Mwishoni mwa wiki iliyopita, Wazanzibari waliambiwa tena kupitia kikao cha Baraza la Wawakilishi kwamba kwenye mazungumzo baina ya ofisi ya Waziri Kiongozi wa Zanzibar na ofisi ya Waziri Mkuu wa Tanzania hakuna kikubwa kinachofanyika. Aliyelisema hilo ni mwakilishi wa jimbo la Gando, Said Ali Mbarouk, akitoa dukuduku lake kwa adha waipatayo wafanyabiashara wa Zanzibar wanaoendelea kulipishwa ushuru mara mbili na Mamlaka hiyo hiyo moja ya Mapato (TRA). Hilo likathibitishwa na Waziri wa Nchi, Afisi ya Waziri Kiongozi, Machano Othman Said, ambaye pamoja na kugaragara kote, mwishowe alikiri kwamba ‘ofisi’ hizo zilikuwa zimekutana mara mbili tu, tena tangu mwaka 2006, katika mwezi Mei na Novemba. Mara mbili tu kwa miaka miwili na kwa Muungano unaotimiza sasa miaka 44 ya kushukiana na kugeukana! Sisi wengine tangu mwanzoni tulishuku kwamba, japokuwa katika semina yake elekezi ya Ngurdoto kwenye unyemi wa kuingia kwake madarakani, Rais Jakaya Kikwete aliwataka waziri kiongozi na waziri mkuu wakutane kushughulikia ‘kero’ za Muungano, hakulisema hilo kwa dhati ya nafsi yake.

Nakusudia kusema kuwa si kweli kuwa kuna dhamira ya makusudi ya kutatua matatizo ya Muungano huu, ikiwa kutatua huko kunamaanisha kurejesha japo chembe ya haki iliyopokwa Zanzibar. Ndio maana hata huo mfumo wa kukutana kuyajadili matatizo yenyewe sio, ukiacha pia ukweli kuwa hao wanaokutana pia sio. Nina sababu mbili; moja ni kwa kuwa katika vikao hivyo Tanganyika haiwakilishwi na, pili, ni kuwa wanaoiwakilisha Zanzibar ni wepesi mno katika mizania ya kitaaluma, kisiasa na, hivyo, nguvu za maamuzi.

Kwa maneno machache, vikao hivi vinadhihirisha mambo mawili tu: moja ni kuendelea kuburuzwa kwa Zanzibar katika Muungano huu na jengine ni kizungumkuti cha Muungano wenyewe. Hebu turudi kwenye chanzo cha suala lenyewe, yaani Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uhusiano uliofungwa kwa makubaliano maalum yaliyokuwa na vipengele kumi na moja na kutambulika kama Makubaliano ya Muungano. Yaliyokubaliana yalikuwa madola, mataifa na nchi mbili huru. Na hapa nataka nisisitize tena na tena kwamba msingi wa kuungana kwetu haukuwa idadi ya watu wala ukubwa wa eneo.

Kwa hivyo, si Jitanganyika kubwa na Kijizanzibari kiduchu zilizoungana, bali Tanganyika kama taifa na dola huru na Zanzibar kama taifa na dola huru. Ni dhambi isiyosameheka kuutafsiri, kuuchambua na au kuuendesha Muungano huu kwa misingi wa idadi ya watu na au ukubwa wa eneo.

Tafsiri yoyote ya Muungano huu, uchambuzi na ama uendeshaji wake unatakiwa uakisi hasa msingi wa kuundwa kwake, ambao ni uelewa wa uwepo wa udola na utaifa wa waundaji wake, Tanganyika na Zanzibar.Hapa ndipo ulipo msingi wa kuungana kwetu. Ni msingi huu ndio ninaoutumia kutafsiri vikao hivi baina ya wawakilishi wa SMZ na SMT. Nani na nani? Upande mmoja ni Nahodha na kundi lake akiiwakilisha Zanzibar. Tunaweza kutafautiana juu ya uhalali wa akina Nahodha kushikilia nafasi wanazozishikilia, lakini lazima tukubaliane kuwa utaratibu wa siasa za kilimwengu unazitambua serikali kama mawakala wa dola.

