Hapa, hata kwa kiwango cha chini cha utumiaji wa akili, utaona kizungumkuti kilichopo. Kwamba sasa wanaokutanishwa kujadili matatizo ya mtoto ni mtoto na mzazi mmoja, badala ya kuwa mzazi na mzazi. Na hilo lisingelikuwa kizungumkuti ikiwa mmoja wa wazazi hao alikufa kifo kilichofahamika na kujuilikana hasa kwamba hayupo tena ulimwenguni. Lakini katika uhalisia uliopo hapa, si kweli kwamba mzazi huyo, yaani Tanganyika, kwamba alikufa. Kiuhalisia na kivitendo, Tanganyika haikufa. Ipo, tena ipo kabisa!
Majuzi mawaziri wa Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT), wakiongozwa na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, walikutana na mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), wakiongozwa na Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, katika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.

Tuliambiwa kuwa ni mkutano wa kujadili matatizo (wakwepaji hoja huziita ‘kero’ ndogo ndogo tu) ya Muungano kama ambavyo ilikuwa imeagizwa na Rais Jakaya Kikwete katika mkutano wake na watendaji wa serikali za Tanzania na Zanzibar huko hoteli ya Ngordoto, Arusha, mwezi mmoja tu baada ya kuapishwa kuwa raisi.

Tuliambiwa kwamba miongoni mwa yaliyoafikiwa ni kubadilisha katiba ili kuingiza madini katika orodha ya mambo ya Muungano kwa kufidia nishati ya mafuta ambayo tayari ilishaingizwa kitambo mno. Paliafikiwa pia kuangaliwa upya suala la utendaji wa bodi ya mapato, ambao unaonekana kuwakandamiza zaidi Wazanzibari. Na, pia pakaafikiwa ushirikishwaji wa Wazanzibari katika chombo kinachohusika na uchimbaji wa mafuta, TPDC.

Hata hivyo, mjadala katika makala hii hauelekezwi huko kwenye maafikiano wala mafanikio ya kikao hicho cha Karimjee. Badala yake, makala hii inarudi nyuma kidogo, wasemavyo Waingereza “back to the basics”, ili kujaribu kujibu suali muhimu sana na lililoko juu ya maafikiano hayo, nalo ni “Nani amekutana na nani kujadili nini?”

Hoja ya msingi ni kwamba, ikiwa kweli dhamira ilikuwa ni kutatua matatizo yanayoukabili Muungano huu, basi waliokutana kuyajadili matatizo yenyewe sio. Nina sababu mbili; moja ni kwa kuwa katika kikao hicho Tanganyika haikuwakilishwa na, pili, ni kuwa walioiwakilisha Zanzibar ni wepesi mno katika mizania ya kitaaluma, kisiasa na, hivyo, nguvu za maamuzi.

Kwa maneno machache, kikao kile kilidhihirisha mambo mawili tu: moja ni kuendelea kuburuzwa kwa Zanzibar katika Muungano huu na jengine ni kizungumkuti cha Muungano huu. Lilikuwa ni igizo jengine la kisanii na ambalo, kwa mara nyengine tena, lilichezwa kwa ustadi mkubwa na wenzetu wa Tanganyika wakitumia mgongo wa Muungano. Na tena na tena Zanzibar ikajikuta kumezeshwa katika tumbo lisilojaa la Mfalme Jeta kwa ‘ridhaa’ ya Wazanzibari wenyewe.

Nimesema turudi kwenye chanzo – Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Uhusiano uliofungwa kwa makubaliano maalum yaliyokuwa na vipengele kumi na moja na kutambulika kama Makubaliano ya Muungano. Yaliyokubaliana yalikuwa madola, mataifa na nchi mbili huru. Na hapa nataka nisisitize tena na tena kwamba msingi wa kuungana kwetu haukuwa idadi ya watu wala ukubwa wa eneo.

Kwa hivyo, si Jitanganyika kubwa na Kijizanzibari kiduchu zilizoungana, bali Tanganyika kama taifa na dola huru na Zanzibar kama taifa na dola huru. Ni dhambi isiyosameheka kuutafsiri, kuuchambua na au kuuendesha Muungano huu kwa misingi wa idadi ya watu na au ukubwa wa eneo.

Tafsiri yoyote ya Muungano huu, uchambuzi na ama uendeshaji wake unatakiwa uakisi hasa msingi wa kuundwa kwake, ambao ni uelewa wa uwepo wa udola na utaifa wa waundaji wake, Tanganyika na Zanzibar.

Hapa ndipo hapo back at the basics. Ni msingi huu ndio ninaoutumia kutafsiri kikao kile cha Karimjee baina ya wawakilishi wa SMZ na SMT. Nani na nani?

