
Maisha ya hapa Bongo ni magumu sana, lazima nikiri hivyo. Lakini pia, lazima nikiri kitu kingine: maisha ya hapa yana matumaini makubwa. Siku zangu za kuishi na watu wa hapa zimekuwa zikinipa fundisho moja: kwamba mabadiliko yawezekana. Kila siku napita mitaani na pikipiki langu, naangalia Wabongo wanavyoishi. Napanda daladala nao. Nasikia na naona dhiki zao. Nayahisi mabadiliko.
Ninapowataja ‘wao’ sikusudii kuwa mbaguzi. Bila shaka, kwa sheria, mimi ni Mtanzania kama walivyo wao. Kwa hivyo ni sehemu yao. Lakini kuzaliwa na kukulia kwangu Zanzibar kunanifanya mgeni kwao, kama nao walivyo wageni kwetu.
Wabongo. Mabadiliko. Nanusa harufu hiyo kila mahala. Nazungumzia mabadiliko katika mfumo wa kijamii, ambao, bila ya shaka, unahusisha kila kipengele cha maisha: uchumi, siasa, utamaduni na mengineyo. Machoni mwa vijana wenzangu ninaokutana nao, nazisoma ishara za mabadiliko.
Ugumu wa sasa wa hali ya maisha na kufeli, kwa kiasi kikubwa, kwa serikali iliyopo madarakani kutoa maisha bora kwa kila Mtanzania, ni jambo lililo wazi. Kila mtu anajuwa hilo. Lakini cha muhimu hapa si ukweli kwamba kila mtu anajuwa hivyo, bali ni kuwa sehemu kubwa ya watu ninaowazungumzia wanajali kuwa hali yao iko hivyo.
Nawaona watu ambao wanajali kuwa wao, na maelfu ya ndugu zao, wanalala na njaa na hivyo lazima mabadiliko yafanyike ili walale na shibe. Wanajali kuwa wao, na maelfu ya wengine, hawana ajira, kwa hivyo mabadiliko yaje ili wapate riziki. Wanajali kuwa vitoto vyao vichanga, na vya wenzao, vinakufa kwa maradhi kutokana na kukosa matibabu yanayostahili, na kwa hivyo mabadiliko yaje ili vitoto hivi visife ovyo ovyo.
Nimewakuta wanajali hayo. Sijaona ile sura ya jumla ya kuvunjika moyo iliyoko kule kwetu, ambako tumelemazwa na dhana ya kila kitu hakiwezekani. Wimbo wa kutowekuzekana hapa uko mbali na fikira za hawa ninaokutana nao. Mabadiliko hapa yanaonekana kuwezekana kabisa, maana hata ukiwa njiani unaweza kuihisi ile imani waliyonayo watu, kwamba mabadiliko ni ya lazima katika maisha yao.
Ishara nyingi zitakwambia hivyo___ pirika zao za maisha kuanzia pale bandarini ukishuka boti kutokea Zanzibar hadi uendako Tabata, ujenzi wa maghorofa Kariakoo katika mitaa yake yote, utanuzi wa barabara, na harakati za kibiashara. Unaiona hasa nchi inakwenda mbele, haikusimama. Ukiwa ndani yake, unajihisi hasa unavyokwenda nayo.
Zanzibar yetu, masikini, ina picha iliyo kinyume cha hiyo. Kuna kuporomoka badala ya kusimama wima. Kuna kurudi nyuma badala ya kwenda mbele. Kuna kuvunjika moyo na kutamauka. Ni kana kwamba, tumeshafika mwisho wa njia. Kila nikienda nyumbani, huiona hali hiyo.
Lakini, je ni kweli kuwa kwetu Zanzibar mabadiliko yameshindikana kabisa kabisa? Siku za kuwa hapa Bara zinanifundisha kitu tafauti. Kwamba nasi, ikiwa kweli tumekusudia, tunaweza kubadilika na kuibadilisha hali yetu.
Tunaweza kubadilisha mlo wetu kutoka ule wa muhogo kwa madagaa kuwa pilau kwa bata. Tunaweza kuzikuza hali zetu kutoka hii ya kutokumiliki hata baiskeli hadi ile ya kumiliki gari. Nakusudia kusema kuwa tunaweza kuishi maisha bora zaidi ya haya, tena katika kila nyanja ya maisha____ kisiasa, kiuchumi, kijamii, kitamaduni. Si kweli kwamba tumekatikiwa na jaala ya maisha. Si kweli kwamba tuliumbwa ili tuishi na tufe hivi hivi.
