Na Mohammed Ghassani

 

Makamo wa Rais, Dkt. Ali Mohammed Shein, akikagua bucha la nyama ya ng'ombe sokoni Buguruni, jijini Dar es Salaam. Dk. Shein amepatiwa nafasi hiyo kutekeleza sharti la kwamba Makamo lazima awe Mzanzibari lakini hana nguvu hasa za kusimamia malahi ya Zanzibar kwenye Muungano. Matokeo yake, hutumia muda wake mwingi kushughulika na mambo ya Mazingira na shughuli za kijamii akiwa Dar es Salaam badala ya kushughulikia nafasi na maslahi ya Zanzibar kwenye Muungano. Hili lilikuwa changa jengine la macho kwa Wazanzibari.
Makamo wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein, akikagua bucha la nyama ya ng'ombe sokoni Buguruni, jijini Dar es Salaam. Dk. Shein amepatiwa nafasi hiyo kutekeleza sharti la kwamba Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lazima awe Mzanzibari, lakini ukweli ni kwamba Makamo huyu hana nguvu hasa za kusimamia maslahi ya Zanzibar kwenye Muungano. Matokeo yake, Dk. Shein amekuwa akitumia muda wake mwingi kushughulika na mambo ya Mazingira na shughuli za kijamii akiwa Dar es Salaam badala ya kushughulikia nafasi na maslahi ya Zanzibar kwenye Muungano. Hili lilikuwa 'changa jengine la macho' kwa Wazanzibari.

Lilifanyika kosa kubwa kuutangaza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar bila ya kwanza kuweka Katiba ya kuusimamia Muungano huo. Kwa maneno ya Arham Ali Nabwa, viongozi wa Muungano huu walitanguliza gari kabla ya farasi; na hilo limekuwa jambo linalotugharimu sasa kisiasa.

 

Wala jambo hili lisingekuwa na gharama kubwa kama hii ikiwa dhamira ya Muungano huu ilikuwa njema tangu mwanzoni. Mimi ni katika wale wanaohoji kwamba hapakuwa na dhamira njema kutoka kwa viongozi wa Muungano, hasa wa upande wa Tanganyika wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere.

 

Ndiye yeye aliyefanya kwamba hata pale ilipong’amuliwa pameshafanyika kosa, iwe ni shida kulirekebisha kosa hilo, kwani alilazimisha iwe ni dhambi kuhoji vipengele vya Katiba au utekelezaji wake, akiamini kwamba kufanya hivyo ni kuuhatarisha Muungano alioutaka yeye. Hili la Muungano alioutaka Nyerere ni la muhimu sana, kwani inaonekana wazi kwamba baina yake na mwasisi mwenzake, Sheikh Abeid Karume wa Zanzibar, palikuwa na sura tafauti za vipi Muungano huu ulitakiwa uwe.

Basi Nyerere akamburuza na kumbiruza mwenzake (na wengine sote, bila shaka) kwa makusudi. Ikawa haramu kuhoji na ikawa uhaini kuonesha kosa la Muungano. Na kwa kufanya hivyo, akawa anayafanya matatizo ya Muungano yazidi kujilimbikiza na kuzaliana huku yeye akizidisha kuongeza orodha ya mambo ya Muungano kutimiza azma ya kuidhibiti Zanzibar na ndoto za kuimarisha Muungano. Kumbe ilikuwa sivyo.

 

Naomba kutumia makala hii kuonesha kosa moja lililofanywa kwa makusudi ndani ya Katiba ya Muungano na ambalo sasa tunaamini kwamba lazima lirejelewe upya na kurekebishwa; nalo ni lile la kumuondoshea Rais wa Zanzibar nafasi yake ya kuwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Hoja yangu ni kwamba, kwa vile utaratibu haukufuatwa, na kwa kuwa Mkataba wa Muungano ndio sheria ya msingi ya Muungano (kuliko hata Katiba ya 1977), basi bado Rais wa Zanzibar ni Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Cha kufanyika sasa ni kutangazwa hilo rasmi Bungeni, au vyenginevyo ni kwa Zanzibar kwenda mahakamani.

