Kwa mara nyengine tena, katika hisabu za uhai wangu, Mapinduzi ya 1964 yanaadhimishwa huku Zanzibar ikiwa kwenye lindi la umasikini wa mali na hali. Haidhuru maneno matamu na takwimu kubwa kubwa za kukuwa kwa uchumi ambazo watawala wanataka tuziamini, lakini mifano hai inaonesha kwamba Zanzibar inarudi kinyumenyume.

Nipige mfano mmoja mdogo wa taashira. Mwishoni mwa mwezi Septemba 2006 niliondoka Zanzibar kuja hapa Dar es Salaam kwa masomo, nikiacha mnara wa jengo la Beit-el-Ajab umewekewa miti kwa ajili ya matengenezo. Ni juzi tu, baada ya miezi mitatu na kitu ndiyo nimerudi nyumbani kwa mapumziko. Unajua kitu cha mwanzo kukishuhudia ni nini? Ile miti nimeikuta pale pale na jengo liko vile vile – ishara kwamba Zanzibar yangu ilikuwa imekwama kwa miezi yote hiyo.

Hii ni ishara tu, si kila kitu kuhusu Zanzibar. Lakini huo ndio muakisiko wa hali ilivyo nyumbani. Kunarudi nyuma. Hali ni tafauti na Tanganyika ambako, nionavyo, kunakwenda mbele. Ishara nyingi zinasema hivyo – tangu majengo hadi pirika za maisha. Si halali kusema kwamba hali ni nzuri sana (juzi imetangazwa kuwa ya 47 kati ya nchi 50 masikini duniani), lakini ikiwa wawili hawa ni wagonjwa, basi Zanzibar yuko kwenye sakaratil-mauti na Tanganyika anaweza angalau kujikongoja. Hivyo ndivyo miaka 43 ya Mapinduzi ilivyomfanya Mama yangu, Zanzibar – mgonjwa zaidi kuliko ilivyomkuta.

Na huo ndio uhuru wetu, Wazanzibari, uliotokana na Mapinduzi hayo. Uhuru wa kuwa na skuli na vyuo visivyo elimu, hospitali zisizo matibabu, mifereji isiyo maji, maduka ya vyakula na masoko ya vitoweo lakini wengi wanashinda na njaa. Kila Mzanzibari, kama mwanaadamu mwengine, hutamani kusoma asiwe wajinga, atibiwe asife maradhi, ale asilale na njaa na, kindharia, watawala wanamwambia ana ‘uhuru’ wa hayo, bali kiuhalisia ‘hayuko huru’ kuyapata!
Kuwa huru ni kuwa na nyenzo na uwezo; na ndicho kilichopiganiwa na wazee wetu walipopambana kumkomboa mkwezi na mkulima wa Zanzibar. Ikiwa walimwaga damu yao kuikomboa nchi, basi ilikuwa ni kwa kumvua Mzanzibari minyororoni mwa dhiki na dhuluma kwa kubadilisha staili ya utawala na sio kubadilisha sura za watawala tu.
Waliofanya Mapinduzi, inaelekea, walichoshwa kuona watu wachache tu, waliokuwa na mahusiano na utawala, ndio pekee waliokuwa na fursa ya kuufaidi utajiri wa nchi, huku wengi wakibakia kuteseka ndani ya nchi yao. Ni akina akrabiina tu, tunavyoambiwa, waliokuwa wananufaika na kila jambo zuri – matibabu, elimu, makaazi na maisha ya kiwango cha juu – wakati makabwela wakiteseka kwa njaa, maradhi na ujinga.

Basi wazee wakadai uhuru. Walipoupata, wakaona haujatosha, wakafanya mapinduzi ‘kuwakomboa’ zaidi Wazanzibari wawe huru, kwa maana ya kupata haki zao, kuwa nazo na kuzimiliki, maana hizo ndizo nyenzo za kuyastawisha maisha. Ikiwa kuna uhalali wowote wa mapinduzi yale, basi ni huo.

Lakini hata baada miaka hii 43 ya mapinduzi hayo, tunajuwa kuwa tumesalitiwa. Yule mkwezi na mkulima aliyelengwa kukombolewa, hajakomboka. Bado anadhalilika vile vile. Ule uhuru wa kweli uliokusudiwa awe nao Mzanzibari, haujapatikana.

