Nipo nje ya nyumbani kwa wiki moja na kitu sasa, lakini nafuatilia kwa karibu, kupitia mitandao, mambo yanavyoendelea kwetu. Nimeona kuwa kwa mara nyengine tena, Zanzibar imeonekana kwenye magazeti ya Tanganyika. Wenyewe, ukimtoa Mchungaji Christopher Mtikila na kaumu yake, hawataki waitwe Watanganyika. Wanajidai kwamba kuna Tanzania tu. Hata sherehe za jana za uhuru wa Disemba 9, wanaziita ni za uhuru wa Tanzania. Unafiki mtupu!

Alaakullihali, turudi kwenye nukta. Zanzibar imetajwa katika magazeti ya Tanganyika kwa matukio mawili: moja ni lile linalohusiana na kadhia ya Jumuiya ya Kiislam (OIC) na la pili ni la uchimbwaji wa mafuta. Yote mawili yamezishirikisha serikali, wawakilishi, wanasiasa na wananchi wa kawaida.

La kukumbushia Zanzibar kurejesha uanachama wake OIC, liliibuliwa, kama kawaida, na Chama cha Wananchi (CUF). Nasema kama kawaida, maana imekuwa ni ishara ya CUF kuipigania Zanzibar pahala popote pale wanapopata nafasi. Mimi ni katika watu wanaoamini kwamba miongoni mwa mambo makubwa ambayo yamewafanya CUF wafanikiwe Zanzibar, ni kujinasibisha kwao na usemaji na utetezi wa Zanzibar, eneo ambalo wenzao wa Chama cha Mapinduzi (CCM), labda kwa woga na hisia za kulipa fadhila, wako ziro kabisa.

Katika semina ya kujadili Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania iliyofanyika Zanzibar mwishoni mwa mwezi uliopita, wawakilishi Said Ali Mbarouk na Rashid Saleh walisema kwamba umeshafika wakati wa Zanzibar kurudi katika jumuiya hiyo ya Kiislam, kwa hoja kwamba sasa sera ya nchi imebadilika kutoka ile ya kuzingatia siasa tu kwenye mahusiano na kuwa ile inayozingatia uchumi. Economic diplomacy, wasemavyo Waingereza.

Kwenye semina hiyo, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, alihudhuria, jibu la Serikali ya Muungano (SMT), kupitia kwake Waziri Membe, lilikuwa kwamba jambo hilo linajadilika, na akatoa matumaini kana kwamba litajadiliwa kweli. Lakini alikuwa anacheza siasa tu kwa kuwa alikuwa kwenye jukwaa la Zanzibar, mbele ya watu wanaojinasibisha na Uzanzibari wao. Kwa mtu kama yeye, ambaye ametokea kwenye system, anajuwa namna ya kucheza na akili za watu. Na akacheza nazo.

Jibu hilo halikuipendeza kaumu ya Mchungaji Mtikila. Na kwa kuwa Makamo wa Rais, Ali Mohammed Shein (mwenyewe Mzanzibari na Muislam), alikuwa ndio kwanza amerudi ziara ya nchi za Misri na Iran, Mtikila akaunganisha yote mawili kuongelea kitu kimoja: chuki binafsi dhidi ya Uislam na Uzanzibari. Halafu, kama mchezo wa kuigiza, Wazanzibari nao wakaingia kichwa kichwa kuelekeza hasira zao kwa Mtikila kama kwamba ni yeye ndiye anayeizuia Zanzibar kupata haki zake katika kizungumkuti hiki cha Muungano.

Kwenye mtandao wa zanzinet.org, jukwaa la Wazanzibari linalojadili mausala mbali mbali kuhusu nchi yao, nilisoma maoni ya wachangiaji wengi wakimtaka Mtikila afumbe mdomo wake panapohusika masuala ya Zanzibar. ’Akosaye la kufanya, azinge mwana akalee’, mchango mmoja ulimwambia hivyo Mtikila ukimfananisha na mtu ambaye hana kazi ya kufanya. Lakini huko kulikuwa, na kumeendelea kuwa, sehemu ya mikakati ya SMT kupindisha hoja muhimu, hasa panapohusika hizi za Zanzibar.

