Na Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi

Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, Rais wa Pili wa Zanzibar na ambaye aliondolewa madarakani kwa kulazimishwa kujiuzulu na vikao vya Chama cha Mapinduzi, Dodoma, mwaka 1984
Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, Rais wa Pili wa Zanzibar na ambaye aliondolewa madarakani kwa kulazimishwa kujiuzulu na vikao vya Chama cha Mapinduzi, Dodoma, mwaka 1984

KUMEKUWA, hasa katika miaka ya karibuni, na malalamiko kadhaa kuhusiana na ukiukwaji wa Katiba. Madai haya yametoka kwenye vikundi, au watu binafsi, na baadhi yao wakiwa ni watu ambao wao wenyewe wamekuwa ndio wakiukaji wakubwa wa Katiba ambayo hivi sasa wanapita wakisema wanailinda.

Nitajaribu tena kuzungumzia ukiukwaji huo ingawa nina khofu kuwa mengine nitayarudia. Hebu kwanza tuoneshe ule ukiukwaji uliopo katika Mkataba wa Muungano na Sheria za Muungano nguzo ambazo ndizo kila moja wao zilikubali kupeleka maeneo maalum kwa serikali ya kati iliyoundwa, na kubakisha mamlaka makubwa makubwa zaidi kwao wao binafsi.

Mkataba wa Muungano 1964, kama tulivyoona, ulitoa sura ya kuwepo kwa shirikisho la serikali tatu ambapo hapangekuwa na serikali moja iliyo na mamlaka makubwa kushinda nyingine.

Kutoa mamlaka ya Chama kushika hatamu na kuvifanya vyombo na taasisi zote za dola kuwa chini yake ni kwenda kinyume na matakwa yaliyopendekezwa na Mkataba wa Muungano na Sheria za Muungano, na kwa hali hiyo hilo kuwa ni kiuko kubwa kuliko yote la mkataba huu wa kimataifa. Upande ulioathirika, katika kiwango cha kimataifa, unaweza kwenda kufungua kesi katika mahakama ya Kimataifa kwa kosa la kukiukwa mkataba, na kama upo ulazima basi pia kwenda katika Mahakama ya Katiba.

Mkataba wa Muungano ulitaka kuwepo kwa serikali tatu au mamlaka ambazo zingeundwa kiuunganishi ambazo katika waraka huo zilitajwa kuwa ni mmoja wa mamlaka kuwa ni Tanganyika, Zanzibar na Jamhuri ya Muungano. CCM haikutajwa kuwa ni mmoja wa mamlaka hzo na kwa hivyo haiwezi kuingizwa na kuwa mshiriki wa mkataba wa Muungano. Na kwa hali hiyo CCM haina uwezo wa kisheria (locus stand) wa kujiingiza kisheria na kulazimisha haki na wajibu wa Muungano kwa upande wa Tanganyika, Zanzibar au Jamhuri ya Muungano.

Vile vile CCM ikiwa si sehemu ya Mkataba wa Muungano wa 1964 haiwezi kisheria kudai kupata manufaa yoyote chini ya mkataba huo kwa kuzilalia au kwa hasara ya Tanganyika na Zanzibar ambazo ni sehemu ya mkataba huo. Hii inaweza kuthibitishwa na mahakama ya kimataifa kuwa ni ukiukwaji wa mkataba wa kimataifa.

Serikali ya Muungano unapoilinganisha na kuipima na Zanzibar au Tanganyika, ni salio la uzawa wa nchi hizo na haiwezi kuwa na mamlaka yake wenyewe, isipokuwa kwa yale mamlaka iliyomegewa. Kinyume na binaadamu, ambaye wakati wa kuumbwa kwake, alipewa nguvu zote isipokuwa ya kula tunda moja, serikali ya Muungano wakati wa kuundwa kwake haikuwa na mamlaka yoyote isipokuwa yale ambayo waumbaji wake waliamua kuyatoa kwake.

Kwa mtu katika hali yoyote mahakama ingependa kujua “Hiki ndicho ambacho haikurushusiwa kufanya? Lakini kwa upande wa Jamhuri ya Muungano suala lapasa kuwa: Hivi ndivyo Jamhuri ilivyoruhusiwa ifanye”. Jee, CCM imepewa mambo ambayo hata serikali ya Muungano yenyewe haiwezi kutungia sheria? Ikumbukwe kuwa hapo 1964 waundaji wa Muungano hawakutaka mambo ya vyama yatiwe katika Muungano.

Wakati ule Zanzibar ilikuwa chini ya udhibiti kamili wa ASP na haikupeleka mamlaka yake haya katika Muungano. Hali kadhalika, TANU haikufanya hivyo. Sio ASP wala TANU zilizoorodheshwa katika mkataba wa Muungano wala Katiba ya Muda ya 1965. Kama hali ndiyo hiyo, Bunge halikuwa na mamlaka ya kutunga sheria kuhusiana na CCM. Tujue kuwa hii dhana ya “mambo yasio ya Muungano” ni ya Zanzibar na Tanganyika pande ambazo zina mamlaka ya kuzungumzia juu ya vyama vyao ndani ya maeneo yao. Kwa hivyo ibara 3 ni haramu na batili.

