znz

Tarehe 19 Novemba 2007 ni siku nitakayoikumbuka daima, si kwa ubaya bali kwa wema. Ilikuwa ni siku ambayo, kama Mzanzibari, nilikumbushwa na wenye mamlaka hapa Dar es Salaam kwamba Tanganyika ipo na kwamba mimi si petu, bali ni raia wa kigeni kama walivyo wageni wengine tu. Moyoni mwangu nilifurahi ukomo wa furaha, hata kama tukio lililopekea kukumbushwa huko lilikuwa na ikirahi kidogo. Nitalielezea kwa muhtasari.

Kuna gari ambayo imeletwa kutoka Zanzibar na ambayo ipo chini ya dhamana yangu. Gari hii ina nambari za usajili za Zanzibar (maarufu huwa tunaziita nambari hizo ZNZ). Rafiki yangu anaichukuwa kutoka chuoni pangu Tumaini kilichopo Kinondoni na kwenda Temeke kuirekebisha baadhi ya mambo. Nusu saa tu baada ya kuondoka, ananipigia simu kwamba amekamatwa na jamaa wa Majembe Auction Mart katika eneo la Chang’ombe kwa kuwa gari hiyo hairuhusiwi kutembea bila kibali maalum.

Suluhisho la haraka ni gari kushikiliwa na wakala hao wa udalali, huku hatua za kutatua tatizo hilo zikifuatiliwa. Chuoni kwetu huu ni wakati wa mitihani ya katikati ya muhula, hivyo kila dakika moja kwenye masomo ni muhimu kwangu, hasa kwa kuwa msimu wote huu wa masomo nimekuwa nikipatwa na mitihani ya hapa na pale, ambayo imeathiri uwezo na ushiriki wangu kwenye masomo.

Lakini hapa kisu kimefika mfupa. Inabidi kuifuatia gari Majembe kwenye ‘jalala’ lao la Mwenge. Naliita jalala kwa kuwa limekaa shaghala baghala na sina uhakika sana na usalama wa magari mazuri mazuri niliyoyakuta pale yakiwa pamoja na gari yangu. Sina lawama yoyote, kimsingi, dhidi ya Majembe, maana wao ni wakala tu wa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA), ambayo sisi Wazanzibari tulishasema tangu zamani kuwa ni alama nyengine ya udhalimu dhidi ya nchi yetu.

Hata kama hakuna anayetusikiliza tunaposema hivyo, lakini kutokusikilizwa kwetu hakubadilishi imani yetu kwa taasisi hii ambayo tunaamini kufanywa kwake kuwa chombo cha Muungano kulikusudiwa, kwa makusudi hasa, kuihusudi Zanzibar kiuchumi. Nilimwambia hivyo yule mama wa TRA kule Kinondoni na nikamkumbusha kwamba, hata kama anafanya kazi ya kutumikia ‘mfumo’ uliopo tu, ambao yeye si mwasisi wake na ni mtenzwa kama nilivyo mimi, hapaswi kuionea fahari kazi anayoifanya, maana ni ya dhuluma. Anatumikia mfumo wa kidhuluma dhidi ya Wazanzibari.

Ni TRA, kwa hivyo, ndio walioshikilia gari yangu kwa sababu ina nambari za nchi ya kigeni, Zanzibar. Majembe wakaniandikia risiti inayoonesha hilo na kuniongoza niende Ofisi za TRA Kinondoni kulipia na baadaye nirudi kuchukua gari yangu. Laitani ingelikuwa rahisi kiasi hicho!

Ni katika ofisi za TRA Kinondoni ndipo suala zima lilipowekwa wazi mbele yangu. Pale mapokezi nikaelekezwa kwenda kumuona “mama mmoja hapo ndani mkono wa kulia.” Nikaenda kumuona huyo mama mwenyewe.

“Una shida gani?”

“Gari yangu imekamatwa na Majembe kwa kuwa na nambari za Zanzibar. Nimetakiwa kuja kulipia ili nikaikombowe.” Nikamjibu.