Hivyo, kwa vyovyote vile, hawa wanaiwakilisha Zanzibar kama vile ambavyo miaka 44 nyuma Abeid Amani Karume alifanya. Zanzibar inawakilishwa kwa kuwa ni mzazi mmoja wa mwana anayeitwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Hapa nisisitize tena kwamba jina hilo ndilo jina halisi la Muungano huu, kwa mujibu wa makubaliano, na sio Tanzania.

Upande wa pili kuna mzazi mwengine, Tanganyika. Wanaokuja kwenye mazungumzo kutoka huko, hata hivyo, wanatambuliwa kama mawaziri wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sio wa Tanganyika. Maana yake hawa ni wawakilishi wa mwana ‘Muungano’ aliyezaliwa na wazazi wawili, Tanganyika na Zanzibar na si wawakilishi wa Tanganyika, ambaye ndiye mzazi mweziwe Zanzibar na ndiye ambaye alistahili kuwa wa kuzungumza naye kuhusu matatizo ya mwana wao, kijana ‘Muungano.’

Hapa, hata kwa kiwango cha chini cha utumiaji wa akili, utaona Wazanzibari tunavyoburuzwa. Ati wanaokutana kujadili matatizo ya mtoto ni mtoto mwenyewe (serikali ya Muungano) na mzazi mmoja (serikali ya Zanzibar), badala ya kuwa mzazi na mzazi. Lakini hilo lisingelikuwa kizungumkuti ikiwa mmoja wa wazazi hao alikufa kifo kilichofahamika na kujuilikana. Uhalisia uliopo hapa, hata hivyo, hauoneshi kuwa mzazi huyo, yaani Tanganyika, alikufa, bali kinyume chake ndio ukweli. Kwamba Tanganyika ipo hai, tena hata kimaandishi. Fomu za kuomba kibali cha kuendesha chombo cha moto kutoka nje zinazotolewa na TRA, kwa mfano, zinamtaka muombaji ataje anwani yake atakapokuwa Tanganyika!

Sitaki kutumia makala hii kuonesha kuwepo kwa Tanganyika (nimeshafanya mara nyingi huko nyuma), lakini itoshe kusema hapa kwamba Waziri Mkuu wa Tanzania hana uwezo wa kukutana na kujadiliana Muungano na Waziri Kiongozi wa Zanzibar panapohusika nadharia ya nani kamzaa nani. Kwa mujibu wa makubaliano ya Muungano, Waziri Mkuu anayeiwakilisha serikali ya Muungano ni mwakilishi wa kiumbe. Muumbaji wake, Tanganyika, ndiye hasa aliyepaswa kukutana na muumbaji mwenzake, Zanzibar. Na si kinyume chake.

Kwa hivyo, ikiwa lengo hasa ni kuyajadili matatizo ya Muungano, basi wanaokutana kuyajadili wanakuwa sio. Mjadala huu, kwa hivyo, hauna maana zaidi ya kula pesa za walipa kodi. Hii ni kusema hata hicho kinachoafikiwa katika mjadala wenyewe, hakina maana kwa ustawi wa Muungano kama Muungano, labda iwe kwa Muungano huu kama kitu chengine kama vile ukoloni, kwa mfano.

Hicho ni kizungumkuti kimoja. Lakini chengine, katika vikao hivi ni nafasi ya Rais wa Zanzibar, ambaye kwa mujibu wa Mabadiliko ya Kumi na Moja ya Katiba ya Muungano, anakuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Muungano. Suali la kujiuliza hapa ni kwamba katika vikao hivi anapaswa kuwa upande gani? Wa kuiwakilisha Zanzibar, ambayo yeye ni rais wake au wa kuiwakilisha Tanganyika iliyo nyuma ya Muungano, ambayo yeye ni katika mawaziri wake?

Lakini, kwa manufaa ya mjadala huu, hebu natukubali upotoshaji huu wa dhana halisi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, tuburuzike kwamba hawa wanaokutana ni wawakilishi wa kweli wa pande mbili za Muungano na tujisahaulishe kuhusu dhima ya Rais wa Zanzibar. Basi hata katika hilo, tukipima uzito wa kiujuzi, kitaaluma na kisiasa baina ya wawakilishi hawa wa pande mbili, jibu litakuwa tena lile lile kwamba wanaokutana sio.