Nimesema kwamba Waziri Membe alikuwa akicheza politiki tu kule Zanzibar kuonesha kuwa eti kuna uwezekano wa kulijadili suala la Zanzibar na OIC. Ukweli hasa amekuja kuutoa Hussein Mwinyi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo Rais (Muungano), aliyesema wazi, Alhamis iliyopita, kwamba hakuna suala la mjadala katika hilo. Kwamba inayoweza kujiunga na OIC ni Tanzania, ikitaka, maana ndiyo nchi. Kwamba chini ya Katiba, si sawa kwa Zanzibar kuingia mashirikiano kama hayo. Huo ndio ukweli mkavu kutoka kwenye kinywa cha SMT yenyewe.

Lakini katika aliyoyasema Waziri Mwinyi siku hiyo hiyo ni kwamba mafuta ya Zanzibar hayajaweza kuchimbika kwa kuwa kwenye Tume ya Pamoja wa Waziri Mkuu Edward Lowassa na Waziri Kiongozi Shamsi Nahodha hakujakuwa na makubaliano. Hakusema, hata hivyo, ikiwa kilichokuwa hakijaafikiwa kinatokana na kukataa kwa nani, ingawa dhana inatwambia kwamba wanaokataa ni akina Waziri Kiongozi Nahodha.

Huku nako kulikuwa ni kuweka mizani baina ya mambo mawili tete. Upande mmoja wa mizani kuna ukweli kwamba suala la Zanzibar na OIC ndio limekwisha, vyenginevyo Katiba ibadilishwe. Uzoefu unaonesha hakuna kitu kama hicho, yaani kuibadilisha Katiba kwa kufuata matakwa ya Zanzibar, bali kilichopo ni kinyume chake, yaani kuibadilisha Katiba kwa kuikandamiza Zanzibar. Wamefanya hivyo takribani mara 14 tangu mwaka 1964. Upande huo wa mizani unatwambia wazi kuwa Wazanzibari tumepoteza.

Upande mwengine wa mizani umetengenezwa utuoneshe kuwa eti tuko madhubuti. Si akina Waziri Kiongozi Shamsi, Wazanzibari, ’wameweka ngumu’ na akina Waziri Mkuu Lowassa, Watanganyika, wameshindwa kuyachimba? Si umadhubuti wa viongozi wetu huo?

Lakini ukweli, hata kwa hili uko tafauti na hapo. Nitakuwa mtu wa mwisho kuamini kuwa Watanganyika wameshindwa kuyachimba mafuta ya Wazanzibari ati kwa kuwa Wazanzibari hao wameonesha ’ukaidi’ wa kuelewa (kama wanavyotwambia). Siamini ikiwa kweli hawa jamaa wamedhamiria kuyachimba mafuta yetu, watahitaji ridhaa yoyote kutoka kwetu. Hakuna uzoefu huo, na hauwezi kuwepo sasa. Hawa jamaa wakitaka kufanya leo kwetu hulifanya tu bila ya kujali hisia wala hasira zetu.

Hoja ninayojaribu kuiwasilisha mbele yako hapa ni kwamba, panapohusika Muungano na nguvu za Tanganyika kwa Zanzibar, chini ya utawala wa CCM, hakuna kitu kama hiari. Ni kile kinachoamuliwa na Tanganyika ndicho ’kizuri’ na kinachofanyika Zanzibar, kutoka kuamua nani awe raisi wetu hadi vipi raisi huyo aiongoze Zanzibar yetu.

Na huo nao ndio ukweli mkavu. Siku watakayoamua, watayachimba. Sababu wanazo, uwezo wanao na nguvu za kufanya hivyo wanazo. Naomba nieleweke, kwamba sizungumzii uhalali wa Tanganyika kuyachimba mafuta ya Wazanzibari, bali nazungumzia kwamba uwezekano wa kufanya hivyo kuwa upo.

Labda kwa kuandika hivi kuna watu watakaonichukulia kuwa ni Mzanzibari niliyekwishavunjika moyo na hatima ya nchi yangu ndani ya kizungumkuti cha Muungano huu, kwa upande mmoja, na wale watakaonichukulia nanuka ubaguzi, kwa upande mwengine. Wa mwanzo ni Wazanzibari wenzangu, naamini, na wa pili ni Watanganyika au kaumu yao, nadhani.

