HATIMAYE ile tunzo ya Rais Bora wa Afrika inayotolewa na tajiri wa Kisudani, Mohammed Ibrahim (Mo Ibrahim), imekwenda kwa Joachim Chissano, Rais Mstaafu wa Msumbiji, huku marais wengine wastaafu, akiwamo Benjamin William Mkapa wa Tanzania, wakiikosa. Labda sisi, Watanzania, tulitarajiwa tusikitike kwa kuwa kiongozi wetu ‘aliyetutumikia’ kwa miaka 10 mtawaliya amekosa tunzo hiyo adhimu, ambayo kama angeipata ingelikuwa pia heshima kwa taifa zima.

Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa.
Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa.


Lakini hilo la kusikitika halikutokea (ama angalau halikuonekana likiakisika katika vyombo vyetu vya habari ambavyo ndio taswira ya mawazo ya Watanzania). Badala yake, kupitia magazeti mbali mbali, tukajisomea habari na makala za uchambuzi zilizoonesha kwamba lilikuwa kosa la Mkapa mwenyewe na kwamba “alikuwa amevuna kile alichokipanda.” Ni kama kwamba Watanzania hawakumhurumia Mkapa.

Mimi pia ni miongoni mwa hao waliokosa chembe ya huruma kwa mtu ambaye tunamchukulia kama ‘hasara’ kwetu. Bali, katika makala hii, nataka niende mbele zaidi kwa kusema kwamba nimefurahishwa sana kwa Mkapa kuikosa tunzo hiyo, maana ingelikuwa bahati mbaya na tusi kwangu na kwa Wazanzibari wenzangu kama angeliipata.

Sijapata kuona vibaya kujitambulisha na Uzanzibari wangu kama vile ambavyo sijizuii kuumizwa na kumchukia mtu anayeijeruhi taswira ya Zanzibar, Wazanzibari na Uzanzibari; na Mkapa alikuwa mtawala aliyeona fahari ‘kumdhalilisha’ Mama yetu Zanzibar.

Hadi kuondoka kwake madarakani 2005, alikuwa ameiraruararua Zanzibar yetu kwa namna ambayo Wazanzibari hawana sababu ya kumpenda maana hawawezi kumlipa kile alichoshindwa kuikopesha Zanzibar yao. Alishindwa kuikopesha Zanzibar mapenzi na ihsani, naye hastahili kulipwa fadhila na imani.

Mkapa kukoseshwa tunzo hii, kwa hivyo, ni zawadi ya mwisho (kwa udogo na udhaifu) ambayo jumuiya ya kimataifa ingeweza kuitoa kwa mamia ya Wazanzibari ambao kwa njia moja ama nyengine waliteseka chini ya utawala wake. Zawadi kubwa ingelikuwa ni kumfikisha kwenye mahakama ya kimataifa kwa makosa aliyoyafanya dhidi ya binaadamu, hasa hasa yale mateso na mauaji ya Januari 2001, Zanzibar.

Zamani nilihoji, na bado naendelea kuhoji kwamba aina yake ya mfumo wa utawala ilifaa kuitwa Mkapakrasia, kwa maana ya utawala uliojitenga sana na raia unaowaongoza kwa imani kuwa nguvu ya kukaa na kuondoka madarakani imo mikononi mwa Jeshi, Usalama wa Taifa na Polisi; na wala sio mikononi mwa umma. Miongoni mwa tabia kuu za aina hii ya utawala ni kiburi, jeuri na utumiaji mbaya wa vyombo vya dola dhidi ya raia; na historia ya nchi hii ni shahidi kwamba utawala wa Mkapa ulikuwa bingwa wa hayo.

Ni katika uraisi wake ambapo Zanzibar, kwa mara ya mwanzo tangu kumalizika kwa kipindi cha giza cha miaka ya ’60 na ’70, ilishuhudia mayatima, wajane, wakimbizi na walemavu wa maisha kutokana na sababu za kisiasa. Damu ya Wazanzibari ilimwagwa, roho changa zikadhulumiwa, wanawake wa Kizanzibari wakanajisiwa na, juu ya yote, heshima ya Mzanzibari ikadhalilishwa. Yote hayo yalifanyika kwa jila la dola; na katika wakati ambao yeye, Benjamin William Mkapa, alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama.

Maafa yale ya 2001 yalitarajiwa, kibinaadamu, kwamba yangeliulainisha moyo wa Mkapa. Alikuwa ‘ameeleweka’ hivyo kupitia hotuba yake ya kusaini Muafaka II na akawa pia amenukuliwa hivyo mara mbili mwaka 2004: mara moja katika ziara yake Marekani ambapo, alipokutana na Watanzania waishio huko, alilitaja suala la mauaji hayo kama jambo baya asiloweza kulisahau na mara ya pili ni katika mahojiano yake na Jonathan Power wa jarida la The Prospect ambapo aliwalaumu wenzake wa Zanzibar kwamba wako tayari kua ili kubakia madarakani.

