Zanzibar ina sheria kali dhidi ya ‘magendo ya karafuu’. Mojawapo ni kifo. Lakini bado magendo yanaendelea Pemba. Kwa nini? Charles Evers anasimulia katika Have No Fear (McGraw-Hill, 1997) kwamba siku zile za Great Depression, Marekani iliweka ‘sheria ya pombe’ kwa lengo la kuzifanya pesa zielekezwe katika mahitaji mingine muhimu ya maisha, kama chakula, malazi na mavazi na sio ulevi. Hata hivyo, sheria hiyo haikudumu kwa kuwa ilipingana na utamaduni wa Wamarekani wanaoichukulia pombe kama sehemu ya maisha. Pombe ikanywewa zaidi kuliko mwanzoni, athari zake zikawa kubwa zaidi kuliko ilivyowahi kuwa na kila siku watu wakikamatwa kwa kuivunja sheria hiyo hiyo. Mwishowe serikali ikang’amuwa kosa lake na ikaibadilisha!

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeshashauriwa mara kadhaa kuibadilisha sheria ya udhibiti wa biashara ya karafuu kwa kuwa inapingana na mabadiliko ya sasa ya kiuchumi yanayoamini ubinafsishaji na uhuru wa soko. Kuendelea na udhibiti huu kunatilika mashaka, na inapozingatiwa mazingira ya kisiasa, ni kana kwamba inalipiza kisasi kwa kukataliwa kwake na Wapemba.

Mtu anapata wasiwasi huo. Kwa nini udhibiti katika biashara ya karafuu tu isiwe kwa utalii, kwa mfano, ambao SMZ imewekeza zaidi kuliko katika mashamba ya karafuu Pemba? Kwa nini SMZ iliyokusudia uchumi, na uchumi tu, iweke mipaka baina ya biashara moja na nyengine? Mwenendo wa uchumi Zanzibar unaonesha kuwa, ikiwa utalii unasimamiwa vyema unazalisha zaidi kuliko karafuu. Kwa hiyo, haiwezekani kuwa udhibiti huu wa SMZ kwa karafuu unatokana na kutokuwa na njia nyengine ya kiuchumi.

Hata ingelikuwa hivyo, bado tabia ya SMZ katika biashara ya karafuu haitetei udhibiti huu, maana mantiki ya kiuchumi inatambuwa kuwa mafanikio ya biashara yanategemea zaidi uwekezaji katika uzalishaji. SMZ haijawekeza katika mashamba ya karafuu kule Pemba, ambayo mengi ni milki ya watu binafsi. Haipotezi muda wala fedha zake kuyashughulikia au kumsaidia mkulima wake kwa semina na mafunzo. Haimpatii hata mkopo wa kuyahudumia wala ulinzi wa kuyalinda. Tangu mwanzo humwacha peke yake tu; na ni hadi mavuno ndio humjia kumpanga urafiki wa lazima.

Kwa SMZ kutokuwekeza chochote katika mashamba haya ya karafuu Pemba, lakini mwisho wa siku ikajitokeza kulazimisha iuziwe karafuu zote, hakuoneshi dhamira njema. Kwa wachumi wote ilionao kushindwa kuja na suluhisho la kuliboresha zao hili, badala yake wakawa wanachokijua ni kuja na bei za chini kununulia karafuu iliyovunwa na kukusanywa kwa tabu, haionekani kudhamiria uchumi. Ni siasa tu. Vyenginevyo, inakuwaje zao hili liwepo zaidi ya karne na bado wataalamu wetu wasiweze kubuni mabadiliko ya msingi katika ukuzaji na uvunaji wake?

Hadi leo, mingi ya mashamba ya mikarafuu yako misituni katikati ya mapori ya mibura na mikekewa. Hadi leo karafuu zinavunwa kwa staili ile ile ya miaka 100 nyuma – mchumaji kwenda shambani alfajiri, kuukwea mkarafuu, ‘kuutawa’ ili asiyumbishwe na upepo, kulidumua shada moja moja la karafuu kutoka mtini na kujaza mapakacha. Kwa taarifa ni kuwa, kuna kesi nyingi za wachumaji kuanguka mikarafuu wakapoteza maisha ama kupata ulemavu wa kudumu.

