MINOLTA DIGITAL CAMERAKwa zaidi ya miaka 40 sasa, misingi halisi ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964 imekuwa ikipotoshwa. Tangu hapo, kundi la watawala wasiojiamini na waliojazwa khofu zisizokuwa na msingi, limekuwa likitumia kutokujiamini kwake huko na khofu zake hizo kueneza agano potofu kwa kizazi cha Zanzibar.

Hivyo ndivyo ambavyo vimekuja kuwa vitu vilivyoisawiri historia nzima ya Visiwa hivi na, bila ya shaka, hata ya Tanzania nzima, kwa miaka yote. Kukosa kujiamini kwa watawala wa Zanzibar, kwa mfano, kumepelekea kuikubali na kuiendeleza imani potofu kwamba Mapinduzi ya ‘64 yalifanyika kwa lengo la kuuondoa usultani na utumwa. Kwamba yalikuwa Mapinduzi yaliyofanywa na Waafrika walio wengi dhidi ya Waarabu walio wachache.

Kisha kuna khofu ya washiriki wakuu wa Mapinduzi haya, Tanganyika kwa mfano. Ni jirani ambaye alikuwa akiiangalia Zanzibar kama mshindani na hivyo adui mtarajiwa. Kwa ufahamu wa Tanganyika, bila ya shaka na wa majirani wengine, Zanzibar ingeliweza kuinuka na kuwa taifa lenye nguvu kuu za kiuchumi na kitaaluma katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, na hivyo kuja kuchochea maasi ya raia kwa dola zilizoizunguka ambazo zingelionekana goigoi.

Khofu hii ndiyo iliyopelekea kubuniwa mikakati ya kuizuia Zanzibar isifike huko. Si ajabu kwamba Mapinduzi ya ‘64 yaliyofuatiwa na Muungano ndani ya siku 100 tu baadaye ni katika mikakati hiyo. Tangu hapo Tanganyika imekuwa ikifanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuhakikisha kuwa viwili hivyo vinadumu daima.

Hapa ndipo dhana ya Mapinduzi ya ‘64 ilipopotoshwa na sasa kuyafanya mapinduzi yenyewe kuwa nyenzo ya kuwagawa Wazanzibari badala ya kuwaunganisha. Ndipo ilipotakiwa ifahamike kwamba kupindua kulimaanisha mauaji ya kikatili dhidi ya wale walioambiwa wamepinduliwa, ubakwaji na uporwaji wa mali zao. Ndipo ilipotakiwa ieleweke kwamba kuendeleza mapinduzi hayo ni kwa kuwazuia ‘masultani’ na vibaraka wao wasirudi tena madarakani.

Kwa fasiri hii, nguvu zote za kiharamia zimekuwa zikiekezwa Zanzibar kuhakikisha kuwa ‘mapinduzi’ yanalindwa. Rejea ya karibuni zaidi ni uchaguzi uliopita wa 2005, ambapo uharamia wa kisiasa ulichanganywa na mikakati ya kijeshi na kuzaa matokeo yaliyomtangaza tena Mheshimiwa Amani Karume kuwa raisi wa Zanzibar. Kuelekea hayo, mwenyewe Mheshimiwa Karume alihakikisha utayarifu wake wa kuyatumia mapanga ya ’64, ikibidi, lakini si kuachia madaraka mikononi mwa ‘wapinga mapinduzi’. Na ndivyo alivyofanya.

Tusizame sana huko. Kiini cha mada ni kwamba mapinduzi halisi, kwa maana ya mabadiliko makubwa katika jamii ambayo huziathiri siasa, chumi na tamaduni za watu, ndiyo kwanza yanaanza Zanzibar. Hivi sasa, nje ya mduara huo wa khofu za kupikwa na ukosefu wa kujiamini na kuaminiana miongoni mwa tabaka tawala, kunajengeka viashiria vya mapinduzi mengine ya kweli mbele yetu.

Ingawa pana tafauti nyingi baina ya ’64 na sasa na, kwa hivyo, mapinduzi haya niyazungumziayo hapa hayafanani na hayo yaliyofanyika miaka 42 nyuma, lakini viashiria vilivyopo vina suluhisho moja tu: kwamba tayari mapinduzi halisi yameanza Zanzibar na kwamba hayawezekani tena kurudishwa nyuma.

Narudia. Si mapinduzi ya mapanga ya ’64. Si mvua ya risasi za Januari 2001. Si luteka la kijeshi la 2005. Ni enzi mpya za mabadiliko ya kisiasa ambayo si mapanga, risasi wala ukaliwaji wa kijeshi vinavyoweza kuyazuia yasitokee. Wasemavyo Waingereza: it’s high time!

