Siku chache tu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2005, nakumbuka, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, wakati huo akiwa mgombea uraisi wa Zanzibar kwa tiketi ya chama chake, alichapisha makala katika gazeti la The East African iliyoitwa “Zanzibar fair elections is Mkapa’s legacy”.

Wakati huo tayari, kila dalili ilishaonesha kuwa uchaguzi wa Zanzibar umeshavurugwa. Tayari kulisharipotiwa kesi za kupigwa na kuteswa kwa raia wa kawaida, kuchomewa moto nyumba na mali zao, kubakwa na hata kuuliwa. Yote yalikuwa katika kipindi cha uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Hadi hapo, tayari Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilishawazuia zaidi ya Wazanzibari 12, 000 haki yao ya kuwa wapiga kura kupitia mtandao wake wa Masheha, Tume ya Uchaguzi, Vikosi vya SMZ na hawa waitwao Majanjawidi.

Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete

Kwa yote hayo, labda Maalim Seif hakuwa tena na haja ya kumpa changamoto ile Mkapa, maana tayari alishayawachia mambo yaende mkorogovyogo mbele ya macho yake. Lakini, alidhani kuwa kuna nafsi nyengine ya Mkapa ambayo angeliweza kuishaiwishi itende wema kabla haijakwenda zake. Mkapa alikuwa amezungumza na mwandishi Jonathan Power wa jarida la Prospect mwezi mmoja tu nyuma, na kueleza masikitiko yake kwa aina ya uongozi uliopo Zanzibar, kwamba ulikuwa tayari hata kuua ili uendelee kubakia madarakani. Mkapa huyo huyo, wakati akiwa katika ziara zake za kuaga, alikuwa amezungumza na wanafunzi wa Kitanzania wanoishi Marekani na kueleza kuwa mauaji ya 2001 (ambayo yalisababishwa na uchaguzi usio huru na haki) ni jinamizi baya katika historia ya uongozi wake.

Kibinaadamu, Maalim Seif alikuwa na sababu ya kuamini kuwa Mkapa anayajutia hayo na hayuko pamoja na viongozi hao. Nguvu za kisiasa na kidola alizokuwa nazo Mkapa, zingeliweza kuwazuia viongozi aliowataja wasifanye usilifu wao, ikiwa angelitaka. Kwa kutumia ile iitwayo benefit of doubt, ndipo Maalim Seif akachukuwa kalamu kuandika changamoto ile.

Wapi! Mkapa alikuwa mtu mwenye nyuso mbili: uso mmoja aliuvaa alipokutana na mataifa ya nje na mwengine alipokabiliana na siasa za ndani. Alichokisema kwa Jonathan Power kilikuwa ni kwa faida ya Nje. Alitaka Marekani na Uingereza wamsikie, kisha vyombo vyao vya habari vimwandike kwa sifa kemkem za kuwa mwanademokrasia. Uwanademokrasia? Mkapa, The Great, alitaka mataifa yamtambuwe kwa hilo.

Lakini alipokuwa akijihusisha na siasa za ndani, Mkapa alivaa uso mwengine. Kabla ya makala hiyo ya Jonathan Power kuchapishwa, Mkapa alikuwa amesema katika hoteli ya Golden Tulip mjini Dar es Salaam, kwamba angelitumia hata nguvu ya dola kuhakikisha ushindi wa Chama chake cha Mapinduzi (CCM). Na katika hilo, alikuwa hatanii. Huyo ndiye Mkapa tuliyemjua katika medani za siasa za ndani. Uchaguzi ulipofika, alifanya alichokiahidi Golden Tulip na hakushughulika kabisa na masikitiko yake kwa Jonathan Power.

Miezi miwili na nusu, baada ya makala ile ya The East African kuchapishwa, Mkapa akauwacha uraisi wa Tanzania huku akiwa ameifelisha Zanzibar, ameifelisha demokrasia na, hivyo, amejifelisha yeye mwenyewe. Uhalali alioueleza Maalim Seif katika makala ile hakuwa kitu muhimu kwake.

