Abeid Karume, mmoja wa waasisi wa Muungano.
Sheikh Abeid Amani Karume, mmoja wa waasisi wa Muungano.

MIMI si mmoja ya wale wanaoamini kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pale mwaka 1964 ulitokana na dhamira njema walizokuwanazo wale tunaowaona kuwa waasisi wake, Sheikh Abeid Karume wa Zanzibar na Mwalimu Julius Nyerere wa Tanganyika. Sikubali kwamba msukumo wa kuungana kwa nchi hizi ulikuwa ni hisia za umoja na udugu wa Afrika (pan-africanism). Na, kwa hakika, nakerwa sana na hoja kwamba Zanzibar iliuhitaji Muungano kwa sababu ya ulinzi na kujiimarisha kiuchumi. Yote hayo yalitumiliwa tu, lakini hazikuwa sababu hasa za kuutosa utaifa wa mataifa mawili hayo.

Moja ya mambo yanayoonesha ukosefu wa dhamira njema, ni zile jitihada za makusudi za kuififisha sura ya Tanganyika siku hadi siku katika Muungano huu kufikia hali ambapo sasa, sio tu kwamba wameifuta vitabuni, bali hata kwenye nafsi za watu, hata sasa imekuwa Watanganyika wote wanafikiri kama Watanzania tu. Na, kwa hakika, sio la kufikiri tu, bali pia wenyewe wanaukana Utanganyika wao. Hili limetufanya hata sisi tusio Watanganyika tujihisi vigumu kuwaita hivyo, labda iwe tunakusudia hasa kuwakera. Na kweli wanakereka sana!

Nina mifano miwili ya wazi. Karibuni nilikuwa kwenye boti pale bandarini Dar es Salaam, nayo ikawa inakaribia kuondoka; mara simu yangu ikaita na nikaipokea. Aliyenipigia akataka kujua niko wapi, na nikamjibu kwamba wakati huo nilikuwa napanda boti kuondoka Tanganyika kurudi kwetu Zanzibar. Unajua nilitazamwa vipi na wale walio karibu yangu, ambao wengi wao walikuwa ni Watanganyika?

“Kwani mpaka useme unatoka Tanganyika? Si useme unatoka Dar tu?” Mmoja wao, mwanajeshi mwenye magwanda, hakuweza kujizuia. “Kwani kuna ubaya gani kusema Tanganyika?” Nami nikamuuliza. “Nyinyi ndio munaoleta chokochoko nyinyi.” Akaanza vitisho vyake. “Za nini? Za kuiita Tanganyika, Tanganyika na Zanzibar, Zanzibar?” Naamini mwanajeshi yule alikuwa anataka kunichukulia hatua zaidi, lakini wenzake waliingilia kati na kubadilisha mazungumzo, na mimi nikapotea mbele ya macho yake.

Mfano mwengine wa kila mara ni hizi sherehe za uhuru wa Disemba 9, 1961, ambapo hutangazwa kwamba panasherehekewa uhuru wa Tanzania. Lakini tarehe hiyo Tanzania ilikuwa bado haijazaliwa. Hata katika tukio hilo la kihistoria, husikii Tanganyika ikitajwa. Aliyewaita Watanganyika ‘wadanganyika’ aliwapatia kwa mengi.

Hapa chuoni pia ninao. Wasomi wanachukua digrii na bado hawataki kujiaminisha kwamba wao ni Watanganyika, ingawa mimi wananiita Mzanzibari. Ninapowauliza msingi wa mimi kuwa Mzanzibari ni upi hata wao wasiwe Watanganyika, wananiambia kwamba Tanganyika ilikufa mwaka 1964 ilipounganishwa na Zanzibar, lakini Zanzibar haikufa! Jibu lililotayarishwa na kutetewa kwa miaka 44 sasa. Hata kama limechoka na kuchosha, wanaolitoa hawana upeo wa kuona hilo. Kwao ni ‘man-qaalal balozi, huwa muwafaqa.’ Yes, boss, wasemavyo Waingereza. Madhali hivyo ndivyo Nyerere alivyosema, itakuwa hivyo milele na milele. Hiki ndicho kiwango alichofanikiwa Nyerere – kuwalisha wenziwe mzugo.

Nyerere anatambuliwa kama Baba wa Taifa huku. Taifa lipi? Tanzania. Lakini kwa nini kama ni ubaba, usiwe kwa Karume pia, ambaye ndiye muasisi mwenzake wa Muungano huu uliozaa Tanzania. Nyerere anatambulika pia kama kielelezo cha ushujaa, uhuru na mshikamano. Ushujaa, uhuru na mshikamano upi, ukiuliza, utajibiwa Muungano. Kwa hivyo, ikiwa kuna lolote, basi Nyerere aliutumia Muungano kujijenga yeye binafsi, na sio kujituma yeye kuujenga Muungano wa kweli.