“Sasa kwa nini usibadilishe nambari basi, ikawa na za hapa!?” Labda alikusudia liwe nusu suali na nusu pendekezo. Mwenyewe, kwa kuwa ni muhanga wa kizungumkuti cha Muungano, nikachukulia kuwa ni nusu dharau kwa nchi yangu ya Zanzibar na nusu ghiliba kwa utambulisho wangu.

“Mama, mimi ni Mzanzibari na ningetaka kila kitu changu kibakie na utambulisho wa nchi yangu. Nataka kuendelea na nambari zangu za Zanzibar.” Jibu hili lilimkasirisha yule mama, kwa namna nilivyomuona usoni mwake. Hawa jamaa hawataki kutajiwa kwamba kuna nchi inaitwa Zanzibar, kuna watu wanaitwa Wazanzibari na kuna utambulisho unaitwa Uzanzibari. Hawataki kutajiwa hayo hata kama wanayajuwa na wanayafanyia kazi kweli kweli kuyamaliza. Mfumo mzima umejengwa hivyo. Ishi hapa Tanganyika na uende kwenye taasisi zao, uone Zanzibar inayowepesishwa!

“Hayo makubwa,” ilikuwa lugha ya mipasho ya mama zetu. “Ngoja basi.” Mara akanyanyua simu. “Bosi, hapa pana foreign vehicle case.” Vipi? Foreign vehicle case? (kesi ya gari kutoka nchi ya kigeni). Alaa, kumbe hivyo ndivyo inavyochukuliwa Zanzibar hapa Tanganyika?

Sikujuwa ni wakati gani neno Alhamdulillah lilinitoka. Mungu anipe nini tena zaidi ya fahari hii ya nchi yangu kutambuliwa kuwa ni nchi mbali, tena ya kigeni, na upande wa pili wa unaoitwa Muungano, kwa ndugu zetu wa damu? Sikuwa nimewahi kupokea zawadi adhimu kama hii kwa siku nyingi. Lazima nikiri!

Yule bosi akatoa maelekezo yake. Kwamba madhali gari hiyo imekamatwa kwenye wilaya ya Temeke, basi hiyo kesi imalizwe na TRA Temeke. Wakati huo ilikuwa tayari saa 10.00 jioni. Msongomano wa magari hapa Dar es Salaam kwa wakati huo, ambapo Dar huwa inarudi nyumbani kulala, haukuruhusu kuwahi kufika Temeke kabla ya saa 11.00 ambapo ofisi za TRA huwa zinafungwa. Hivyo, hiyo ingekuwa kesi ya kesho yake na huko kungekuwa kuwapa Majembe fedha zaidi za kushikilia.

Na ndivyo ilivyokuwa. Hata pale Temeke, walijidai hawakuwa hawajui namna ya kushughulikia kesi kama yangu ya gari ‘kutoka nchi ya kigeni.’ Nao pia wakanishauri nibadilishe nambari. “Utasumbuka na kuliwa pesa zako bure, ndugu yangu. Hata kama watakupa hicho kibali, itabidi kila mwezi ulipe dola 20….kama utakipata, maana siku hizi ni wagumu sana. Kwa nini usibadilishe tu nambari?” Ndivyo alivyoniambia yule Bwana niliyekutanishwa naye, eti akijifanya mwema sana kwangu!

Dharau na ghilba ile ile. Ni dharau kwa kuwa kama tayari wameshaitambua gari yangu kwamba inatoka nchi ya kigeni, wanaitakia nini kuwa na nambari za hapa? Ili nchi yangu ya kigeni isahaulike kwenye rikodi? Ili uwepo wake usionekane? Ni ghilba kwa kuwa wananitega kuwa aidha niukane Uzanzibari wangu ili niruhusiwe kuendesha gari yangu kwenye nchi yao, au waendelee kunisumbua na wanililie pesa yangu ili nibakie na utambulisho wangu. Nikachagua la pili, kama ambavyo Mzanzibari angefanya katika mazingira yoyote anayotakiwa kuchagua baina ya Uzanzibari wake – na kama ana ubavu wa kufanya hivyo!

