HOJA kwamba Tanganyika inatumia Muungano wa Tanzania kuimeza Zanzibar si mpya hata kidogo. Ni kongwe na ina mashiko. Ilianza kujengwa zamani, tokea 1964. Tokea wakati huo hadi leo, hoja hii imekuwa ikitetewa na kuchambuliwa kwa dalili na mifano ya kutosha kiasi ya kwamba imeshazoeleka mno vichwani mwetu.

Muokote Mzanzibari yeyote leo hii, ama kutoka pale Dada Njoo – Darajani, Kizimkazi – Mkunguni, Mapinduzi – Mkoani au Maziwa Ng’ombe- Micheweni, na umuulize ni ipi nafasi ya Zanzibar katika Muungano huu, atakujibu: ‘kutawaliwa’ au atakupa neno lolote mfano wa hilo – kumezwa, kuburuzwa, na kadhalika.
Kwa hivyo, hoja hii imefahamika vya kutosha na imejengeka vichwani mwa watu. Walioitoa, wamefanikiwa. Imekuwa kama mbegu iliyopandwa: imechipuwa, imekuwa na sasa inamea!
Zanzibar inabadilika na kwenye kubadilika huko inaelekeza kutokuridhika kwake.
Zanzibar inabadilika na kwenye kubadilika huko inaelekeza kutokuridhika kwake.

Na mashiko ya hoja hii hayapo katika umaarufu wake tu, yaani sio ile inayoitwa katika Falsafa Argumentum ad Populum, bali yapo katika ule ukweli inayouwasilisha. Yaliyotahadharishwa na hoja hii miaka 40 iliyopita, ndiyo yanayotokezea leo.

Kwa bahati mbaya sana ni kwamba kile ambacho bado hakijafanyika, tokea wakati huo hadi sasa, ni dhamira ya kweli ya kuifanyia kazi hoja hii. Na hii ni kutokana na mapuuza na dharau za watawala wetu.
Ni mapuuza, maana wanaona kuwa hoja hii itakuwa ikiibuka na kuzama yenyewe kwa yenyewe na hatimaye itakufa kifo cha kawaida (natural death) tu. Na ni dharau, maana wanaamini kuwa hata kama hoja hii itaendelea kudumu, Wazanzibari wenyewe ni wachache kulinganisha na hao waliounganishwa nao na, basi, hawatakuwa na nguvu za kuweza kulazimisha vyenginevyo visivyokuwa hivi vilivyo sasa. ‘Waache Wazenji waseme tu, maji ya moto hayaunguzi nyumba!’
Hilo ni koseo. Kwanza, katika jambo kama hili, Wazanzibari si maji, bali ni cheche za moto. Hakuna asiyejuwa kuwa Zanzibar ni kituo cha usambazaji –  usambazaji wa kila kitu. Historia inaonesha kuwa itikadi, dini, biashara na hata misimamo mbalimbali inayoathiri maisha ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, ni vitu vilivyoanzia hapa na kusambazwa ndani ya Bara la Afrika kupitia Tanganyika. Kwa hivyo, uwezekano wa zumari kupulizwa tena hapa, na wa Maziwa Makuu wakaicheza, bado ungalipo. Lazima watu watanabahi hilo!
Lakini, pili, ni koseo kwa kuwa jambo kubwa kama hili linalohusu khatima ya nchi na uwananchi wa wananchi wake, halifunikiki kombe kiasi hicho. Haliwezi kupuuziwa na kudharauliwa namna hii. Hili ni jambo la watu na hii, Zanzibar, ni nchi yenye watu wake. Basi ni wazi kuwa hoja hii itakwenda ikijirudia hadi moja lijuilikane – ama khatima ya kuwa au ukomo wa kufana!
Kwa hivyo, si kitu cha kushangaza kwamba leo hii Wawakilishi wetu katika Baraza wanaitaka serikali iifanyie kazi hoja hii. Lakini cha kushangaza ni kwamba Waziri Kiongozi, ‘Msomi’ Shamsi Vuai Nahodha, ndio kwanza anawataka wawakilishi hao wajenge hoja kuhusiana na matatizo ya Muungano na sio kutoa malalamiko tu kuwa upande mmoja (Tanganyika) unaumeza mwengine (Zanzibar).
Akina mie tunajiuliza: “Hivi wahishimiwa wetu wajenge hoja ipi tena?” Kwamba, tuonavyo sisi na ambavyo ndivyo vilivyo, ni kuwa hiyo hoja tayari imeshajengeka kwa premises na conclusion zake?
