Nizungumzie kinadharia zaidi kuliko kimaada, kwani mifano hai inayohusu makala hii ya leo imekuwa mingi mno hapa Tanzania kiasi ya kwamba sisi wengine tunahisi kichefuchefu hata kuitaja. Kuna ya Richmond na Dowans, ya Karamagi na Buzwagi yake, ya ‘ujasiriamali’ wa Benjamin Mkapa na mkewe, ya Daudi Balali na minara yake pacha, ya IPTL na hiyo ya Meremeta. Uchafu tu. Uchafu mtupu unaotia kinyenyelezi cha kufumba pua na kutema mate. Po!

Andrew Chenge, mmoja wa viongozi waliotuhumiwa takribani katika kila kashfa kubwa ya hivi karibuni ya ufisadi serikalini.
Andrew Chenge, mmoja wa viongozi waliotuhumiwa takribani katika kila kashfa kubwa ya hivi karibuni ya ufisadi serikalini.

Lakini katikati ya uoza huo, au pengine kwa sababu ya uoza huo, utakuta hii tabia yetu mbovu ya kuuzungumzia uchafu kwa maneno yanayochuja kimaana. Mojawapo ni hili la kuuita ufisadi kuwa ni rushwa. Rushwa tu!

Ukweli ni kuwa rushwa ni kitu kidogo sana panapohusika uoza wenyewe tunaokusudia kuuzungumzia. Yenyewe ni utowaji na au upokeaji wa kitu (mara nyingi huwa pesa) kwa ajili ya kutoa au kupokea huduma, ambayo kimsingi ingelikuwa haki kutolewa bila ya kitu hicho.

Wengi wetu tunadhani rushwa ni sawa na ule msamiati wa Kiingereza ‘corruption’, ndiyo maana hata taasisi inayoshughulika na kadhia hiyo hapa petu, TAKUKURU, tunasema inafanya kazi ya kupambana na kuzuia rushwa. Mifano ya karibuni ya chaguzi za Chama cha Mapinduzi (CCM) ni ushahidi kwamba tunauangalia uoza huu kwa jicho dogo sana.

Lakini ufisadi, na hapa nazungumzia ufisadi wa kisiasa, unakwenda mbali zaidi ya hapo. Huu ni utumiaji mbaya wa madaraka unaofanywa na maafisa wa serikali na, au, wa taasisi za kisiasa kwa maslahi binafsi. Aina zake ni za viwango tafauti, na hiyo rushwa moja tu miongoni mwao. Katika upana wake utakuta pia udugunaizesheni, wizi wa kura, milungula, wizi wa mali ya umma na ubadhirifu, kwa kutaja chache.

Ufisadi huu wa kisiasa, kwa hakika, ndio mama wa maovu mengine kwenye jamii husika, kama ilivyo hapa petu. Uovu wa madawa ya kulevya, ujambazi, ukahaba na umasikini wa watu wetu, kwa mfano, ni matokeo ya ufisadi wa kisiasa ambao umekuwa ukiila nchi yetu kwa zaidi ya miongo minne sasa.

Bahati mbaya ni kuwa ufisadi huu una khulka moja ya hatari sana: kuzoeleka. Kila anayechukua nafasi ya uongozi wa umma katika serikali au taasisi ya kisiasa huona sawa kwake kuwa fisadi, na kwa hakika jamii humtarajia awe hivyo. Kwamba atumie fursa ile kujinufaisha binafsi. Ndio maana tume za uchaguzi huiba kura, wagombea hununua wapiga kura, polisi hula mkono kwa mkono na wahalifu, maprofesa hupasisha au kufelisha wanafunzi vyuoni kwa kuzingatia maslahi yao binafsi, alimradi ni mchafukoge.

Jamii hii ya mchafukoge ni muakisiko wa ufisadi wa kisiasa uliopea na kuzoeleka. Utamaduni wa chukua chako mapema, wa iba ulindwe na kemea udhibitiwe (kama anavyoonekana kutaka kudhibitiwa Zitto Kabwe leo hii), ndio unaojenga fikra za Watanzania uwaonao mbele yako leo.

