Wakati mazungumzo ya kuisaka suluhu ya kudumu Zanzibar yakiendelea baina ya timu za majadiliano kutoka vyama cha CCM na CUF, kuna mambo machache tunayopaswa kukumbushana kwa nia safi ya kujenga mustakbali mwema.Hili la nia safi ni mojawapo na, nasisitiza, lifahamike vyema kwa nia safi pia. Zanzibar ni yetu sote, na ni mahala pekee kwa sisi, tunaojitambua na kujitambulisha kuwa Wazanzibari, tunapoweza kupaita petu. Na hili neno petu lenyewe lina maana ya ndani zaidi kuliko linavyoonekana. Linahitaji nia safi kwelikweli kulifahamu na kulifahamisha. Waingereza huita home, kwa kulitafautisha na house. Wana msemo kwamba ‘a house is built of bricks and stone, but home is built by love alone’.

Ushereheshe kadiri uwezavyo msemo huu, ndivyo utakavyoyakuta mapenzi yetu yalivyo kwa mpendwa Mama yetu, Zanzibar. Kwetu hatuna mbadala kwaye. Pengine popote katika sayari hii ya Mungu Muumba, hatupahisi. Kupahisi, nakusudia, ni kupatia moyoni, kupavaa na kupaamini. Popote tuwapo, pasipokuwa Zanzibar, twajihisi kwamba tu wageni na watu wa kupita tu. Ni kwa Zanzibar tu, ndiko tujitambulishako na tujifakharishako. Namna hiyo ndivyo tumpendavyo Mama yetu!

Kwetu sisi, hakuna chochote tukipendeleacho zaidi ya kupaona petu pametulia, watu wetu wameshikana mikono kuijenga nchi yao na wenetu wanacheza wakikuwa pamoja kwa mapenzi na mshikamano wa kidugu uliomo ndani ya damu zao, maana sisi, Wazanzibari, wazazi wao, tu wamoja. Hakuna cha thamani zaidi ya hicho.

Basi mpenzi na rafiki yetu ni yule anayesaidia hicho kuwa; na adui na hasimu yetu ni yule anayekizuia kisiwe. Kumpapatikia mtu anayetusaidia kumtukuza Mama yetu, Zanzibar, kwetu ni jambo akhasi. Na vivyo kumpiga pande mtu anayemdhalilisha Mama yetu huyo, kwetu ni jambo la wajibu. Hakuna ubaya kuyatekeleza mawili hayo. Hatuyaoenei aibu.

Na hapa ndipo penye nukta nyengine. Maneno hayatoshi kuelezea matarajio waliyo nayo Wazanzibari, hivi sasa, kuhusiana na khatima ya nchi yao. Kama kuna zawadi yoyote ambayo Rais Jakaya Kikwete amewapatia watu hawa ni jitihada zake za kuanzisha mjadala wa kuelekea suluhu ya kudumu.

Licha ya ukweli kwamba Rais Kikwete alipaswa kuutekeleza wajibu huu kama kiongozi wa watu, lakini wenziwe waliopita kabla yake walikuwa pia viongozi wa watu na hawakusimamia jukumu lao la kiuongozi. Kwa hivyo, yeye anayeutekeleza anastahili sifa na shukrani maalum. Na sisi, Wazanzibari, si wachache wa shukrani. Hali tukitambua kuwa Rais Kikwete hatufanyii ihsani katika hili, lakini pia sisi si wizi wa fadhila. Tunamthamini kama kiongozi na rafiki wa kweli kwetu. Kwa jitihada hizi, anastahili heshima hiyo.

Maana twajuwa kwamba, ikiwa Zanzibar yetu itazidi kutopea kwenye ubaya zaidi ya hapa ilipo sasa, yeye atajeruhika heshima yake kama kiongozi wa nchi tu, lakini hatapoteza zaidi ya hapo. Kinyume chake, tutakaopoteza mengi ni sisi, Wazanzibari – heshima, mali, roho na, juu ya yote, mustakabli na jaala ya watoto wetu.

Kumbe Rais Kikwete angeliweza kujivalisha miwani ya kiza na kujitia pambani, akajifanya haoni wala haisikii Zanzibar ikizama shimoni, akamaliza kipindi chake cha uongozi, akastaafu na akaiacha nchi yetu ikiwa mbovu zaidi ya vile alivyoikuta. Kwani, kama hilo lingejiri, la ajabu hasa lingelikuwa lipi? Kwani sio siye tuliozowea kusalitiwa na kudharauliwa ndani ya Jamhuri hii ya Muungano?

Sio siye tuliozoea kuachwa katikati ya vilio na taharuki, mithali ya madude yasiyo thamani, huku viongozi wa juu tuwaliliao wakigeuza shingo zao au hata wakithubutu kutukejeli? Kwani sio siye tuonekwao watu-mwitu mbele ya watu-wastaarabu wenye hatamu za nchi hii? Pasingelikuwa na la ajabu, kwa hivyo, japo lawama na shutuma zisingekwisha mpaka siku ya ufufuo! Na kwani nani kasema kuwa lawama na shutuma zinazuia pishi za wakubwa kujaa?

