HAYA niyaandikayo hapa ni marejeo tu ya kile nilichokiandika karibuni mwaka mmoja nyuma, katika mwezi wa Aprili 2007. Nakirudia hapa si kuonesha tu khofu zangu kama Mzanzibari, bali pia kuonesha matarajio kama kijana mwenye matumaini ya siku za usoni kwa nchi yangu niliyoapa kuishi na kufa kwayo.

Siku chache tu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2005, nakumbuka, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, wakati huo akiwa mgombea uraisi wa Zanzibar kwa tiketi ya chama chake, alichapisha makala katika gazeti la The East African iliyoitwa “Zanzibar fair elections is Mkapa’s legacy.” Wakati huo tayari, kila dalili ilishaonesha kuwa uchaguzi wa Zanzibar umeshavurugwa. Tayari kulisharipotiwa kesi za kupigwa na kuteswa kwa raia wa kawaida, kuchomewa moto nyumba na mali zao, kubakwa na hata kuuliwa. Yote yalikuwa katika kipindi cha uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Hadi hapo, tayari Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilishawazuia zaidi ya Wazanzibari 12, 000 haki yao ya kuwa wapiga kura kupitia mtandao wake wa Masheha, Tume ya Uchaguzi, Vikosi vya SMZ na hawa waitwao Majanjawidi.Ulikuwa ni wakati ambao Maalim Seif hakuwa tena na haja ya kumpa changamoto ile Benjamin Mkapa, aliyekuwa rais wa Tanzania, amiri jeshi mkuu na mwenyekiti wa CCM, maana tayari Mkapa huyo alikwishayawachia mambo yaende mkorogovyogo mbele ya macho yake.

Lakini Maalim Seif alidhani kuwa kuna nafsi nyengine ya Mkapa ambayo angeliweza kuishaiwishi itende wema kabla haijenda zake. Mkapa alikuwa amezungumza na mwandishi Jonathan Power wa jarida la Prospect mwezi mmoja tu nyuma, na kueleza masikitiko yake kwa aina ya uongozi uliopo Zanzibar, kwamba ulikuwa tayari hata kuua ili uendelee kubakia madarakani. Mkapa huyo huyo, wakati akiwa katika ziara zake za kuaga, alikuwa amezungumza na wanafunzi wa Kitanzania wanoishi Marekani na kueleza kuwa mauaji ya 2001 (ambayo yalisababishwa na uchaguzi usio huru na haki) ni jinamizi baya katika historia ya uongozi wake.

Kibinaadamu, Maalim Seif alikuwa na sababu ya kuamini kuwa Mkapa alikuwa ameyajutia hayo na hayuko pamoja na viongozi hao. Nguvu za kisiasa na kidola alizokuwa nazo Mkapa, zingeliweza kuwazuia viongozi aliowataja wasifanye usilifu wao, ikiwa angelitaka. Kwa kutumia ile iitwayo ‘benefit of doubt,’ ndipo Maalim Seif akapata ujasiri wa kuchukuwa kalamu kuandika changamoto ile. Wapi!

Mkapa alikuwa mtu mwenye nyuso mbili: uso mmoja aliuvaa alipokutana na mataifa ya nje na mwengine alipokabiliana na siasa za ndani. Alichokisema kwa Jonathan Power kilikuwa ni kwa faida ya nje. Alitaka Marekani na Uingereza wamsikie, kisha vyombo vyao vya habari vimwandike kwa sifa za kuwa mwanademokrasia.

Lakini alipokuwa akijihusisha na siasa za ndani, Mkapa alivaa uso mwengine. Kabla ya makala hiyo ya Jonathan Power kuchapishwa, Mkapa alikuwa amesema katika hoteli ya Golden Tulip mjini Dar es Salaam, kwamba angelitumia hata nguvu ya dola kuhakikisha ushindi wa Chama chake cha Mapinduzi, na kwamba katika hilo alikuwa hatanii. Huyo ndiye Mkapa tuliyemjua katika medani za siasa za ndani. Uchaguzi ulipofika, alifanya alichokiahidi Golden Tulip na hakushughulika kabisa na masikitiko yake kwa Jonathan Power.

Miezi miwili na nusu, baada ya makala ile ya The East African kuchapishwa, Mkapa akauwacha uraisi wa Tanzania huku akiwa ameifelisha Zanzibar, ameifelisha demokrasia na, hivyo, amejifelisha yeye mwenyewe. Uhalali alioueleza Maalim Seif katika makala ile haukuwa kitu muhimu kwa kiongozi huyu ambaye angalau sasa tunajuwa kuwa kumbe aliutumia muda wake Ikulu si tu kuidhulumu Zanzibar, bali pia kuigeuza nyumba hiyo takatifu kituo cha biashara ya nipa nikupe.

