Nilitaka sana Spika Kificho asahau utiifu wake kwa mabwana wa Chimwaga na akumbuke sana utiifu wake kwa Zanzibar. Athamini kwamba hadi leo, sisi Wazanzibari tuliompa Uspika, tungali tukiendelea kujinasibu, kujilabu na kujilindia Uzanzibari wetu. Sikutaka atumie nguvu zake kuzima mchemko wa fikra za kizalendo kutoka kwa umma na wawakilishi wao kama wanavyofanya mabwana wa Chimwaga.

Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho.
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho.

SITAKI Spika Pandu Ameir Kificho wa Baraza la Wawakilishi anishawishi niutilie shaka uelewa na uzalendo wake kwa Zanzibar, nchi ambayo yeye anasimamia moja kati mihimili mikuu ya utawala, yaani chombo cha kutunga sheria. Sitaki kabisa anilazimishe niandike jambo baya dhidi yake, kwamba ndani ya akili yake anahisabu kuwa chama chake cha Mapinduzi (CCM) kilichoko Dodoma ni kikubwa kuliko nchi yake.

Hivi Spika Kificho hakumbuki kidogo ile taarifa ya Tume ya Uchunguzi ya Kituo cha Katiba cha Afrika ya Mashariki ya mwaka 2003 iliyosema kuwa: “Wazanzibari wana uzalendo wa hali ya juu na wanajivunia sana Uzanzibari wao… mila na utamaduni wao, bila ya kujali tafauti zao za kisiasa…. wanaamini kwamba Zanzibar ni dola na Muungano ni makubaliano kati ya dola mbili huru na ni muhimu hilo lieleweke hivyo.”?

Ndiyo, ningetamani pia Spika Kificho aelewe hivyo. Kisha, baada ya kuelewa, aheshimu mawazo ya Wazanzibari wenzake. Asitake niamini kwamba naye yu katika kundi la wale wanaotumiliwa dhidi ya maslahi ya Zanzibar.

Badala yake, nataka Spika Kificho akiri kuwa alichokifanya Barazani hivi karibuni, kuzuia mjadala na maandamano ya Zanzibar ni nchi au la, lilikuwa jambo silo. Limetujengea shaka na shukuki juu yake. Anataka kukificha kisichofichika? Ataweza?

Taarifa niliyoinukuu hapo juu ilitokana na uchunguzi uliofanywa baina ya Machi na Mei, 2003 katika maeneo ya Pemba, Unguja na Dar es Salaam, ambapo Wazanzibari kutoka fani, vyama, umri na nafasi tafauti walihojiwa. Yalikuwa maoni halisi ya Wazanzibari halisi. Sitaki kukubali kuwa Spika Kificho halijui hilo.

Sitaki niamini kuwa ukweli huu ni mpya kwa Spika Kificho, maana nimjuavyo mwenyewe ni Mzanzibari toka-nitoke. Simshangai mwenzake wa Bunge, Spika Samuel Sitta, kuusitisha mjadala, maana yeye ana maslahi tafauti na ya Wazanzibari katika hili. Amekuwa sehemu ya tatizo la Zanzibar kwa miaka nenda-rudi kutokana na nafasi mbalimbali alizozishikilia kazi kwenye ‘system’, kwa hivyo kutoka kwake hatuwezi kutegemea kitu tafauti.

Lakini nilitarajia kuwa Spika Kificho, akiwa Mzanzibari kwanza, angelitumia fursa hii iliyojitokeza, kuthibitisha kwamba bado Zanzibar ina wenyewe. Angelitumia wasta wake kuwaonesha maadui wa Zanzibar kuwa mikakati yao ya kuizika Zanzibar imeshindwa na kamwe haiwezi kufanikiwa. Angeliwapa jukwaa, kwanza, wale wawakilishi wa wananchi wa Zanzibar waliowakilisha hoja binafsi, kuuthibitishia ulimwengu kwamba Uzanzibari ungalipo licha ya miaka 44 ya kuukandamiza. Na, pili, angeliwapa fursa wale wananchi 10,000 waliotaka kuandamana ili kuonesha kuwa Uzanzibari bado umo katika hisia zetu kwa kiwango kile kile cha miaka ya ’60.