Si hasha, kwa hivyo, kusikia hata miongoni mwa kada za hao waitwao wasomi leo hii wakisema: “Naye Zitto kazidi kidomodomo.” Kwao wao ufisadi ni ada ya maisha ya kila siku. Mwisho wa utamaduni huu huwa ni kile kinachoitwa kleptocracy (rule by thieves), yaani utawala wa wizi. Nami nataasafu kusema kwamba, hapo ndipo ilipo Tanzania yetu leo hii.

Ufisadi una hatari kubwa na ya pekee katika maendeleo ya taifa. Katika siasa, hufifisha na wakati mwengine kuua kabisa mfumo wa kidemokrasia na utawala wa sheria. Kwamba ufisadi una kiburi cha kuingilia kati chochote ambacho kinaonekana kiko dhidi yake. Ukweli ni kwamba demokrasia na utawala wa sheria ni kinyume cha ufisadi; na kilipo kimoja chengine hakikai.

Kwa hivyo, kwa jamii kama yetu ambayo imejikita katika uoza wa kupindukia wa ufisadi, mafisadi wenyewe hawataki kabisa kuona mfumo wa demokrasia ukistawi ama utawala wa sheria ukisimama. Si ajabu, kwa hivyo, kuona wakiingilia kati taratibu za kawaida za kidemokrasia na za utawala wa sheria kila pale wanapoona zinachukuwa mkondo wake. Ya kuharibiwa kila mara kwa chaguzi za Zanzibar kwa kupelekwa majeshi yenye silaha nzito nzito ni katika hizo jitihada za ufisadi kupingana na demokrasia na utawala wa sheria.

Ufisadi katika chaguzi hupelekea ofisi za umma kukaliwa na watu wasiotokana na ridhaa ya umma na hivyo nao matokeo yake huzikalia ofisi hizo kwa maslahi yao binafsi na sio kwa maslahi ya umma, maana sio uliowaweka ofisini. Leo hii wananchi wanapolilia ukosefu wa uzalendo miongoni mwa viongozi wetu walioko madarakani, wanaofikia hadi kusaini mikataba ya kuuza madini yetu katika hoteli, wanapaswa kujiuliza namna hao watiaji saini walivyofika hapo madarakani. Je, ni kwa demorasia au kwa ufisadi wa kisiasa?

Ufisadi katika vyombo vya kutunga sheria hupunguza au huondosha kabisa uwajibikaji na uwakilishi wa kweli katika vyombo hivyo. Kauli ya yule mbunge wa Biharamulo Magharibi, Phares Kabuye, hivi majuzi kwenye kikao cha Bunge kilichomalizika, inaakisi hasa aina ya uwakilishi tulionao Watanzania katika vyombo vyetu.

Ufisadi kwenye mahakama huiweka rehani haki ya wananchi; na ufisadi kwenye utawala husababisha ukosefu wa uadilifu katika utowaji wa huduma za kijamii.

Kwa jumla, ufisadi hukokozoa kabisa uwezo wa kitaasisi wa serikali, kwani husababisha taratibu kupuuzwa, rasilimali kuporwa, na ofisi za umma kuuzwa na kununuliwa kama bidhaa nyengine yoyote. Hiyo mifano niliyoitaja mwanzo wa makala hii yote inaakisika, kwa namna moja ama nyengine, na ukweli huu.

Ufisadi wa kisiasa ukipevuka, kwa hivyo, huufanya uhalali wa serikali iliyopo madarakani uhojike na vivyo misingi ya demokrasia na kuaminiana itoweke. Ni mapema, pengine, sasa kwa wananchi wa Tanzania kuhoji uhalali wa serikali yao, lakini kwa mwenendo huu tunaokwenda nao, si muda mrefu tena ujao, hilo la kuhoji litakuwa wajibu wetu wa mwanzo!