Ule wimbo kuwa haiwezekani kwa kuwa dunia nzima iko hivi hivi, ni uzushi mtupu. Ziko ‘dunia’ zisizokuwa hivi. Kama nilivyosema, hata hapa Bara tu hapako kama ilivyo Zanzibar yetu. Kwa nini ‘dunia yetu’ ya Zanzibar tu ndiyo iendelee kuwa hivi. ‘Dunia nyengine’ za wenzetu, hata kama zamani zilikuwa kama hivi ilivyo yetu sasa, kitambo zimeshabadilika. Wenyewe, wenye dunia hizo, wanajibadilisha na wanazibadilisha dunia zao, maana mabadiliko yawezekana!
Hata hao wanaotuimbia wimbo huo, wanajuwa kuwa hivyo si kweli. Wanatuimbia kwa kutukejeli tu. Maana hata ‘dunia yao’ wao haiko kama hivi ilivyo ya Sogea, Miembeni, Konde na Wete. Wao wameweza kujibadilisha, wakaibadilisha na kujipa dunia yao nzuri ya Mazizini na Mbweni.
Kuna wakati, si zamani sana, sote tuliishi katika dunia moja, hii hii ya giza totoro na ya kuhangaika kwa madumu ya maji. Ghafla wakayabadilisha maisha yao yote na, sasa, hayo ya giza totoro na madumu ya maji yamebakia hekaya tu kwao. Sasa kama wao wameweza kuibadilisha dunia yao, kwa nini na sisi tusiweze kuibadilisha yetu? Kwa nini watufanye tuamini kuwa haiwezekani kuwa na Zanzibar mpya, yenye matumaini, iliyobadilika?
Lakini ukitafiti kidogo, utagundua kuwa misamiati hii ya ‘haiwezekani’ na ‘hakuna liwalo’ ni mwangwi wa sauti za woga zitokazo vinywani mwa watawala (nasikia hivi sasa hata wanakanusha kuwa hakuna mazungumzo baina ya Chama cha Mapinduzi, CCM, na Chama cha Wananchi, CUF). Hawa jamaa wana woga kuwa mabadiliko yakiwezekana, yatawaathiri ‘wao’ moja kwa moja. Wao hii inamaanisha wachache na familia zao. Wanadhani ikiwa utajiri wa nchi utatawanyika mikononi mwa Wazanzibari wengi, tafsiri yake ni umasikini mikononi mwao ‘wao’. Hisabu mbovu. Mawazo mgando.
Bahati mbaya ni hiyo niliyoitaja kuwa, kuna namna fulani ya raia kulemazwa na kasumba hii ya ‘kutokuwezekana’. Kuna wale anaowataja Dk. Said Ahmed Mohammed katika riwaya yake ya Babu Alipopofuka (Jomo Kenyatta Foundation, 2001) kuwa ni wanunuliwa (akiwatafautisha na watawawaliwa).
Mtawaliwa ana afadhali, maana huthubutu angalau kujipapatuwa na kupigana kujikombowa, mnunuliwa hata hajuwi kuwa analotendewa silo, kwa hivyo hana habari kabisa na ukombozi. Kwamba yeye mwenyewe huwa ni milki ya bwana mithili ya kitambaa dukani: hakina kauli, hakina amri. Hukaa awekwapo, akaenda apelekwapo!
Panapohusika mabadiliko, wanunuliwa lazima kwanza wapunguzwe kwa wingi unaowezekana. Kwamba kwanza wabadilishwe wao kabla ya kuwaingiza katika mchakato wa kutaka mabadiliko ya jumla ya hali yenu. Hawa wana kazi nzito. Wenyewe huwa hawanyanyuki kuleta mabadiliko na hata wakinyanyuliwa na wenzao, hutamauka haraka. Rafiki yangu mmoja humuita mnunuliwa, a looser.
Kinyume chake, mtawaliwa, hata akiona kuwa mwenendo wa matukio na matokeo katika harakati zake za kujikombowa unasuasua, hafiki pahala pa kusema kuwa haiwezekani kubadilisha hali au hakuna litakalokuwa. Bado ataendelea kujali na kuamini kuwa lazima mabadiliko yaje na hivyo lazima ayapiganie.
Siku nyingi za kuwa katika harakati zinaweza kumuhofisha kuwa mafanikio yako mbali, lakini bado hawezi kuacha kuwa mpambanaji. Hata katika wakati mgumu kiasi gani, bado sauti kutoka ndani kabisa ya nafsi yake humwambia kuwa mabadiliko yanawezekana na kwamba yako mengi yatakayokuwa.