Ushahidi kuwa hoja hiyo ilijengwa na kujengeka ni haya matukio ambayo yamekuwa yakiendelea kutokea tangu Aprili 1964 hadi sasa. Kutokea mambo 11 ya Muungano hadi 22, yaani ongezeko la asilimia mia moja, na yote yako dhidi ya Zanzibar kama nchi huru, ni uchambuzi na ithibati kwamba hoja hii ni madhubuti (sound argument).
Hapa ifahamike kuwa matukio haya, kama yalivyokuwa yakipigiwa mifano na wahishimiwa Wawakilishi wetu mule Barazani, ni uchambuzi na ithibati tu kwa hoja iliyokwishajengwa zamani mno. Yenyewe si hoja inayokusudiwa hasa, kama alivyoyachukulia Msomi Maalim Shamsi.
Wawakilishi wetu waliposema, kwa mfano, kuwa uchumi na biashara ya Zanzibar hivi sasa ni vitu vinavyoendeshwa kwa maamuzi kutokea Bara, hawakuwa wakijenga hoja mpya. Walikuwa wanatoa moja kati ya shuhuda nyingi zinazothibitisha hoja kongwe kwamba Zanzibar, kama nchi huru, basi katika Muungano huu haina lake jambo –  imekufa dungu msooni. Ni nchi yenye uhuru lakini siyo huru!
Changamoto iliyopo mbele ya msomi na mwalimu wetu huyu, kwa hivyo, akiwa kama kiongozi wa shughuli za serikali Barazani na pia akiwa na dhamana kubwa katika serikali anayoiongoza, sio kuibomoa hoja hii ya Zanzibar kumezwa na Tanganyika, maana haibomoki wala haivunjiki, bali ni kujenga hoja ya kuimezua Zanzibar – kama kweli ni mjenzi wa hoja – kwamba tayari Zanzibar yake imeshamezwa!
Na wala asidanganyike kwamba umezuwaji wa Zanzibar umo katika kuundwa kwa Tume ya Pamoja ya Fedha au kupewa asilimia 4.5 ya mgao wake wa misaada na serikali ya Muungano tu. Hivyo visimdanganye kwa kuwa vyenyewe ni vijimambo vidogo vidogo, ambavyo vinafanywa sasa ili kuuviza huo mchakato wa umezuwaji, wanaouona kuwa umeanza.
Umezwaji wa Zanzibar haukuanzia katika vijimambo hivi – vyenyewe ni matokezeo tu ya kumezwa huko – na, basi, umezuwaji wake hauwezi kuanzia kwavyo. Suluhu ya Zanzibar katika Muungano haimo katika Tume ya Fedha wala katika hiyo 4.5% ya mgao, bali imo katika siasa inayouzunguka na kuuendesha Muungano wenyewe. Mwenye siasa hizi ndimo mulimo na tatizo lenyewe.
Hapa nazungumzia siasa kwa maana yake halisi, yaani nguvu na maamuzi. Hali ya kuwa na nguvu na uwezo wa kuzitumia nguvu hizo katika kufanya na kuyasimamia maamuzi, huko ndiko kufanya siasa. Na hiyo ndiyo siasa.
Kwa maana hiyo ya siasa, Tanganyika, kwa jina la Muungano imeitawala Zanzibar. Inaifanyia maamuzi na inatumia nguvu zake kuona kuwa maamuzi hayo yanatimizwa na yanatimia. Hilo halijali ikiwa ama maamuzi hayo yanaendana au hayaendani na hali halisi ya Zanzibar kijiografia, kisiasa, kiuchumi au kiutamaduni. Linachojali ni kuendana kwake na matashi ya Tanganyika tu.
Sitii chumvi na wala sikathirishi maneno kusema kuwa mipaka na thamani ya uhuru wa Zanzibar imo ndani ya mipaka ya matashi ya Tanganyika, kwa jina na kwa baraka za Muungano. Nje ya hapo au kinyume cha hivyo, hapana Muungano – kwa tafsiri hii ya Muungano tulionao. Hivyo ndivyo siasa za Muungano zilivyo, na hapo ndipo penye uhalali wa hoja hii ya kumezwa kwa Zanzibar na Tanganyika.
