Kihoro kilichomuingia Mwalimu Nyerere kwa kuangushwa na chaguo lake, naamini, kilisaidia kuzisogeza siku zake haraka kuelekea kuzimu. Si mchezo mtu wa heshima kama yeye kunyanyuka katika umri ule kuzunguka nchi nzima na kumnadi mtu wake, kisha mtu huyo akaja kumwangusha mwangusho wa kioo – ulio vigumu kuungika tena. Mwalimu Nyerere hakuunga tena tangu Mkapa alipoanza kuyatekeleza madaraka yake.
Rais Benjamin Mkapa aliyeiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka 1995 hadi 2005.
Rais Benjamin Mkapa aliyeiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka 1995 hadi 2005.

Nianze kwa kipande cha ushairi cha rafiki yangu, There Stands a Looser:

I may be the one when I loose
But you remain the same always
Neither you nor I
Can deny the consequences
Nor can we tune otherwise
But as these counted minutes
Finish our day
Our children shall rise and say:
“Look, hey!
There stands a looser!”
And believe you me
That looser won’t be I

Ndiyo, there stands a looser. Tahriri ya wiki iliyopita ya gazeti la Fahamu Mwananchi ilikuwa inazungumzia kauli ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, kwamba, pamoja na kasoro ndogo ndogo za kibinaadamu, alijitahidi kuiongoza nchi kwa amani na upendo na kwamba anapaswa kumshukuru Mungu kwa kumlinda.

Makala hii haiendi mbali na tahriri hiyo. Hoja ni ile ile: Mkapa hakuiongoza vyema nchi hii. Na ufuatao ni uthibitisho kwamba, kama kuna chochote chema ambacho Mkapa aliifanyia nchi hii, basi ni vile kuondoka kwake madarakani muda wake ulipofika kwa kutokuwa na ndoto ya kubadilisha katiba na kuendelea kubakia kama wafanyavyo wenzake.

Kwa mara ya kwanza, Mkapa aliyeingia madarakani kwa mgongo wa Marehemu Mwalimu Julius Nyerere aliyedhani kwamba mwanafunzi wake huyo ataendeleza kile alichokiamini yeye (Mwalimu), alikuwa na staili ya aina yake ya uongozi (utawala?). Kwa mfano, zile siku za unyemi wa fungate yake madarakani, alikuwa akihubiri mno kaulimbiu ya “Ukweli na Uwazi”.

Alikuwa akitaka nchi imuamini kwamba yeye ndiye hasa yule Mr. Clean wa Mwalimu Nyerere kwa kuwa mkali mno dhidi ya rushwa. Basi akianza fungate hiyo kwa kutaja mali zake alizokuwa nazo, kisha akawashawishi mawaziri wake, akina Waziri Mkuu Fredrick Sumaye, wafanye vivyo.

Hakuishia hapo. Akawataka wananchi wamuamini kwamba yeye ni mpambanaji kwelikweli dhidi ya ufisadi na rushwa kwa hivyo akawaomba wamtajie majina ya watu wanaowajuwa kuwa ni wala rushwa. Akaunda pia Tume ya Jaji Warioba kulihakiki suala lenyewe lote. Si unajuwa kuwa serikali iliyomtangulia ya Mzee Ali Hassan Mwinyi (Babu Ruksa) ilikuwa ‘imeminyiwa’ na wafadhili kwa madai ya kuwa kwake ovyo mbele ya ubadhirifu wa mali ya umma na ufisadi ulioota mizizi? Sasa otea nini kilitokea baada ya hashuo lote hilo?

Kwanza, baada ya kupelekewa majina ya ‘wala rushwa’ katika serikali yake, aling’aka kama mbogo kwamba watu wana wivu wa kike na, badala ya kuangalia maendeleo yao, wanaendekeza choyo cha kuona kila mwenye mali basi ameipata kwa rushwa.

Akasema kwamba watu wasimpelekee majina tu, bali wampelekee ushahidi, hali anajuwa fika kwamba katika kutoa na kupokea rushwa kila jitihada huchukuliwa kuhakikisha kuwa hakuna nyayo za ushahidi inayoachwa. Kama ilivyo dini, rushwa ni imani. Ama uamini kama ipo au la.