Kuibadilisha hali ya Zanzibar kunawezekana. Changamoto ni hilo la kupunguza idadi ya wanunuliwa kwa kuongeza idadi ya watawaliwa. Kuzidi kuwa ngumu kwa hali ya maisha kunalifanya hilo liwe rahisi. Kuna kugongeshwa ukuta kwa kasi hivi sasa. Kumgongesha mtu ukuta ni kumfikisha katika kilele cha dhiki ya maisha na mwisho wa njia. Anayefikishwa hapo, hubakiwa na uchaguzi wa kufanya jambo moja tu kati ya mawili haya: ama kuyasubiri mauti yamfike hapo alipo, au kugeuka nyuma na kumgeukia aliyemfikisha hapo ukutani.
Wanaokaa kitako kuyasubiri mauti, hujidai kuwa hiyo ndiyo jaala yao waliyoandikiwa na Mungu, na wao hawakuweza kuiepuka. Hao ndio wanunuliwa. Sijuwi ni mungu gani huyo wanayemkusudia wao, aliye dhalimu kiasi hicho? Kwamba Mungu huyu tunayemuamini sisi wengine, ametakasika na ila hiyo ya udhalimu. Mungu wetu hamfelishi kiumbe chake. Mungu huyu aliyejaa mapenzi kwetu na aliyetupa kila uwezo na nyenzo za kuyafurahia maisha aliyotukirimu, hajatuumba tuishi maisha ya udhalilifu na mateso katika ardhi yake mwenyewe. Kukubali kufa hapo ukutani ni fedheha kwa ubinaadamu wetu na kumnasibisha Mungu na fedheha hiyo ni kumkosea. Huko ndiko kufa kikondoo___ bila ya hata kujitetea.
Badala yake, kunyanyuka na kuigeukia sababu na msababishi aliyekugongesha ukuta kwa nia ya kujinasuwa hapo ulipotupwa, ndiko kumshukuru na kumtakasa Mungu. Na huko ndiko kupambana. Ndiko kuleta mabadiliko. Huko ndiko kusema kuwa: “ninaweza kuwa mtawaliwa kwa siku chache, lakini siwezi kuwa mnunuliwa wa milele!”
Narudia. Kazi kubwa ni kuwabadilisha wanunuliwa kuwa watawaliwa. Wakubali kuusaka ukombozi. Na hilo wanaliweza. Hata watu hawa ambao mwanzo walikwisha kuvunjika moyo, wanaweza kuleta mabadiliko, wakitaka. Waswahili husema: “kuweza, kutaka!” Kama hutaki, hakuna unaloweza kulifanya hata liwe dogo kiasi gani na, kama unataka, hakuna litakalokushinda hata lile kubwa, kubwa kabisa. Inahitajika saikolojia katika hili. Labda ile Dk. David Schwartz anayoiita the magic of thinking big!
The magic of thinking big inaanza na imani kwamba kuja na kutokuja kwa mabadiliko ni jambo lililomo katika mikono yetu, na wala si suala la mtu mmoja au kikundi fulani cha watu. Ni suala la kila mmoja wetu, la kila aliyegongeshwa ukuta, kunyanyuka akajifuta vumbi na kuazimia mabadiliko. Kwamba wabadilishaji ndio sisi kwa sisi. Hakuna wengine. Ni kutokana na sisi, na ni kwa kupitia kwetu sisi tu, ndio mabadiliko yanawezekana.
Ni mimi na wewe tunaoweza kuleta mabadiliko katika jamii hii. Hivi hivi utuonavyo: mburumatari, walalahoi, masikini au kama anavyotuita Sembene Ousomane God’s Bits Of Wood, waja wa Mungu, maana ulimwenguni kote, historia ya mabadiliko imechorwa katika migongo ya akina sie pangu-pakavu. Kwa jasho na nguvu zetu.
Kote kote___ tokea Ulaya hadi Amerika, Arabuni hadi Afrika, ni akina Masanja na Shaame waliotutumua migongo yao kukabiliana na sulubu ili kuleta mabadiliko. Na kwetu, Zanzibar, ukisikia uhuru na mapinduzi yaliwezeshwa na akina sie!
Kwa hivyo, suala muhimu katika kuleta mabadiliko ni kutaka na kujali. Ikiwa tunajali kuwa hapa tulipo sipo na kwamba lazima twende mbele zaidi ya hapa, basi nina hakika kuwa tutakwenda na tutafika. Wanasema: “never say impossible in this world, for the dream of yesterday is the hope of today and the reality of tomorrow! ‘Kamwe usiseme haiwezekani katika dunia hii, maana ndoto ya jana ndio matarajio ya leo na ukweli wa kesho’. Muhimu ni kuamua, kujali na kutaka. Yote yawezekana.
Share this:
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to email this to a friend (Opens in new window)
- Click to share on LinkedIn (Opens in new window)
- Click to share on Reddit (Opens in new window)
- Click to share on Skype (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Pinterest (Opens in new window)
- Click to share on Tumblr (Opens in new window)