Nilitaka sana Spika Kificho asahau utiifu wake kwa mabwana wa Chimwaga na akumbuke sana utiifu wake kwa Zanzibar. Athamini kwamba hadi leo, sisi Wazanzibari tuliompa Uspika, tungali tukiendelea kujinasibu, kujilabu na kujilindia Uzanzibari wetu. Sikutaka atumie nguvu zake kuzima mchemko wa fikra za kizalendo kutoka kwa umma na wawakilishi wao kama wanavyofanya mabwana wa Chimwaga.

Ndani ya nafsi ya Spika Kificho ukweli huu ungelikuwa wazi. Kwamba kamwe Muungano huu haujawahi kuwafanya Wazanzibari wauamini au wauhisi Utanzania waliovishwa katika kiwango wanachouamini Uzanzibari wao. Kwamba kwao wao Utanzania ni nguvu na sheria tu, lakini Uzanzibari ni moyo, mapenzi na imani. Na nguvu na sheria, kwa hakika, hazina nguvu mbele ya mapenzi na imani.

Sikutaka, kwa hivyo, asaidiane na wale tunaowachukulia kuwa maadui wa Zanzibar kutufungulia Katiba waliyoandika wenyewe eti kutuonesha namna tunavyopaswa kuamini na kufikiri, bali nilitaka ashirikiane na wawakilishi na umma wa Wazanzibari kuifungua milango ya historia iliyotukuka na nyoyo zetu zilizojaa mahaba kwa nchi kuonesha ilipo imani na mapenzi yetu. Awaoneshe na wengine wajuwe, kwamba ikitukanwa Zanzibar, huwa tumetukanika Wazanzibari.

Na, kwa hakika, Spika Kificho, kuliko wakati mwengine wowote huko nyuma, sasa alikuwa na fursa ya kutupa jukwaa Wazanzibari kuonesha kukerwa kwetu na matusi hayo na pia kujenga msimamo wetu wa leo na wa baadaye. Kwa nini lakini naye awe sehemu ya tatizo letu, badala ya kuwa sehemu ya utatuzi wa tatizo hilo? Nimeshindwa kumuelewa.

Kwa nini Spika Kificho anifanye niamini kuwa naye ni muumini wa kile nikiitacho Chimwaga Supremacy, au Nyerereism, kwa lugha nyepesi? Wenye imani hizo hutaka ikubalike kuwa ni dhambi isiyosameheka kuuzungumzia Uzanzibari nje ya muktadha wa Tanzania kwa lugha kama hii ambayo imekuwa ikitolewa na Wazanzibari kipindi hiki cha kutukanwa na Waziri Mkuu Pinda.

Kama Mwalimu Julius Nyerere angelikuwa hai, makala hii angeliita dhambi ya ubaguzi, maana alitutaka sote tuamini kuwa hakuna Uzanzibari nje ya Muungano. Kwa nadharia zake za ajabu ajabu ni kuwa Mzanzibari asingeliweza kujiita Mzanzibari kama usingelikuwepo Muungano huu. “Nje ya Muungano hakuna Uzanzibari…. kuna Uzanzibari na Uzanzibara… Upemba na Uunguja…!”

Naziita hizi nadharia za ajabu kwa kuwa Zanzibar ilikuwepo hata kabla ya huu Muungano, na siku hizo watu walijiita Wazanzibari na wakajifaharishia kwa Uzanzibari wao. Si kweli, kama alivyotaka Nyerere iaminike, kuwa Zanzibar ilijengwa na Muungano. Bali kinyume chake ndio ukweli – yaani Muungano unaivunja Zanzibar, huku Zanzibar ikiujenga Muungano huo. Maskini, Mwalimu Nyerere hakubakia hai hadi leo, akaja kuushuhudia uhalisia ukimsuta na kuiaibisha nadharia yake!

