Kwa kawaida, kuna vitu ambavyo huleta pumbazo la akili. Hivi ni vile vinavyoweza kumpelekea mwanadamu kupumbazika na akaweza kuyasahau baadhi ya mambo ambayo yamemzonga na kuisumbua akili yake. Vipumbazio hivi vinajumuisha michezo, vilevi na hata mikusanyiko ya kawaida au ile ya kisiasa. Ukweli ni kuwa haviliondoshi tatizo husika, lakini humfanya mwenye tatizo apumbazike na asahau angalau kwa muda mfupi.

Katika maeneo mengi ya jiji letu la Dar es salaam ni kitu cha kawaida kuwaona wazee au vijana wapo kwenye vijiwe vya karata, bao, draft au viwanja vya mpira, hata mchana wa saa sita. Wakati mwingine watu hawa hudiriki kujitwisha mizigo ya karata za zamani vichwani mwao mithili ya wehu au huamua kucheza mpira mchana, wakati jua lipo utosini.

Hali hii mara nyingi husababishwa na kutokuwa na shughuli ya maana ya uzalishaji na kuweza kujiingizia kipato. Ni hali ambao husababisha tafrani (frustration) na hupelekea mtu kukata tamaa, na kwa wengine kuwa ndio mwanzo wa kujiingiza kwenye vitendo viovu kama vya wizi, ukahaba na utumiaji wa kupindukia wa pombe na madawa ya kulevya.

Ni katika vijiwe na viwanja hivi ambamo mambo mengi hujadiliwa (kwa maana yetu ya mitaani ya mjadala). Khabari za fulani kafumaniwa au idadi ya vimada alivyonavyo, humu ndio mahala mwake. Au kuwakuta vijana wakibishana kuhusu utajiri wa Salim Bakhresa na Mohamed Dewji, hilo ni jambo la kawaida katika maeneo haya. Ni nadra kusikia mambo ya maana.

Lakini, kwa siku za karibuni, imeanza kutokezea kuwa katika sehemu hizi ndimo ambamo lawama na uoza dhidi ya serikali iliopo madarakani zinamozungumzwa na kusikika kwa sauti ya juu kupita ile ya redio. Maeneo haya ndio ambayo pia wanasiasa wajanja hupenda kuyatumia ili kufikia malengo yao ya kisiasa. Si kitu cha ajabu kuona mwanasiasa akigawa maboksi ya karata au mpira na jezi pindi anapohitaji kura za kuingia madarakani. Hii ni kwa sababu mengi wa watumiaji wa maeneo haya ni watu wenye uelewa au elimu ndogo kuhusu mambo mbalimbali.

Lakini pia, maeneo haya ni muafaka kwa watu wa Usalama na wale maajenti wa kuwazuga watu ili mambo mabaya na kashfa nyingine ambazo zinaiandama serikali zisahaulike vichwani mwa watu. Na mara nyingi hawa watu wa vijiweni ndio ambao hutumika kama makasuku wa kusambaza taarifa hizo za kubuniwa bila wenyewe kijijua.

Kwa mara ya kwanza baada ya kumalizika uchaguzi mkuu wa raisi, wabunge na madiwani wa mwaka 1995, ndio lilipoibuniwa suala hili la Popobawa. Kwa wakati ule liliibuliwa kisiwani Pemba.
Itakumbukwa kwamba uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 1995 uligubikwa ni hujuma mbali mbali, wizi na ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu. Ni uchaguzi ambao hata wafadhili waliupigia kelele na wakakatisha misaada yao kwa Zanzibar. Wakati suala la Zanzibar kutengwa ni jumuia za kimataifa likifukuta, ndipo ghafla lilipobuniwa suala hili la Popo Bawa.

Mengi yalisikika kuhusiana na Popo hilo, lakini kitu cha kushangaza ni kwamba hakuna mtu ambae aliwahi kujitokeza au ambaye watu waliwahi kumuona na kuthibitisha kwamba aliwahi kufanyiwa kitendo cha kulawitiwa, ambacho jini huyo anadaiwa kuwafanyia wanadamu, kinyume na inavyodaiwa na watu kwamba pindi jini huyo anapokulawiti ni lazima utangaze.

Wakati suala hili halikuweza kuwapumbaza wananchi wale wa Pemba, ambao kwa wakati huo walikua kwenye madhila na manyanyaso makali kutoka kwa watawala, cha kushangaza ni kwamba kwa kiasi kikubwa hili lilifanikiwa kuzipumbaza akili za watu wengi ambao walikuwa wakipata taarifa kupitia magazeti ya udaku yalioamua kuzishabikia taarifa hizo kwa dhumuni la kuuza biashara yao zaidi.

Mara baada ya maajenti wa usambazaji wa hizi taarifa za Popo Bawa kushindwa kuzipumbaza akili za Wazanzibari, ndipo wakaibuka na jingine: kwamba Wapemba walikua wanapakaza vinyesi kwenye mashule na kwenye visima vya maji ya kunywa. Lakini tujiulize, je inawezekana kwa mtu mwenye akili timamu kuweka kinyesi kwenye maji au majengo ya shule ambayo mwanawe anayatumia?

Kwa wale wasioifahamu Pemba, wanaweza kusumbuka kupata picha halisi. Lakini ukweli ni kwamba, hadi wakati huo, maeneo mengi ya kisiwa cha Pemba hayajafikiwa na maji ya bomba, badala yake maji yanayotumika ni maji ya visima vifupi au vile vya kutumia kamba. Na mara nyingine visima hivi huwa si zaidi ya kimoja kwa kila kijiji. Sasa vipi mtu mwenye akili timamu aweze kukihujumu kile ambacho hana mbadala nacho?