‘Sio’ hii ya mara ya pili inamaanisha ukiwapima, kwa mfano, mawaziri wawili wanaoongoza wizara zinazofanana, mmoja kutoka kila upande wa Muungano, utaukuta mpishano mkubwa wa kimizania.

Lichukuwe Baraza zima la Mawaziri la Zanzibar na ulipambanishe na lile la Muungano, utakutana na ukweli mchungu mbele yako. Kwamba ukiacha wale mawaziri na manaibu waziri wachache waliotokea upande wa Zanzibar, Baraza la Mawaziri la Muungano (Bara?) lina ‘wazito’ watupu. Kwamba Baraza la Mawaziri la Zanzibar ni jepesi mno mbele yao na, kwa hiyo, wanaweza kuliburuza (na kwa hakika wanaliburuza hasa) wapendavyo. Kisha mwisho wa siku, Wazanzibari wakinung’unika, huwambia: “lakini haya ndiyo tuliyokubaliana na serikali yenu!”

Sasa nini cha kufanya, ikiwa kweli tunataka kuuimarisha Muungano wa kweli, na sio magube haya yaliyopo. Tuna sehemu mbili za kuanzia ambazo zinaingiliana na kutegemeana.

Pa kwanza ni kuitambua kwa kauli serikali ya Tanganyika. Nasema kwa kauli na sio kivitendo, maana kivitendo serikali hii ipo na inafanya kazi. Lakini kwa makusudi mazima ya kuuficha ukweli, inatakiwa iaminike kuwa hakuna kitu kama Tanganyika. Huo ni uongo ambao umedumu kwa miaka mingi sasa, lakini haujapata kutunufaisha.

Lazima mabadiliko ya makusudi yafanywe sasa katika maandishi yetu ili kuikiri Tanganyika, maana Tanganyika ipo na serikali yake ipo na inafanya kazi kwa jina tu la Muungano. Hilo lifanyike kwa upande wa Bara.

Kwa Zanzibar, ni kuwa na watu katika serikali ambao wana uwezo wa kitaaluma na uzoefu kwenye siasa za ndani na za nje, ili itakapohitajika kufanya majadiliano kuhusu Muungano, Zanzibar iwakilishwe hasa. Waliopo sasa ndio hivyo wapo tu, lakini hawana uwezo wala uthubutu wa kuitetea Zanzibar mbele ya wenzao wa Bara.

Nimesema mawili haya yanaingiliana na kutegemeana kwa kuwa, ili Zanzibar ipate watu wa aina hiyo, mathalan, basi ni lazima siasa za Muungano kuelekea Zanzibar zibadilike. Zibadilikeje? Ikiwa Tanganyika itajitokeza dhahiri shahiri, basi haitakuwa tena na la kupoteza kwa kuwepo Zanzibar kama Zanzibar. Maana sasa itakuwa haingalii Zanzibar kwa jicho la husuda la sasa kama mshindani wake, bali kama mshiriki mwenzake.

Likitokezea hilo, basi Wazanzibari watakuwa na uwezo wa kuwapata wawakilishi halali na wenye uwezo wa kitaaluma na kisiasa kujadiliana na wenzao sio kuhusiana na Muungano huu tu, bali hata Shirikisho la Afrika Mashariki na, au, la Afrika, bila ya gubu lolote kutokea Bara. Haitakuwa tena lazima kwa Bara kusimika utawala inaoutaka Zanzibar kusudi ipate kuutumilia, maana ustawi wa Zanzibar utakuwa ni muhimu kwa uhusiano wa Tanganyika na Zanzibar, kwa upande mmoja, na uhusiano wa Muungano huu na nchi nyengine za Afrika Mashariki na Afrika nzima, kwa upande mwengine.

Hadi hapo mawili hayo yatakapofanyika, Zanzibar itaendelea kuburuzwa katika vikao hivi vya undumilakuwili, ambapo mawaziri wa Muungano watakuja wakiiwakilisha Tanganyika kwa uso mmoja na uso mwengine wakiwa mahakimu wa Muungano. Kila siku, Zanzibar itaendelea kuonekana kama inasaidiwa tu, na sio kupewa kilicho stahiki yake na malalamiko ya akina Said Ali Mbarouk hayatanyamazapo.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.