Turudi kwenye nukta: Inakuwaje Spika Kificho aingie katika kundi la watu vibubusa? Kuna wakati, Novemba 2003, Baraza la Wawakilishi liliwasilishiwa Mswaada wa Usafiri Majini 2003 na Serikali ya Muungano. Wajumbe wa CUF na CCM wakasimama kwa pamoja kuupinga, maana waliamini kuwa haukuwa na maslahi kwa Zanzibar kwa sababu mbili: moja ni kwamba ulikusudia kuongeza orodha ya Mambo ya Muungano kwa njia isiyo sahihi na pili ulikusudia kuipokonya Zanzibar uwezo wake wa matumizi ya bahari na rasilimali zake na mapato yatokanayo na vyombo vya usafiri wa baharini.

Wakati huo mwakilishi wa Donge, Ali Juma Shamhuna, alisema kwamba kama wangekubali, basi kungelikuwa: “ni kugongomelea msumari wa mwisho katika jeneza la Zanzibar” maana kulikuwa ni kuinadi Zanzibar kwa bei ya chee. Naye Spika Kificho akiwa kiongozi wa Baraza akaridhia upinzani huo. Sasa vyereje leo?

Labda pana jawabau hapa: tunakumbuka kuwa mswaada huu huu ulikuja tena baadaye ukapitishwa na Baraza hili hili huku ukiungwa mkono na wawakilishi wale wale wa CCM walioupinga kwa mara ya mwanzo. Kipi kilitokea baina ya vikao hivi viwili – cha kuupinga na kuupitisha mswaada – ndicho ambacho, nadhani, ni jawabu la ugoigoi huu wa fikira wa mara hii.

Yumkini wakati ule waliitwa wawakilishi wale wa CCM, wakatishwa, wakaambiwa na mabwana wa Chimwaga: ”Sasa nini munafanya? Kwani hamujui malengo yetu? Munajifanya wakubwa kuliko Muungano? Mumesahau mulifikaje hapo mulipo? Bado munayataka madaraka?” Pengine waliambiwa hivyo, na huo ukawa mwisho. Mswaada ukaja ukapitishwa.

Sasa na hili nalo; tayari mabwana wa Chimwaga wameshalichukulia ni kuukosea adabu Muungano na anayefanya hivyo hana manufaa kwao. Kwa kiongozi wa Zanzibar kuwa na manufaa, ni kukubali kila wanachokitaka wao juu ya hatima ya Zanzibar. Akikataa huwa si mwenzao. Na kwa kuwa hatamu za nchi ziko mikononi mwao, basi si hasha kumshughulikia kwa njia zao wenyewe za kushughulikiana. Lakini sitaki Spika Kificho aogopeshwe na hilo, maana akifanya hivyo atasita kustahiki heshima yangu na ya Wazanzibari wengine. Nani amuheshimu kiongozi mwoga, ashindwaye kujaa kitini pake? Sitaki aogope jina lake kujitokeza kwenye daftari jekundu la Chimwaga, maana akiogopa atakuwa mnafiki; nami namuheshimu sana, siwezi kumuita mnafiki.

Najua kwamba mang’weng’we wa Chimwaga hawajazowea kupingwa na Wazanzibari. Walichozowea ni kusema watakalo hata kama silo, wakapigiwa makofi na kisha wakatuburuza wapendavyo. Chimwaga haijazowea kupokea changamoto kutoka Zanzibar, na hili la mara hii, limeshakuwa tusi kwao. Lakini ya nini Spika Kificho kuwapa viganja vya kuficha nyuso zao? Si awawache tu ’watukanike’ kama walivyoitukana wao Zanzibar?

Sikutaka Spika Kificho asimame katikati ya njia waliyotaka kupita wawakilishi wa Zanzibar na umma wao kuonesha kuchokozeka kwao. Angeliwacha ikafahamika kuwa huu ndio msimamo wa Wazanzibari na hiyo ndiyo kauli yao. Kwamba hawataki kuyasalimisha tena mamlaka ya nchi yao zaidi ya hapo walipokwisha kuyasalimisha. Ambacho angelikifanya Spika Kificho, ni kuwasaidia tu wenzetu wa Chimwaga kuelewa kuwa Wawakilishi wetu waliposimama kuipinga kauli ile Waziri Mkuu Pinda, walifanya vile kwa niaba yetu, Wazanzibari sote.

