Wazee walisema, ukitaka kuijua sumu ya nyoka, mbane koo. Tarehe 6 Machi 2007, huko Mkoa wa Pwani, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, alipokea zawadi kutoka uongozi wa mkoa huo kwa ‘utumishi mwema’ kwa kipindi cha miaka 10 ya urais wake na akatumia fursa hiyo kuionesha rangi yake halisi.

Akakumbuka kiburi chake cha uraisi kwa kuwakemea wale ‘wanaomsemasema’ sasa. Kwa kuwa, kwa siku za karibuni, Mkapa amekuwa akisemwa kuhusu kashfa ya ununuzi wa Rada na kwa kuwa tunaomsema ni wananchi, tukiwemo wanahabari (japokuwa mwenyewe alitaka ionekane kwamba ‘wanaomkera’ hivyo ni wapinzani wake wa kisiasa tu), hapa tuseme wazi kwamba hatukuridhika na kemeo lile.

Ametuchefua; na ametukumbusha kuwa yeye hakuwa rais wa kusikiliza malalamiko ya wananchi. Hata akiambiwa watu wameuawa, kama sio watu wa karibu yake kwa mambo yanayomkereketa, sio tu kwamba aliipuzia, bali alihakikisha mfanyaji hapati tatizo lolote. Kwa mfano, kuna yale mauaji ya kutisha yaliyofanywa na Polisi kule Pemba dhidi ya raia zaidi ya 45 wasio na hatia. Alichofanya Mkapa ni kuhakikisha kuwa, waliofanya mauaji yale hawachukuliwi hatua yoyote ya kisheria.

Kwa kipindi cha miaka 10 ya urais wake, nchi hii ilishuhudia ukandamizaji mkubwa wa sauti za umma na demokrasia. Hakuna uchaguzi hata mmoja uliofanywa katika kipindi chake ukawa angalau na asilimia 40% ya uhuru na wa haki ya kweli. Ndiye Mkapa huyo huyo aliyekwenda Zanzibar katika viwanja vya Lumumba mwaka 1996 kuwaambia Wazanzibari ‘wamkome’ kumpelekea barua za kumtaka kushughulikia hali mbaya ya kisiasa na mateso ya Serikali dhidi ya raia hao. Akasema kwamba yeye ni CCM na serikali ni ya CCM. Hataishughulikia wala hatoshughulishwa.

Ndio maana Mkapa sasa anasema hashughulishwi na maneno ya wananchi. Anajua ni yale yale: yeye ni CCM, Rais Jakaya Kikwete na serikali ni CCM; na CCM wana tabia ya kulindana. Labda ndio Kikwete anasema aachwe Mkapa apumzike, asisumbuliwe. Ulinzi huo anaanza kupewa na mwenyewe kauona. Ameanza kujivunia mkoani Pwani.

Hatutaki kuhesabu tena na tena kila kibaya alichokifanya Mkapa kwa nchi hii, lakini tunataka tuseme kwamba huyu bwana aliboronga sana. Si uchuro kumtaka sasa ajibu shutuma na lawama zinazomkabili. Ana mengi ya kujibu kuhusu zahma za Zanzibar katika kipindi cha utawala wake akiwa Amiri Jeshi Mkuu wa nchi.

Kwa mfano, wakati wa kampeni mpaka upigaji kura, Zanzibar aliigeuza Darfur kwa kupeleka majeshi, wengine hata Kiswahili hawajui, kazi yao ni vitisho na kupiga watu tu. Historia ya Zanzibar sasa inaingiza mkasa mpya wa Mtendeni Siege ambapo Wazanzibari walizingirwa katika eneo lote la Makao Makuu ya Chama cha Wananchi (CUF) kwa muda wa siku nne wakiwa na funga ya Ramadhani.

Kwa Jamhuri ya Muungano, ana mengi pia ya kujibu kuhusiana na hilo la Rada na la ndege ya kifahari. Serikali yake iliitumbukiza nchi katika lindi kubwa la ufukara, licha ya kelele za wananchi na nasaha zao kwake. Hakujali. Hakubalilisha msimamo wake na wa chama chake dhidi ya matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi wa nchi hii.

Ni Mkapa, alipokuwa Rais, aliyepewa dhamana katika mikataba hewa na mibovu, ununuzi wa vifaa vibovu na bei ghali wakati huku elimu ikiwa duni, wanafunzi kusoma chini ya miti kwa kukosa vikalio, walimu wenye ujuzi na ukosefu wa madarasa, na huku akiwa na msaada wa mamilioni ya MMEM na MMES.

Sasa ameondoka na ameiacha nchi maskini zaidi kuliko alivyoikuta kutokana na tabia yake mbaya ya kiutawala. Mali ya nchi inakwenda kuwanufaisha watu wa nje, sisi wenyewe tumo kwenye adha chungu nzima za kukosa maji, umeme wa uhakika, barabara mbovu za vijijini na, juu ya yote, ukosefu wa usalama.

Alipokuwa madarakani alijifanya si mtu wa kuambiwa akasikiliza. Na sasa anataka tusimuulize. Basi hata kwa pesa zetu alizozikusanya kwa jasho letu na kodi zetu na kuzigeuza kama mali yake? Alipokuwa madarakani, tulimwambia, hakutaka kusikia. Leo amestaafu, baada ya kuboronga kote huko, halafu anataka bado tuendelee kunyamaza tu, kwa sababu Bwana Kikwete atasema asishughulishwe?

Basi tunamwambia, Kikwete ni Rais wetu sote. Kama ni kuingia madarakani, ni kwa kura zetu sisi, wananchi. Hivyo, hata yeye anawajibika kwetu. Hawezi kutufunga midomo tusiulizie hela yetu. Vyenginevyo, naye aamue kukaa madarakani kwa staili zile zile za kwako, za kimkapamkapa.

Kwa hivyo, tujibu hoja zetu: Ni vipi rada imeingia kwenye rushwa kiasi hiki? Ukiacha ile bei ‘halali’ mulouziana, kile cha juu kiko wapi? Ni vipi ulipitisha mikataba mibovu ya madini? Na, juu ya yote, ni kwa nini watu wengi waliuawa kwa risasi bila ya hatia, tena kwa silaha zilizonunuliwa kwa pesa za walipa kodi wa Tanzania? Tunataka majibu na sio ugeuke mbogo kwa ukali, Mheshimiwa Rais Mstaafu.

 

Gazeti la Fahamu Mwananchi, 12 Machi 2007

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.