Kwamba Zanzibar haina nguvu za kufanya maamuzi yake yenyewe wala uwezo wa kuyasimamia maamuzi hayo. Na kama haina nguvu katika maamuzi yake, maana yake ni kusema kuwa imemezwa, imetawaliwa.
Zanzibar haiwezi kujitungia sera za kuinua uchumi wake kama Zanzibar na kutaraji kufanikiwa kama Zanzibar, maana baada ya yote nguvu za utekelezaji wa sera hizo lazima ziende sambamba na maslahi ya Tanganyika, kwa jina la Muungano. Kwa mfano, haiwezi kujiundia mfumo wake wa kodi kando ya huu wa Muungano kwa kuwa haina nguvu hizo. Zanzibar haina nguvu kama nchi, kwa kuwa imeamuliwa iwe ni kijisehemu tu cha jinchi!
Hapo ndipo hata ile shaka kuwa pana azma ya kuundwa kwa serikali moja ya Tanzania na kuiua kabisa serikali ya Zanzibar inapopata uhalali wake. Waache akina msomi na mwalimu wetu wakatae, ati kwa kuwa katiba inasema wazi ‘kutakuwa na serikali mbili, ya Zanzibar na Tanzania.’ Kwao wao, wanataka kila mtu akiamini kile kilichomo katika katiba, hata kama anachokishuhudia katika uhalisia ni kitu tafauti.
Ni kweli, panapohusika katiba iliyopo sasa, serikali moja haionekani ndani yake. Lakini panapohusika uhalisia, serikali moja inaonekana kila mahali. Haihitaji kwenda kwenye maabara ya kisayansi kulitafiti hilo. Uangalie tu utendaji kazi wa serikali zetu mbili, kisha fanya tathmini hata ya kiwango cha chini kabisa (the least-effort-evaluation), na nina hakika utafikia hitimisho (conclusion) la kuwepo kwa serikali moja.
Hakuna usomi hata mmoja ulimwenguni utakaotafautiana na zile ziitwazo basic facts kwa kuzingatia theoretical facts. Hapa nakusudia kusema kuwa kilichomo katika katiba zetu ni ukweli wa kinadharia tu (theoretical), ambao mara nyingi huthibitishwa vyenginevyo na ukweli halisi (basic). Kwani ni mara ngapi hata hao viongozi wakubwa wa serikali huvunja katiba za nchi kwa matashi yao? Tupige mifano mingapi kulithibitisha hilo?
Sijuwi ni nadharia gani ya kisayansi, ama iwe Applied Science au iwe Social Science, inayokiuka misingi ya ukweli halisi. Msomi na mwalimu wetu huyu, Mhe. Shamsi, sijuwi kaegemea ipi? Kwa maoni yangu yasiyo na hata chembe ya usomi – kwa kuwa mimi si msomi – ni kuwa hata kama hakitajwi popote katika katiba, tuna kiwango kimoja tu cha serikali, na serikali hiyo ndiyo yenye huo userikali wote mikononi mwake. Kwangu, sio kuwa serikali moja inakuja, bali tayari (kimatendo) imeshakuwepo.
Labda, Msomi Shamsi, alikuwa aulizwe kwa nini pameundwa serikali moja bila ya Baraza la Wawakilishi kujulishwa na sio kuambiwa kuwa pana khofu ya kuundwa kwa serikali moja. Hapo angelielewa!
Serikali, kwa maana ya chombo cha utawala chenye maamuzi ya juu kuhusu khatima ya taifa, ni ya Muungano. Khatima ya Zanzibar inaamuliwa Dodoma. Nani aongoze, vipi aongoze, kipi kiwe na kipi kisiwe hapa Zanzibar ni kutokana na amri, maagizo na maelekezo kutoka huko kwenye serikali yenye userikali.
Kwa hivyo, kuambiwa kuwa tuna serikali mbili, huo ni u-wili mtakatifu wa vitabuni mwetu tu. Wa kinadharia tu. Kwenye uhalisia, kuna serikali moja tu inayotenda na kutawala. Kuna u-moja wa milele!
Siasa hii ya mkubwa kummeza mdogo ndiyo iliyouzunguka Muugano huu na ndiyo waliyoikhofia Wazanzibari tokea zamani. Huu Muungano haujaanza kukosolewa leo. Kwa bahati mbaya, huko mwanzo utawala ulikuwa ni wa mkono wa chuma zaidi kuliko hivi sasa. Wengi walizizungumzia khofu zao hizi vibuyuni, na wale wachache waliothubutu kuzisema wazi, waliishia pabaya.