Katika hotuba yangu niliyoitoa Mkoani, Pemba, Juni 15, 1976 katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya ASP wakati huo nikiwa Rais wa Afro Shirazi, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Rais wa Zanzibar nilitoa kasoro zilizojitokeza kwa nafasi ya Zanzibar katika Muungano kufuatia mabadiliko yaliyofanywa katika Katiba ya Muda ya Tazania chini ya ibara ya 3(3). Nilisema bila ya kuwa dhahiri, kuwa mamlaka y Zanzibar katika mambo yasio ya Muungano yalikuwa ndio masharti ya kuwa Zanzibar iungane na Tanganyika, nikasema hivi:

“Watungaji wa Katiba ya Muda wakati wakifikia dhana ya kuwa hatimaye kutakuwa na chama kimoja cha kisiasa kwa Zanzibar walichukua hadhari ya kuhakikisha kuwa shughuli za kisiasa za Chama hazingeingilia vyombo vya dola vya Jamhuri ya Muungano wala vile ya kutunga sheria na Rais wa Zanzibar. Fikra iliyokuwa ikitiliwa mkazo hapa ni kuwa nchi mbili hizi zilikuja pamoja chini ya maelewano maalum ambayo nayo yanalinda maslahi ya pande mbili hizo. Kwa upande wa Zanzibar kitu ilichokuwa ikikitizama mno na ambacho ilihakikishiwa kuwa kitalindwa ni vyombo vya Muungano kwa sababu ya vyombo hivyo kuwa na wajibu na haki juu ya Zanzibar katika mambo ya Muungano na Zanzibar kuendeleza mamlaka yake kwa mambo yasiyo ya Muungano. Lakini mabadiliko ya Juni, 1975 yanaathiri pa kubwa nafasi ya Zanzibar kwa sababu kazi za vyombo vote vya dola vya Jamhuri ya Muungano sasa zinapaswa kufanya chini ya maagizo ya Chama na shughuli zote za kisiasa Tanzania sasa itabidi ziendeshwe kwa mujibu wa matakwa ya Chama na hiyo ikiwa inajumlisha pia shughuli za kutunga sheria. Hii inafanya kuweko na mwanya kwa chama kimoja, bila ya kuwa na kuzuizi, kuhodhi shughuli zote za kisiasa na kwa hali nyingi kuweza kulazimisha mabadiliko yenye hasara kwa Zanzibar. Hali hii ni ile ambayo kila mwanachama wa ASP, kupitia ngazi za Chama, angependa kuizuia isitokee kwa gharama yoyote ile.

Hilo halikuwashughulisha watungaji wa Katiba ya 1977, na baada ya Muungano wa ASP na TANU, kifungu hicho kuhusiana na chama kushika hatamu kiliundwa upya na kuongezewa nguvu, bila kujali mkataba wa Muungano. Chini ya ibara ya 3(a) ya Mkataba wa Muungano, 1964, washiriki wa mkataba, yaani Rais Nyerere akiwa ni kwa niaba ya Tanganyika na Rais Abeid Amani Karume kwa niaba ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, walikubaliana kuwa Katiba itaweka nafasi kwa:

Mamlaka tofauti ya kutunga sheria na serikali ya Zanzibar kama itakavyoundwa kila wakati kwa mujibu wa sheria za Zanzibar na kuwa na mamlaka kamili kuhusu Zanzibar kwa mambo yote isipokuwa kwa yale ambayo yametengwa kwa Bunge na serikali ya Muungano.

Kwa hivyo ikakubaliwa kuwa katika utekelezaji wa kazi zake, Serikali ya Zanzibar itakuwa na mamlaka kamili ndani ya Zanzibar na haitaweza kudhibitiwa au kuingiliwa na chombo chochote, mtu au ofisi yoyote. Kama hivyo ndivyo ilivyo, kuingizwa kwa dhana ya “Chama kushika hatamu” ambapo chini ya ibara ya 3 ya Katiba ya 1977 ilidai kutoa mamlaka kwa CCM ya kudhibiti vyombo vyote vya dola, kulikuwa ni kukiuka mkataba kitendo ambacho kiliuweka Muungano katika hatari kubwa. Ilikuwa ni dhahiri kuwa lile sharti, ambalo Zanzibar ililitanguliza kabla ya kuingia katika Muungano sasa halikuwepo tena. Mkataba wa Muungano uliingia mashaka. Ilikuwa ni hapo nilipomwandikia Rais na kumueleza uwezekano wa kutofautiana naye katika baadhi ya mambo.

*Kutoka kitabu chake cha The Partner-ship

4 thoughts on “*Serikali ya Muungano imekuwa ikiuka Katiba ili kuikandamiza Zanzibar”

  1. Naomba Muungano udumu zaidi na zaidi kwani watanganyika na waunguja ni wamoja.
    Tusibaguane mungu hapendi

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.