Hivyo ndivyo historia ya ndani inavyomuandika Mkapa, kama kiongozi aliyefeli. Si tatizo kwamba mashirika ya fedha ya kimataifa na nchi za Magharibi (wanaoheshimika kwa unafiki wao) wanataka aonekane nabii mdogo wa sera zao za utandawazi. Hii ni kwa kuwa, ndani ya Mkapa waligundua aina ya mtawala wa Kiafrika wanayeweza kumtumilia kupora utajiri wa nchi hii huku naye akijimegea wake. Kumjengea jina kulikuwa na gharama ndogo sana kulinganisha na faida walizozipata kwa kukomba tani za dhahabu, tanzanite na almasi.

Ukweli ni kwamba yaliyofanywa na Mkapa yalikuwa ni muakisiko tu wa taasisi alizokuwa akizisimamia, kubwa zaidi ikiwa ni chama chake, CCM. Ndio maana hoja yangu ni kwamba, leo hii Rais Jakaya Kikwete anaweza, akitaka, kuiongoza taasisi hiyo hiyo kufanya maamuzi mazuri kwa Zanzibar na hivyo kuifanya CCM yake isiwe ile ya Mkapa. Alianza kufanya hivyo na mapema. Mara tu baada ya kupokea madaraka, Rais Kikwete akaanza kuonesha, angalau kwa kauli zake, kwamba mtangulizi wake hakuwa chochote zaidi ya sehemu ya tatizo la Zanzibar. Kukiri kwake kwamba pana tatizo kubwa hapa na ahadi ya kulitatua, kulimaanisha kwamba amelitambua alilorithishwa.

Je, Kikwete ana pa kuanzia katika hili la Zanzibar? Anamo mwingi. Na pamojawapo, na muhimu zaidi, ni kwa ile ile CCM ya Mkapa iliyomrithisha tatizo hili. CCM ile ina mengi ya kuifunza CCM ya Kikwete, maana Mkapa na wenzake walikuwa miongoni mwa waumbaji wa mgogoro huu. Sharti pekee wanalopaswa kulitimiza wawili hawa ni kubadilisha mitazamo yao kuelekea Zanzibar. Kubadilisha mtazamo, paradigm shift, ndilo pekee litakalowarejeshea heshima yao kwa Zanzibar.

Kosa moja kubwa la CCM ya Mkapa kuhusiana na Zanzibar ni hilo nililolitaja: kuwa na nyuso tafauti. Japokuwa Mkapa alihubiri ukweli na uwazi, lakini kwa Zanzibar hakuwa mkweli wala hakuwa muwazi. Hakuwa mkweli, maana alikataa kuutambua mgogoro huu kikamilifu na badala yake akawa anatambua tu ile sehemu ambayo ingelimnufaisha yeye na chama chake. Ni hadi Tanzania ilipozalisha wakimbizi, baada ya vikosi vyake kufanya mauaji ya kutisha Januari 2001, ndipo alipoona ulazima wa kulishughulikia suala la Zanzibar. Tupo tunaoamini kwamba, kilichomvuta hasa Mkapa kuja katika meza ya mazungumzo na CUF sio ukweli kwamba kuna raia waliouliwa na askari wake, bali aibu ya nchi yake kuzalisha wakimbizi ambayo ilitishia kulichafua jina lake kimataifa. Chibui hiki cha kimataifa, hakikutaka kionekane kichafu mbele ya G8, International Monetary Fund na World Bank.

Hilo lilikuwa ni kosa ambalo CCM ya Kikwete haitakiwi kulirejea. Isisubiri mauaji ya raia na wakimbizi wengine ili kuchukua hatua. Maana hali ikifikia hapo sasa, kwa mara ya pili, itakuwa vigumu kudhibitika kama ilivyowezekana mara ya mwanzo.

Kosa la pili la CCM ya Mkapa kwa Zanzibar ni kupuuzia kwake nafasi na dhima ya kila mshiriki wa mgogoro uliopo. Kuna wakati yeye mwenyewe alikuwa akijitoa kwa kudai kuwa ya Zanzibar hana mamlaka nayo. Alikuwa akijidanganya, maana yalipokuja kuvoromboka kwa umwagaji damu na wakimbizi, alijitokeza haraka haraka kuyashughulikia. Matokeo yake ndio Muwafaka II ambao, hata hivyo, hakuusimamia vyema.