Vibweka na viroja hivi havikuishia hapo, kwani mara tu baada ya uchaguzi wa mwaka 2005, na ambao, kama kawaida, ulishuhudia pia uvunjaji mwengine mkubwa wa haki za binadamu ambao ulisimamiwa na kuratibiwa na vyombo vya dola kwa upande wa Zanzibar, ghafla likaibuka pumbazo jipya. Hili likawa pumbazo la keki kujiandika maandishi ya Kiarabu yaliyomtaja Mwenyezi Mungu (S.W) au Mtume Muhammad (S.A.W).

Ni mapumbazo ambayo mara zote kwa Zanzibar yamekuwa yakibuniwa wakati ambao jamii inakuwa kwenye lindi la machafuko na huzuni. Kwa bahati nzuri, ni kuwa mara zote ambazo mapumbazo haya yamekuwa yakibuniwa, Wazanzibari wameweza kuwa makini na wagumu wa kutolewa kwenye fikra za kutoyafikiria matatizo yanayowasibu. Wamekuwa bado wakiiona mitego iliyobuniwa na wajanja kuwasahaulisha watu ili wasiyazungumze wala kuyajadili mambo maovu yanayofanywa na wale walio madarakani kwa maslahi yao binafsi.

Katika miezi ya hivi karibuni, vyombo vingi vya habari vimekuwa vikizungumzia matatizo mbalimbali yanayoikabili nchi yetu kwa upana wake na bila ya woga. Mengi yamezungumzwa na kuandikwa na pia kuhojiwa na vyombo hivyo. Hii ni baada ya kujitokeza kwa masuala mazito ambayo ni dhahiri kwamba utekelezaji wake una walakini mkubwa na ambao kwa sasa unaitafuna na kuigharimu nchi yetu. Masuala kama ya rada, ambayo inadaiwa kwamba wajanja wametafuna bilioni kumi na mbili pesa za walipa kodi wanyonge wa Tanzania, pamoja na masuala ya mikataba mibovu ya kuingamiza nchi, ndege mbovu ya raisi ambayo pia ina harufu ya rushwa na migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu dhidi ya bodi ya mikopo isiyokwisha, haya yote yanaiandama serikali na ndio yaliyotawala vichwa vya Watanzania wengi.

Ghafla limeibuka tena pumbazo la “Popo Bawa kaingia Dar anafanya vitu vyake.” Watu wanazikimbia nyumba zao kwa vile wanamuogopa Popo Bawa huyo. Wanaibuka wanaojiita watabiri na waganga maarufu kwenye vyombo vya habari, nao wanazungumzia Popo Bawa! Kibaya zaidi ni kwamba watabiri na waganga hao maarufu, wanamnasibisha huyo Popo Bawa wao waliyembuni na watu wa jamii ya Kipemba.

Kama nilivyoeleza kwamba, mara zote ambazo mapumbazo haya yamekuwa yakibuniwa, Wazanzibari wameweza kuwa makini na daima wamekuwa wakicheza ndani ya lindi la matatizo yanayowasibu na sio kwenye mitego iliyobuniwa na wajanja kwa lengo la kuwasahaulisha. Hawajapata kuacha kuzungumzia wala wala kuyajadili mambo maovu yanayofanywa na wale walio madarakani kwa maslahi yao binafsi.

Kutokana na magazeti mengi ya udaku na ambayo yanapendwa na wasomaji wengi kushabikia uzushi huu, mitaani nako kila upitapo kuanzia masokoni, vijiweni, viwanjani mpaka nyumbani, ni khabari za Popo Bawa. Popo Bawa tu!

Ni dhahiri kwamba sasa ngoma imepata wapigaji na wachezaji. Watu hawana tena muda wa kufikiria na kujadili kuhusu tatizo la umeme wa Richmond, wala suala la rada pamoja na ndege mbovu ya Raisi. Wamezugwa wamezugika!

Hayati Bob Marley aliwahi kutahadharisha, ingawa watu wengi wanadai kwamba aliimba. Bob alitahadharisha kwa kusema: You can fool some people sometime. But you can’t fool all the people all the time. Akimaanisha kwamba: “Unaweza kuwadanganya baadhi ya watu kwa wakati fulani. Lakini huwezi kuwadanganya watu wote muda wote.” Haya ni maneno aliyozungumza Bob, ambaye kuna watu kwao ni mvuta bangi asiye na maana.

Imewezekana leo kupumbaza watu hawa kwa pumbazo la Popo Bawa. Kesho mnaweza pia kuwapumbaza kwa kuwaambia kwamba “Real Madrid wanakuja Tanzania” hata kama ujio huo hautoshibisha matumbo yao wala kuondoa dhiki walizonazo, zaidi ya kuligharimu Taifa hili mnalodai maskini mabilioni ya pesa.

Lakini kuna siku wataamka kama walivyokwishaamka wale wa Zanzibar, na watahoji. Sasa ikijakufikia hatua hiyo, muwe na jibu la kuja kuwapa, kwani mapumbazo ya kitoto hayatowanusuru na hayatofua dafu mbele ya ghadhabu watakazo kuwa nazo. Na wale wasanii wabunifu wa wimbo wa Popo Bawa, hawatokua tena na wimbo wala mziki wa kuwatuliza mzuka wao wa mabadiliko utakaokuwa umekwisha panda. Kuna siku itakuwa kweli, chembilecho mpenzi wetu, Marehemu Ali Nabwa. Na hiyo siku haiko mbali hivyo.

abdullahahmad21@yahoo.com
Simu Na. 0717 198980

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.