Wakati unaisoma makala hii, hivi leo, maofisa wa serikali ya Mauritania wanajitayarisha kuipokea meli iliyosheheni wale wanaoitwa ‘wahamiaji haramu’ kutoka nchi za Kaskazini na Kaskazini Magharibi ya Afrika ambao walikuwa wanakwenda kujaribu jaala yao Ulaya wakipitia visiwa vya Afrika Kaskazini vinavyotawaliwa na Hispania.

Ni bahati mbaya kwamba, huko Ulaya nako hawatakiwi (au kwa usahihi zaidi hawatakiwi hivyo walivyo). Kwa hivyo, wanarudishwa kwanza katika nchi ya Kiafrika ili wakachujwe na ikibidi kuchukuliwa, wawe wachache sana ambao watakuwa na faida ya wazi wazi na ya moja kwa moja kwa Ulaya. Na hii inaeleweka.

Makala hii, pamoja na ijayo, itazungumzia sababu za Waafrika kuhama kwao na kupendekeza baadhi ya njia za kufuatwa. Tuanze kwanza na sababu ya ndani ya bara letu, na tuanze pia kwa tabaka la hawa tuwaitao ‘wasomi’.

Katika A Man Of the People, Chinua Achebe anamnukuu Chief Nanga, mwanasiasa asiye na uelewa mkubwa wa mambo lakini aliyefanikiwa kupanda kisiasa kiujanjaujanja tu, akimuambia Odili, msomi aliyekuwa ndio kwanza ametoka chuo kikuu: “It doesn’t matter what you know, but whom you know!” Sio ukijuwacho, bali umjuwaye.

Hii ndiyo khulka ya kawaida kwa Afrika nzima. Baada ya kuwa nchi imeshatumia fedha na muda mwingi kumsomesha kijana wake, msomi huyu hurudi nyumbani kuja kukumbana na udhalilifu kama huu. Chote kile alichokisoma chuoni, huwa si mali kitu. “Hawezi kuishi maisha ya kitabuni katika uhalisia.”

Huu ni ukweli unaomtesa msomi huyu kiuchumi, kijamii na kisaikolojia. Hujikuta mgeni kwenye jamii yake mwenyewe aliyozaliwa. Kama mwanaadamu, angelitamani kuishi waishivyo watu, angalau kwa kupata mahitaji muhimu ya maisha. Kama mwanajamii, angelihitaji awe mshiriki katika shughuli za kijamii kwa kuwasaidia watu wake. Na kama msomi, angelihitaji kupata utambulisho wake kutoka jamii hiyo kwa stahiki yake. Angelitaka aheshimiwe, angalau kwa maana nyepesi tu.

Lakini anajikuta hana fursa yoyote ya kuutumia usomi wake kuyapata hayo, maana hapa sio nini anakijuwa bali ni nani ahli yake katika system, ndiye atakayeweza kumsaidia angalau apate kijisehemu cha kutarazaki, mkono uende kinywani. Anatakiwa asahau kabisa mchango wake kwa watu, asifikirie heshima yake, apuuze elimu yake. Tusi gani kwa msomi wetu! Ni tusi hili ambalo ni miongoni mwa sababu za kukimbilia Ughaibuni, ambako kuna uwezekano wa kuyapata anayoyakosa kwao.

Binafsi, hadi hivi karibuni tu, nilikuwa nimefungika na mawazo kuwa msomi anayeihama nchi yake na kwenda kufanya kazi kwengine huwa ni mpungufu wa uzalendo kwa kisingizio cha hali ngumu ya maisha kwao. Nilipingana na kisingizo hiki, maana niliona ni kukimbia tatizo ambako hakusaidii utatuzi wake. Kama ni shida zilizopo petu, hapa ndipo pao, kwa nini wasingelikaa tukashirikiana pamoja kupambana nazo? Kwa nini wasikae kusaidia kuleta mabadiliko?

Hesabu yangu ilikuwa ni kiwango cha faida wanachokizalishia nchi wanazofanyia kazi. Ingelikuwa wapi leo Afrika, ikiwa faida hiyo ingelikuwa inazalishiwa hapa? Kwa mfano, vijana wangapi wa Kizungu kwa mwaka humaliza digrii zao kwa kusomeshwa na wasomi wetu? Au miradi mingapi huiandika kwa mwezi na kuzalisha mamilioni ya dollar na euro katika kutekelezwa kwake?