Lakini haikuwa hivyo. Mkapa hakuwa mtu wa kubadilika panapohusu hatima ya Zanzibar. Kuelekea uchaguzi mkuu wa 2005, aliinuka pale New Africa Hotel, Dar-es-Salaam, akiapa kwamba angelitumia uwezo wake binafsi na wa dola kuhakikisha kuwa CCM inashinda; muktadha ulikuwa ni mwenendo wa siasa za Zanzibar, hasa katika wakati ambao kila dalili ilishaonesha kuwa chama chake kimeshapoteza udhibiti wa mambo.Sisi Wazanzibari tuliutambua uzito wa kauli hiyo. Kwa kusema hivi, Mkapa alikuwa anatumia saikolojia ya kikatili kututesa. Alikuwa anatukumbusha zile roho zilizotoka, ile damu iliyomwagwa na ile heshima iliyovunjwa wakati nguvu ya dola ilipotumika dhidi ya watu wetu.

Alikuwa anatukumbusha ya Shumba Mjini (Micheweni, Pemba) mwanzoni mwa siasa za vyama vingi, 1992. Huko vyombo vya dola vilitumia nguvu zake kumpiga risasi na kumuua kijana Omar Ali Haji, aliyekuwa akipachika bendera ya Chama cha Wananchi (CUF). Huko kulikuwa ni katika kusimamia kauli ya Mkuu wa Wilaya hiyo wa wakati huo kwamba, asingeliruhusu bendera ya CUF kupepea katika wilaya yake. Ingawa baadaye bendera hiyo ilipepea, lakini ilipepea na roho ya mtu. Hili, hata kama lilitokea kabla ya yeye, Mkapa, kuingia madarakani, lakini ulikuwa mfano wa kuitumia dola kuhakikisha uwepo wa CCM madarakani.

Alitukumbusha ya Kilimahewa, katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2000, ambapo kwa mara nyengine, nguvu za dola ziliuvamia umma uliokuwa katika hadhara ya CUF na kumimina risasi. Matokeo yake watu sita wakakatwa miguu kutokana na risasi hizo. Huo ni mwaka ambao tayari Mkapa alishakuwa Amiri Jeshi Mkuu na akawa amepeleka Zanzibar magari ya deraya na kuongeza vikosi vya polisi na jeshi vyenye silaha nzito nzito. Kwa kauli ile, akatufanya tuunganishe kuwa, kumbe lengo la kuleta vikosi vile siku zile lilikuwa ni hili la kuhakikisha kuwa CCM inaendelea kubakia tena madarakani, hata kwa gharama za damu ya Wazanzibari.

Alikuwa anatukumbusha tena na tena hayo ya Januari 2001, ambayo ati alikuwa amesema kwamba ni mambo mabaya ambayo kamwe hatayasahau. Kwa makusudi kabisa, Mkapa alikuwa anatukumbusha Wazanzibari haya, yumkini kutuonya kuwa yangelirejea. Mateso ya kisaikolojia.

Mkapa alikuwa anaturudisha nyuma kwenye kauli kama hiyo iliyotolewa na Waziri wake wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Profesa Philemoen Sarungi, akiwa Zanzibar Agosti 2004. Alichosema wakati huo Waziri Sarungi ni kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lisingelivumilia watu wanaotaka kuuvunja Muungano wa Tanzania.Wakati huo niliandika makala katika gazeti moja la kila wiki la Kiswahili kufafanua maana ya kauli hiyo. Kwamba, kwanza, kwa watawala wetu, anayehatarisha Muungano ni yule anayezungumzia aina tafauti ya Muundo wa Muungano huo, kwa mfano anayesema uwe wa serikali tatu badala ya huu wa mbili wa CCM. Pili, upande mmoja, tuna vyama vyengine visivyokuwa CCM na vyenye sera tafauti ya Muundo wa Muungano na, upande mwengine, tuna Wazanzibari walio wengi wasioridhika na muundo huu wa Muungano.

Katika uchaguzi wa 2005, kwa hivyo, Wazanzibari hawa kwa wingi wao wangeliweza kukichagua chama kisichokuwa CCM ili kikidhi haja yao ya kuwa na aina tafauti ya Muungano. Sasa hapo, kwa mujibu wa kauli hizo za Sarungi na Mkapa, ni kuwa jeshi lisingelikubali hilo, kwa mintarafu ya kwamba jeshi lisingekiruhusu chama kisichokuwa CCM kuingia na kuyashikilia madaraka.

Ni katikati ya kumbukumbu kama hizo, ndio maana wakati huo gazeti jengine la kila siku la Kiswahili la Jumatatu, 21 Machi, 2005, likashauri katika tahriri yake kuwa ni bora pasiwe na uchaguzi. Kwamba madhali Mkapa alishaamua kuwa angelitumia nguvu za dola kuhakikisha kuwa CCM inashinda, basi hakukuwa na haja ya kupoteza mabilioni ya shilingi, nguvu na wakati wetu kwa uchaguzi ambao matokeo yake yalishaamuliwa na Mkapa.