Hadi leo, karafuu husanifiwa kwa njia ile ile ya mababu zetu – mchumaji kukaa kitako kwa nusu nzima ya usiku kuzinyambua (kunyambua ni kuchukuwa shada moja moja la karafuu na kuzitenganisha kokwa zenyewe kutoka konyo lake), asubuhi kuzianjaza kwenye majamvi na magunia uwanjani kwa kutegemea jua lifanye karama zake. Siku mvua ikinyesha, mali yote inakuwa ‘mpeta’ (karafuu mbovu) na zile nguvu zote zilizokwishatumika huwa zimekwenda patupu!

Sasa kwa nini, kwa SMZ inayojali watu wake na iliyokusudia kufanya uchumi kweli, isijenge mfumo wa ukuzaji na uvunaji wa karafuu, badala yake ijikaze kupanga bei na kudhibiti soko tu? Kwa nini, ikiwa lengo hasa ni maendeleo ya watu na uchumi pekee?

Wiki iliyopita, nilijaribu kuwasilisha picha ya umasikini wa Pemba. Nia haikuwa kuwahurumia mno Wapemba kiasi ya kuwavumilia wanapovunja sheria za nchi. Nilitaka tu uelewe maana ya uvunjaji huo wa sheria; na kama u mtambuzi utambuwe kuwa, dhati ya sheria ni kuwasaidia walengwa na sio kuwakomoa.

Hebu tuseme ni kweli serikali haiyafanyi maisha ya Pemba kuwa magumu kwa makusudi, lakini hivi haijuwi kuwa hali ya kule ni ngumu sana na kwamba wale raia wake wanateseka? Basi kama inajuwa, inawajibika kuchukuwa jitihada za makusudi kuziinua hali za watu wake hawa. Kabla ya hata kuwalazimisha waiuzie karafuu zao kwa bei hafifu, SMZ ilikuwa iweke mazingira yanayowavutia Wapemba kufanya biashara nayo!

Hebu tuseme ni kweli SMZ ni masikini na, hivyo, haina uwezo wa kuyakidhi mahitaji yote ya watu wake wote, kwa vile umasikini wa Pemba ni muakisiko tu wa umasikini ulionea nchi nzima kwa jumla na usiopaswa kuangaliwa kama kesi tafauti. Basi kama hivyo ndivyo, kwa kuzalisha kwake karafuu, kunaifanya Pemba iwe mzalishaji wa pato la SMZ, ambayo inalazimika kuihakikishia mgao wake unaifika na unaifaidisha. Kabla ya kuutumia mgao huo kununulia boti mpya za doria na risasi za kuwafyatulia Wapemba, ilikuwa kwanza ijenge miundo mbinu na isambaze huduma za kijamii!

Hebu tuseme kuwa si kila pesa inayotokana na mapato ya karafuu ya Pemba inapaswa kutumika kwa ajili ya Pemba tu maana inakuwa ni fedha ya Zanzibar kwa ujumla wake, na sio ya upande mmoja tu wa Zanzibar. Basi kama ni hilo, watu hawa wamekuwa wa mwanzo kulifahamu. Ndio maana dai lao kubwa ni bei nzuri ya karafuu, halafu maswala ya mgao ni juu ya SMZ yenyewe. Wao wafaidike tu na karafuu zao, na ukusanyaji na ugawaji wa mapato utategemea mizania za kiserikali!

Lakini kwa kuwa SMZ inaujuwa umasikini wa Wapemba na inaupuuzia, na kwa kuwa haitaki kuiona Pemba inafaidika na karafuu zake, na kwa kuwa inashindwa kutoa bei nzuri, ndipo Wapemba wenyewe wakalazimika kutafuta njia ya kufaidika na karafuu zao. Wapemba wanajifanyia wenyewe kile kilichokuwa kifanywe na serikali yao.

