Na Ally Saleh

Yanayotokea sasa ambayo tunaweza kuyaita ni Pinda-Gate, yaani Kashfa ya Pinda, si mambo ambayo yamezuka tu kama uyoga katika siku za umande mzuri au mimea iliyoota kwa sababu ya kupeperuka mbegu kwa upepo. Ingekuwa ni nchi za wenzetu, waandishi wangeanza kuchimba mpaka wakajua ni kwa nini Pinda akasimama kama alivyosimama, anapata nguvu wapi na nguvu zake ni za kina gani.

Ila naamini  wapanga mikakati wa CCM  wamefurahia sana  kuzuka  kwa suala la Zanzibar kwa maana ya hii kadhia  iliyoshitadi  sasa hivi kuwa Zanzibar ni nchi au si nchi kwa sababu  itakuwa imewatoa wananchi kwenye suala la Muwafaka.

Si hasha, huu inaweza ikaja ikagundilikana huko mbele  kuwa ulikuwa ni mkakati maalum uliokuwa ukichezwa kwa  mtindo wa chess na kila hajari inayochezwa kupangwa kwa ufundi  wa hali ya juu.

Maana ni ukweli kuwa CCM kwa faida ya kuwa ndio chama tawala inapata fursa kubwa ya kupata ushauri wa chombo cha usalama ambacho kina uwezo mkubwa wa kiutendaji na  wachambuzi na wapanga mikakati.

Ndio maana tokea hapo suala la Muwafaka lilikuwa limeshasukumwa pembezoni, kwamba halikubaliki na wala  halitawezekana kufanyika Zanzibar na kinara wa ukataaji huo ni Chama cha Mapinduzi, CCM.

Sisi wengine tumekuwa na mtizamo kuwa katika siasa mambo hayatokei kwa bahati mbaya, na yale yanayotokea kwa bahati  mbaya basi watu mara moja huyachukulia kuwa ni fursa ya  kuyaingiza katika mipango yao.

CCM imekataa kupikuliwa na CUF, ni hili lilisemwa kwa  maandishi katika waraka wa chama hicho uliopelekwa  Butiama,  na kwa hivyo imesimamia kukataliwa kukubaliwa kuundwa kwa  Serikali ya Pamoja jambo ambalo kila mtu anaelewa kuwa lingeleta ustawi na maelewano makubwa miongoni mwa Wazanzibari.

Lakini kwa bahati mbaya pia, Wazanzibari walio CCM walifurahia sana jambo hilo bila ya kujua kuwa kukosekana  ujambo kama hilo kungeathiri umoja wao kama ambavyo inadhihirika sasa hivi.

Wengi tumebaki kusema yalaitani!!! Tunabaki kujiuliza hivi hali ingekuwaje kama kungekuwa na Serikali ya Pamoja na likazuka hili la Waziri Mkuu Mizengo Pinda?

Umma wa Kizanzibari ungesimama vipi nyuma ya uongozi ulioimarika wa pamoja wa vyama vikuu viwili vya CUF na CCM?  Unatamani kuchora picha ambapo Kiongozi wa Upinzani Seif  Shariff Hamad na Rais wa Zanzibar Dk. Amani Karume  wangekuaje hivi sasa.

Lakini wapi!!! Chembilecho Hamad kuwa Wazanzibari wametiwa fitna ya kugawiwa na wao wamekubali kugawika. Na ni wazi kuwa waliogawiwa ndio wanaotawaliwa na Zanzibar leo iko hali hiyo.

Zanzibar imekuwa na matatizo ya kisiasa tokea ulipoanzishwa  mfumo wa siasa za vyama vingi mwaka 1992 lakini mambo  yakajitokeza wazi wazi katika uchaguzi wa kwanza wa  1995,  yakajirudia 2000 na pia mambo ya kuwa ni vivo ilipofika  mwaka 2005.

Kwa miaka 15 hivi sasa Zanzibar imekuwa haina utulivu  wa  kisiasa ambao ungeweza kuimarisha umoja wa wakaazi wa  visiwa hivi na tabaan kuwa na athari katika kupiga hatua za  kimaendeleo.

Lakini tuseme tuyaweke kando yaliotokea mwaka 1995 na 2000 lakini hebu tutizame haya ya sasa ya mwaka 2005 ambapo tunayo mpaka hivi sasa na suluhu ya kisiasa ikishindikana  kupatikana.

Kila mtu anajua jinsi ambavyo suluhu ilivyokuwa karibu kupatikana. Na ni mkutano wa siku mbili tatu uliofanyika huko Bitiama ndipo mambo yote yalipovurugika na hadi hii  leo Zanzibar kwa hakika imepoteza dira.

Ilikuwa karibu mno kama pumzi za binaadamu na pua yake, lakini CCM ikaifuja fursa hiyo kwa sababu ya  kutoitakia  mema na utulivu Zanzibar, ingawa ni wazi kuwa katika  waliohusika na ufajaji wa fursa hiyo Wazanzibari  wenyewe walikuwemo.

Kinachotia uchungu tukeo tukio la Zanzibar litokee kumekuwa na mazingira mengine yanayofanana na haya ya Zanzibar ambapo utata wa uchaguzi ulitokea lakini suluhu ikafikiwa.