Ikumbukwe kuwa ni baada ya kauli hiyo tu Mkuu wa Jeshi la Polisi wa wakati huo, Omari Idi Mahita, (ambaye hatafautiani na Mkapa panapohusika Zanzibar) alipoanzisha kile alichokiita Operesheni Dondola, ambayo iliwapeleka Zanzibar mamia ya askari polisi kutoka Bara ati kwa lengo la kudumisha amani wakati wa uchaguzi. Kuelekea uchaguzi wa 2000 pia yalikuwa ymaefanyika hayo hayo chini ya wawili hao (Mkapa na Mahita).

Si lazima kukumbushana kila ambacho kilitokea mwaka 2005 kumalizia hoja kwamba Mkapa aliitenda tena vibaya Zanzibar. Tupo tunaoamini kwamba, kama si busara za viongozi wa juu wa CUF kuwazuia wafuasi wao kutumia kile walichokiita ‘nguvu ya umma’ dhidi ya matukio na matokeo ya uchaguzi wa mwaka huo, basi maafa mengine makubwa zaidi ya yale ya 2001 yalikuwa tayari yameshawashiwa taa ya kijani na Mkapa kwa nafasi yake kama Amiri Jeshi Mkuu.

Tulishuhudia kumiminwa kwa kombania za kijeshi na magari ya kivita Zanzibar katika mfano ambao aliufananisha mwenyewe na uwepo wa “majeshi ya Marekani nchini Iraq.” Alhamdulillah kwamba wakati huo hekima ilifurika kwenye vichwa vya viongozi hao wa CUF na ile hasara kubwa tunayoamini ilikwishapangwa ikafeli. Yote ni kwa kuwa Mkapa hakuwa ameyajutia yale maovu ya Januari 2001 na ndiyo maana tunaamini kuwa ilikuwa sawa kwake kuikosa tunzo ya Rais Bora.

Ilikuwa sawa kuikosa, maana huyu alikuwa rais aliyethibitisha kuwa bila ya nguvu za dola, basi chama chake kisingeliweza kusalia madarakani. Alithibitisha kuwa vyombo hivyo ndivyo vinavyotoa madaraka na kisha vikamlinda viliyemuweka madarakani. Alithibitisha kwamba uthubutu, jeuri na kiburi chake na chama chake ni kwa kuwa pana vyombo vya dola vilivyosimama na mitutu ya bunduki dhidi ya yeyote anayekihatarashia uwepo wao madarakani.

Ilikuwa sawa kuikosa maana huyu alikuwa rais aliyethibitisha kuwa kiongozi anaweza kupendwa na mataifa ya nje yanayojidai kupigania demokrasia na haki za binaadamu hata kama yeye mwenyewe ni mkandamizaji wa haki za watu wake. Wakati wakubwa huko nje wakimsifu kwa kila sifa, huku ndani kwake aliukuza na kuulea mgogoro wa Zanzibar katika kiwango ambacho kila siku unazidi kufura.

Ilikuwa sawa kuikosa maana huyu alikuwa rais aliyethibitisha kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano anaweza kuichafua Zanzibar kwa kuhakikisha kuwa kamwe haiwi na uchaguzi huru na wa haki. Ndivyo alivyoufanya ule wa 2000 na wa 2005. Kwa kauli ile ya Machi 2005 ya kutumia nguvu za dola kuhakikisha ushindi wa CCM, kwa mfano, Mkapa ‘alishauchafua’ uchaguzi wa mwaka huo hata kabla ya kura kupigwa.

Nasema ’aliushachafua’, kabla ya kura kupigwa kwa sababu uchaguzi haungaliwi kwa tukio moja tu la kutumbukiza vikaratasi vya kura kwenye kisanduku, bali mkufu mzima ambao una mambo mengi yanayotegemeana na kuathiriana. Hili la kauli yake lilikuwa katika mambo hayo yanayouhusu moja kwa moja uchaguzi huo na ndio maana hali ikawa kama ilivyo.

Ingawa Mkapa alijuwa kuwa, hasa kwa Zanzibar, nafasi ya kuuharibu uchaguzi ule kwa makusudi ya kutegemea kuja kusaini Muafaka mwengine ilikuwa finyu sana. Alikuwa ameshaelezwa hivyo si mara moja wala mbili na, kwa hivyo, akawa anakabiliwa na moja kati ya mawili: ama kuuwachia umma kufanya maamuzi yake na kuyaheshimu maamuzi hayo au kuitumbukiza nchi hii katika maafa mengine. Yeye akachagua la pili.

Tupo Wazanzibari tunaoamini kwamba Mkapa alikuwa raisi aliyekuwa na hamu na ghamu ya kuona kila mara Wazanzibari wanagongana na dola. Kwamba hakuwa ametosheka na wale wakimbizi waliozalishwa na serikali yake mwaka 2001, hakuwa ametosheka na ile damu iliyomwagwa na vikosi vyake vya ulinzi na usalama, hakuwa ametosheka na ile heshima ya mama na dada zetu iliyovunjwa kwa kunajisiwa na kwamba hakuwa ametosheka na wale mayatima na wajane wa Kizanzibari.

Na kwa imani hii, hatuoni sababu ya kumhurumia kwa kukosa tunzo ya Mo Ibrahim wala sababu ya kumpenda, maana si stahiki yake.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.