Zanzibar inapoteza fursa kwa kuwa ilijikusuru kumuamini mtawala ambaye hana nia ya kuisaidia kuondokana na mgogoro wake wa siku nyingi, maana hilo si katika vipau-mbele vyake vya kiutawala. Ukiacha ukweli kwamba, katika ilani ya uchaguzi ya chama chake, hamuna lolote linalozungumzia hatima ya Zanzibar katika hili, hata katika mipango ya ziada, ambayo kikawaida raisi anaruhusiwa kuwa nayo, maafikiano ya Wazanzibari si kitu muhimu kwake.

Nilikuwa Zanzibar wakati Rais Jakaya Kikwete alipotoa ile hotuba yake ya mwanzo Bungeni, mwishoni mwa mwezi Disemba 2005, ambapo miongoni mwa aliyoyasema ni kutambua kwake kuwepo kwa ‘mpasuko’ wa kisiasa wa Zanzibar, baina ya Pemba na Unguja na hasa baina ya Pemba na sehemu nyengine za Tanzania.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Kukiri huko kwa Rais Kikwete katika chombo kikubwa kama kile, kilikuwa kitu muhimu katika historia ya kisiasa ya nchi hii, na basi hapo hapo akajivunia uungwaji mkono wa ajabu kutoka kwa Wazanzibari, hasa wale wanaounga mkono Upinzani, yaani viongozi na wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF). Nililishuhudia jambo hili adimu kwa siasa za Zanzibar likitokea.

Wakati huo nchi ilikuwa imetoka kwenye uchaguzi ambao uliijeruhi tena – haki za binaadamu zilikuwa zimevunjwa kwa kiwango cha kutisha, demokrasia ilikuwa imewekwa jela, na hatima ya nchi yetu ilikuwa majaribuni. Haikuwa ajabu, kwa hivyo, kwa CUF kuyakataa matokeo ya uchaguzi huo na, sasa, ilipotokea Rais Kikwete kuzungumzia maumivu yao Bungeni, wakainuka na kumuunga mkono. Ndivyo walivyofanya, bila ya shaka, Watanzania na Wazanzibari wengine, hata ambao si wafuasi wa CUF.

Lakini mimi sikuwa miongoni mwao tangu hapo mwanzoni. Japokuwa sikuwa nimekaa kuchakura chochote katika historia ya Kikwete binafsi kuweza kumpinga hadharani, lakini katika ile hotuba yake nilikuwa nimenusa harufu ya kiongozi anayekwepa uhalisia.

Kwa mfano, alikuwa ametumia rejea ya mgogoro wa Zanzibar kwa kutaja mifano ya upande mmoja tu, ya wa watu wa kisiwa cha Pemba kuonekana kujitenga na sehemu nyengine za Tanzania, ilhali wakifaidi kila fursa ya Muungano huo. Kwa kumbukumbu zangu, kulikuwa na mambo mawili yaliyomsukuma kusema yale: kwanza ni kuwa ‘kujitenga’ huko alikokuzungumzia, kulikuwa ni kule wananchi wa kisiwa hicho kizima kutokukichagua chama chake cha Mapinduzi (CCM) na badala yake kuichagua CUF tu.

Siku chache kabla ya uchaguzi uliomuweka yeye madarakani, nilikuwa nimesoma mahojiano yake na gazeti moja la Kiswahili hapa nchini ambapo aliyaelezea matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar kwa mtazamo wa ‘uvisiwa’. Kwamba Wapemba waliichagua CUF kwa kuwa ni chama chao na Waunguja waliichagua CCM kwa sababu hiyo hiyo. Alipoulizwa kuhusu CUF kupata jimbo moja la Mji Mkongwe kisiwani Unguja, alisema kwamba hata jimbo hilo ni kwa kuwa linakaliwa na Wapemba wengi. Kwangu, jibu hilo na kauli yake Bungeni, yote, yalikuwa ni maneno ya kiongozi anayekwepa wajibu wake kisiasa. Kwa hili, sikuwa na sababu ya kumuamini.