Lakini wakati tukisubiri wakati huo ufike, sote ni mashahidi wa namna ambavyo ufisadi wa kisiasa unadumaza maedeleo ya kiuchumi kwa kuchochea ubadhirifu na ukosefu wa ufanisi. Mali za nchi yetu zinaibiwa mbele ya macho yetu: mchanga wa dhahabu unasafirishwa makontena kwa makontena, meli za kigeni zinavua tani kwa tani za samaki kwenye bahari yetu, na wenye vyeo wanajikopesha na kujikatia juu kwa juu kutoka hazina ya taifa. Nchi inakwenda. Ufisadi unatula.

Tu mashahidi pia wa namna ufisadi unavyoiangamiza sekta binafsi, licha ya kelele za serikali yetu kwamba inaitanua sekta hiyo ili kumkomboa Mtanzania na umasikini. Hapa wa kulaumiana ni wenyewe kwa wenyewe, maana mara nyingi huwa tunajikubalisha kuongezewa gharama za kuendeshea biashara kupitia malipo yasiyokuwa rasmi. Tumekuwa mahodari wa ‘kuongea’ na wakubwa ili biashara zetu zituendee, na huku wakati huo huo tukiishi na woga wa kudumu wa kufungiwa biashara hizo kwani makubaliano mengi tunayoyafanya na hao ‘wakubwa’ huwa ni ya kufoji na hayawezi kutulinda kisheria.

Ndio matokeo ya watu wanaojenga majumba yao leo asubuhi na kesho jioni kubomolewa na serikali. Serikali hiyo hiyo moja ambayo afisa wake mmoja alitoa kibali cha ujenzi asubuhi hii, jioni yake huja afisa wake mwengine, ambaye ama kwa kusimamia sheria au kwa kutaka naye ‘akatiwe’ chake, hutoa amri ya jengo hilo kuvunjwa. Hizo ndizo gharama za ufisadi. Kuyafanya maisha yasiwe na uhakika.

Tu mashahidi pia wa namna ufisadi unavyochochea upotoshaji katika sekta ya umma kwa kuitoa miradi ya kijamii na kuingiza katika miradi ya kibiashara ambapo rushwa na milungula iko ya kutosha. Maafisa wetu ni mahodari wa kuongeza ‘tabu za kiufundi’ au kisheria katika mradi fulani au kusafisha njia haraka kwa mradi mwengine ili kupata chao haraka. Shule zilizojengwa katika mpango wa MMEM, kwa mfano, na kuja kubainika baadaye kwamba hazikufikia viwango vilivyotakiwa na thamani halisi ya fedha iliyotolewa, ni moja tu kati ya mifano mingi ya namna ufisadi unavyoitafuna sekta ya umma.

Ndiyo, sote tu mashahidi wa hayo na mengineyo mengi kama hayo, lakini kuwa kwetu mashahidi kumetusaidia nini? Kwa karibuni miongo minne, hiyo imekuwa hali ambayo taifa hili limeishi nayo. Leo hii tunajikokota kwenye mstari wa mwisho wa umasikini duniani, huku watoto wetu wakifa kwa maradhi na njaa. Bado tumeendelea kuwa mashahidi tu. Ushahidi hautusaidii kitu.

Tunapaswa leo kuchukuwa hatua dhidi ya uoza huu. Miongo hiyo minne imewashuhudia watawala wale wale wakituzoesha kuupenda na kuushabikia ufisadi na kuufanya kuwa utamaduni wetu. Wametupotosha vya kutosha. Tumefanywa tuone jambo la kawaida kutoa na kupokea rushwa. Wametufanya tuutarajie ufisadi na tuutegemee kama njia ya kupita kufika twendako. Tunapaswa sasa kukataa na kusema hapana. Hapana kwa ufisadi wa kisiasa. Hapana kwa mafisadi wa kisiasa.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.