Nilizaliwa mnyonge
Nikakulia unyonge
Lakini
Nilipambana niishi
Niishi waishivyo watu
Watu waitwao watu
Nami nikajikuta
Katika mpambano huo
Naingia ulingoni
Nikarusha makonde
Nami harushiwa pia
Kwamba ndivyo maisha yalivyo
Maisha zama na zamu

Nakumbuka
Mtaa nalozaliwa
Uliitwa Kisiwandui
Zama hizo zikiitwa
Za usultani
Kwetu tulikuwa masikini
Lakini hatukufa njaa
Senti kumi na tano
Nilizopewa na mama
Kununua maandazi
Na uji wa mbaazi
Zilitosha sana
Mimi naye tukaishi
Maisha zama na zamu

Nakumbuka
Nilioshea harita
Ama sabuni ya chokaa
Lakini
Sikuwa mchafu
Wala sikunuka kikwapa
Kwa kuwa usafi wa nguo
Na uswafihi wa nyoyo
Ilikuwa ni khulka
Ya nyumbani
Zanzibari
Mambo ni zama na zamu

Nyumbani?
Ndiyo nyumbani
Japo kwa maana ndogo
Ya kwamba Mola Jalali
Alinijaalia
Nizaliwe Zanzibari
Na pano pawe ni petu
Wazungu huita home
Bahati mbaya ingawa
Waja watawala waovu
Walitaka kwa yakini
Nife na hali si kwetu
Ati niwe stateless
Hawakuweza
Nilikufa Mzanzibari
Kama nalivyozaliwa
Maisha zama na zamu

Nakumbuka
Kisiwandui yetu
Ya ‘mabondia’ wa mitaani
Akina Msafiri Rocki
Ya Ba Manga na Kaiza
Wekuwa wakipigana
Utadhani wauwana
Hakuna kuamuliza
Ukiingia katikati
Konde mzigo mzima
Vimulimuli machoni
Mbio mtindo mmoja
Maisha zama na zamu

Nakumbuka
Maduka ya mtaani
Kwa Baba Hadi
Majani ya chai pesa mbili
Sukari pesa nne
Mkate wa pesa sita
Kwa Bi Buluu samaki
Kwa Bi Makiya mbaazi
Maisha zama na zamu

Nakumbuka
Kisiwandui kuna misikiti
Mmoja tuliuita Makuti
Mwengine Mabati
Nilisali ndani yake
Nikasujudi kwa Mola
Kwamba nami nalikuwa
Dhaifu mbele ya Bwana
Kama walivyo waja wengine
Wajuao Mungu wao
Maisha zama na zamu

Nawakumbuka
Wanawake wa kikwetu
Walikuwa na heshima
Wakivaa mitandio
Wakijipamba kwa liwa
Kung’arisha ngozi zao
Wakinukia marashi
Na udi wa mawaridi
Nakumbuka kila kitu
Kilichopita maishani
Na hapa sasa nakiri
Maisha zama na zamu

11 Machi, 2007

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.