Hivyo ndivyo historia ya ndani inavyomuandika Mkapa, kama kiongozi aliyefeli. Si tatizo kwamba mashirika ya fedha ya kimataifa na nchi za Magharibi (wanaoheshimika kwa unafiki wao) wanataka aonekane nabii mdogo wa sera zao za utandawazi. Hii ni kwa kuwa, ndani ya Mkapa waligundua aina ya mtawala wa Kiafrika wanayeweza kumtumilia kupora utajiri wa nchi hii. Kumjengea jina lake kulikuwa na gharama ndogo sana kulinganisha na faida walizozipata kwa kukomba tani za dhahabu, tanzanite na almasi.

Lakini suala la Zanzibar limeonesha picha tafauti ya taswira hiyo. Labda hii ndiyo sababu, mara tu baada ya kupokea madaraka, mrithi wake, Jakaya Mrisho Kikwete, akaanza kuonesha, angalau kwa kauli zake, kwamba mtangulizi wake hakuwa chochote zaidi ya sehemu ya tatizo hili. Kukiri kwake kwamba pana tatizo kubwa hapa na ahadi ya kulitatua, kulimaanisha kwamba amelitambua alilorithishwa.

Je, Kikwete ana pa kuanzia katika hili la Zanzibar? Anamo mwingi. Na pamojawapo, na muhimu zaidi, ni kwa Mkapa mwenyewe aliyemrithisha tatizo hili. Mkapa ana mengi ya kumfunza Kikwete, maana yeye ni mmoja wa waumbaji wa mgogoro huu. Sharti pekee analopaswa kulitimiza Mkapa, bila ya shaka hata na Kikwete mwenyewe, ni kubadilisha mtazamo wake kuelekea Zanzibar. Kubadilisha mtazamo, paradigm shift, ndilo pekee litakalomrejeshea Mkapa heshima yake aliyokwishaipoteza Zanzibar.

Sasa, akiwa nje ya madaraka, panajitokeza dalili kuwa Mkapa hataki kufa kama alivyoishi. Wiki iliyopita, gazeti la Mwananchi (Julai 16, 2006) lilichapisha habari katika ukurasa wake wa mbele inayojenga picha kwamba Mkapa ameanza kujutia baadhi ya mambo aliyoyafanya katika zama zake madarakani. Muhimu yaliyoelezwa humo yalihusu hatua zake za mageuzi ya kiuchumi ambazo zilishirikisha ubinafsishaji wa njia kuu za uchumi na mikataba ya aibu.

Hili la kung’amua makosa yake ni nyenzo muhimu sana katika utatuzi wa matatizo yanayotukabili sasa, ambayo kwa sehemu kubwa yeye ni sehemu yake. La Zanzibar, hata kama hajanukuliwa akilijutia, lazima limo katika majuto yake. Kikwete anaweza kumtumia Mkapa kama asset ya utatuzi wa Zanzibar, kwa kujifunza kwake makosa yake, ambayo ni mengi.

Kosa moja la Mkapa kuhusiana na Zanzibar ni hilo nililolitaja: kuwa na nyuso tafauti. Japokuwa alihubiri ukweli na uwazi, lakini kwa Zanzibar hakuwa mkweli wala hakuwa muwazi. Hakuwa mkweli, maana alikataa kuutambua mgogoro huu kikamilifu na badala yake akawa anatambua tu ile sehemu ambayo ingelimnufaisha yeye na chama chake.

Ni hadi Tanzania ilipozalisha wakimbizi, baada ya vikosi vyake kufanya mauaji ya kutisha Januari 2001, ndipo alipoona ulazima wa kulishughulikia suala la Zanzibar. Tupo tunaoamini kwamba, kilichomvuta hasa Mkapa kuja katika meza ya mazungumzo na CUF sio ukweli kwamba kuna raia waliouliwa na askari wake, bali aibu ya nchi yake kuzalisha wakimbizi ambayo ilitishia kulichafua jina lake kimataifa. Chibui hiki cha kimataifa, hakikutaka kionekane kichafu mbele ya G8, International Monetary Fund na World Bank.

Hilo lilikuwa ni kosa ambalo Kikwete hatakiwi kulirejea. Asisubiri mauaji ya raia wakimbizi wengie ili kuchukua hatua. Maana hali ikifikia hapo sasa, kwa mara ya pili, itakuwa vigumu kudhibitika kama ilivyowezekana mara ya mwanzo.