 

Lakini wapi lilichimbukia suala la kumuondoa Rais wa Zanzibar kwenye nafasi hiyo? Chimbuko la jambo hili ni ile tume ya Jaji Mark Bomani ya mwaka 1992 iliyoundwa kuipitia Katiba ya Muungano ili kukidhi matakwa ya mfumo wa vyama vingi vilivyoanzishwa tena mwaka huo.

 

Katika taarifa yake ya Agosti 1992, Tume ya Jaji Bomani ilipendekeza jambo hili la ajabu: “Kuwe na Makamu wa Rais mmoja tu badala ya wawili na achaguliwe kwa cheo hicho. Mgombea wa Makamu wa Rais kwa kila chama cha siasa kilichoingia kwenye uchaguzi asimame kama mgombea mwenza wa mgombea wa urais kutoka chama chake na wapigiwe kura kwa pamoja. Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu wa Muungano wasishike wakati huo huo wadhifa wa Makamu wa Rais. Kuwe na Baraza la Dola (Council of State) linalojumuisha Rais wa Muungano, Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi wa Zanzibar.”

 

Akina Jaji Bomani, wenyewe wakiwa mang’weng’we wa Chama cha Mapinduzi (CCM), waliona kwamba kulikuwa na uwezekano wa Rais wa Muungano na yule wa Zanzibar kutoka katika vyama tofauti, maana dalili za chama cha upinzani, Chama cha Wananchi (CUF), kuchukua madaraka Zanzibar zilikuwa wazi.

 

Lakini wenyewe wakatoa sababu za kimaandishi kwamba kuwa na maraisi wawili kutoka vyama tafauti kungeliweza kuleta mgongano wa mawazo baina ya Rais wa Jamhuri ya Muungano na msaidizi wake (Rais wa Zanzibar). Pia wakasema kwa vile Rais wa Zanzibar hachaguliwi na Watanzania wote, basi haitokuwa sawa kwake kurithi uongozi wa Muungano pindi ikitokea sababu ya Rais wa Muungano kushindwa kufanya kazi zake (kama vile kufariki).

 

Kuna kumbukumbu kwamba mapendekezo haya ya Tume ya Jaji Bomani yaliwasilishwa kwa serikali zote mbili, yaani ile ya Muungano na ya Zanzibar, yajadiliwe na kwa pamoja zije na rasimu ya mswaada wa mwisho kupelekwa Bungeni. Lakini hakuna rekodi kwamba jambo hili liliafikiwa na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar (BLM), ambalo lilikuwa na hoja zake.

 

BLM lilisema kwamba Mkataba wa Muungano (Articles of Union), 1964, ndio msingi wa kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar na inaelezwa kinagaubaga katika mkataba huo kwamba “mmoja wa Makamu wa Rais atakuwa mtu ambaye kwa kawaida makaazi yake yatakuwa Zanzibar na Makamu wa Rais huyo kuwa msaidizi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika kutekeleza majukumu yake ya uongozi kwa upande wa Zanzibar na, kwa hadhi ya Rais wa Zanzibar, atakuwa kinara wa uongozi wa Zanzibar.”(sehemu 5-(1) (c) ya sheria ya kuidhinisha Makubaliano ya Muungano baina ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika, 1964 na kifungu 9(a) (1) ya Sheria za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, 1964).

 

Labda tukumbushane kuwa mantiki ya kuwa na kifungu kama hiki kwenye Mkataba wa Muungano ni ule ukweli kwamba Rais wa Zanzibar ndiye mwenye jukumu la kusimamia madaraka ya Zanzibar, na kwa kuwa baadhi ya madaraka hayo yametolewa na kuingizwa kwenye Muungano, basi ni yeye tu aliyeidhinishwa na Wazanzibari kuyalinda madaraka hayo.

 

Aidha Jaji Bomani na wenzake walipitikiwa kwamba sio tu kwamba Zanzibar iliingia kwenye Muungano kama nchi kamili, bali pia kama taifa na dola huru, au walifanya kwa makusudi kupendekeza jambo ambalo lilimaanisha hasa kuinyima Zanzibar nafasi yake kwenye Muungano.

