yoyote awaye lakini ajue kuwa Zanzibar katika hili haitakubali kabisa kabisa, maana Wazanzibari kwa hakika wanaumwa na Uzanzibari wao.

Sijui kama Watanzania wengi wanajua, kwa Wazanzibari utambulisho wao unakuja kwa kutanguliza kwanza Uzanzibari halafu Utanzania, na kwa haya yanayotokea hilo litazidi kushika kani.

Matamshi ya Naibu Waziri Kiongozi Ali Juma Shamhuna; ya Waziri wa Nchi Hamza Hassan; ya Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Ali Mzee; ya Waziri wa Nishati Mansour Yusuf Himid kwa upande mmoja; na kwa upande wa pili Seif Shariff Hamad Katibu Mkuu wa CUF na ya Abubakar Khamis Bakar mkuu wa upinzani katika Baraza la Wawakilishi ni kielelezo tosha kuwa Wazanzibari hawataki nchi yao.

Katiba iseme isemavyo Zanzibar itabaki kuwa nchi na kuanzia sasa watapigania kwa nguvu zao zote ili Katiba iseme kuwa Zanzibar ni nchi. Zanzibar hawatakuwa wa kwanza kupigania kurudisha nchi hiyo hata iwapo ilikuwa imeptoeaLeave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.