Na huu ulikuwa ni msimamo na mshikamano tulioutarajia zamani, si leo, tukawa tunaukosa. Kukosekana kwake ndiko kulikowalemaza ndugu zetu wa Chimwaga wakawa wanaamini kuwa: “Haka kazanzibari ni kashamba ketu tu. Tunaweza kukiamulia tunavyotaka”. Hilo lilikuwa ni kosa; na mara hii ilikuwa waoneshwe kuwa wanakosea.

Nilitaka sana Spika Kificho aikiri haki ya Wazanzibari kujieleza katika chombo chao. Wajieleze kwa sauti kubwa, hadi walioko Dodoma wafahamikiwe kuwa wamekuwa wakifanya kosa kubwa kuichukulia Zanzibar, kutokana na udogo wake, kuwa ni sehemu tu ya Tanganyika. Haifai kuwachukulia Wazanzibari, kutokana na uchache wao, kuwa hawana ubavu wa kupinga kauli itolewayo dhidi yao.

Sikutaka Spika Kificho asaidie kufanikiwa kwa jitihada za kuilaza doro Zanzibar, ambazo huko nyuma zimewahi kufanikiwa kutokana na uzembe na ulafi wa baadhi ya Wazanzibari wenzetu walio kwenye madaraka. Ni pupa yao ya vyeo vigaiwavyo Chimwaga iliyotugharamu hadhi na nafasi ya nchi yetu katika Muungano. Ni uzembe na ulafi huo ndio ulioiruhusu kasumba ya ubaguzi kupenya haraka katika vichwa vyetu hata tukashindwa kusimama kama watu wamoja. Kwa sababu tu ya vyeo na madaraka, sisi ndugu wa baba na mama mmoja tukakubali tuitwe na tuitane kama Waafrika na Waarabu na Wapemba na Waunguja.

Huu ulikuwa, na unaendelea kuwa, woga wa kipuuzi sitaki Spika Kificho ajioneshe kuwa sehemu ya upuuzi huu. Usingelikuwa upuuzi huu, hivi sasa hadithi ya nafasi ya Zanzibar katika Muungano ingelikuwa ikisimuliwa vyengine. Aidha pasingelikuwa na malalamiko ya kudhalilishwa na kudunishwa au, kama yangelikuwepo, yangelitokea upande wa pili wa Muungano, na sio huu wetu. Kwa nini kila siku tulalamike sisi tu kama wana wa kambo?

Mwisho, sitaki niamini kuwa Spika Kificho ameshachelewa kutumia fursa aliyonayo Barazani kuwaunganisha Wazanzibari kwa ajili ya nchi yao. Tulifurahishwa na msimamo na mshikamano uliooneshwa na wawakilishi wetu mara hii. Wengine tunaogopa kujenga matarajio sana ya mshikamano huu, maana tuna uzoefu mbaya na wenzetu wa CCM wanapofikia mahala wakatishiwa ’usalama’ wa madaraka yao, lakini lazima tuseme kwamba inatia moyo kidogo kuona kuwa wawakilishi wa Wazanzibari wanasimama na kushikamana kama Wazanzibari kuitetea Zanzibar yao. Fahari ilioje katika siasa za petu!

Mshikamano huu unaweza kuwa nyenzo kwa Spika Kificho. Asiufifilishe mjadala wa nafasi ya Zanzibar katika Muungano bali aupe uhai. Auchechemushe uchemke. Kisha aliwache Baraza, ambacho ndicho chombo kinachowakilisha sauti ya Wazanzibari kutoka na azimio la pamoja kwa ajili ya Zanzibar. Asiogope mtu. Chembilecho Ali Juma Shamhuna: ”muda wa kutishana umepita.”

Spika Kificho: una katiba, una muda na una umma, kwa hivyo una kila sababu na na kila uwezo, kinachogomba ni nia tu. Je, unayo nia ya kuitetea Zanzibar? Sitaki unambie kuwa huna!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.