Pili, ile taarifa ya Tume ya Jaji Warioba ikaishia kapuni (na kwa taarifa ni kwamba hii si tume pekee ya Mkapa ambayo ilimalizikia kiaina tu). Ikachapwa, bila ya shaka, katika magazeti, lakini mambo yakaenda taratibu mno. Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKURU) aliyoiunda ikawa ni showcase nyengine. Lilikuwa jibwa kubwa la kutisha lakini lilikuwa kibogoyo kisicho meno ya kutosha. Lawama ni kwamba, limepewa koti kubwa kuliko umbile lake. Huyo ndiye Mkapa kwenye rushwa.

Kihoro kilichomuingia Mwalimu Nyerere kwa kuangushwa na chaguo lake, naamini, kilisaidia kuzisogeza siku zake haraka kuelekea kuzimu. Si mchezo mtu wa heshima kama yeye kunyanyuka katika umri ule kuzunguka nchi nzima na kumnadi mtu wake, kisha mtu huyo akaja kumwangusha mwangusho wa kioo – ulio vigumu kuungika tena. Mwalimu Nyerere hakuunga tena tangu Mkapa alipoanza kuyatekeleza madaraka yake.

Kisha kuna mkasa kama ule wa akina Jenerali Twaha Ulimwengu ambaye, licha ya kuwa mpiga debe wake mkubwa katika siku za kampeni, alipoanza kumuona anakwenda njia siyo naye kumsema kwa hilo, mara akatangazwa si raia. Nisisahau kwamba sakata la uraia wa Mzee wangu, Ali Nabwa, lilianza katika siku za mwisho mwisho za utawala wa Mkapa na kwa hakika alilijua vyema, lakini akaondoka na kuliacha kama lilivyo.

Kuna mauaji ya Mwembechai ya mwaka 1997. Shaka kwamba alikuwa ‘mdini’ wa kutupwa zilianza kujengeka hapa. Maana pamoja na serikali yake kufanya ilivyowafanyia waumini wa Kiislam ndani ya msikiti, bado alikataa kabisa kuunda tume ya uchunguzi wa sakata lile. Na hata alipotokea msomi mmoja, Dk. Hamza Njozi, kuandika kile hasa kilichotokea katika kitabu chake cha The Mwembechai Killings, serikali yake ilikipiga marufuku kitabu hicho.

Kuna kasheshe la Bulyanhulu ambako madai ya wazi ni kuwapo kwa kaburi la pamoja la watu waliofukiwa mgodini. Sio tu kwamba serikali yake ililikanusha lakini pia ilizuia vyanzo vyovyote vya habari kutoa taarifa hizo kwa ulimwengu. Huyo ndiye Mkapa katika haki za watu.

Kisha kuna hili suala kubwa kabisa la mauaji ya Januari 2001, Zanzibar, ambalo mwenyewe aliwahi kusema eti liliwahi kumkosesha usingizi na karibuni na mwisho wa utawala wake, alipokuwa ziarani Marekani, akasema kwamba linamsononesha katika siku anapomalizia uongozi wa Tanzania.

Mimi, hata katika siku za kuwapo kwake madarakani, niliwahi kutaka tumuite Mkapacratic, msamiati niliotaka umtofautishe na ule wa democratic. Bado ninaamini hivyo hivyo hadi sasa. Kwamba mfumo wake wa utawala ulikuwa ni mkapakrasia na sio wa demokrasia.

Sababu yangu ni kwamba, huyu alikuwa akiamini sana juu ya nguvu ya vyombo vya dola katika utawala na sio nguvu ya wananchi. Mdomoni, alikuwa akisema kwamba watu ndio wenye nguvu, katika vitendo alikuwa akionesha kuwa yeye na vyombo vyake vya dola ndio waliokuwa Alfa na Omega wa maamuzi na madaraka.

Ni shakhsia hii ya ukapakrasia ndiyo iliyozaa mauaji yale ya 2001. Ndiyo iliyowafanya dada zetu wabakwe na ndugu zetu waikimbie nchi yao ya uzawa. Mkapa hakuwa aina ya Raisi anayekubali changamoto katika utawala wake. Basi ni hivyo tu.