“Sijali hata kusumbuka wala kulipia. Hata kama itanichukua mwezi mzima kupata kibali hicho na itakuwa dola 100 kwa mwezi, niko tayari kuubakisha utambulisho wa Uzanzibari wangu. Ninachotaka ni gari yangu kuwa na nambari zake za ZNZ.” Sina hakika ikiwa alitarajia jibu kama lile, lakini yule bwana hakuonesha kama ameshitushwa nalo. Labda Wazanzibari wengine wameshawahi kumpa majibu kama hayo huko nyuma, kwa hivyo haikuwa ajabu kwake.

Lakini hata baada ya hakikisho hilo, bado nilielekezwa kwenda ofisi za TRA zilizoko Samora House, mtaa wa Samora, mjini. Jibu la kule lilikuwa fupi na kukatisha tamaa. “Hatutoi vibali.” Hata kusikilizwa, ilibidi niombe sana seuze kukubaliwa nilitakalo. “Basi nenda kwa msajili wa magari.” Ofisi nyengine ya TRA, pale karibu na bandari ya kupandia meli za kwendea kwetu.

Lakini mimi ni Mzanzibari. Ninajuwa kuwa kuna njia za kushughulika na hawa jamaa hapa. Badala ya kwenda kule nilikoelekezwa, ‘nikapotea njia’ na ‘nikasahau’ namba ya mlango niliofahamishwa, nikaangukia ghorofa ya saba, kwa mkurugenzi mwenyewe. Maridadi kama alivyo, nilipoingia alikuwa anaongea na simu na rafiki yake kuhusu mafanikio yao ya kimaisha, kielimu. Wakawa wanapongezana. Alipomaliza akanigeukia, nikajitambulisha na kumueleza shida yangu.

“Hatutoi vibali.” Jibu lake lilikuwa lile lile, lakini kama kuna kitu ambacho maisha yangu yamenifundisha kwa mafanikio kabia ni kuwa nisiwe mtu wa kukubali kushindwa kirahisi hivyo. Nikamuonesha hoja ya mimi kupewa kibali, na kwamba sina mpango wowote wa kubadilisha nambari ya gari yangu hata kama nitaendelea kuwa mgeni siku zote, maana kwa hakika mimi ni raia wa kigeni kweli hapa, au angalau ningependa nionekane hivyo.

“Muna hoja gani ya msingi ya kuzuia gari yangu kupata kibali?” Lilikuwa suali langu la nne. “Sisi hatuna database ya magari ya Unguja. Watu wengine wanatumia magari hayo kufanyia wizi.” Hili lilikuwa jibu la kufunika kombe.

Mbona wizi unafanywa kwa magari yanayotoka Arusha, Morogoro na kwengineko, na wala hawatakiwi kuyasajili upya hapa wanapokuja nayo? Mbona kuliweka gari nambari za hapa hakuzuwii gari hiyo kutumika kwa wizi? Mbona kama hawana hiyo database (kumbukumbu), hiyo si kazi yangu mimi, ni yao wao wenyewe? Inahusikaje na kunizuia kutumia haki ya kuendesha gari yangu? Mbona hukumu ya jumla jumla hivi?

“Kwani nani kakuleta kwangu? Mimi sihusiki kabisa na operesheni” Nikamtajia jina. Akanyanyua simu na kumuamuru kwamba suala langu lishughulikiwe haraka. Likashughulikiwa kweli na masaa mawili tu baadaye kibali kikatoka.

Kibali kilipotoka, baada ya kila aina ya usumbufu, kilikuwa na ushahidi wa kutosha kwamba sisi, Wazanzibari, tunakumbushwa kuwa, kwanza, Tanganyika ipo na, pili, Tanganyika si petu. Ithibati hii ilifurahisha mno. Inasema hivi: “This is to inform you that the approval has been granted for extension of foreign vehicle permit……..after payment of US $ 20 permit fee.”

