HUKU kwetu kuna hadithi maarufu ya bwana mmoja aliyekitumia kipindi chake cha sakaratil-maut kwa kupiga kelele: “Jamaa njia yote n’shaitia miba, sasa mie n’pite wapi?” Sakaratil-maut ni kipindi cha kukaribia kufa kwa mtu na ambapo mtu hubainishiwa na Mungu makazi yake yatakavyokuwa huko akhera aendako. Mtu hujijengea akhera yake hapa hapa duniani. Anayeyaishi vyema maisha yake, atapata akhera njema; vivyo na kinyume chake!

Katika hadithi hii, bwana huyu hakuyaishi vyema maisha yake ya duniani. Aliishi katika starehe lakini kwa kuwadhulumu watu, alikuwa na madaraka lakini alikithirisha ufisadi na alikuwa na utajiri lakini aliupata na kuutumia kwa maasi. Ndipo hapa katika sakaratil-maut yake, akawa anaoneshwa jaza ya yale aliyoyatenda katika uhai wake. Hapana shaka, ilikuwa ni akhera mbaya.

Katika wakati huu wa mwisho wa uhai wake, alikuwa akijuta na kujilaumu, lakini, maskini, majuto hayo yasingeliweza kumuepushia mauti yaliyokwishamchanulia makucha mbele yake.

Na zaidi ni kuwa asingeliweza kuibadilisha mizani ya malipo kwa wakati ule tena. Ile miba aliyoitupa katika njia (dhulma, ufisadi na uasi), sasa ilimlazimu kuikanyaga auone uchungu wake. Kwani si imeandikwa kuwa kila mtu atabeba mzigo wake mwenyewe? Basi na mtu wetu naye alikuwa yumo kuubeba wake!

Na CCM nayo inaelekea kuubeba mzigo wake yenyewe. Kwamba nayo pia imeshaichafua njia yake iliyokuwa iipite na kuvuka salama katika uchaguzi ujao wa mwaka 2005. Haina makazi mema huko iendako – nalo yalielewa fika – kwa kuwa haikuyaishi vyema maisha yake ya kisiasa. Iliishi kwa ubaya, dhulma na ufisadi. Na huko ndiko kulikoitia miba na kuiharibu njia ambayo kwayo ilikuwa ipite kufikia pepo yake ya kisiasa. CCM imeuharibu umma!

Ndiyo, umma. Katika siasa, umma ndio kila kitu, ndio njia na ndio lengo. Kwa chama cha kisiasa kuweza kupita na kusimama mbele, hupaswa kwanza kutataga juu ya vichwa vya watu. Nakusudia kusema kuwa huhitaji kuwavuna na kuwatumia watu ili kukifikisha katika madaraka.

Lakini, hata baada kuyashika hayo madaraka, ili chama hicho kiendelee kuwapo pale, basi lazima kivithamini hivyo vichwa kilivyovitataga. Nakusudia kusema kuwa ni lazima kwa chama kinachotawala kuwapembejea watu kwa kuwatekelezea muradi wao, yaani kuwaletea maendeleo, kuwalindia na kuwadumishia haki zao pamoja na kuutukuza utu na heshima yao.

CCM imeacha zamani kuyafanya hayo. Kimekuwa si chama cha kupembejea, bali cha kuwatisha na kuwakomoa watu. Kimekuwa ni chama kinachojitahidi kujitofautisha na watu waliokinyanyuwa na sio kujifananisha nao. Sio tena kile cha wakulima na wafanyakazi, bali sasa ni kikundi cha watawala wa mkono wa chuma, ambacho kwacho ufisadi na uatokrasia ni misamiati ya kawaida. Hapo ndipo CCM ilipojiharibia!

CCM imeudhi na kukera hadi ikakirihisha. Kwa Zanzibar na Wazanzibari, ikirahi ya CCM ndio imefurutu ada. Na kulibaini hilo, haihitaji kuchakuwa historia yake sana. Chukuwa kipande chochote cha historia hiyo –  iwe mwanzo wake, katikati au mwisho – au kundi lolote lile la kijamii, na utakuta jinsi CCM ilivyosimama kuwadhulumu, kuwafisidi na kuwaasi Wazanzibari!.

Hapa tutaje mifano michache ya hivi karibuni tu. Mwaka 2003 ulimalizika kwa serikali ya CCM kutunga na kupitisha sheria za usalama barabarani zilizolalamikiwa na madereva wa daladala kwamba ziko dhidi ya maslahi yao. Licha ya Wazanzibari hawa kupiga kelele sana, serikali ya CCM haikuwasikiliza. Mwisho madereva hawa wakagoma kuonyesha malalamiko yao.