Turudi kwenye Tanganyika. Tangu mwanzo kabisa, Nyerere alikuwa anajuwa anachokifanya katika suala hili la kizungumkuti cha Muungano. Alijuwa kwamba kwa kulififilisha jina tu la Tanganyika, alikuwa hauuwi wala kuuzika utambulisho wa Tanganyika. Na sio tu kwamba alijuwa kwamba hafanyi hivyo, bali pia hakutaka iwe hivyo. Alichokuwa akikitafuta ni kile kielezwacho kwenye nyimbo moja ya kikwetu:

Msegeju yuna ng’ombe
N
g’ombeze
Nami n’na ng’ombe wangu
Anambia tuchanganye
S
itaki
Kwaheri nakwenda zangu

Hadithi ya nyimbo hii ni kwamba, kulikuwa na wachugaji wawili wa ng’ombe: mmoja (mwimbaji) alikuwa na ng’ombe mmoja tu na mwengine (Msegeju) alikuwa na kundi kubwa la ng’ombe. Lakini pamoja na kuwa na kundi hilo kubwa, bado Msegeju alimtaka (kwa kumlazimisha) mwimbaji wachanganye ng’ombe wao. Mwenzake ndipo akaimba kwa malalamiko kwamba anatenzwa nguvu kumchanganya ng’ombe wake mmoja kwenye kundi lile kubwa, naye jambo hilo hakulitaka. Akihofia kuja kumpoteza ng’ombe wake mmoja kwenye kundi kubwa la mwenzake, akaamua kuaga: “kwa heri nakwenda zangu!”

Msegeju ni Nyerere. Karume ndiye mwimbaji mwenye ng’ombe mmoja. Lakini bahati mbaya ni kwamba yeye, Karume, alipotakiwa na Nyerere kuchanganya ng’ombe, alikubali kumuingiza ng’ombe wake mmoja kwenye kundi kubwa la Nyerere. Bahati mbaya zaidi, kama alivyohofia mwimbaji, Karume naye akafa hajaweza kumuengua ng’ombe huyo kutoka kundi lile wala kufaidika naye, ingawa kila mara alilalamika. Wakati Karume alipoaga kwenda zake, yule ng’ombe alimuacha mule mule kundini. Lakini lile kundi akaliwacha mikononi mwa Nyerere. Sasa ng’ombe wa Karume ni wa Nyerere.

Mzee wangu, Arham Ali Nabwa, alikuwa akikuita huku ndiko ‘kufa dungu msooni.’ Msemo maarufu kwenye mchezo wa kitoto wa gololi, ambapo aliyekufa dungu msooni, hulazimika kutoka mchezoni akiwa amepoteza kila kitu na pia kutakiwa alizokula mwanzo azitowe. Akaondoka pangu pakavu, keshabunwa, kwa lugha ya kitoto.

Kwa miaka yote hii 44 ya Muungano, habari imekuwa ndiyo hiyo. Kwa jina la Tanzania, Tanganyika imeendelea kuhuika, na kwa jina la Muungano, Zanzibar imezidi kufa. Sasa, kwa kuwa Tanganyika imeambiwa haipo, basi Zanzibar imekosa mshirika wa kuongea naye matatizo ya Muungano, kwani anayewakilisha Tanganyika hivi sasa ni huo huo Muungano.

Lakini kimsingi, wakati Muungano unasainiwa, haikuwa dhamira (angalau ya Karume) kupoteza kila kitu. Kwa hakika, mnasaba wa Mkataba wa Muungano unaonesha kwamba palikusudiwa kuwepo kwa mamlaka tatu: ya Zanzibar, ya Tanganyika na ya Muungano. Hivyo ndivyo muundo ulivyokusudiwa uwe. Kwamba hautekelezwi hivyo, hilo ni suala jengine.

Na kwa nini muundo huu hautekelezwi? Ni kwa sababu tangu mwanzoni kabisa palikuwa na dhamira mbaya ya kisiasa kwa upande wa Tanganyika, ambayo ilikusudia hasa kuikalia Zanzibar kwa gharama yoyote iliyostahili. Kwa hivyo, kama nilivyotangulia kusema, Muungano huu tulionao haukuchimbukia kwenye nia njema kama tunavyoambiwa.

Lakini kwa nini palikuwa na dhamira mbaya? Kuna sababu zaidi ya moja, hapa nitazitaja tatu. Kwanza, dhamira ya Muungano huu ilikuwa ni kuitumilia Zanzibar kiuchumi. Hadi tunapata uhuru wa Disemba 1963 na kufanya Mapinduzi ya 1964, Zanzibar ilikuwa miongoni mwa nchi zilizokuwa zimeendelea sana. Tanganyika waliopata uhuru miaka 3 kabla yetu, walikuwa katika hali ngumu kiuchumi.

Kwa nafasi yake ya kijiografia, Zanzibar ni mlango wa kuingilia na kutokea katika soko kubwa la Afrika ya Mashariki. Kwa nafasi yake ya kihisoria, Zanzibar ni kituo cha usambazaji. Nyerere alikihitaji kituo hiki kuiendeleza Tanganyika yake.

Ni bahati mbaya sana kwamba hakuwa na ujanja wa kutosha kuweza kutumia fursa hiyo ya kiuchumi iliyonayo Zanzibar kwa miaka 20 ya utawala wake badala yake akazifanya zote mbili, Tanganyika na Zanzibar, kuwa masikini zaidi kuliko alivyozikuta. Ujamaa wake ulikuwa ni kuugawa umasikini kwa watu wote na sio kuugawa utajiri.