Na hilo hata si kubwa sana kama ile fomu ya maombi, ambayo ingawa juu ina nembo na jina la Mamlaka ya Mapato Tanzania, kule chini kuna sehemu ambayo nilitakiwa kuijaza: “My address while in Tanganyika shall be……” na hapa nikaandika anwani yangu nikiwa hapa Tanganyika, huku nikiwa na furaha ya kuniyanyuwa juu. Sikuwa nimewahi kufurahi siku nyingi wakati wa kuandika au kusaini karatasi kama siku hii!

Je, unadhani ni kichekesho kwamba hii mamlaka ni ya mapato ya Tanzania, lakini fomu inanielekeza niandike anwani yangu nitakapokuwa Tanganyika? Hapana, si kichekesho, ni uhalisia wa kizungumkuti cha huu unaoitwa Muungano wa Tanzania. Kwamba ukweli ni kwamba Tanganyika ipo, nasi Wazanzibari hapa si petu. Tu wageni kama walivyo wa Rwanda na wa Burundi. Ni uongo mtupu kusema kwamba Tanganyika ilikufa. Tanganyika iko hai na fomu hii ni miongoni tu mwa dalili za wazi wazi, tena za kimaandishi, kwamba Tanganyika ipo, ukiacha dalili kibao zisizo za wazi.

Sasa kwa Wazanzibari wenzangu swali linaloulizwa ni nini basi vile kujiita nchi moja? Jibu ni kwamba, nchi moja ina tafsiri tu kwamba panapohusika utawala, kwa maana ya kuikalia Zanzibar kwa staili ya kikoloni, hii ni nchi moja. Wataonesha kuwa ni nchi wakati wa kuelekea uchaguzi. Watakaa Dodoma waamue nani awe mgombea uraisi wa Zanzibar. Hata kama Wazanzibari watakuja na maamuzi mengine, wao ndio wenye nguvu za kuamua na kusimamia maamuzi yao. Hapo tuko nchi moja.

Wakimaliza uteuzi, watasimamia kuhakikisha kuwa huyo mtu wao ndiye pia anayekuwa raisi wa Zanzibar. Watamimina majeshi ya kila aina na silaha zote za kivita kuhakikisha hilo linatokea. Watatoa hotuba kusema kwamba hawako tayari kuona kwamba Muungano huu unavunjika na kwamba Jeshi la Wananchi wa Tanzania halitavumilia hilo hata kidogo (rejea hotuba ya Profesa Philemon Sarungi ya mwaka 2003, wakati huo Waziri wa Ulinzi wa Tanzania). Hicho ndicho kiwango cha kuonesha ‘umoja’ wa nchi hii.

Hiyo hiyo TRA, ambayo ilipingwa sana na Wazanzibari, itapeleka maafisa wake Zanzibar kukusanya pesa za Wazanzibari asubuhi na jioni watapanda boti kurudi kwao Tanganyika na mifuko iliyojaa tele noti za Wazanzibari. Hiyo ndiyo maana ya nchi hii kuwa moja. Kuitawala Zanzibar na kuibinya kiuchumi isisimame, ndiyo maana ya umoja. Lakini patakapohusika maslahi ya kiuchumi, Tanganyika huinuka na kusimama kama nchi tafauti na kuingalia Zanzibar na Wazanzibari kama raia wa kigeni.

Ni bahati mbaya sana kwamba Wazanzibari hawaichukulii Tanganyika hivyo. Kesi hii hii ya nambari za magari inachukuliwa tafauti Zanzibar. Hakuna gari yenye nambari za Tanganyika ambayo inazuiwa kutembea Zanzibar au kutakiwa kuwa na kibali cha nchi ya kigeni.

Kwa nini? Je, ni kweli kuwa Zanzibar ni koloni tu?

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.