Lakini, pili ni kwamba, hata ile kauli yenyewe ya Bungeni ilikuwa ni kopi ya maneno ya mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, ambaye katika sherehe zake za mwisho za Muungano akiwa raisi, zilizofanyika Uwanja wa Amani, Zanzibar, alikuwa amesema hivyo hivyo, kuonesha namna wenyeji wa kisiwa cha Pemba walivyo ‘wakorofi’. Wakati huo niliandika makala niliyoiita ‘Alichokikosea Mkapa kuhusu Muungano’ iliyochapwa na gazeti la Rai. Mimi sikuwahi kumuhusudu Mkapa kwa jeuri na kiburi chake, na mara nyingi niliandika kulisemea hilo, hata nikapendekeza tuuite utawala wake ‘Mkapakrasia’, kwa maana ya utawala unaoamini juu ya jeuri, kiburi na matumizi ya nguvu za dola dhidi ya raia wake kama njia bora ya kuwatawala. Kwa hivyo, Kikwete alipotumia maneno yale yale, kishipa kikanipiga kwamba naye ni Mkapa mwengine kwa Zanzibar. Nalo hilo likanifanya nianze kuzishuku siasa zake kuelekea Zanzibar.

Nakiri kwamba nina udhaifu wa kuwa na mziya na viongozi wote wa Tanzania Bara panapohusika hatima ya Zanzibar. Sijapata kuwaamini kuwa sehemu ya utatuzi wa matatizo ya Zanzibar, badala yake nawahisabu kuwa ndio chanzo chake. Na hili, kwa hivyo, halimhusu Kikwete kama Kikwete tu. Hatima ya Zanzibar haiwezi kuaminiwa mikononi mwa wana-CCM wa Tanzania Bara. Mnisamehe, lakini hivyo ndivyo niaminivyo!

Basi wakati huo nikawa hata nimeshangazwa na tamko la Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye mara tu baada ya hotuba hiyo, alitoa taarifa ya kuiunga mkono. Mshangao wangu ulikuwa kwamba, chama chake kilikuwa kimeshatangaza rasmi kutokumtambua Mhe. Karume kama raisi, kwa upande wa Zanzibar, na, kwa upande wa Muungano, wakawa wamesema wanayatilia shaka matokeo ya uraisi, ambayo kwa mujibu wa msamiati ulioibuka, yalimpa Kikwete ushindi wa ‘kichinachina.’ Lakini, kabla shaka za matokeo hayo hazijawekwa sawa, Maalim Seif akawa ametoa tamko hilo la kumuunga mkono Kikwete na kumuahidi mashirikiano!

Mimi si mwanasiasa (na itanichukuwa muda mrefu kuwa), lakini nilipowauliza watu walio karibu na duru hizo, wakaniambia hiyo ilikuwa ni hatua muhimu kuelekea kuufundua mfundo ulioifundika Zanzibar kwa kipindi kirefu, na kwamba kwa Maalim Seif kunyoosha mkono wa mashirikiano, hata katika mahala ambapo pana ukungu wa shaka, ni kupevuka kisiasa na kuonesha njia ya kupita. Wanaomjuwa Maalim Seif, kwa hivyo, hawashangazwi, maana ana kiapo cha kuitendea mema Zanzibar hata kwa gharama ya yeye binafsi kupoteza kila kitu!

Sikuendelea kuhoji zaidi, lakini sikuacha kumshuku Rais Kikwete; na sasa shaka zangu zikaanza kupata sura, baada ya yeye kufanya ziara za kuwashukuru wapiga kura wa Zanzibar, akianzia na Pemba na kumalizia Unguja. Katika ziara hizo, pamoja na yote aliyokuwa ameyasema, alizungumzia tena huo aliouita mpasuko wa visiwa vya Zanzibar, kwa kurejea mifano ile ile ya watu waliokuwa wakiwagomea wenzao katika sehemu mbali mbali za Pemba. Tena akawa amefanya vile vile alivyofanya Bungeni, Disemba 2005. Na tena, kwa kuwa alikuwa amesema sentensi mbili tatu za kuwataka wana-CCM wenzake waache kumtafuta mchawi wao kwenye upinzani, basi hata upande wa Upinzani ukaona kwamba amezungumza vyema. Mimi nikaendelea kumshuku na nilipopata nafasi nikazisema shaka zangu.