Katika wakati huo huo, wenzao wa Kenya walikuwa na mgomo kama huo na malalamiko hayo hayo. Lakini, ambapo serikali ya NARC iliwaita madereva hawa kuzungumza nao, hii ya CCM, kwa kibri na jeuri, ikazifuta leseni za magari yote ya daladala. Angalia hii tafauti iliyopo hapa: serikali ya NARC, kwa kujuwa kwake thamani ya watu hawa kwake, iliwaita kuwapembejea, ya CCM, kwa kutokujali umuhimu wao, iliwakomoa.

Kukomoa raia ndio uthubutu wa serikali ya CCM, maana huona kuwa inapofanya hivyo hujuilikana hasa ule userikali wake. Itakuwaje bwana serikali nzima isalimu amri kwa raia wake? Lakini jeuri hii na ujuba wa CCM kwa raia, ndizo zinazokichongea chama hiki.

Maana kule hakukuwa ni kuwakomoa madereva wale tu, bali pia familia zao na hata abiria wao, ambao wote, kwa pamoja, hutegemea usafiri huu ili maisha yaende. Huko kulikuwa ni kuitia miba njia ambayo CCM ilipitia kufikia madarakani. Na sasa ni wazi kuwa vichwa vyote vile vilivyokomolewa, vimeshakoma kuiunga mkono CCM. Na hilo CCM inalijuwa vyema, ingawa imechelewa kulijuwa.

Mwaka huo huo serikali hii ya CCM kwa kuvutiwa na ushauri wa kuiboresha bandari bila ya kuzingatia hali halisi ya nchi, iliamua kuwafukuza makuli wa bandarini Zanzibar kwa madai ya kulinda usalama wa wasafiri na mali zao. Makuli hawa walikashifiwa kwa kuitwa ni vibaka na wahuni, maana walikuwa wanarundikana pale bandarini ilhali wakijuwa kuwa hapana ajira.

Hili, licha ya kuwa kwake tusi kwa makuli hawa, ambao kiwango chao cha uaminifu hakiwezi kukaribiwa na kiongozi yeyote wa nchi hii, ilikuwa pia ni kashfa kwa historia ya kijamii na kiuchumi (socio-economic history) ya Zanzibar, ambayo inaitambua bandari kama njia kuu ya uchumi wa Visiwa hivi. Lakini CCM haijapata kuitilia maanani historia ya kweli ya Zanzibar katika maamuzi yake, na ndio maana ikazuka na hatua hii ya kuwafukuzilia mbali wale makuli.

Ni maamuzi kama haya ya kibabebabe ya CCM ndiyo yanayoigharimu nafasi yake ya kisiasa hapa Zanzibar. Ndio maana kwa uamuzi huu wa kuwafukuza makuli wale pale, hakuna msamiati wa kuwaeleza ili kuisamehe CCM. Hawawezi kuisamehe maana imeyafisidi maisha yao na ya watu wao nyumbani.

Na zaidi hawawezi kuisamehe, kwa kuwa hatua hii ilikuwa imefuatiwa na kuanzishwa kwa chama cha kisiasa kilichoitwa SAFINA. Chama hiki kilikuwa ni tishio kubwa kwa uhai wa CCM hapa Visiwani, maana kiliasisiwa na watu walitoka ndani yake. Kuhusishwa chama hiki na hatua ile kulitokana na ule ukweli kwamba shina lake lilikuwa ni Kaskazini Unguja kwahala ambako wanatokea wengi kati ya wale wanaofanya kazi za uchukuzi pale bandarini. Kwao, hatua hii ilikuwa ni kuwakomoa kwa kuwa wanatokea upande ambao umejitenga na CCM.

Na dhambi ya kuwakomoa watu kwa kuwa wanatokea sehemu ambazo inapingwa, ndio kanuni ya CCM. Yaliwahi kuwapata mambo kama hayo Wazanzibari wenye asili ya Pemba, hata wakawa wanafukuzwa ovyo makazini na kuachishwa masomo kwa kuwa tu Pemba ni ngome ya CUF. Kwamba hapa kanuni hii ilikuwa inarejewa, haishangazi sana.Na wote, Wakaskazini na Wapemba, hawawezi kuisamehe CCM kwa dhambi hii.

Mwaka huu wa 2004 ukaanza kwa mgogoro baina ya serikali ya CCM na baadhi ya makundi ya Waislam. Kwa kutumia lile linaloonekana kuwa ni ‘tawi la kidini’ la CCM, yaani ofisi ya Mufti wa Zanzibar, serikali ikaanza kubana uhuru wa watu kuabudu kama walivyopewa na katiba zao. Kwa mamlaka ya kisheria iliyopewa na serikali ya CCM, ofisi hii huzuia Waislam kuswali swala zao, kufanya mihadhara yao na maandamano yao.