 

Ipi ikawa hoja ya BLM katika hili? BLM lilihoji kwamba suala halikuwa Mzanzibari tu ndiye wa kuwakilisha maslahi ya Zanzibar katika Muungano, bali suala ni kuwapo pale kiongozi wa utawala wa Zanzibar ambaye atahakikisha uendelezaji wa madaraka ya utawala huo. Sababu kuu, BLM likasema, ni kwamba wakati Zanzibar inaingia kwenye Muungano, haikusalimisha utaifa wake wote (ama kwa kutumia lugha ya Arham Nabwa, “Zanzibar haikusalimisha kutoka kofia hadi makubadhi), bali ilichangiana tu sehemu fulani ya utaifa huo na mwenzake katika Muungano, yaani Tanganyika.

 

Na hadi hapo, wala BLM halikuwa linaogopeshwa na ukweli kwamba Zanzibar ingeweza kutawaliwa na chama tafauti na kile kinachotawala Serikali ya Muungano. Kwa BLM, khofu hiyo haikuwa na msingi maana liliona kwamba, madhali tumekubali mfumo wa vyama vingi, lazima pia tukubali kuwa huenda vyama vinavyopingana vikashika madaraka kwa wakati mmoja katika maeneo tafauti ya Muungano. Lakini pia inawezekana hata ndani ya eneo moja, vyama tafauti vikawa vimeshikilia mihimili ya utawama, kama vile kuwa na Rais wa Zanzibar kutoka lakini Baraza la Wawakilishi kuwa na wajumbe wengi kutoka CUF. BLM haikuona kuwa ushindani wa kisiasa ni uadui, bali ni namna tu ya kuliendeleza na kulisimamia taifa.

 

Lakini kulikuwa na sababu zaidi ya kulikataa pendekezo hili la kumuengua Rais wa Zanzibar kutoka nafasi yake ya umakamu wa Rais wa Muungano. Kuwa na makamu wa Rais ambaye hachaguliwi moja kwa moja bali anayebebwa tu na mgombea uraisi ni sawa na kuwa tarishi. Huyu hawezi kabisa kuwa msemaji wa Wazanzibari kwenye masuala ya Muungano, bali atakuwa mtu anayesubiri kuamrishwa tu la kufanya na Raia wake.

 

Nini basi kilichopendekezwa na BLM? Ikiwa ni lazima kuwa na mgombea mwenza kwenye nafasi ya uraisi wa Muungano, basi mgombea huyo awe ni yule yule mtu aliyekwishapendekezwa na chama chake kugombea nafasi ya uraisi wa Zanzibar. Hili likawa jambo gumu zaidi kukubalika na upande wa pili wa Muungano, hasa walipofikiria kwamba, kwa upande wa CUF, mtu huyo ilimaanisha Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye taarifa zote za Intelligence ya nchi zilishaonesha kuwa angelishinda uraisi wa Zanzibar kwa kura. Ikasadifu pia kwamba wakati huo kulikuwa na suala la Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislam (OIC) na madai ya kundi la akina Samuel Sitta na Philip Marmo ya serikali ya Tanganyika.

 

Alimradi mambo yalichanganyika (au yalichanganywa kwa makusudi) hata ikafikia mahala mapendekezo haya hayakufika Bungeni. Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa wakati ule, John Malecela, alitoa tamko katika Bunge Februari 1993 kwamba suala la Makamu wa Rais litajadiliwa kwa undani na pande mbili za Muungano na Mswada wa Sheria  kupelekwa  Bungeni, Februari 1995. Ukweli ni kuwa hakukuwahi kuwepo na mazungumzo ya pamoja ya serikali mbili kuhusiana na jambo hilo hadi leo. Isipokuwa katika mwezi Oktoba 1994, Rais wa Zanzibar wa wakati huo, Dk. Salmin Amour, akatakiwa kutoa kibali cha kuridhia jambo hilo, lakini naye akagoma akisema kwamba kimsingi ni BLM ndilo lenye mamlaka hayo kwa vile ndilo lililopitisha Mkataba wa Muungano.