Hapo ni pale kilipofika kipindi cha kuadhimisha siku zake 100 madarakani, ambapo magazeti mengi hapa nchini yalijaa tathmini za waandishi na wahariri zilizompa Kikwete alama za juu kwamba ameonesha dalili ya mafanikio. Kwangu ikawa siyaoni mafanikio yake, madhali tu hakuwa, hadi hapo, amefanya lolote kuhusu mgogoro wa Zanzibar. Ndipo nikaandika makala niliyoiita ‘Kikwete ni Mkapa mwengine kwa Zanzibar’, ambayo baada ya kupigwa chenga na magazeti mbali mbali ya hapa Bara, yaliyokwishalewa Kikwetephilia, ikachapwa katika gazeti la An-Nur kwa jina la ’Muniwie radhi mupendao chongo mukaita kengeza.’

Humo nikaonesha kuwa Rais Kikwete hakuwa na nia wala sababu za kuutatua mgogoro wa Zanzibar. Nikasema kwamba, miongoni mwa dalili ya hayo ni vile kutumia kwake mifano ya kibaguzi kukemea ubaguzi.

Inawezekana kwamba wangu ulikuwa ni msimamo mkali sana na wa kushitukizia, hasa kwa kuwa ilikuwa ni miezi mitatu tu tangu Kikwete achukuwe madaraka ya nchi na kwamba hizo hazikuwa siku zilizotosha, ndani ya kipindi cha miaka mitano, kuweza kumuhukumu kwamba hakuwa na nia wala sababu ya kuushughulikia mgogoro wa Zanzibar.

Siasa za kidiplomasia zilinihitaji kumpa kile wanachokiita ‘benefit of doubt.’ Kikwetu huiita dhana hiyo ‘husnudhanna’, msamiati wa Kiarabu unaomaanisha hali ya kumfikiria mtu mema na kumpa fursa ya kuyaonesha mema hayo, kabla ya kumnyooshea kidole cha lawama. Nikajaribu sana, katika maandishi yaliyofuatia baada ya hapo, nami kunyoosha mkono wa mashirikiano ambao, hata hivyo, ulikuwa umejaa kitetemeshi cha shaka.

Hii ni kwa kuwa, kama nilivyosema, mimi si mwanasiasa. Ni mdadisi na mdodosaji tu wa hapa na pale. Ni udadisi na udodosaji huo, ndio ulionifanya nimuone Kikwete kwamba si mtu afaaye kuaminiwa; na siku zote nikawa nimejiweka katika nafasi ya kumsubiri anisute kwa kutenda tafauti na shaka zangu. Lakini amekosa uthubutu wa kufanya hivyo, na sasa hoja yangu ya wakati ule, ndiyo hiyo hiyo niliyonayo leo hii, katika wakati ambao inaonekana wazi kwamba mazungumzo baina ya CCM na CUF yanavunjika, huku ushahidi ukionesha kuwa CCM hawakuingia katika mazungumzo haya kwa lengo la kuitafuta suluhu ya Zanzibar, bali kupitisha wakati. Angalau sijilaumu kwa kutokumuamini Kikwete wakati ule, lakini naumia kwamba nchi yangu inapoteza fursa ya kukwamuka.

Zanzibar inapoteza fursa kwa kuwa ilijikusuru kumuamini mtawala ambaye hana nia ya kuisaidia kuondokana na mgogoro wake wa siku nyingi, maana hilo si katika vipau-mbele vyake vya kiutawala. Ukiacha ukweli kwamba, katika ilani ya uchaguzi ya chama chake, hamuna lolote linalozungumzia hatima ya Zanzibar katika hili, hata katika mipango ya ziada, ambayo kikawaida raisi anaruhusiwa kuwa nayo, maafikiano ya Wazanzibari si kitu muhimu kwake.