Ndivyo alivyotufanya mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, na pishi yake haikupungua hata kibaba. Alitukuta wabovu, tumeoza, twanuka. Na ingawa tulikuwa raia wake, tulioishi kwenye vipande vya ardhi vinavyotambuliwa kwamba ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo yeye alikuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wake, yayumkini hakututambua hivyo. Na kama alitutambua, basi ndiyo hivyo hakutuhisi.

Nasema hakutuhisi kwa kuwa, kwenye ubovu na uoza wetu huo, Mkapa aliishi nasi kwa miaka kumi ya utawala wake, lakini hakushugulika na kuoza na kuharibika kwetu. Kubwa alilolifanya Rais huyu, alipotuona tunavunda, ilikuwa ni kufumba pua yake, na sio kuuondosha uovu na uoza uliokuwepo. Hata tuliponyayuwa mikono ya kutaka msaada, alijibu kwa kuongeza wanajeshi na silaha nzito nzito. Akaondoka akituwacha na ubovu wetu, husemi ila mateso yetu ndiyo iliyokuwa starehe yake na kudhalilika kwetu ndizo andasa zake. Tabaani, alikuwa anastaaladhi vikubwa mno nafsini mwake pindi akiarifiwa na watu wake namna tulivyoadhibika ndani ya mikono ya serikali yake.

Basi nasema, naye Rais Kikwete angeliweza, chembilecho wasanii wa Zanzibar, kwa raha zake, kuja kustaafu na kumalizia muda wake Chalinze, kama anavyoumalizia mwenzake sasa kwenye hekalu la Lushoto, huku akiiwacha Zanzibar na Wazanzibari kwenye mateso ya kuchukiza kwa kisingizio cha kulinda historia ya Mapinduzi na kudumisha Muungano. Lakini inavyoonekana, hadi sasa, Rais Kikwete ameamua kutokuyadharau mateso yetu. Ameamua kutokuufanya udhalilifu na dhiki zetu kuwa andasa zake. Ameamua kutukubali na kutuhisi kwamba sisi ni raia wake.

Ndipo kwa hilo, inapokuja nukta hii ya kumalizia: kwamba kuna haja ya kumsaidia Rais Kikwete ili naye atusaidie. Hilfen Sie hilfen, wasemavyo Wajerumani. Na miongoni mwa yale machache ambayo sisi wengine tunaweza kumsaidia Rais Kikwete ni kumkumbusha kwamba, uhalisi wa tatizo la Zanzibar ni zaidi ya mifano apigayo kila mara anapozungumzia huu anaouita mpasuko.
Nimemsikia mara mbili tatu akipiga mifano ya mpasuko wa Zanzibar kwa kutaja hatua zilizokuwa zinachukuliwa na wananchi kuwasusia wenzao ambao wana imani tafauti za kisiasa. Mara mbili za mwanzo ni katika mikutano yake aliyoifanya mwanzoni mwa mwaka jana Pemba na Unguja akiwashukuru wananchi wa visiwa hivyo kwa uchaguzi uliomuingiza yeye madarakani. Mara nyengine ni majuzi katika mazungumzo yake na wahariri wa vyombo vya habari.

Mifano anayopiga Rais Kikwete ni kama ule wa anayevuusha watu kwa kidau baina ya Mkoani na Kisiwapanza (Pemba) kutokuwapa huduma hiyo wale wanaowaona kuwa wapinzani wao kisiasa. Ama katibu mmoja wa CCM ambaye aliachiwa maiti ya mzazi wake na majirani zake, ambao kwa vyovyote vile watakuwa ni wana-CUF. Au watu kuacha kumfuata imamu katika sala kwa kuwa si mwenzao.

Sasa, inawezekana kabisa kwamba, hii ndiyo mifano pekee aijuwayo Rais Kikwete katika kuuelezea uzito wa mpasuko wa Zanzibar. Yayumkini ndiyo mifano apewayo na watu wake wa karibu waliomzunguka. Na ni mifano ambayo ni ya kweli. Lakini, ukweli wa uwepo wa mifano hii hautoshi kulielezea tatizo lenyewe lilivyo. Ukweli huu, badala yake, unaonesha kuna kitu chengine cha ziada na, kwa hivyo, chenye kutoa mifano mingi zaidi.

Nakusudia kusema kuwa, mpasuko wa kisiasa Zanzibar hauelezeki tu kwa kisa cha Katibu wa CCM kususiwa maiti ya mzazi wake na majirani zake, ambao ni wana-CUF, bali pia kinaelezeka kwa Katibu huyo kutangulia kwenda kutia fitina Polisi ili majirani zake hao waje wakamatwe, wapigwe, wateswe na kisha waswekwe ndani ambako wasingeliweza kutoka hadi kwa kutoa kiasi kikubwa cha pesa, vyenginevyo wabambikiziwe kesi za kubuni!