Kwa ufupi, inawanyima haki yao ya kutekeleza imani zao kwa uhuru bila ya kuingiliwa kati. Hivi sasa, kuna Waislam kibao ambao wameathirika kwa njia moja ama nyengine kutokana na amri za tawi hili la kidini la CCM. Huko ni kuwakera kwa makusudi kabisa wapiga kura wa chama hiki, nako ndiko kuitia miba njia ya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2005.

Lakini kushindwa kwa serikali ya CCM kuzilinda na kuziheshimu haki za watu wake hakuko katika siasa na dini peke yake, bali pia katika huduma za kijamii na sekta ya utumishi. Ukosefu wa maji hivi sasa Zanzibar ni wa kutisha na kuaibisha, kwa nchi ambayo meli kubwa za nje zilikuwa zikija zikiegesha kwa ajili ya kuchota maji tu.

Usizungumzie kuhusu matibabu katika hospitali zetu za serikali. Ni kukumbusha kilio matangani. Ile kauli ya matibabu bure imebakia kuwa ya kisiasa tu, ingawa hali za watu kutokumudu gharama za matibabu haijabadilika. Bado Mzanzibari hana uwezo wa kujitibu mwenyewe kwa kuwa hana pato la kumruhusu hivyo.

Matokeo yake ndio hivi vifo vinavyotokea kizembe sana katika hospitali zetu eti kwa kuwa tu mtu hakuja na vifaa vyake vya kufanyiwa operesheni. Wazanzibari waliopoteza watoto, ndugu na jamaa zao hawawezi kuwa na upumbavu wa ‘kuifyagilia’ tena CCM hata baada ya idhilali na msiba wote huo. Hawawezi!

Kwenye utumishi kuna tatizo lile lile la udogo na ucheleweshwaji wa mishahara. Wafanyakazi wa serikali ya CCM wanalipwa pesa ndogo mno kuweza kujikimu na bado pesa hiyo inacheleweshwa hadi kuanzia tarehe 35. Hili limewafanya wengi wao kuwa maskini hohe hahe, wanaonuka madeni. Wanadhalilika, wanadhulumika. Sioni kuwa, kwa akili zao huru, watapata uthubutu wa kuirudisha tena CCM madarakani kwa kura zao, huku wakijuwa kufanya hivyo ni kuurudisha udhalilifu na udunifu wao.

Kwa hivyo, ikiwa tutawagawa Wazanzibari kwa mujibu wa makundi ya kijamii, basi tutakuta kuwa CCM imeshalikera kila kundi. Imelikera kundi la vijana kupitia ajira ya daladala; matajiri kupitia biashara na bandari; Waislam kupitia tawi lake la kidini; wanawake kupitia madumu ya maji; Wakaskazini kupitia presha za Safina; Wapemba kupitia ukandamizaji wa upinzani na hata wafanyakazi kupitia mishahara duni na inayocheleweshwa. Sasa ililie bega lipi?

Haina bega jingine, na yenyewe inalijuwa hilo. Tatizo ni kwamba imechelewa mno kulijuwa, na sasa kujuwa kwake hakusaidii tena kitu, maana tayari imeshaingia katika sakaratil-maut. Ndio maana sisi wengine tuliopo Zanzibar hivi sasa hatushangazwi hata kidogo na hivi vimbwanga vinavyozushwa na kutokea hapa.

Hatujashitushwa, kwa mfano, na habari za kuwepo kwa ndugu zetu wenye asili ya Tanganyika wanaofukuzwa hapa. Kwamba twajuwa si kweli, illa ni kutapatapa tu kwa CCM. Bali hatushitushwi na hata hii miripuko ya mabomu ‘bomu’ inayotokea kila siku, maana nayo haina maana yoyote zaidi ya harakati za kupapia roho za mtu aliye katika sakaratil-maut! Hali i vivyo kwa jitihada za kuugawa Uzanzibari kama karanga shambani na zile za kuyagawa upya majimbo ya uchaguzi ya Zanzibar.

Hakuna chochote katika hayo kiihakikishiacho CCM uhai zaidi au hata, angalau, kuiepusha kukanyaga miba iliyokwishaimwaga katika njia yake ya kupitia. Mwisho wa siku, CCM itajikuta ikilazimika kuipita njia hii hii kuyakabili mauti yake, maana hivyo ndivyo ilivyojichagulia mwisho wake uwe!

Hali Halisi, Na. 3, Mei 2004

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.