Kwa makundi yote mawili, mimi si mtu wa kuvunjika moyo kiasi hicho. Nimezaliwa miaka 13 baada ya Muungano wa 1964 ulioichukua Zanzibar kimzobezobe, na tayari nilifumbua macho nikikuta kwamba ’natakiwa kuisahau Zanzibar.’ Ndivyo mfumo unavyotutayarisha sote. Lakini, kama ilivyo kwa mamia ya maelfu ya Wazanzibari wengine, nimegoma kuisahau nchi yangu na kuuzika Uzanzibari wangu.

Tunawaachia wanaokaa madarakani kuifanya kazi hiyo ya kuizika Zanzibar, lakini sisi tulio nje ya madaraka tumekataa kuhudhuria maziko wala kukaa matanga ya kifo cha Mama yetu, Zanzibar. Bado tuna moyo. Moyo wa kwamba Zanzibar ipo daima, ilikuwepo jana, ipo leo na itakuwepo kesho…… na milele.

Akina Mtikila wanatwambia tuache kabisa kufikiria OIC ndani ya Muungano. Kwamba ikiwa tunataka kufanya hilo, labda tujitoe kwenye Muungano.

Pamoja na ukweli kwamba hata pale Julius Nyerere alipomlazimisha Salmin Amour kujitoa kwenye jumuiya hiyo kwa kuwa alikiuka Katiba, alikuwa, yeye mwenyewe Nyerere, anavunja Katiba, maana hadi hapo ushirikiano wa kimataifa haikuwa sehemu ya mambo ya Muungano, bado akina Mtikila wasidhani kwamba ni Wazanzibari wenye shida ya Muungano katika kiwango hicho cha kutwambia, ama tubakie au tutoke.

Ni kiwango cha mwisho cha matusi kwetu, Wazanzibari. Hata kama tunajuwa kuwa watawala wetu wanaung’ang’ania Muungano huu na mfumo wake kwa kuwa ndio wanaoutumilia kujiweka na kujirejesha madarakani, hilo halitujumuishi sote katika kundi moja. Waingereza walimwambia Tony Blair alipoamua kushirikiana na George Bush kwenda kuivamia Iraq: ’Not in our name.’ Vivyo ni kwa sisi, Wazanzibari.

Ni kosa kudhani kwamba udhalilifu wote unaofanywa na utawala wa Tanganyika dhidi ya Zanzibar mbele ya macho ya hao waitwao viongozi wa Zanzibar, hufanyika kwa baraka zetu. Hapana. Na kwa uelewa huo, basi tusipeane ‘ultimatum’.

2 thoughts on “Zanzibar Daima…jana, leo na kesho”

  1. bulbul! bakhti ndio kwanza leo kwa mara ya kwanza nakumbana na blog hii ,hakiak nna staladh na kula makala ,,ustadh mohammed endelea na mchango wako wa uzanzibar ,wengi wanahitajia kufumbuliwa macho na kufahamu ukweli wa njama za tanganyika dhidi ya unguja! keep it up

  2. Kaka hongera sana kwa mawazo mazuri, lakini mm binafsi kila siku najiuliza hivyo kwanini Zanzibar ni kisiwa kidogo na kina matatizo mengi ambayo yanatufanya tusiendelee? Na nimekuwa nikilifanyia kazi swali hilo kila siku, nahisi jibu lake ni wazanzibar wenyewe, how? Ni UBAGUZI WAO wa Mpemba, Muunguja, mwenye rangi na aso na rangi na hata vyama vikuu vya siasa Zanzibar wananchi na viongozi wapo katika misingi hiyo hiyo. Hali hii inaifanya Zanzibar kuto endelea na adui to take advantages however watu wengi wanaisigizia T. BARA but inahusika lakini Wanzanzibar wenyewe ndo wamwazo.Samahani kama nimekosea ni mawazo yangu, AS YOU KNOW “NO BODY IS PERFECT”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.