Baada ya Wazanzibari kujitokeza kupingana na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda iliyoitangaza Zanzibar si nchi, mtazamo wa jumla kutoka upande mwengine wa Muungano huu, yaani Tanganyika, umekuwa wa kihasama zaidi. Umekuwa ni wa kuwakumbusha Wazanzibari ule msemo wa kale wa Kiengereza: you can not eat your cake and have it. Ukipitia magazeti mbali mbali yanayochapishwa hapa Dar es Salaam ndani ya kipindi hiki, utasikia muakisiko wa sauti hiyo.

Mwansheria Mkuu wa Zanzibar, Iddi Pandu Hassan. Kauli yake ya kupinga kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ilikuwa madhubuti, lakini ameshindwa kuisimamia
Mwansheria Mkuu wa Zanzibar, Iddi Pandu Hassan. Kauli yake ya kupinga kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ilikuwa madhubuti, lakini ameshindwa kuisimamia

Wazanzibari tunasutwa na ndugu zetu hawa wa damu kuwa tumeikuza mno kauli hiyo kiasi ya kupotosha kabisa kile ‘hasa’ alichokikusudia Waziri Mkuu Pinda. Tunatishwa kwamba kujaribu kuhalalisha unchi wa Zanzibar ni kuhatarisha Muungano; na wito wa kudhibitiwa umeshatolewa!

Tumekumbushwa tena kuwa hatuwezi kuizungumzia Zanzibar kama nchi, huku tukijuwa kuwa ilijiingiza kwa hiari yake kwenye Muungano. Hatuwezi kuzungumzia Zanzibar yenye nguvu zaidi ya hivi ilivyo, halafu wakati huo huo tukasema sisi ni waumini wa Muungano huo. Tunaambiwa, sio tu kwamba kufanya hivyo ni kwenda kinyume na Katiba, bali pia ni upuuzi wa kuila keki na bado tukataka tubakie nayo!

Ufupi wa maneno ni kwamba, kwa mara nyengine tena Wazanzibari tunagombezwa kwamba tuna ubaya na Muungano huu; na wagombezi wetu ni wale wale, ndugu zetu wa damu, ’wenye’ mapenzi makubwa na Muungano wetu ’wa kupigiwa mfano.’

Makala yangu iliyotangulia kuhusu kadhia hii, labda ilionekana kumuunga mkono Pinda na ilipingana na Mwanasheria wa Zanzibar, Idi Pandu. Kupatia kwa Pinda na kukosea kwa Pandu, kote kuwili, kulikuwa ni kwa kuinukuu Katiba. Lakini vipi ikiwa Katiba yenyewe imekosea? Vipi ikiwa Katiba yenyewe imekiuka msingi wa makubaliano ya kuandikwa kwake? Ukatiba wa Katiba hiyo unasimamia wapi?

Mimi si mwanasheria, lakini hoja ya siku nyingi ya kisheria kwa upande wa Zanzibar ni kwamba mara nyingi Mkataba wa Muungano umekuwa ukivunjwa kwa makusudi ili kutoa fursa ya kuongeza mambo kwenye orodha ya Mambo ya Muungano, nyongeza ambayo kwa makusudi imekuwa ikiila hadhi ya Zanzibar. Mfano wa hilo ni lile la kumfuta Rais wa Zanzibar kuwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kama yalivyo matakwa ya Mkataba wa Muungano.

Kwa hivyo, kulijibu suto la ndugu zetu hawa wa damu ni kwamba, tukubali kurudi kwenye msingi uliounda Katiba yenyewe, Mkataba wa Muungano, ikiwa kweli tunataka kujenga nguvu ya hoja, maana tayari Katiba imeonekana kuwa binafsi ni hoja ya nguvu. Ni nadra kusikia Mkataba huu ukitajwa, badala yake mara zote wakitaka kuwazuilia Wazanzibari kuisemea nchi yao huenda katika Katiba, ambayo wanajua vyema kwamba wameichezea na kuikoroga vya kutosha kuweza kuhalalisha dhamira yao dhidi ya Zanzibar.

Ni kwenye Mkataba ndiko tutakakogundua kwamba ni kweli kuwa muundo na utendaji kazi wa sasa wa Muungano huu unadhihirisha ukweli tafauti na hiyo methali ya Kiengereza wanayotumia kutusutia; nao ni uwezekano wa mmoja kuila keki yake na kuendelea kubakia nayo, huku mwengine kutokuila lakini asiwe nayo. Tanganyika imeila lakini bado imebaki nayo, Zanzibar haikuila na hainayo!