Kilichopatikana, badala yake, ni mabadiliko ya sura za watawala na mstari mwekundu wa mfarakano. Hilo ndilo linalotufanya tuamini kuwa bado Zanzibar, kama nchi, haijawa huru__ haijawa na uwezo na nyenzo za kupata, kuwa nacho na kukimiliki. Uhuru wa kweli uliopiganiwa na wazee wetu sio tulionao. Mapinduzi tunayoyasherehekea leo, hayabebi tena ile azma yake yaliyolengwa.

Yale yale yaliyotakiwa yaondoke miaka 43 nyuma, ndiyo yaliyopo sasa, tena kutokana na mabadiliko ya wakati na ongezeko la mahitaji, yapo kwa kiwango cha kutisha. Na ikiwa hivyo ndivyo, ni msamiati gani wa kuhalalisha kujiita kwetu huru?

Nitoe mifano. Wakati Zanzibar inapata uhuru wake mwaka 1963, hamani ya dola ya Kimarekani ikiwa ni shilingi saba, ilikuwa inaingiza kiasi ya shilingi milioni mbili kwa mwaka kwa kusafirisha samaki wakavu Tanganyika. Kwa sasa, hiyo ingelikuwa ni zaidi ya shilingi bilioni tatu.

Mbali ya kuhakikisha kwake kuwepo kwa nafasi za kazi zisizopunguwa 500 kwa mradi huo tu, pato hili pia lilihakikisha kujitanua kwa Zanzibar kiuchumi. Miaka 43 baada ya Mapinduzi, sio tu kwamba Zanzibar haina tena inachozalisha kuiuzia Tanganyika, bali yenyewe inategemea yazalishwayo huku. Huko hakuitwi kwenda mbele. Ni kurudi nyuma. Na huo sio uhuru uliopiganiwa.

Hadi Mapinduzi yanafanyika, nchi pekee za Kiafrika zilizolingana na Zanzibar kwa pato kubwa la taifa zilikuwa Ghana na Afrika Kusini. Wakati huo, Zanzibar ilikuwa inatowa misaada ya chakula na pesa kwa nchi nyingine ulimwenguni, kama vile Yemen. Leo Zanzibar ya miaka 43 ya Mapinduzi ni sehemu fukara kabisa duniani. Wazee wetu hawakupinduwa ili tuje tuwe masikini!

Zanzibar haikuwa na uchache wa wataalamu. Ni aibu kuwa miaka 43 baada ya Mapinduzi, bado tunaagizia wataalamu wa sheria, kwa mfano, kutoka nje ya nchi, ilhali hadi Mapinduzi hayo, ni Sudan tu katika Kusini nzima ya Jangwa la Sahara iliyokaribiana nasi kwa wataalamu wa kutosha, na wa ziada, wa kizalendo. Ikiwa tumerudi nyuma kiasi chote hiki, ni fedheha kujiita huru.

Katika huduma za kijamii, hali ni mbovu hivyo hivyo. Miongoni mwa maazimio ya Mapinduzi ni kuwapatia wakulima na wakwezi makazi bora, huduma nzuri kwa wazee wasiojiweza, elimu bora zaidi, chakula cha kutosha na matibabu yanayomstahikia mwanaadamu. Huko nyuma, tunaambiwa, watu wengi walishindwa kuyapata hayo kwa kuwa, hata kama walikuwa na uhuru nayo, hawakuwa na uwezo wa kuyagharamikia.

Matokeo yake, watoto wengi wa kimaskini wakaishia kuwa wajinga kwa kutokumudu kwenda skuli. Watu wengi wakawa wanalala na njaa, au kwa ‘kugongeana mwiko’, katika vibanda vyao vya makuti, na hata wengine wakawa wanakufa kwa kukosa matibabu. Wachache waliokaribiana na watawala au waliojiweza kifedha, ndio walioyafaidi maisha.

Leo, miaka 43 baada ya Mapinduzi, kuna yapi Zanzibar? Si mfano wa yale yaliyotokea kabla ya miaka ya ’60? Wale wale watoto wa makabwela, waliozungukwa na skuli, wanakosa elimu bora kwa kuwa hawana uwezo wa kulipia. Skuli za serikali zipo, lakini zimefuiya na mfumo mzima wa elimu umeporomoka. Kupata elimu nzuri kunalazimu kulipia masomo ya ziada au kusoma katika skuli za binafsi, ndani na, au, nje ya Zanzibar. Na kwa kuwa hayo yote yanamaanisha pesa, na pesa ni adimu kwa wakulima na wakwezi, basi elimu bora haipatikani kwao!