La kufurahisha sana ni kuwa waliosimamia suluhu hiyo, uongozi wa Tanzania, kinara wetu Rais Jakaya Kikwete akiwa mbele kabisa. Na alihakikisha kuwa dunia inajua kuwa mambo yamefanikiwa kwa sababu ya mchango wake.

Matatizo ya uchaguzi yalitokea Kenya mwezi wa Diusemba tena  mwishoni kabisa na baada ya miezi mitatu tu nchi hiyo ikawa na Serikali ambayo imewakutanisha mahasimu wawili  wakuu  Raila Odinga na Mwai Kibaki na vyama vyao.

Alikuwa ni Kikwete ambaye aliyependekeza kuundwa kwa  Serikali ya Pamoja akiona hiyo ndio njia pekee ya  Muwafaka,  na kwa kweli viongozi wa Kenya wakakubaliana nae na Serikali  hiyo ikaundwa.

Hayo yakitokea, huku kwetu chama chake yeye Kikwete  kilikuwa kina mazungumzo ya zaidi ya miezi 18 na kile cha  CUF na ilipokaribia kundwa kwa Serikali ya Pamoja, Kikwete  huyo huyo akaziba macho na masikio yake na pengine hata  akili yake akaizima.

Tokea Feburari hadi leo Julai, Kikwete hajachukua hatua  yoyote ya maana kuhakikisha angalau kuwa anaona aibu  kuwa amekuwa msuluhishi Kenya lakini ndani ya nchi yake  ameshindwa kufanya suluhu.

Mara likazuka la Zimbabwe. Huko mbabe Robert Mugabe  akanyakua madaraka dhidi ya Morgan Tvsangirai  na tena  viongozi wetu wakawa mstari wa mbele na Rais wetu akiwa ni bosi wa Umoja wa Afrika akahimiza upatanishi.

Na habari za karibuni kabisa zinasema kuwa Mugabe na Tvsangirai wametia saini makubaliano ambayo yataongoza kwenda kundwa Serikali ya Pamoja katika nchi hiyo, ambapo ni dhahiri wapinzani wameibiwa.

Lakini inaelekea kuwa hii sasa itakuwa ndio sera rasmi ya chaguzi za Afrika. Aliyeko madarakani ataiba, kisha atasema asiingiliwe katika mambo yake ya ndani ya  nchi, atatoa wito wa wapinzani kuingia katika mazungumzo halafu  itaundwa Serikali ya Pamoja.

Na viongozi kama Rais Kikwete watabariki Serikali kama  hizo kwa hoja kuwa ni kwa ajili ya kujenga utengamano na  sio kuvunja umoja wa taifa. Na Afrika nzima itaitikia amin, maana hawana njia nyengine zaidi ya kuwakubalia wezi wa uchaguzi wabaki madarakani.

Ila kinachonishangaza mie ni nguvu gani ambazo CCM hii yetu inazo kukataa suluhu ambayo inaonekana hivi sasa ndio mtindo wa kote Afrika? Inapata wapi tambo hizi za  kukataa?

Halafu pia najiuliza baada ya kukataa ni vipi nchi za  Kiafrika au viongozi wake wanaweza nao kunyamaza kimya  suluhu kama hiyo ikikataliwa kutekelezwa Tanzania ilhali ni  wao pia husimamia mambo kama hayo kwengineko Afrika?

Maana haingii akilini kabisa kuona yanayotokea hapa  Zanzibar yakiwa hayasemewi kabisa katika rubaa za kisiasa  kote Afrika, ilhali kila nchi inajua kuwa Zanzibar kulifanyika uchaguzi, na uchaguzi huo matokeo yake yakamalizika kwa njia ya utata?

Sasa imefika wakati Wazanzibari kumuuliza Rais Kikwete, jee kwa nini Zanzibar haupatikani Muwafaka? Jee ni kwa sababu Zanzibar si nchi?

Na kama yetu hii si nchi basi kutakuwa na maana gani  ya  kuendelea na kufanya chaguzi kila mwaka lakini zikiishia  kwa utata na utata huyo usitafutiwe suluhu kwa sababu yetu  si nchi?

Jee si imefika wakati Zanzibar ambayo si nchi iwache kufanya chaguzi na kiongozi wake atafutiwe utaratibu  mwengine wa kuchaguliwa au labda sahihi niseme kuteuliwa?

La kama si hivyo, ni haki Zanzibar kudai usawa na  chaguzi  nyengine zinafanyika Afrika na Tanzania iwajibike sawa  inavyowajibika kwenye jukwaa la Afrika na katika suala lake  la ndani.

La sivyo naomba mtu anieleze CCM wanapata wapi jeuri hii ya kuepuka suluhu kufanyika Zanzibar? Kwa akili yangu nimeshindwa kun’gamua.

Au ndio kwa sababu Zanzibar sio nchi kwa hivyo hakuna litalokuwa? Na hivi baada ya matamshi ya Pinda inaonekana kama ndio mwisho wa njia hakuna tena pa kupinda.

* Makala ya Ally Saleh katika Taifa Tanzania, Julai 2008

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.