Sasa ni zama mpya. (Shukrani kwa uhuru zaidi wa kujieleza, na ole kwa wanaoonekana kutaka kuturudisha kule kule kwa kutiwa shemere na bakora mbili mbili mgongoni. Inshallah, huko hatutarudi!) Sasa ni wakati wa umma kutumikiwa na sio kutumikia. Sasa umma unapokuwa hauridhishwi na jambo fulani, hata kama jambo hilo linapendwa mno na watawala wao, hulisema kwa sauti na nguvu zote. Sasa ni zama za watawala kuakisika kwa matakwa ya umma na sio umma kuakisika kwa matakwa ya watawala.
Matakwa ya Zanzibar ya sasa ni kuwa na nguvu zaidi za kufanya maamuzi na uwezo wa kuyasimamia maamuzi hayo. Ni kuwa na uwezo wa kujipangia mustaqbal wake na kuhakikisha kuwa inaufikia. Kwa mfano, Vision 2020 haiwezi kutekelezeka katika hali ya sasa ya Muungano. Lazima hali hii ibadilike kwa haraka.
Hii haimaanishi, na wala haitamaanisha hata kidogo, kutoka nje ya Muungano na Tanganyika, lakini itamaanisha kutokuwa mfano wa koloni la Tanganyika. Maana, kuwa katika muungano ni kitu kimoja na kuwa chini ya ukoloni ni kitu chengine. Na lazima tukubaliane kwamba kumekuwa na mambo mengi sana yanayodhihirisha kuwa Zanzibar imetawaliwa na Tanganyika kuliko kuiita nchi huru iliyo katika muungano na nchi nyengine huru.
Nani atayapeleka matakwa haya mbele na kuhakikisha kuwa yanatimia? Bila ya shaka ni Wazanzibari wenyewe. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuona kuwa anaifanyia jambo la kheri nchi yake kwa kutoa mchango wake katika kuimezua. Mwenye kalamu aandike, mwenye chaki naasomeshe na mwenye nafasi ya kuingia vikaoni, naanzishe mdahalo na, au, aendeleze ule uliokwishaanzishwa.
Sote natuelewe kuwa hilo la siasa za Muungano ndilo tatizo letu la pamoja. Na hili nawashajiisha hata ndugu zetu wa Tanganyika waliangalie kwa muktadha huo huo. Kwamba sisi hatuna tatizo la kuungana nao, bali siasa za kuungana huko ndizo zinazotutatiza. Kwa pamoja, tunaweza, kwa haraka na kwa ufanisi kabisa, kuzirekebisha siasa hizo bila ya kuuathiri Muungano wenyewe.
Makhsusi hapa naelekeza kauli hii kwa wenzetu wote walio katika chama kilichokamata dola hivi sasa. Wao, kwa siku nyingi, wameuchukulia Muungano kuwa ni suala nyeti kuweza kuzungumzika. Ndio maana, kuliibua suala hili vikaoni mwao kulihitaji kwanza kuwa mpinzani wa CCM na serikali zake. Sasa nawaache woga wao wa ‘kukatwa vichwa’!
Kwamba sasa imeshabainika kuwa kinachohitajika katika kulizungumzia hili ni kuwa Mzanzibari au mwenye kuipendelea kheri Zanzibar tu, na si zaidi wala pungufu ya hilo. Hii ndiyo maana waliolichangia hili Barazani mara hii hawakuwa wapinzani tu, bali hata CCM nao. Kwamba kuwa mwana-CCM ni kitu kimoja na kuwa mzalendo kwa nchi yako ni kitu chengine.
Kwa hivyo, kwa Msomi wetu Maalim Shamsi, na wengine wote waliomo serikalini na chamani, Barazani, ama iwe watawala au wapinzani, sisi Wazanzibari tunachokihitaji kutoka kwenu ni Zanzibar iliyo na nguvu zaidi, iliyo bora zaidi na makini zaidi. Tunahitaji kuimezua Zanzibar kutoka hali iliyopo hivi sasa.

Narudia tena, hatuhitaji hata kidogo kuvunja Muungano huu, lakini pia hatutaki gharama za kuudumisha Muungano huu ziwe ni kuipopotowa Zanzibar yetu. Itendeeni mema Zanzibar, nchi yenu, mkumbukwe na mkalipwe kwa hayo. Nasema tena kwamba tukishirikiana sote, twaweza kuimezua nchi yetu!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.