Nimesema kuna viashiria vinavyoonesha uwepo wa mapinduzi hayo. Hapa nitavitaja na kuvifafanua vinne. Cha kwanza ni hali ya kuchoka kwa umma wa Kizanzibari kutokana na ugumu wa maisha. Hili limewapelekea kuvunjwa moyo na tajiriba yoyote kati ya tajiriba za kisiasa ambazo nchi hii imekuwa ikizijaribu kwa miaka mingi sasa, ikiwemo hiyo ya mapinduzi ya mapanga.

Kuelekea ’64, tunaambiwa hali ya maisha kwa kundi kubwa la watu ilikuwa ni mbaya. Hautajwi ubaya huu uliopo sasa, maana hadi wakati huo Zanzibar ilikuwa miongoni mwa nchi zinazotoa misaada kwa nchi nyengine. Lakini inawezekana huo ulikuwa ni utajiri wa serikali, huku raia wengi wakiwa na hali zisizoridhisha. Hivi sasa tumo katika hali ngumu zaidi kuliko wakati huo, maana sio tu ni raia wenye maisha magumu, lakini hata serikali iko taabani.

Ni wakati huu ambapo kila kitu kinapanda bei Zanzibar kwa kasi ya ajabu na huku pato la mtu wa kawaida likishuka kwa kasi hiyo hiyo. Hakuna uwiano hata wa mbali baina ya kile mtu anachokihitaji kwa matumizi yake ya siku moja na kile anachokizalisha kwa wiki nzima. Kundi kubwa la watu halina ajira. Kundi dogo lililo na ajira halipati ujira unaokidhi mahitaji yake ya kila siku. Na hata ujira huo mdogo unapopatikana kwa kundi hilo dogo, huwa umeshapitwa na wakati, maana ni kipindi sasa wafanyakazi wa serikali hupata mishahara yao ya mwezi uliopita katikati ya mwezi unaofuatia.

Hali ni ngumu kuliko maelezo haya yanavyojieleza. Unaothirika ni umma usio bega la kulilia isipokuwa wingi wa shida zao. Imesemwa kwamba inaposhindikana kuwaunganisha watu katika furaha zao, basi shida huwaunganisha. Ukali wa maisha Zanzibar hauchagui ufuasi wa vyama. Miezi minane baada ya serikali kujirejesha madarakani, furaha imepotea katika nyuso za Wazanzibari, lakini shida inaendelea kuwakusanya wahanga hawa pamoja, maana msiba wa wengi harusi. Na hii ni nyenzo muhimu kwa mapinduzi halisi.

Ni nyenzo muhimu inapounganishwa na ukweli kwamba umma huu hauna uhakika na uwezo wa watawala kuzitatua shida zao. Kinyume chake, watawala wamekuwa sehemu kubwa ya shida hizo. Mapinduzi halisi yana mashiko yake hapo: umma unapochoka na unapopoteza imani kwa mfumo uliopo (mistrusting and rebelling against the old establishment).

Kiashiria cha pili ni kiwango cha juu cha hamu ya taaluma kilichopo Zanzibar hivi sasa. Walio kwenye kada ya elimu wanaweza kulithibitisha hili haraka. Inawezekana kwamba madarasani mwetu hamutolewi elimu yenye kiwango (na yumkini ndio sababu idadi ya wanafunzi wa Kizanzibari wanaoingia katika elimu ya juu ni ndogo ikilinganishwa na wingi wa wanaotafuta fursa hiyo) lakini ule ukweli kwamba vijana wameigeukia elimu kama njia ya kupita, unaashiria mengi kwenye mapinduzi halisi.

Kwamba mchango wa elimu katika mabadiliko hauna mbadala. Utafiti usio rasmi unaonesha kwamba masomo ya History na Civics yanafeliwa sana katika vidato vya nne na sita, lakini bado madarasa yake ndiyo yenye wanafunzi wengi zaidi kuliko madarasa mengine. Ikiwa kweli wanafunzi huyafeli masomo hayo na bado tunayakuta madarasa yamejaa, basi miongoni mwa tafsiri zinazowezekana ni kuwa, katika madarasa hayo wanafunzi hawafuatii credits tu, bali wanatafuta kujijua (self-awareness).

Kujijua ndiko kunakozindua (concretization kwa msamiati wa Paulo Freira) ambako tumekuwa tukinyimwa kwa miaka 40 sasa. Mapinduzi yoyote duniani yanategemea zaidi mwamko wa watu wake. Mapinduzi yaendayo bila mwamko hayaleti neema ila maafa na nakama.