Kwa hakika, hata hizi kelele unazozisikia hivi sasa kutoka pande zote mbili zinathibitisha ukweli huo huo tu. Waliopoteza keki yao bila kuila wameshtuka sasa na walioila keki na kubakia nayo wana khofu kwamba sasa wameshagundulika. Na kwa umri wote wa keki hii, kila yule aliyepoteza keki yake anapofanya jitihada za kujipatia sehemu fulani ya keki hiyo, mlaji keki hakubaliani na hilo. Badala zake, zaidi ya mara kumi na moja, mlaji keki ameshayaendea kinyume au kuyavunja makubaliano ya mapishi ya keki yao kwa kisingizio cha kuyaimarisha mapishi hayo!

Waziri Mkuu Pinda: Zanzibar si nchi
Waziri Mkuu Pinda: Zanzibar si nchi

Tusiwe wanafasihi sana katika hili tukatumia maneno ya mafumbo. Ninachosema wazi ni kuwa Makubaliano ya Muungano ndiyo msingi na sehemu muhimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kuyavunja Makubaliano hayo haimaanishi tu kuvunja Katiba, ambayo imejengwa juu ya Makubaliano hayo, bali pia ni kuwatovukia adabu Watanganyika na Wazanzibari wote, kwa ujumla wao. Na hilo ndilo ambalo limekuwa likitendeka kwa muda wote huu: tumekuwa tukikosewa adabu. Hakuna anayehatarisha Muungano huu wala anayevunja Katiba zaidi ya yule anayetumia nguvu zake kuyavunja Makubaliano ya Muungano!

Mkataba wa Makubaliano hayo ulisainiwa na waasisi wake ukiwa na vipengele kumi na moja tu, leo hii vipengele hivyo ni zaidi ya ishirini na mbili, ikimaanisha kuwa vimeongezeka kwa zaidi ya asilimia mia moja, tena huku kila nyongeza ikiingizwa kuipotezea Zanzibar nguvu na hadhi yake kwa makusudi. Hili ndilo linalotufanya sisi Wazanzibari kuziangalia siasa zilizouzunguka Muungano huu kwa mashaka kwamba zinailazimisha Zanzibar iendelee kupoteza kadiri Muungano huu ‘unavyoimarika.’ Na kupoteza huko si kwa kuridhika, bali kulazimishwa tu. Na kulazimishwa hakujaanza leo na Waziri Mkuu Pinda tu, bali mtu wa mwanzo kufanya hayo alikuwa ni Mwalimu Nyerere mwenyewe, ambaye kimsingi angelitarajiwa kuyaheshimu makubaliano baina ya Tanganyika na Zanzibar na sio kuyakengeuka, kwa kuwa ni mwasisi wa Muungano huu.

Nitatoa mfano. Tunajua kuwa Makubaliano ya Muungano yaliwaweka wazi washirika wa Muungano huu kuwa ni Tanganyika na Zanzibar. Hatua zilizofuatia hapo zilitakiwa kuwahakikishia washirika hao uwezo sawa katika maamuzi. Uwepo na uwezo huo ungelidhihirika kwa washirika hawa kuwa na kauli sawa wakati wa kufanya maamuzi, katika kutafuta suluhisho la matatizo na pia kuwa na fursa sawa ya kuzijadili, kuzitunga na kuzipitisha sheria zinazohusu mambo ya Muungano kitaifa na kimataifa. Lakini nini alikifanya Mwalimu Nyerere? Ndani ya mwezi mmoja tu, baada ya kutiwa saini kwa Makubaliano ya Muungano, alianza kuipopotowa Zanzibar kwa kutunga sheria ya kuzibatiza jina la Muungano shughuli zote za Tanganyika ambazo hazikuwa katika yale mambo 11 ya Muungano.

Kati ya sheria hizi ni ile iliyoitwa The Transitional Provision Decree (N0. 1) ya mwaka 1964, ambayo iliwapa uhamisho wafanyakazi wote wa serikali ya Tangayika na kuwa wa serikali ya Muungano. Kwa sheria hii, ndio Mahkama kuu ya Tanganyika ikafanywa kuwa Mahkama Kuu ya Tanzania. Sheria hiyo ilichapishwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 01.05.1964.

Wiki mbili baada ya hapo, yaani tarehe 15.05.1964, akachapisha sheria nyengine iliyoitwa The Transitional Provision Decree (No. 2) ambayo ilielekeza kuwa kila pale penye neno au kumbukumbu inayosomeka Tanganyika sasa pasomeke Serikali ya Muungano wa Tanzania.

Ni vipi sheria hizi mbili ziliikosea Zanzibar? Ni kwamba yule mshirika wa Zanzibar katika Muungano (Tanganyika) sasa alikuwa ametoshatoroshwa (kwa makusudi) na hivyo Zanzibar haikuwa na upande wa kujadiliana nao panapohusika mambo ya Muungano.