Mpasuko huu haulezeki tu kwa kisa cha mwenye dau Kisiwa Panza kukataa kumchukuwa Sheha wa Shehia yake, bali pia unaelezeka zaidi kwa Sheha huyo kuwakaribisha vijana wa makambi ya Janjaweed katika shehia yake ili kuja kuchoma moto majumba ya watoto na wajukuu wa mwenye kidau, na kuwaibia mali zao. Ndivyo ulivyokuwa mfano wa kijiji cha Kianga katika siku za uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mkoa wa Mjini Magharibi.

Mpasuko wa Zanzibar hauelezeki tu kwa familia moja kukataa kuiozesha mtoto wao katika familia nyengine, bali unaelezeka zaidi kwa kufahamu kuwa hiyo familia iliyokataliwa kuoa, iliwahi kuwawekea pingamizi ya kuandikishwa kuwa wapiga kura wanafamilia ambao sasa wanataka ukwe nao, kwa madai kwamba hawajatimiza muda wa kuishi katika eneo lao ilhali kwa miaka 20 mutawaliya wamekuwa wakiombana chumvi na moto mlango kwa mlango. Kichekesho ni kuwa, hata huyo mtoto anayeposwa, ambaye sasa ana miaka 21, alizaliwa katika nyumba hiyo hiyo na mama mkwe mtarajiwa ndiye aliyekuwa mkunga!

Mpasuko wa kisiasa wa Unguja na Pemba hauelezeki kwa mfano tu wa kukataa kununua na kuuza kwa mtu anayedhaniwa kuwa ni kijana wa Janjawidi na vikosi vya SMZ, bali unaelezeka zaidi kwa mifano ya hasara kubwa ya mali, damu na heshima iliyosababishwa na vijana hao kwa hao ambao leo wanakataa kununua na kuuza kwao. Ndiyo mifano ya duka la Sana Express kuchomwa moto pale Lumumba Unguja ambapo zaidi ya mali ya milioni 500 iliteketezwa. Ndiyo mifano ya kupigwa na kujeruhiwa vibaya kwa Mzee Hamad Salum na Muhunzi Juma wa Jang’ombe. Ndiyo mifano ya kubakwa kwa mke wa mwalimu wa skuli ya Dole. Ndiyo mifano ya watu wa Kinuni kukamatwa na hawa tuwaitao Polisi wetu wakitoka msikitini na kwenda kupigwa, na hadi kufikia upeo wa kunyweshwa mikojo yao. Ndiyo mifano ya watu hao kuvamiwa katika mistari ya kujiandikisha kuwa wapiga kura wakakatwa kwa mapanga vichwani na kufundwa kwa nondo.

Kwa maneno machache, na kwa dhamira nzuri, tumsaidie Rais Kikwete kwamba wale waliouliwa ndugu zao, wakabakiwa watoto na wake zao, wakawachiwa mayatima na vizuka, wakavunjiwa nyumba na kuchomewa moto mali zao, wakaswekwa ndani kwenye mateso na idhilali hizo zilizoepuka kabisa mipaka ya ubinaadamu, ndiyo hao ambao waliamua kuwagomea wale wote wanaoamini kwamba walishiriki kwa njia moja ama nyengine katika unyama huo waliotendewa.

Kibinaadamu watu hawa wangeliweza kulipiza visasi kwa yale waliyotendewa. Hiyo ingelichukiza, lakini bado ingefahamika. Lakini, kwa ubinaadamu huo huo, wakaamua kutokunyanyua mkono kuwarudi wadhalilishaji wao, bali kutokushirikiana nao tu. Hizi huitwa politics of non-cooperation, siasa za kupiga pande. Tanzania iliifanya hiyo, wakati wa Mwalimu Julius Nyerere, dhidi ya Afrika Kusini kupingana na utawala wa kibaguzi. Ni matawi miongoni mwa matawi ya siasa za kupigania haki kwa njia ya amani, nonviolence politics.

Kama hili si halali katika ujenzi wa Zanzibar mpya, ni sawa. Lakini kwamba lilitumika, kama Civilian Based Operations (CBO), harakati za kiraia, dhidi ya Military Based Operations (MBO), harakati za kijeshi, zilizokuwa zikifanywa na serikali, kwa hakika lilikuwa jambo ndilo.

Nihitimishe kwamba, inawezekana, kwa nia ile ile safi niliyoitaja mwanzoni, Rais Kikwete hataji mifano hii ya upande wa pili katika kuuelezea uzito wa mpasuko, kwa kuwa hajawahi kuelezwa hali halisi. Inawezekana pia, kwa nia hiyo hiyo safi, alikuwa ameshaelezwa, lakini kwa kuwajuwa CCM wenzake wa Zanzibar walivyo, hataki kuwatahayarisha kadamnasi. Yote mawili yanaeleweka. Husnu dhanna, tusemavyo Wazanzibari.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.