Sasa nina shaka na hukumu niliyokuwa nayo kwao. Na ni baada ya kuongoea na baadhi yao, nikiwa na msimamo kwamba wao wanakosea na kwamba nami nina wajibu wa kuwakosoa kama watu wangu. Mmoja ‘aliniondosha njiani’ tu, “Nitarudi.” Lakini mwengine hakuniwachia hivi hivi tu: “Ungeliniuliza kwa nini nimeondoka kwetu na sio kwa nini sirudi kwetu, labda lingelikuwa suali muwafaka zaidi!”

Akanitanabahisha kwamba, si kweli kuwa watu wa aina yake wanaondoka kwao kuzikimbia shida zilizopo, maana ni shida hizo ndizo zilizowalea na kuwasomeha hadi wakafika walipofika. Na pia ni shida hizo walizoapa kupambana nazo katika maisha yao yote ya masomo ili kuipa maana elimu yao katika maisha ya watu wao. Lakini linalowakimbiza ni kuwa ‘hawatakiwi’. Wanakanwa na nchi zao wenyewe, nchi za uzao wao. Na katika wakati huu ambao sisi ndugu zao tunawakana, kuna wenzetu wanaowatafuta kwa udi na uvumba.

Vipi msomi wetu anakanwa katika nchi ya uzao wake? Kwa kuwa hapewi kazi ya mamilioni ya shilingi? Kwa kuwa hapewi gari la kifakhari, wala nyumba nzuri kama wapewavyo wanasiasa? Hapana, hayo si makubwa kiasi ya kwamba akiyakosa anahiyari kupasamehe pao, lakini la muhimu zaidi kwake ni kupewa utambulisho wake na kutambuliwa kama msomi.

Kuna mifano mingi ya wasomi walioamua kurudi kwao, baada ya masomo, ili waje wafanye kazi kwa ajili ya mataifa yao, lakini walipofika wakakumbana na kejeli za wanasiasa visirani, ambao kwao wao msomi ndiye adui nambari moja.
Afrika kuna ugomvi usiokwisha baina ya wanasiasa na wasomi, maana wawili hawa kila siku huyaona mambo kutokea vipembe tafauti. Wakati mmoja huyaona kutokea kipembe cha kisiasa na kutaka kila kitu kifanywe kwa kufuata muono huo, mwengine huyaona kutokea kipembe cha kitaaluma, na haja yake ni kuyafanya mambo kupitia muono huo.

Wakati mwanasiasa anataka mtu amuendeshe, msomi anagoma kuendesheka na, hivyo, anakuwa hatari kwa nguvu za mwanasiasa. Siku zote watu hawa ni Lila na Fila. Henry Peter aliwahi kusema: Education makes people easy to lead, but difficult to drive; easy to govern, but difficult to enslave. Elimu huwafanya watu rahisi kuongozeka, lakini wagumu kuendesheka; rahisi kutawalika, lakini wagumu kuwatia utumwani!

Ubaya wa mambo kwa msomi, ni kuwa yeye huwa hana nguvu za kufanya maamuzi ambayo yatafuatwa hapo hapo. Mwanasiasa anazo nguvu hizo. Akisema mashine ya maji ifunguliwe Lumumba ikafungwe Bwejuu ili Mhishimiwa Sana akapate kufunguwa mradi wa maendeleo huko, jambo hilo litafanyika siku hiyo hiyo hata kama ni kinyume na ushauri na matakwa ya kitaalamu.

Msomi akiinuka kulisemea hilo, huyo anaanza kuonekana ‘mpinga maendeleo’, na mchochezi. Na hayaishii hapo tu, huenda siku kumi zijazo akakuta kibarua kimeshaota majani. Kisa? Kukidhi mahitaji ya kitaaluma badala ya mahitaji ya kisiasa!

Akiepukana na hilo, msomi wetu anakumbana na jengine kutoka system. Kwa mfano, mtu anarudi nyumbani baada ya kumaliza kuchukuwa mafunzo ya Uhandisi huko atokeako, lakini akifika anakabidhiwa chaki akasomeshe Kiingereza kwa wanafumzi wa Darasa la Saba. Mwengine aliyesomea masuala ya kilimo, anapangiwa akawe fundi wa vinu vya maji. Wapi na wapi?

Lakini kwa kuwa wanasiasa wetu wana ugomvi wa kudumu na wasomi hawa, basi si ajabu kuwa wanawafanyia haya kusudi washindwe na wapate la kuwadharaulia. Wawaite maprofesa uchwara, madaktari feki na majina mengine kama hayo ya tashtiti. Hiyo ndiyo mbeleko Afrika inayombebea msomi wake. Atadumuje?