Kwa hivyo, hata lile agizo lililokuwemo katika Katiba ya Muda kwamba Tanganyika and Zanzibar are one United Sovereign State likabadilika na sasa ikawa Tanzania is one State and is a Sovereign United Republic, ambayo ndiyo iliyomo hadi sasa, na ndiyo inayotumiwa na akina Pinda kuhalalisha madai yao kuwa Zanzibar si nchi. Kumbe tamko hili lenyewe liko kinyume na Mkataba wa Muungano, ambao ni sehemu muhimu ya Katiba yenyewe.

Kuanza hapo haijakuwa tena ajabu wala aibu kwa vikao vya chama na serikali kukaa Chimwaga kwa jina la Tanzania, kupitisha maamuzi yoyote wanayoyapendelea wakubwa wa Tanganyika bila ya kuzingatia upande wa pili wa Muungano huu, lakini imekuwa dhambi kubwa kwa Wazanzibari kukaa na kuizungumzia khatima ya nchi yao ndani ya Muungano huu.

Hata viongozi wanaowekwa au kutumwa na Wazanzibari wenyewe wanapothubutu kufanya jambo ambalo linamaanisha kunyanyua sauti ya Zanzibar, basi hukiona cha mtema kuni. Ndiyo yaliyowapata akina Aboud Jumbe, Maalim Seif Sharif Hamad na Salmin Amour. Sasa, kuna wasiwasi wa kutumiwa utaratibu huo huo wa kudhibitiana kichama dhidi ya wana-CCM wa Zanzibar walioinuka na kushikilia msimamo wao kuwa Zanzibar ni nchi.

Hizi zimekuwa ndizo siasa za Muungano huu, za mkubwa kummeza mdogo, za mbinu na hila na vituko na vitimbi. Kuna kauli maarufu sana ya kumezwa kwa Zanzibar na kufutwa kabisa. Inasemwa kuwa hii ndiyo sera ya siri ya CCM, ingawa wenyewe wanalikanusha hilo. Lakini mtiririko kama huu wa matukio unaonesha kuwa muna angalau nusu ukweli katika kauli hii, kama si ukweli mtupu, maana kila tukienda mbele, ndivyo Zanzibar inavyozidi kupoteza kwa kuuimarisha Muungano, tena kwa gharama hata za kuvunja Makubaliano ya Muungano.

Kwa miaka yote 44 ya Muungano, kanuni inayouendesha Muungano huu imekuwa ni moja tu: kadiri Tanzania inavyozidi kupanda, Zanzibar izidi kuanguka. Tumeona kuwa Tanganyika ilibadilishwa na Mwalimu Nyerere iwe ndiyo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hivyo si kweli kwamba Tanganyika ilipotea baada ya Muungano, bali ilitiwa kikutini na kubadilisha jina tu. Kwa maana nyengine, gharama kubwa iliyoingia Tanganyika katika Muungano huu, kama ipo, ni huko kupoteza jina lake la asili na faida kubwa ya Zanzibar, kama ipo, ni huko kubakia na jina lake.

Na hiki ni kizungumkuti tu. Jina ni nini ikiwa huna nguvu, huna uwezo: huna lako, huna chako? Ikiwa kuna chochote kinachoweza kuthibitishwa na huu uhusiano baina ya Tanganyika na Zanzibar kwa jina la Muungano, kwa hivyo, basi ni huo uwezekano wa mmoja kuila keki yake na akabakia nayo na mwengine kutokuila na bado asiwe nayo. Muungano huu umekuwa ajali ya kisiasa kwa Zanzibar, Wazanzibari na Uzanzibari!

2 thoughts on “Tanganyika iliila keki yake na bado inayo”

  1. ahsante ndugu yangu Mohammed, hii ni kweli tupu unayoisema ila hivi kuwa zanzibar si nchi tokea mwaka 1964 tumeyataka wenyewe sisi wazanzibari kwani sisi tukiimbiwa mapinduzi daima basi vichwa hutanuka na kupata ujasiri wa kupoteza hata tulivyovishikilia. kuipoteza zanzibar yetu kwa kuichanganya kwenye tanganyika tukapata tanzania ni sawa na ile hadithi ya suleiman na kondoo 99, na mmoja. sisi wazanzibari kondoo wetu tumemchanganya kwenye kundi la 99 na sasa hatumjui ni yupi katika hao 100 wa sasa, hata tukimtaka tunaweza kuambiwa amekufa,hata kama hajafa,amepotea hata kama bado,ameliwa hata kama yu hai, hichi ni kizungumkuti au kiini macho. yumkini yale yanayoitwa mapinduzi tuliugawa uzanzibari wetu na matunda yake ndio haya

  2. Lakini tunapaswa kufanya kitu kaka yangu Abou Khalid. Haitoshi tena kusema kuwa nchi imegaiwa Tanganyika tu, lazima sisi wa kizazi cha sasa tufanye jambo linaloweza kuirudisha nchi mikononi mwetu wenyewe.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.