Waliojidhani wanamjuwa, walifikiri kwamba vile kufanya kwake kazi Zanzibar katika nyakati fulani za kutumikia chama chake na kuwa kwake mtu wa pwani kama walivyo Wazanzibari wengi, yalikuwa mambo yanayomjenga nia Kikwete kuiona Zanzibar inatulia.

Wakati ni kweli kwamba Rais Kikwete ana mafungamano ya kibinafsi na Zanzibar, hilo kabisa halimfanyi ajenge nia ya kisiasa ya kuiona Zanzibar inatoka matatizoni, maana nia ya kisiasa hujengwa pia na malengo ya kisiasa. Malengo yake binafsi ya kisiasa, na ya chama chake, ni kuendelea kushikilia madaraka, tena yote, peke yao, na kwa gharama yoyote ile. Harakati na mapambano yake ya kufikia nafasi ya juu ya uongozi wa nchi ni shahidi wa hili. Na ikiwa hivyo ndivyo, hana sababu ya kuwa na nia ya kuutatua mgogoro wa Zanzibar, ikiwa, na ndivyo ilivyo, uwepo wa mgogoro huo unamaanisha kuendelea kushikilia madaraka.

Hili ndilo linalotupeleka katika hoja ya Rais Kikwete kutokuwa na sababu ya kuutatua mgogoro wa Zanzibar. Hana sababu kwa kuwa, mgogoro huu ni zao la makusudi la siasa za Dodoma kuelekea Zanzibar. Ni fitina ya makusudi ya uwagawe uwatawale, ambayo imeanza muda mrefu sana, kabla ya hata Uhuru, Mapinduzi na Muungano, lakini ikapata kasi zaidi baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana, mwaka 1964. Tangu hapo, jitihada zozote za kuileta pamoja Zanzibar zimekuwa zikifelishwa kwa makusudi.

Kila siku nimekuwa nikisema, na hapa ninarejea tena, kwamba Dodoma ina sera yake maalum kuelekea Zanzibar. Kwa sera hiyo, Dodoma inadhani kwamba kuweza kuidhibiti Zanzibar ni kuwa na Zanzibar iliyo dhaifu. Kinyume chake, wanadhani, Zanzibar imara inamaanisha Muungano dhaifu, kwa mintarafu ya kwamba ushawishi wa Bara kwa Zanzibar utapungua sana, kitu ambacho daima Dodoma imekuwa ikipigania kukidumisha.

Sasa Kikwete, ambaye tunaambiwa amezaliwa na kukulia katika mfumo wa siasa hizo, tangu TANU hadi CCM, na sasa ni raisi wa nchi na mwenyekiti wa chama chenye mtazamo huo, ana sababu gani ya kuiona Zanzibar inakuwa imara? Zanzibar imara ni Zanzibar iliyokuja pamoja, inayozungumzia yale mengi yanayowaunganisha watu wake na sio yale machache yanayowatenganisha. Zanzibar ya aina hiyo, kwa mtazamo huo wa Dodoma, ni hatari kwa ‘Muungano.’ Na hili la kuuhatarisha Muungano ni kitu cha mwisho ambacho Dodoma ingestahmili kukisikia.

Si ajabu, kwa hivyo, kwa jina lile lile la kulinda Muungano na Mapinduzi, Rais Kikwete sasa ataanza kufanya kama alivyofanya mtangulizi wake, Mkapa, kwa Zanzibar. Ataongeza wanajeshi kutoka Bara, atapeleka silaha nzito nzito, atamuweka mtu anayemtaka madarakani, kisha atakuja uwanja wa Amani, anadi “Mapinduziiiiii!”, kisha awatake wananchi waliohudhuria waitikie “Daimaaa!” kwa nguvu “mpaka vijukuu vya Masultani visikie!” Chuki, izaya na siasa ya wagawe uwatawale.

Na kwa hilo, sina sababu ya kumuamini Kikwete!

One thought on “Kwa nini sikumuamini Rais Kikwete tangu mwanzoni”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.