Hakuna la ajabu lililotokea. Nisameheni kwa kusema hivyo, lakini narudia, kilichofanywa majuzi na kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Butiama, kilikuwa kitu cha kawaida kwa chama hicho. Kuukana muafaka wa kisiasa wa Zanzibar ni kitu cha mwanzo kilichotarajiwa. Kuukubali kilikuwa kitu cha mwisho. 

Wao wamefanya cha mwanzo, kwa hivyo wamefanya jambo la kawaida sana. Ajabu ingelikuwa kama wangeliukubali na kuupa baraka zake. Kwamba, hata kama wangefanya hivyo, basi wengine tungebakia na shaka na shukuki kwamba hawa jamaa wanakusudia kuikwamisha nchi pahala. Haiwezekani wakubali tu kirahisirahisi.

Hao ndio CCM. Mzee Shaaban Mloo, mwanasiasa wa siku nyingi wa Zanzibar, aliwahi kusema kwamba CCM wakikwambia wanakwenda Tabora, kawasubiri Mtwara. Ndivyo walivyo. Wageuzi wa kauli zao na watu wa nyuso mbili. Kuwaamini ni kosa nambari moja na kuwashuku ni halali kabisa. Nakusudia kusema kuwa ukiwaamini CCM umekosea, lakini ukiwatilia shaka umepatia!

Sitaki kuamini kwamba kilichowafanya wakatae hoja na haja ya kuundwa kwa serikali ya pamoja Zanzibar ni haraka ya Chama cha Wananchi (CUF) kuyataja hadharani makubaliano yao waliyoyafanya faraghani. Eti kwamba hilo limezua tafrani miongoni mwa viongozi wa CCM na wanachama wao.

Hicho ni kisingizio tu, ukweli ni kuwa tangu awali maamuzi yalikuwa yawe hivyo. Kwamba wakae na CUF shudu ya kukaa, kisha mwisho wa siku kila mwana ashike njia yake, lolote lisiwe. CCM ilijuwa itafanya hivyo. Hata kama wangelikaa kimya, bado uamuzi wa kuzuia makubaliano ya Zanzibar na Wazanzibari ni ajenda ya ndani nay a siku nyingi ya chama hiki tawala. Kwa Chimwaga, Zanzibar ni ya kuwachwa ikaselelea kwenye chuki, fitina na uhasama usiokwisha ili izidi kutawalika kirahisi.

Vile vile sitaki kuamini kwamba CCM wameliakhirisha tu suala hilo hadi hapo ajenda hiyo itakaporudishwa kwa wanachama wa kawaida kujadiliwa na kufanyiwa maamuzi. Hakuna utaratibu kama huo kwa chama hiki wa maamuzi kutoka chini yakaenda juu. Hakuna hata kwa vyama vyengine vya kidemokrasia zaidi huko duniani.

Ukiwa kiongozi wa chama, maana yake kikatiba na kitamaduni umekabidhiwa dhamana na wanachama wako kufanya maamuzi kupitia vikao vyenu halali kwa mujibu na kwa maslahi ya chama chako. CCM isinambie kwamba inakuja sasa kumuuliza mzee wangu, Mcha Silima wa Matemwe, ikiwa iingie kwenye serikali ya pamoja na CUF au la! La wazi na la karibu zaidi kuliona ni kwamba, umoja wa kitaifa Zanzibar si kwa maslahi ya CCM kama mtawala. Tena na tena, nitarudia neno hili: Zanzibar iliyogawika ni akhuweni kubwa kwa Chimwaga.

Sitaki kuamini pia kwamba, CUF ilisema uongo ilipoutangazia umma kuwa kipengele cha serikali ya umoja wa kitaifa kabla ya 2010 kilijadiliwa kwa upana na urefu baina ya timu mbili za CUF na CCM na hatimaye kufikiwa makubaliano. Ina ushahidi wa kutosha wa kuuwasilisha hata mahakamani ikitaka, kwamba ilikubaliana kadhaa na kadha.

Lakini, kuna uwezekano mkubwa sana kwamba uongozi wa CUF nao ulikuwa na mawazo ya wengi wetu, kwamba CCM hawaaminiki. Kwamba huenda wakayakhalifu hadharani tuliyokubaliana faraghani. Kwa hivyo, wakaamua kuyasema na mapema kwa moja kati ya dhamira hizi tatu: ama kuondoa uwezekano wa kusalitiwa mwishoni, au kuwajengea wenzao wa CCM uthubutu wa kufanya maamuzi magumu ya kukubalia walichokubaliana na, au, angalau kujivua na lawama, hasa zetu waandishi ambao kila siku tuliwasema kwa kuyafanya mazungumzo ya nchi kuwa kijaluba chao wenyewe tu.