Kwa hivyo, nguvu kazi hii iliyoko madarasani inajinoa kitaaluma hivi sasa na ni kiashiria kikubwa cha kuwapo kwa mapinduzi halisi Zanzibar.

Kiashiria cha tatu ni kuwapo kwa kundi kubwa la Wazanzibari lililotupwa nje ya mstari wa maslahi, yawe ya kisiasa ama ya kiuchumi katika wakati ambao tabaka tawala limejisahau kabisa kwamba lina jukumu la kuongoza taifa na badala yake linasimamia uongozi wa kifamilia tu. Nakusudia kusema kwamba, utawala uliopo madarakani Zanzibar umewacha kuwatumikia Wazanzibari wote kama watoto wa nyumba moja na badala yake unawatumikia wachache mno, na hasa hasa kutoka familia kubwa.

Tunaambiwa kuwa miongoni mwa sababu za kufanikiwa kwa viongozi wa Mapinduzi ya ’64 ni ugoigoi wa uongozi wa serikali iliyokuwapo wakat huo. Tunaambiwa kwamba akina Marehemu Ali Muhsin Barwani walijisahau sana kwamba kuna upinzani wa karibu nusu nzima ya nchi na hivyo wakawa wanapanga mambo yao kana kwamba Zanzibar nzima na majirani zake walikuwa wakiiunga mkono Zanzibar Nationalist Party na Zanzibar and pemba people’s party tu. Ndipo wakakaribia kupitisha mswaada wa sheria kuzuia uhuru wa habari na wa kisiasa.

Hivyo ndivyo pia ilivyo Zanzibar ya sasa. Maslahi ya nchi yaonekana kujikita sana katika kuendeleza koo fulani, au wafuasi wachache Fulani wa chama tawala, huku yakiwatupa wengi wa Wazanzibari nje ya duara la kufaidika. Kujisahau kwa watawala, ingawa linaweza kuonekana jambo bay asana, lakini katika siasa za mageuzi ni kiashiria muhimu kuwapo ili kufanikisha mapinduzi halisi. Na hilo lipo Zanzibar.

Namna familia ya kifalme inavyojijenga na kujiimarisha kibiashara na kiuchumi Zanzibar, ndivyo inavyoshindwa kuzisoma alama za nyakati. Kadiri inavyojishughulisha zaidi na kupata mapesa, ndivyo inavyojitenganisha na umma, ambao toka hapo haikuwa na mualaka nao mwema. Himaya ya kibiashara si lazima sana iendane na himaya ya kisiasa.

Na kwa hakika siasa hasa za Zanzibar ndani ya tabaka tawala hivi sasa hazidhibitiwi tena na familia ya kifalme. Familia imebaki kuwa jina tu, huku ‘wengine’ wakiziendesha na kuzisanifu siasa hizo. Wengine hawa wanaweza kuwamo ndani ya chama tawala, lakini wana motisha tafauti ya kuwapo pale na ile iliyomo katika nafsi za familia ya kifalme.

Hakuna la ajabu ikiwa mgogoro wa mwanzo mkubwa unaweza kuihusisha familia ya kifalme, kwa upande mmoja, na watu walioizunguka lakini ambao hawatokani na falimia hiyo, kwa upande mwengine.

Kiashiria cha nne na cha mwisho ni kutawanyika kwa ushawishi wa kisiasa miongoni mwa makundi, kama vile ya kidini, ambacho huchochewa na kufunuka kwa mawazo ya watu. Wakati nguvu za kisiasa zikikosekana mikononi mwa tabaka moja tu, hupelekea udhibiti wake kuwa katika mikono ya kila mwenye satwa ya kuzieleza na kuzichambua.

Kwa sasa Zanzibar, ukiacha wagonganao ndani ya chama tawala, taasisi za kidini nazo zimekuwa na uwezo mkubwa wa kuzieleza na kuzichambua siasa za petu. Kidogo kidogo taasisi hizi zinapata nafasi ya kuzitawala na kuziendesha siasa za nchi hii.

Bila ya shaka dini haitakuja kuwa taasisi pekee ya kijamii ambayo itaona umuhimu wa kujishughulisha na hatima ya nchi. Huko twendako taasisi nyingi nyengine zitajitokeza kwa mintarafu hiyo hiyo. Na hapo ndipo mapinduzi mapya yatakapokamilika.

Lakini kuna maswali yanayojitokeza hivi sasa kama vile nani hasa atayaongoza mapinduzi ya sasa? Nini itakuwa matokeo ya mapinduzi haya? Zanzibar itafaidika nini na majirani zake watayaangaliaje? Je watakuwa tena kikwazo kwa Zanzibar mpya? Makala inayofuatia itajaribu kuyajibu maswali haya.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.