Pili ni kuitumilia Zanzibar kujijenga kisiasa. Tanganyika ilihitaji kujitanua na Nyerere alihitaji sifa ya kuonekana mwanasiasa wa Kiafrika anayethubutu. Kuitwaa Zanzibar ilikuwa hobi yake hata kabla ya Uhuru wa Tanganyika wa 1961. Mara nyingi alikuwa amesema kwamba hakuwa tayari kuwa na jirani wa Kiarabu na Kiislam mlangoni pake. Aliumwa na hilo na kuichukua Zanzibar hata halikuwa suala la kufikiria mara mbili.

Zile hadithi alizokuwa akizitoa Nyerere kwamba ni Karume ndiye aliyeshauri waungane, na kisha kumuambia kuwa yeye Nyerere awe Rais na yeye Karume awe makamu, zina shaka sana. Karume alivyokuwa akiupenda ukubwa, haingii akilini kwamba aliutoa sadaka uraisi wake kiasi hicho. Hadithi hizo alizisema wakati Karume keshakufa. Alijua kuwa kwa adabu za Karume zilizvyokuwa nyingi, angeliweza kulikanusha hilo mbele za watu tena hata bila kumsubiri amalize. “Julius, msalie Mtume, bwana!” Karume baba aliweza na alikuwa na uthubutu huo.

Sababu ya nne iliyo nyuma ya Muungano huu ni ya kidini, ambayo ilichochewa sana na Uingereza, ambayo inalaumiwa kuyawezesha Mapinduzi ya 1964; lakini ikawa na tahadhari kuelekea Muungano ikihofia kwamba athari ya Uislamu iliyoko Zanzibar ingelikuwa imepata jukwaa lake Tanganyika kama ingelikuwa nchi moja.

Lakini katika mtindo wa kutumiliana, Nyerere akashinda ushawishi wake wa kuonesha kwamba Zanzibar kuna ‘makomunisti’ ambayo kuyadhibiti kulihitaji kuiingiza katika makucha yake. Akasaidiwa katika hilo na likawa kama lilivyokuwa na leo ndio huu Muungano tulionao.

Sababu hii inaogopwa sana kutajwa kwa kuwa siasa za leo za kilimwengu zimefanikisha kuubatiza Uislamu jina la ugaidi. Wengi wa wanaojiita wasomi, au watu walioendelea, hawataki kujihusisha na Uislam wala kuuhusisha Uislam na Uzanzibari. Mimi si mmoja wao. Nisiwe msomi wala mtu niliyeendelea, lakini nitasema kwamba chuki za Nyerere dhidi ya Zanzibar zilichangiwa pia na imani yake ya kidini. Nyerere hakuupenda Uislamu na aliwachukia Waislamu. Hata historia ya kwao, Tanganyika, inaonesha hivyo.

Soma kitabu cha Mohammed Said, Maisha ya Abdulwahid Sykes, ikiwa unataka ushahidi madhubuti. Waingereza pia, tangu mwanzoni mwa karne ya 14 wamekuwa na vita maalum dhidi ya Uislamu na Waislamu. Zanzibar kilikuwa kitovu cha Uislamu kwa ukanda huu wa Afrika. Ilikuwa lazima kidhibitiwe kwa namna yoyote ile.

Kwa hivyo, hata kama Waingereza hawakufikia upeo mkubwa zaidi wa kuitosa Zanzibar, lakini angalau walifanikiwa kuichora vibaya historia ya Visiwa hivi kwa kutumia ukabila, na kisha wakazunguka kwa mlango wa nyuma kusaidia kufanikishwa kwa Mapinduzi ya 1964 na hatimaye ndio Muungano ukaja.

Kwa haya yote, bado kuna sababu ya kutufanya tuamini dhamira njema nyuma ya Muungano huu? Na kama, shaka yetu ni ya kweli, basi kwa nini iwe sawa kuutangaza Muungano huu kuwa ni batili tangu kwenye msingoi wake kabisa? Kama hilo ni gumu, kwa nini Mkataba wa Muungano usiwekwe hadharani ukajadiliwa upya na pande zote mbili kiadilifu? Kama hilo pia haliwezekani, kuna ubaya gani kuuitisha sasa kura ya maoni kuwauliza wananchi wa Zanzibar wanachokitaka kwenye Muungano huu?

Kama yote haya hayawezekani kwa kuwa hayatakiwi na watawala, kwa nini Mzanzibari kama mimi nisihitimishe kuwa nchi yangu haimo kwenye Muungano na nchi mwenzake, bali ni mahmiya ya kijeshi, na inakaliwa kimabavu na dola ya kigeni?

One thought on “Muungano na ajenda ya siri dhidi ya Zanzibar”

  1. ASSALLAM ALLAYKUM ?
    MASHALLAH ; JAMANI TUPO PAMOJA KWA LOLOTE KUITOA ZANZIBAR KATIKA UKOLONI WA TANGANYIKA

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.