Kitu pekee ninachotaka kuamini ni hicho nilichokionesha mwanzoni, kwamba CCM imefanya u-CCM wake tu, ugeugeu. Imegeuka kwenye mpindo na imeitosa Zanzibar. Kwamba ilikuwa inanunua muda kwa siku zote hizo na sasa imeupata wa kutosha, imeridhika na imefanya kile ilichokikusudia tangu asubuhi.

Nataka pia niamini kitu chengine cha ziada, kwamba CCM haikufanya hivi kwa bahati mbaya, bali kwa makusudi. Na makusudi hiyo ndiyo inayoogofya na kuchukiza. Mwaka mmoja uliopita, niliwahi kuandika kwenye gazeti hili hili khofu zangu kwa muendelezo na maendeleo ya mazungumzo baina ya CUF na CCM, hasa kwa kurejea misimamo mikali iliyokuwa imeoneshwa na akina Ali Juma Shamuhuna dhidi ya mazungumzo hayo.

Wakati huo wale tuwaitao ‘wahafidhina’ wa Zanzibar walikuwa wameonesha kukasirishwa na hata kule kuwepo kwa wazo la mazungumzo yenyewe tu, sambe yatakayokubaliwa kwenye mazungumzo hayo. Na miongoni mwa hoja walizozitumia ni hizo hizo kwamba wanachama wao hawakuwa wakitaka mazungumzo yoyote na CUF zaidi ya CUF kuitambua serikali na kufanya nayo kazi.

Nikasema kwamba angalau kuna nadharia tatu ya kuiilezea misimamo hii. Kwamba, moja ni kuwa huo ulikuwa ndio msimamo wa CCM nzima, yaani Bara na Zanzibar, pili, huo ulikuwa ni msimamo wa CCM Zanzibar peke yake na, au, tatu, ulikuwa ni msimamo wa wana-CCM mmoja mmoja wa Zanzibar, na wakati huo Shamuhuna alikuwa ndiye mfano wa karibu.

Nikasema lolote kati ya hayo linawezekana, lakini la hatari zaidi kwa Zanzibar ni ikiwa huo ndio uliokuwa msimamo wa CCM nzima, maana kama ulikuwa wa CCM Zanzibar peke yake au wa wana-CCM mmoja mmoja tu, CCM yenyewe inajuwa namna ya kushughulika nao. Ni weledi wa kazi hiyo wala hawataki washauri.

Sasa tumeshuhudia kwamba uwezekano ulikuwa ni ule wa mwanzo, yaani ule ulikuwa ni msimamo wa CCM nzima, na kwamba wale waliokuwa wakipaza sauti zao kutokea Zanzibar, walikuwa wakiakisi tu yale yaliyokuwa yakisemwa ‘ndani’ ya vikao vya ndani kwa undani. Wenzangu miye wakawa hawawezi midomo yao, hivyo wakija nje wakayatapika yale yote yaliyopangwa na kudadauliwa (kwa kutumia Kiswahili cha Tanganyika).

Ningekuwa na akili ya kuona mbali wakati ule, ilikuwa niandike kuwashukuru kwa kuwaonya Wazanzibari kwamba wasipotezewe muda na kujengewa matumaini ya bure. Kwa hakika hicho ndicho walichokuwa wakikifanya Wazanzibari wenzetu wale. Haki yao tuwape hata kama walikifanya kwa nia na njia zao wenyewe.

Wakati wajumbe wa vikao hivyo vya Butiama wakiondoka Zanzibar majuzi, palikuwa pamezuka vijineno kwamba wanakwenda kuukwamisha muafaka na kwamba eti akina Rais Jakaya Kikwete na watu wake walikuwa wamekusudia kuusimamisha muafaka na CUF. Haikuwa kweli. Haiminiki kuwa CCM Bara ilikuwa imesimamia dhamira yake ya kuiona Zanzibar ikiondokana na mkwamo wake wa siku zote, lakini ikaelemewa sana na wenzao wa Zanzibar, nayo ikabwaga manyanga. Si kweli hata kidogo kwamba jambo hili limekwamishwa na CCM Zanzibar tu. Si kweli hata kidogo.

Kwa nini si kweli? Nimekuwa nikiishi na sijali ikiwa nitakufa na imani kwamba, kwa CCM yenyewe hasa (nikisema ‘yenyewe hasa’ nakusudia CCM Bara), Zanzibar ni afadhali iwemo kwenye mgogoro wa maisha kuliko kuwa katika makubaliano hata ya mwezi mmoja. Mimi nahusisha moja kwa moja kutokupitishwa kwa hoja na haja ya serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar na siasa za Muungano kuelekea Zanzibar. Kwa Chimwaga, ni bora kuwa na Zanzibar iliyogawika, ambayo ni rahisi kusarifika kuliko kuwa na Zanzibar iliyoungana, ambayo wanaamini ni ngumu mno kutawalika.