Upande mmoja ni Nahodha na kundi lake akiiwakilisha Zanzibar. Tunaweza kutafautiana juu ya uhalali wa akina Nahodha kushikilia nafasi wanazozishikilia hata wakawa na ujuburi wa kuiwakilisha Zanzibar, lakini lazima tukubaliane kuwa, utaratibu wa siasa za kilimwengu unazitambua serikali kama mawakala wa dola.

Hivyo, kwa vyovyote vile, hawa walikuwa wanaiwakilisha Zanzibar kama vile ambavyo miaka 42 nyuma, Abeid Amani Karume alifanya. Zanzibar imewakilishwa kwa kuwa ni mzazi mmoja wa mwana anayeitwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Hapa nisisitize tena kwamba jina hilo ndilo jina halisi la Muungano huu, kwa mujibu wa makubaliano, na sio Tanzania.

Upande wa pili kuna mzazi mwengine, Tanganyika. Waziri Lowassa na wenzake wanatambuliwa kama mawaziri wa serikali ya Jamhuri ya Muungano. Kwa maneno mengine ni wawakilishi wa mwana ‘Muungano’ aliyezaliwa na wazazi wawili, Tanganyika na Zanzibar. Kinadharia hawa si wawakilishi wa Tanganyika, ambaye ndiye mzazi mweziwe Zanzibar na ndiye ambaye alistahili kuwa wa kuzungumza naye kuhusu matatizo ya mwana wao, kijana ‘Muungano’.

Hapa, hata kwa kiwango cha chini cha utumiaji wa akili, utaona kizungumkuti kilichopo. Kwamba sasa wanaokutanishwa kujadili matatizo ya mtoto ni mtoto na mzazi mmoja, badala ya kuwa mzazi na mzazi. Na hilo lisingelikuwa kizungumkuti ikiwa mmoja wa wazazi hao alikufa kifo kilichofahamika na kujuilikana hasa kwamba hayupo tena ulimwenguni. Lakini katika uhalisia uliopo hapa, si kweli kwamba mzazi huyo, yaani Tanganyika, kwamba alikufa. Kiuhalisia na kivitendo, Tanganyika haikufa. Ipo, tena ipo kabisa!

Sitaki kutumia makala hii kuonesha uwepo wa Tanganyika, lakini itoshe kusema hapa kwamba Lowassa hakuwa shudu ya Nahodha kukutana naye kujadili Muungano panapohusika nadharia ya nani kamzaa nani. Kwa mujibu wa makubaliano ya Muungano, Lowassa anayeiwakilisha serikali ya Muungano, ni mwakilishi wa kiumbe. Muumbaji wake, Tanganyika, ndiye hasa aliyepaswa kukutana na muumbaji mwenzake, Zanzibar. Na si kinyume chake.

Kwa hivyo, ikiwa lengo hasa lilikuwa ni kuyajadili matatizo ya Muungano, basi waliokutana kuyajadili walikuwa sio. Mjadala ule, kwa hivyo, haukuwa na maana. Hii ni kusema hata hicho kilichoafikiwa katika mjadala wenyewe, hakina maana kwa ustawi wa Muungano kama Muungano, labda iwe kwa Muungano huu kama kitu chengine kama vile ukoloni, kwa mfano.

Hicho ni kizungumkuti kimoja. Lakini chengine, katika kikao kile ni nafasi ya Rais wa Zanzibar, ambaye kwa mujibu wa Mabadiliko ya Kumi na Moja ya hiyo inayoitwa katiba ya Muungano, anakuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Muungano. Majuzi tu Rais Amani Karume ameapa kiapo cha uaminifu na utiifu mbele ya Rais Kikwete kushikilia wadhifa huo.

Suali la kujiuliza hapa ni kwamba katika kikao hiki alipaswa kuwa upande gani? Wa kuiwakilisha Zanzibar kama alivyofanya marehemu baba yake au wa kuiwakilisha Tanganyika iliyo nyuma ya Muungano, kama alivyoapa mbele ya Rais Kikwete? Ilikuwa sadfa kwamba kwa wakati wa kikao hiki, Rais Karume alikuwa nje ya nchi, lakini hatujuwi angelisimamaje katika mjadala ule.

Lakini hebu, kwa manufaa ya mjadala huu, tuukubali upotoshaji huu wa dhana halisi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na tuburuzwe kwamba wale waliokutana walikuwa wawakilishi wa kweli wa pande mbili za Muungano na tujisahaulishe kuhusu dhima ya Rais wa Zanzibar. Basi hata katika hilo, tukipima uzito wa kiujuzi, kitaaluma na kisiasa baina ya wawakilishi hawa wa pande mbili, jibu litakuwa tena lile lile kwamba waliokutana sio.

‘Sio’ hii ya mara ya pili inamaanisha ukiwapima, kwa mfano, mawaziri wawili wanaoongoza wizara zinazofanana, mmoja kutoka kila upande wa Muungano, utaukuta mpishano mkubwa wa kimizania.