Kosa la pili la Mkapa kwa Zanzibar ni kupuuzia kwake nafasi na dhima ya kila mshiriki wa mgogoro uliopo. Kuna wakati yeye mwenyewe alikuwa akijitoa kwa kudai kuwa ya Zanzibar hana mamlaka nayo. Alikuwa akijidanganya, maana yalipokuja kuvoromboka kwa umwagaji damu na wakimbizi, alijitokeza haraka haraka kuyashughulikia. Matokeo yake ndio Muwafaka II ambao, hata hivyo, haukuusimamia vyema.

Wakati historia inaionesha wazi nafasi ya uongozi wa Tanganyika katika siasa za Zanzibar, Mkapa alitaka kuigiza nafasi ya Mr Clean, akijifanya hahusiki kabisa na matatizo ya Visiwa hivi, wakati anajuwa fika kwamba watawala wa Tannganyika ya wakati huo na Tanzania ya sasa ni pawa na miko, part and parcel, ya mgogoro wa Zanzibar. Kama ilivyo nafasi ya Marekani kwa mgogoro wa Mashariki ya Kati, ndivyo ilivyo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mgogoro wa Zanzibar. Mataifa yote mawili, Marekani na Tanzania, yamekuwa yakilinda maslahi yake ya kisiasa na kiuchumi katika sehemu husika na hivyo hayawezi kujivua dhamana ya migogoro yanayoiibua.

George Bush anayeongoza taifa lililo maelfu ya meli kutoka Mashariki ya Kati ni muhimu sana kwa utatuzi wa mgogoro huu. Ndivyo pia alivyo Kikwete kwa mgogoro wa Zanzibar, ambaye siyo tu kwamba anaongoza taifa lililo kilomita chache kutoka Zanzibar, bali pia hiyo Zanzibar yenyewe imefanywa kuwa sehemu ya himaya yake. Mkapa alilikataa hilo kijuujuu lakini kwa udhati kabisa aliuendeleza mgogoro uliopo.

Kosa la tatu la Mkapa lilkuwa ni kuwatenga na kuwatimba wahusika wakuu wa mgogoro katika utatuzi wa mgogoro wenyewe. Katika mfano huo huo wa Mashariki ya Kati, kosa hili lilifanywa na Waisraeli na Wamarekani kwa Marehemu Yasser Arafat wa Palestina. Ingawa hatimaye waliweza ‘kumuua’ akiwa kazingirwa na vifaru vya Israel, walishindwa kuiua shakhsia, image, yake ya kuwa kiongozi wa Wapalestina. Ni kwa kukosa kumshirikisha katika utatuzi, ndio maana leo hii Hamas, hasimu wa Arafat katika uhai wake, kimechukuwa madaraka. Kama Israel na Marekani ziliamini kuwa Arafat hakuwa mtu wa kuzungumza naye, sasa wamejikuta wanakabiliana na wagumu zaidi yake. Hawa, sio tu ni adui wao, bali pia walikuwa adui wa adui wao.

Kuelekea uchaguzi wa 2005, Mkap aliitimba na aliitenga kabisa CUF. Mara kadhaa Maalim Seif alimuandikia akimuomba wakutane kuzungumzia hali ya Zanzibar, lakini hakujibu hata barua moja. Aliigiza kana kwamba Maalim Seif na CUF yake ni non-entity, haipo kabisa. Matokeo yake ndiyo huu mzigo aliomrithisha Kikwete. Kosa hili litakuwa na gharama kubwa hivi sasa ikiwa litaendelea kufanyika.

Kwa kila hali, Mkapa alijitahidi sana kuzifanya siasa zake kuelekea Zanzibar zilingane na za George Bush kuelekea Mashariki ya Kati. Unafiki na ubabe. Kwa kufanya hivyo, Mkapa ameiwacha Zanzibar iliyopasuka na kugawika zaidi kuliko aliyoikuta. Kikwete ana kazi ngumu sana ya kuwa tafauti.

Mgogoro wa Zanzibar haumtaki Mkapa mwengine kutatuka, lakini mtu tafauti kabisa. Kwa hivyo, Kikwete awe mpya kwa kila hali panapohusika suala la Zanzibar. Kwa Mkapa ajifunze alichokosea, na sio staili yake ya kulishughulikia. Akifanya hivyo atafeli kuliko alivyofeli Mkapa na miaka kumi ijayo, tutakuja kukaa kuandika makala kama hii ya kueleza uovu wake na sio mchango wake katika Zanzibar mpya.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.