Wakati historia inaionesha wazi nafasi ya uongozi wa Tanganyika katika siasa za Zanzibar, Mkapa alitaka kuigiza nafasi ya Mr Clean, akijifanya hahusiki kabisa na matatizo ya Visiwa hivi, wakati akijuwa fika kwamba watawala wa Tanganyika ya wakati huo na Tanzania ya sasa ni pawa na miko, part and parcel, ya mgogoro wa Zanzibar.

Kama ilivyo nafasi ya Marekani kwa mgogoro wa Mashariki ya Kati, ndivyo ilivyo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mgogoro wa Zanzibar. Mataifa yote mawili, Marekani na Tanzania, yamekuwa yakilinda maslahi yake ya kisiasa na kiuchumi katika sehemu husika na hivyo hayawezi kujivua dhamana ya migogoro yanayoiibua. George Bush anayeongoza taifa lililo maelfu ya meli kutoka Mashariki ya Kati ni muhimu sana kwa utatuzi wa mgogoro baina ya Wapalestina na Waisrael, ndivyo pia alivyo leo Kikwete kwa mgogoro wa Zanzibar, ambaye siyo tu kwamba anaongoza taifa lililo kilomita chache kutoka fukwe za visiwa vya Zanzibar, bali pia hiyo Zanzibar yenyewe imefanywa kuwa sehemu ya himaya yake. Mkapa alilikataa hilo kijuujuu lakini kwa udhati kabisa aliuendeleza mgogoro uliopo.

Kosa la tatu la CCM ya Mkapa lilikuwa ni kuwatenga na kuwatimba wahusika wakuu wa mgogoro katika utatuzi wa mgogoro wenyewe. Katika mfano huo huo wa Mashariki ya Kati, kosa hili lilifanywa na Waisraeli na Wamarekani kwa Marehemu Yasser Arafat wa Palestina. Ingawa hatimaye waliweza ‘kumuua’ akiwa kazingirwa na vifaru vya Israel, walishindwa kuiua shakhsia yake ya kuwa kiongozi wa Wapalestina. Ni kwa kukosa kumshirikisha katika utatuzi, ndio maana Hamas, hasimu wa Arafat katika uhai wake, ilichukuwa madaraka kwa njia ya kura za wananchi, na sasa inashikilia ukanda wa Gaza ikiungwa mkono wa raia wa huko. Kama Israel na Marekani ziliamini kuwa Arafat hakuwa mtu wa kuzungumza naye, sasa wamejikuta wanakabiliana na wagumu zaidi yake. Hamas sio tu ni adui wao wakubwa, bali pia walikuwa adui wa adui wao, Arafat.

Kuelekea uchaguzi wa 2005, Mkapa aliitimba na aliitenga kabisa CUF. Mara kadhaa Maalim Seif alimuandikia akimuomba wakutane kuzungumzia hali ya Zanzibar, lakini hakujibu hata barua moja. Aliigiza kana kwamba Maalim Seif na CUF yake hawapo kabisa. Matokeo yake ndiyo huu mzigo aliomrithisha Kikwete. Rekodi hadi iliyopo sasa, angalau kupitia kufanyika na kumalizika kwa mazungumzo baina ya CUF na CCM, inaonesha kwamba Rais Kikwete amejitahidi kuliepuka hilo, japo si kwa ukamilifu. Hili litakuwa kosa lenye gharama kubwa kama litachukuliwa na CCM ya Kikwete kuwa njia ya kuishughulikia CUF.

Kosa la kuzifanya siasa za CCM kuelekea Zanzibar ziwe sawa na Bush kuelekea Mashariki ya Kati limetugharimu sana kama nchi na kama taifa. Unafiki na ubabe wa CCM ya Mkapa haukutuvunia chochote zaidi ya kuulea na kuukuza mgogoro. Ni halali kusema kuwa CCM ya Mkapa iliiwacha Zanzibar iliyopasuka na kugawika zaidi kuliko waliyoikuta. CCM ya Kikwete inayokutana mwisho wa mwezi huu Butiama ina kazi ngumu na muhimu ya kuwa tafauti.

Mgogoro wa Zanzibar haumtaki Mkapa mwengine kutatua. Unamtaka mtu tafauti kabisa. Kama kiongozi, Rais Kikwete anapaswa kuwa mpya na tafauti kwa kila hali panapohusika suala la Zanzibar. Yeye na CCM yake wanapaswa kujifunza walipokosea akina Mkapa, kamwe wasijifunze na kuigiza ile staili yao ya kulishughulikia. CCM hii ikifanya ya CCM ile, itafeli kuliko alivyofeli Mkapa na kaumu yake. Miaka kumi ijayo, tutakuja kukaa kuandika makala kama hii ya kueleza uovu wa Rais Kikwete na sio mchango wake kwa ujenzi wa Zanzibar mpya.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.