 

Rekodi zinaonesha kuwa mkutano ule aliouahidi Malecela Februari 1993 Bungeni ulikuja ukafanyika Novemba 21, 1994 kwa njia ya zimamoto. Ilikuwa zimamoto kwa kuwa zilikuwa ni dakika za lala salama kabla ya Mswaada wa Marekebisho ya 11 ya Katiba haujapelekwa Bungeni. Hata hivyo, katika kikao hicho cha hadi usiku wa manane, upinzani wa Zanzibar ulikuwepo pale pale na hatimaye ikakubalika kuwa “Rais wa Zanzibar anaweza kuwa Makamu wa Rais.” Ikatayarishwa rasimu kwa mazingatio ya Kamati ya Sheria na Masuala ya Katiba ya Bunge.

 

Lakini kumbe hadi hapo kulikuwa ni kuchezewa shere tu kwa Wazanzibari, kwani mara baada ya wao kuondoka, msimamo ukawa ni ule ule: Rais wa Zanzibar hawezi kuwa Makamo wa Rais na kama anataka kusimama kwa wadhifa huo basi kwanza ajiuzulu uraisi wa Zanzibar. Habari ilipoifikia SMZ, ikashauri kwamba muda ulikuwa hautoshi tena kwa mjadala zaidi, kwa hivyo jambo hilo liakhirishwe hadi hapo siku za baadaye. Malecela, kwa kisingizio kwamba alikwishaliahidi Bunge kwamba katika kikao cha safari ile angelikwenda na mswaada huo, akaupeleka mswada Bungeni. Hadi hapo ilikuwa tayari utaratibu umeshakiukwa, maana kwa vile suala hili lilikuwa linakuja kubadilisha kabisa mfumo wa utawala wa Serikali ya Muungano, maoni ya Rais wa Zanzibar yalikuwa lazima yazingatiwe.

 

Na bado hata humo Bungeni mwenyewe utaratibu ukazidi kukiukwa. Kifungu 98-(1) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kinasema kwamba “Bunge linaweza kupitia sheria kubadilisha kifungu chochote cha katiba  hii iwapo utaratibu ufuatao utazingatiwa:

 

“(b)Mswada wa sheria kubadili vifungu vyovyote vya katiba hii au vifungu vyovyote  vya sheria yoyote  inayohusiana na mambo ya  sehemu II ya nyongeza ya pili ya katiba hii, hautapitishwa  na Bunge isipokuwa kama umeungwa mkono na kura zisizopunguwa thuluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Bara na si chini ya thuluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Zanzibar.”

 

Rekodi zinaonesha kuwa wajumbe wa Zanzibar katika Bunge siku ya kupitishwa kwa Mswaada wa Marekebisho ya 11 ya Katiba walikuwa hawafiki idadi inayotakiwa na sheria. Inasemekana kuwa Spika wa wakati huo, Pius Msekwa, licha ya kuwa kwake mwanasheria kitaaluma, aliamua kuidharau sheria na kufuata zaidi matakwa ya kisiasa na hivyo kuamuru kura zipigwe kwa kuzingatia wingi wa kura za wabunge wote.

 

Hii maana yake ni nini? Ni kwamba Marekebisho haya ya 11 ambayo yamefanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa utawala wa Jamhuri ya Muungano, hayakupitishwa kwa taratibu za kisheria. Hivyo sheria hiyo ni batili, na kwa hivyo hoja yangu ni ile ile: kwamba, kwanza, kwa kuwa utaratibu haukufuatwa, na pili, kwa kuwa Mkataba wa Muungano ndio sheria ya msingi ya Muungano (kuliko hata Katiba ya 1977), basi, tatu, bado Rais wa Zanzibar ni Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Cha kufanyika sasa ni kutangazwa hilo rasmi Bungeni, au vyenginevyo ni kwa Zanzibar kwenda mahakamani.

 

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.