Mchukuwe, mathalan, Mansour Yussuf Himidi kutoka Zanzibar na Dokta Ibrahim Msabaha kutoka Muungano, ambao wote wanaongoza wizara zinazohusiana na nishati katika serikali zao. Dokta Msabaha ni daktari wa falsafa, mzoefu wa kitaifa na kimataifa katika fani yake. Niseme ni daktari kwa maana halisi ya daktari. Mansour ni mtoto mdogo sana mbele yake kwa kila hali____ kielimu, kiuzoefu na hata kisiasa. Wawili hawa kuwakutanisha ati wajadili nishati ni kuiburuzisha kwa makusudi Zanzibar. Hawafanani hawa.

Huo ni mfano mmoja tu, lakini kama utachukuwa Baraza zima la Mawaziri la Zanzibar na kulipambanisha na lile la Muungano, basi mwisho wa siku utakutana na ukweli mchungu mbele yako. Kwamba ukiacha wale mawaziri na manaibu waziri wachache waliotokea upande wa Zanzibar, Baraza la Mawaziri la Muungano (Bara?) lina ‘wazito’ watupu. Kwamba Baraza la Mawaziri la Zanzibar ni jepesi mno mbele yao na, kwa hiyo, wanaweza kuliburuza (na kwa hakika wanaliburuza hasa) wapendavyo. Kisha mwisho wa siku, Wazanzibari wakinung’unika, huwambia: “lakini haya ndiyo tuliyokubaliana na serikali yenu!”

Sasa nini cha kufanya, ikiwa kweli tunataka kuuimarisha Muungano wa kweli, na sio magube haya yaliyopo. Tuna sehemu mbili za kuanzia ambazo zinaingiliana na kutegemeana.

Pa kwanza ni kuitambua kwa kauli serikali ya Tanganyika. Nasema kwa kauli na sio kivitendo, maana kivitendo serikali hii ipo na inafanya kazi. Lakini kwa makusudi mazima ya kuuficha ukweli, inatakiwa iaminike kuwa hakuna kitu kama Tanganyika. Huo ni uongo ambao umedumu kwa miaka mingi sasa, lakini haujapata kutunufaisha.

Lazima mabadiliko ya makusudi yafanywe sasa katika maandishi yetu ili kuikiri Tanganyika, maana Tanganyika ipo na serikali yake ipo na inafanya kazi kwa jina tu la Muungano. Hilo lifanyike kwa upande wa Bara.

Kwa Zanzibar, ni kuwa na watu katika serikali ambao wana uwezo wa kitaaluma na uzoefu kwenye siasa za ndani na za nje, ili itakapohitajika kufanya majadiliano kuhusu Muungano, Zanzibar iwakilishwe hasa. Waliopo sasa ndio hivyo wapo tu, lakini hawana uwezo wala uthubutu wa kuitetea Zanzibar mbele ya wenzao wa Bara.

Nimesema mawili haya yanaingiliana na kutegemeana kwa kuwa, ili Zanzibar ipate watu wa aina hiyo, mathalan, basi ni lazima siasa za Muungano kuelekea Zanzibar zibadilike. Zibadilikeje? Ikiwa Tanganyika itajitokeza dhahiri shahiri, basi haitakuwa tena na la kupoteza kwa kuwepo Zanzibar kama Zanzibar. Maana sasa itakuwa haingalii Zanzibar kwa jicho la husuda la sasa kama mshindani wake, bali kama mshiriki wake.

Likitokezea hilo, basi Wazanzibari watakuwa na uwezo wa kuwapata wawakilishi halali na wenye uwezo wa kitaaluma na kisiasa kujadiliana na wenzao sio kuhusiana na Muungano huu tu, bali hata Shirikisho la Afrika Mashariki na, au, la Afrika, bila ya gubu lolote kutokea Bara. Haitakuwa tena lazima kwa Bara kusimika utawala inaoutaka Zanzibar kusudi ipate kuutumilia, maana ustawi wa Zanzibar utakuwa ni muhimu kwa uhusiano wa Tanganyika na Zanzibar, kwa upande mmoja, na uhusiano wa Muungano huu na nchi nyengine za Afrika Mashariki na Afrika nzima, kwa upande mwengine.

Hadi hapo mawili hayo yatakapofanyika, Zanzibar itaendelea kuburuzwa katika vikao hivi vya undumilakuwili, ambapo mawaziri wa Muungano watakuja wakiiwakilisha Tanganyika kwa uso mmoja na uso mwengine wakiwa mahakimu wa Muungano. Kila siku, Zanzibar itaendelea kuonekana kama inasaidiwa tu, na sio kupewa kilicho stahiki yake.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.