Kiongozi yeyote anayeshikilia madaraka Tanganyika, lazima awe na uwezo wa kumuweka na kumsanifu atakavyo mwenzake wa Zanzibar na wao wanadhani kuwa pakiwa na serikali ya pamoja, hilo halitawezekana. Inawezekana ni kweli CCM Zanzibar hawaitaki, lakini sababu yao ya kutokuitaka ni tafauti kabisa na sababu iliyotumiwa na wenzao Bara kuizuia. Ilhali CCM Zanzibar hawataki serikali ya pamoja na CUF kwa kukhofia kupoteza vyeo na ulwa, wenzao wa Bara hawaitaki kwa kuchelea kupoteza satwa yake kama nchi na si kama chama.

Huenda, kwa hivyo, hivi sasa CCM Zanzibar wanachekelea kwa kuwa serikali ya aina hiyo imezuiwa kuwepo, lakini bei ya kicheko hicho ni utu na heshima yao na ya nchi yao, Zanzibar. Kwamba mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar ni ni kijaluba kilichotayarishwa Bara, huko ndiko kwenye baraka na msingi wake. Nitakuwa Mzanzibari wa mwisho kuamini kuwa eti Chimwaga ina nia njema na Zanzibar.

Na Rais Kikwete? Huyu ni mwana-CCM kwanza, tena ndiye mwenyekiti wa chama hicho, halafu ndiyo ni mtu mwengine. Ikiwa ni katika sera za dhahiri au za siri za chama chake kuwa na Zanzibar mbovu inayotawalika kirahisi, ni yeye ndiye msimamizi mkuu wa sera hiyo. Jukumu lake la mwanzo ni kuhakikisha kuwa dhamira na muono wa sera hiyo unafanikiwa. Ndivyo anavyofanya na ndivyo atakavyofanya.

Sasa nini kinakuja? Mengi, lakini mambo matatu yatakuja haraka haraka, pengine hata kuanzia leo. Moja, kama alivyofanya Benjamin Mkapa, Rais Kikwete naye atatumia nguvu za ziada za dola kuanzia sasa kukabiliana na chochote atakachohisi kiko kinyume na maslahi ya chama chake Zanzibar.

Kwa hivyo, Wazanzibari tutegemee kurudi kwa mkong’oto ambao ‘tumeu-miss’ sana kwa kipindi chote hiki cha miaka miwili ya mazungumzo. Mwaka 2010, kama kutakuwa na uchaguzi, Zanzibar itageuzwa tena kuwa kituo cha kijeshi. Wanajeshi kutoka Mrima, na ikibidi hata wa kuazimwa kutoka kwengineko, watamwagwa hapa na silaha nzito nzito. Kikwete atakuwa anataka kumuweka mtu wake kama Mkapa alivyokuwa akifanya.

La pili, ni kuongezeka kwa manung’uniko ya chini kwa chini ya Wazanzibari na kurudi hali ya kutokuaminiana baina yetu. Ile chuki ndio kama imeanzishwa upya sasa. Kama kulikuwa na chembe ya imani iliyokwishaanza kujengeka baina yetu, basi ndio imekwenda na maji. Hilo, kisaikolojia na kishakhsia, litazidi kuitia ufukara Zanzibar. kwa hivyo, tutegemee hali ya maisha kuzidi kuwa ngumu, maana nafsi zetu zina fukuto la ndani na la hasira.

La tatu, na la uhakika zaidi ni kupanda kwa hisia kali za kisiasa. Ikiwa kila siku tulikuwa tukiwalaumu CCM Zanzibar kwa uhafidhina, hivi sasa kuna kila dalili za uhafidhina kuhamia upande wa pili pia, yaani CUF. Bila ya shaka, uongozi wa CUF utakuwa na kazi ya ziada ya kujenga muelekeo mpya wa kisiasa. Sitarajii hata kidogo kwamba uhafidhina huo mpya utakuwa na sura ya kijeshi, lakini natarajia sana utakuwa na changamoto kubwa si kwa CUF tu, bali kwa nchi kwa jumla.

CCM ndio wameendelea kuitosa Zanzibar hivyo. Kikwete ndio ameshazima njozi zote. Wanasema eti wanalirudisha jambo hili kwa wananchi. Lakini wakati wao wakienda kutaka maoni ya watu wao kuhusu serikali ya pamoja Zanzibar, si hasha Wazanzibari nao wakataka maoni ya umma kuhusu hoja na haja ya kuendelea kuwepo kwa Muungano. Tusubiri tuone khatima.

 

One thought on “Huyu ndiye Kikwete na hii ndiyo CCM”

  1. HOW CAN WE STILL HAVE A DOUGHT ABOUT ZANZIBAR? AND WHAT WILL THE PROBLEM IF DEPART WITH ZANZIBAR?

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.