Ndio maana, licha ya kuwa mbele ya watu wake aliowapenda na kuwahusudu, mataifa ya magharibi, alikuwa akitoa maneno ya kistaarabu na kidemokrasia, alipowageukia wananchi wake alikuwa akitoa ujuba wa kidikteta. Sote tunakumbuka kauli zake za kuapa kutumia nguvu ya dola kuzima nguvu ya umma ikiwa baada ya uchaguzi kuna watu watakaoamua kuandamana kupinga matokeo yatakayotangazwa na tume zake za uchaguzi.

Alikuwa anaonesha msimamo wake kwa Wazanzibari ambao ndio waliokuwa wamefikia maamuzi hayo. Na akautekeleza msimamo huo kwa kuleta Zanzibar wanajeshi na silaha nzito nzito ambao hawakuondoka mitaani hadi lile lengo alilolikusudia limetimizwa. Na ikiwa hivi ndio kuongoza nchi kwa amani na upendo, nahofia kama angelioongoza kwa vurugu na chuki ingelikuwa vipi?

Alimradi mifano ya Mkapa kutuendesha ovyo ni mingi sana tu. Na yote inamuharamishia kustaafu akiamini kwamba alikuwa mtawala mzuri, maana ukweli ni kwamba hakuwa. Hakuwa na uzuri wa kusifiwa, hata kama, inayumkinika sana, wale watu wake aliowapenda na wao kumpenda sana (watawala wa Magharibi) walijitahidi kumjengea sifa hiyo.

Ukweli ni kwamba, mataifa hayo ambayo kitu pekee yanachokijali kwetu ni maslahi yao ya kiuchumi, yalikuwa yamepata kutoka kwa Mkapa kiongozi wanayeweza kumtumilia kwa yao. Ikiwa ‘aliyagawia’ makampuni ya nchi zao eka kwa eka za ardhi yetu, wachimbe madini na wafanye watakavyo, hapakuwa na shida yoyote ikiwa wao watamlipa Mkapa huyo kwa kumsifu. Kwa kumfanya chibui chao.

Kwa mfano, kuna suala la ununuzi wa rada na ndege ya raisi. Hivi sasa polisi ya Uingereza inachunguza kashfa ya ununuzi wa rada hiyo kwa kuwa tangu mwanzo ilishaonekana kwamba kulikuwa na harufu kali ya rushwa.

La ndege ndilo lilitutukanisha nchi nzima. Waziri wake wa Fedha, Basil Mramba, akatwambia ingelikuwa sawa ikiwa hata kama sisi raia tungelikula udongo lakini ndege ya raisi ilikuwa lazima inunuliwe. Na ni kweli, nchi hii inayohisabiwa kuwa miongoni ya zile za mwisho kwa umasikini, ikanunua ndege ya kupanda raisi wake akienda kuomba misaada kwa wale ambao wenyewe hupanda ndege za kawaida kuja kwetu.

Kuna namna alivyomkingia kifua Waziri wake Mkuu, Fredrick Sumaye, ambaye kila kidole cha tuhuma kilikuwa kinamuotesha yeye kwa namna alivyokuwa na miradi ya ajabu ajabu. Akatutukana sote kwamba tuna wivu wa kijinga. Kwamba si kila kiongozi aliyepata mali (hata kwa njia za ajabu?) kwamba amekula rushwa au ameiibia serikali.

Kumbe ilikuwa anajenga kabisa ukuta wa kinga, maana hata naye mwenyewe, kama nilivyosema, aliondoka bila ya kutangaza mali yake aliyoichuma akiwa madarakani. Alishatwambia kabisa kwamba haimaanishi wizi wala rushwa kuwa na mali zaidi ya mshahara tunaokulipa sisi tuliokuajiri.

Basi kwa haya, na mengine mfano wake, ndipo wengine tunaona kwamba Mkapa hastahili kabisa kujifariji kwamba aliiongoza nchi hii kwa amani na mshikamano. Ni bora tu kwamba amekwenda. Ni bora tu kwamba yeye si tena kiongozi wetu, maana hakutukinai sisi kama raia wake. Ni bora tu kwamba anamalizia umri wake huko aliko na hivyo alivyo.

Lakini asitutafiri kutukumbusha kilio matangani, hali anajuwa kuwa msiba aliotuwachia umetushinda kukimaliza kilio chake hadi leo. Naasifanye hivyo, maana nasi tutainuka tuseme: “Oneni, there stands a looser!”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.