Hayo ya msomi kupangiwa kazi kinyume kabisa na taaluma yake huenda yakawa madogo, lakini hebu fikiria mtu ambaye amepoteza miaka yake kumi kuchukuwa fani ya udaktari huko nje, anakuja hapa na kuamriwa kupiga deki hospitali, eti ni kumkomoa na usomi wake! Lipi tumfikirie atalifanya msomi huyu?
Lakini adui wa msomi wetu si mwanasiasa tu, hata jamii yenyewe anayokuja kuifayia kazi na kuishi nayo. Wengi wetu huwa tunadhani kupata fursa ya masomo ya juu kumempa fursa nzuri ya kuyatengeneza maisha na hivyo kumpa pia wajibu wa kutusaidia kwa hali na mali.

Kwetu, kuwa na digrii, kwa mfano, kunamaanisha kukunja mapesa na kuja nayo nyumbani. Anaporudi mikono mitupu, msomi huyu huonekana kayasaliti matarajio ya watu wake. Na akitaka ayatimize mahitaji hayo, basi lazima afanye kazi kuwatimizia haja zao. Na kazi ipi atakayoifanya hapa petu kuyakidhi mahitaji ya familia zetu kubwa?

Kwa hali hiyo, msomi wetu huwa amesukumwa ukutani, ambapo hana jinsi ya kung’amuka ila ajitolee muhanga kwa kufanya moja kati ya matatu haya: ama akae kupambana na mfumo kwa kucha na meno, au abadilike kwa mujibu wa mahitaji ya mfumo wenyewe au aikimbie nchi yake ya uzawa

Kila moja kati ya matatu haya yana gharama kubwa sana, na lolote atakalolifanya, hujikuta anajilaumu kwa kutolifanya jengine. Kwa mfano, kuamua kubakia na kuukabili mfumo uliopo ni kujikubalisha kukosa na kupoteza kila kitu. Ni kukubali kujiundia maadui wengi na wenye nguvu kuliko yeye kutoka tabaka la watawala. Anaweza kukosa hata mlo wa siku moja yeye na familia yake na mwisho wa hadithi akafa dhalili na madhulumu. Mifano ya wasomi wa aina hiyo ipo mingi sana.

Chaguo la kujibadilisha na kwenda sambamba na mahitaji ya mfumo uliopo ndilo linalofuatwa na baadhi ya wasomi tulionao nyumbani. Lakini chaguo hili huwa linamsuta msomi anayeheshimu maadili ya taaluma yake. Mfumo wetu, kwa hakika, ni wa kifisadi sana na kuwa fisadi ni kitu alichojifunza na kuamini kuwa ni kiovu. Sasa, kuishi kwa mujibu wa matakwa ya mfumo ni kukubali kuwa fisadi.

Tunao hapa wasomi na digrii zao, lakini ndio hao wala rushwa wakubwa na ambao huhongwa kuitikia Ndio Mzee ili waidhinishe mambo maovu kufanyiwa watu wao kwa jina la taaluma zao na, au, vyeo vyao. Ndio hao waliopitisha miradi ya rada, ndege ya raisi, mikataba ya IPTL na mengineyo lukuki nzima.

Hawa si wasafi na wala hawawezi kusafika madhali wamesimama na wanaishi na wachafu. Hawa ni wasaliti wa taaluma zao, wasaliti wa uelewa wao wenyewe. Wanaweza wasife madhulumu, lakini hawawezi kuepuka kufa madhalimu.

Na, mwisho, yule asiyeweza kuyastahamilia hayo yote hulazimika kupahama pao na kwenda ugenini. Huko ataweza kufanya kazi na kupata visenti vya kuwasaidia watu wake. Huko ataweza kuilinda na kuidumisha heshima yake kitaaluma. Huko kutamuepusha kufa dhalili au kufa dhalimu.

Lakini huko kutamnyima kwao, kunakiapoteza kizazi chake kinachokuja kuwa kigeni kwao pia. Atazaa watoto wasio utambulisho___ Waafrika sio wala Wazungu sio. Ndiyo akina hao tuwaitao Amefricans, Eurofricans au Asifricans. Watandawazi, labda tuwaite hivyo kwa Kiswahili. Na hilo ni poteo kubwa kwa msomi wa kipetu, ambaye kujitowa kwake muhanga kwa staili hii kunamkosesha, yeye na wanawe, titi la mama.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.