Badala yake ni watoto wa wakubwa na wenye pesa zao, ndio wanaoipata hiyo elimu bora. Wengi husomeshwa nje ya nchi na wachache wanaosoma Zanzibar ni katika zile zinazoitwa international schools, ambako pesa za walipa kodi huyeyushwa kila mwezi.

Mwishowe, kwa kuwa kuipata kazi kunategemea kisomo mtu alichonacho, basi watakaokuja kupata kazi (ikiwa zipo) watakuwa ni hao hao waliopata elimu bora. Mtoto wa mkulima na mkwezi atarudi kule kule kwenye pingu na jembe la mzazi wake.

Wakati huu wa kusherehekea miaka hii 43 ya Mapinduzi, pita mitaani kwa makabwela ushuhudie hali ilivyo. Pita Miembeni, Mikunguni, Jang’ombe, na Sogea, uone maandamano ya madumu ya maji. Pita vijijini kwetu ushuhudie hali ya watu walio ‘huru’. Pita Mtende, Kojani, Kiuyu na Marumbi usikie harufu ya njaa ikikunukia puani mwako.

Lakini kejeli ilioje, huko Mazizini na mwenginemo muchache, watu wanakula na kumwaga katika madebe ya taka. Huko kunasherehekewa hasa miaka 43 ya Mapinduzi na uhuru wa mkulima na mkwezi. Huko ndiko uhuru na ukombozi ulikofika!

Hebu nenda jumba la wazee Sebleni, pale karibu na uwanja wa Amani, ukamuone huyo mkulima na mkwezi ‘alivyokombolewa’. Mzee wa miaka 70 amechakaa na kuchafuka kama lilivyo jengo lenyewe, anajikokota kwenda kutafuta makozi ya kupikia hadi karibu ya Mwera. Serikali iliyomvundika mule, imeshindwa kumtunza kikweli na, badala yake, anadhalilika. Miaka 43 iliyopita, huyu alikuwa ni mtafutaji uhuru, alikuwa mpiganiaji ukombozi; na sasa ni dhambi kumuita yeye kuwa ni raia huru!

Hebu tembelea hospitali zetu, zile tulizoahidiwa huduma bora na bure. Wakwezi na wakulima hawapatiwi muda wa kuangaliwa sawasawa na madaktari kwa kuwa hawana pesa za kuhonga. Na hata wakishaangaliwa kwa hayo macho matupu, hakuna dawa. Wao, wakulima na wakwezi, wanatakiwa kununuwa dawa za zaidi ya elfu tano, pato lao la mwezi mzima. Huo ndio uhuru walioupigania?

Wakati huo huo, huku wao wakiteseka kwa maradhi bila ya dawa, fedha nyingi zinatumika kuwatibu nje wale walio na fursa katika utawala, hata kama maradhi hayo yangeliweza kutibiwa hapa hapa kwa pesa kidogo au bure kabisa. Watakatifu hawa wanajuwa namna ya kuufaidi uhuru na ‘wako huru’ kufanya hivyo. Wana nguvu, uwezo na nyenzo za kuutumia uhuru wao. Wao ndio ‘waliokombolewa’ na Mapinduzi ya 1964.

Marehemu Jaramogi Oginga Odinga wa Kenya aliwahi kuandika kitabu na kukiita Not yet Uhuru, akimaanisha kuwa hata baada ya mkoloni wa Kiengereza kuondoka, bado Kenya haikuwa huru, maana waliochukuwa madaraka baada yake, walijigeuza wakoloni weusi na wakaila nchi yao wenyewe. Walikuwa wanaitawala nchi kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha ya umma, ufisadi na utumizi mbaya wa madaraka. Walikuwa wanaifakamia keki ya uhuru kwa matonge.

Nachelea kusema kwamba hali i vivyo kwa Zanzibar. Waliochukuwa madaraka baada ya Mapinduzi wameigeuza nchi hii kuwa shamba lao, mali yao na vizazi vyao. Wao peke yao ndiyo wameojihalalishia kuila keki ya Mapinduzi kwa staili wanayoitaka wenyewe. Wao peke yao ndio wanaopata makazi mazuri na ya kuridhisha, maji salama na safi, matibabu bure na bora, elimu ya kiwango cha juu na ya manufaa, chakula kizuri na cha kutosha, na mavazi ya kuvaa na kujipamba. Sisi, watoto wa wakwezi na wakulima, tungali kule kule walikokuwa wazazi wetu miaka 43 iliyopita. Kwetu, ni not yet uhuru!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.