Sasa, kwa kuwa wameshaipunguzia mzigo serikali baada ya kuiona imeshindwa kutimiza wajibu wake kwao, kitu pekee kilichobakia, na ambacho SMZ inapaswa kukifanya, ni kile kiitwacho participation at the least effort, angalau kujitoa kimasomaso. SMZ ijitowe kimasomaso kwa kusimama baina ya wakulima na wafanyabiashara waliojitokeza kununua karafuu kwa bei nzuri na ihakikishe kuwa raia wake hawa hawadhulumiani. Huku, ingawa kunaonesha kufeli kwa SMZ, angalau hakuichonganishi na raia. Madhali tayari raia wenyewe wameshaonesha njia, ushiriki huu utaleta ushindi kwa upande wa raia na ungamo kwa upande wa serikali – na la raia kuwa mshindi, ndilo linalotakiwa na serikali zinazojali.

Ikifanya hivyo, SMZ itafaidika mara mbili: kwanza kwa kuvuna imani za raia wake katika dakika za lala salama, kwa kujenga daraja la utangamano baina yao na, pili, kwa ushuru na kodi zitakazotokana na biashara hiyo. Huko ndiko siasa kutumikia uchumi!

Kijiografia na kiuchumi Pemba ni ndogo sana. Haina eneo kubwa la nchi wala idadi kubwa ya wakaazi. Kwa hivyo, neema ndogo tu huweza kuenea kwa kasi na kuwafikia watu wote. Pamoja na mbano wa SMZ, walioweza kupenya leo hii wanaibadilisha Pemba. Pita maeneo ya Kiungoni, Wingwi, Msuka, Konde, Mtambile, Piki na Pandani, kwa kutaja machache, na utakuta nyumba mpya za matofali, mikahawa na maduka makubwa. Kuna baadhi ya vijiji watu wameweza hata kununua magari ili kutatua tatizo sugu la usafiri. Hata watoto wadogo wamefikia umbali wa kununua vibaiskeli vyao.

Hatuwezi kusema kuwa watu hawa wamepata kila kitu katika maisha yao, lakini hali hii inaleta matumaini. Hiyo ndiyo jaza ya karafuu zao. Sasa SMZ kuwakamata watu, kuwanyang’anya mali zao, kuwafunga na hata kuwapiga risasi kwa kushiriki biashara ya karafuu zao wenyewe, si inamaanisha kwamba haitaki watu waneemeke?

Jibu la serikali ni kuwa watu waneemeke kwa kufuata na sio kuvunja sheria. Lakini nimeshaonesha kuwa sheria hii inayozungumziwa hapa, haijali haki za watu kiuchumi na kijamii, bali inasisitiza tu wajibu wa raia kuitii. Inasemwa kuwa, bad law is no law, sheria mbaya si sheria kamwe. Mimi sisemi kuwa hii si sheria, lakini ni sheria iliyokwenda upogo na, kwa hivyo, yenyewe inashawishi kuvunjwa.

Kwa mtazamo wa mbali zaidi, ‘magendo ya karafuu’ ni miongoni mwa miito ya mabadiliko Zanzibar, maana ni uwepo kwa kundi kubwa linalokaidi, kwa haki kabisa, sheria fulani ya nchi na kuunda ‘umoja wa kuivunja’. Kuuitika mwito huu si kuongeza risasi na vikosi vya askari kule Pemba, bali ni kurejea katika chanzo cha tatizo na kukipatia dawa.

Kuuitikia mwito huu ni kwa SMZ, kwanza, kuiangalia hali ya Pemba kwa jicho maalum na kuchukuwa dhamana yake kwayo; pili, kujenga mazingira ya Wapemba kuwa na njia nyengine za kutafutia riziki zao na sio karafuu tu ili serikali ipate muda wa kulishughulukia zao hilo; na, tatu, ni kuifuta sheria ya udhibiti wa biashara hii, ambayo imeshapitwa na wakati.

Hadi hapo mwito huu utakapoitikiwa, itaendelea kuwa ni kinyume cha busara, hekima ya kawaida ya kibinaadamu na mantiki ya kiuchumi, kwa SMZ kutumia mtutu wa bunduki na kuta za jela kupambana na harakati za watu wanaotafuta maisha yao kwa gunia la karafuu zao wenyewe.


Fahamu No 114, 11-17, Disemba 2006

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.