HAPA pana upotoshaji na hila zinafanyika. Wiki iliyopita amenukuliwa Rais Benjamin Mkapa akisema kwamba hatawavumilia wanaotaka kujitangazia matokeo ya kura kabla ya kutangazwa na tume ya uchaguzi. Kwamba huo ni uvunjifu wa amani na yeye akiwa kama raisi wa nchi hataliwacha hilo litokezee mbele ya macho yake. Kijuujuu inafahamika, lakini kiundani amepotosha.

Rais Mkapa ni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na, kwa nafasi yake ya uraisi, ni Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania. Kwa kauli hii, kisiasa alikuwa anajibu kauli ya Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kimekuwa kikiahidi kwamba, kama na mara hii matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar yatapotoshwa kama ambavyo imewahi kutokea mara mbili huko nyuma, basi kitatumia nguvu ya umma kurejesha haki iliyoporwa.

Rais Benjamin Mkapa
Rais Benjamin Mkapa

Na kijeshi alikuwa anawatisha Wazanzibari kwamba atatumia nguvu za dola dhidi yao, baada ya kuwa wamedhamiria kutokubali tena kutawaliwa na mtu wasiyemchagua kwa kura zao. Uzoefu wa kutumika nguvu hizi ni mbaya kwa Zanzibar ikikumbukwa maafa ya 2001 na hivi vituko vinavyousindikiza uchaguzi wa 2005.

Narudia tena. Si kwamba Rais Mkapa hauelewi ukweli ulivyo, lakini anafanya upotoshaji wa makusudi na nyuma yake kuna hila iliyojificha. Nitakuwa mtu wa mwisho kuamini kuwa Rais Mkapa ni muumini wa demokrasia ya kweli na kwamba kweli amedhamiria kuiwacha demokrasia ichukuwe mkondo wake Zanzibar.

Nimewahi kuandika huko nyuma, kwamba huyu ni mkapacratic, sio democratic. Kwake yeye, mipaka ya demokrasia inaanzia na kuishia pale nafasi ya chama chake kushika hatamu inapohusika. Imani yangu ni kwamba anatumia ‘kila njia’ ili kuona kuwa demokrasia inafeli Zanzibar, ikiwa kupasi kwake kutamaamisha kung’olewa kwa CCM madarakani.

Ninasema ‘kila njia’, maana kwa watawala wa aina yake, fahamu yao ni moja tu: power, power, by any means. Na miongoni mwa njia hizo ni kumkandamiza kila ambaye anatishia kuwaondosha madarakani hata ikibidi kwa mbinu chafu na mbaya. Ndio maana sasa Rais Mkapa na chama chake wanafanya kile ambacho watawala wa aina yao hukifanya, yaani kukipa jina baya kinachotishia ulwa wao ili wapate ‘uhalali’ wa kukikandamiza.

Kabla ya Adolf Hitler hajawaangamiza Mayahudi wa Ujerumani, kwanza ‘aliwapakazia’ kuwa ni wasaliti. Kabla Saddam Hussein hajawaua kwa gesi ya sumu Wakurdi, kwanza aliwatangazia kuwa waasi. Kabla Muisraili hajawapiga maroketi Wafalastina, kwanza hueneza kwamba ni magaidi. Na kabla George Bush hajamvamia Saddam Hussein, kwanza alitaka sote tuamini kuwa ana silaha za maangamizi. Ndivyo pia afanyavyo Rais Mkapa. Kabla hajaamuru vikosi vyake kuwamiminia risasi Wazanzibari ili CCM iendelee kubakia madarakani, kwanza anataka iaminike kuwa ni wavunjifu wa amani na sheria. Anatafuta uhalali!

Lakini ni bure, Rais Mkapa hana uhalali huo, hata kama anataka kulazimisha jawabu. Huenda akapata vyombo vya habari, ambavyo vina waandishi na wahariri wenye chuki na Zanzibar na Wazanzibari, na hivyo wakamsaidia kujenga picha ya uhalali anaoutafuta, lakini vyovyote jambo hili litakavyopambwa katika kurasa za magazeti na vioo vya televisheni, halitampa uhalali wa kuwamiminia risasi Wazanzibari. Uhalali huo hana!

Kinyume chake ni kuwa ni Wazanzibari ndio wenye uhalali wa kutumia nguvu ya umma kuhakikisha kuwa madaraka yamo mikononi mwa kiongozi wanayemuamini na kwamba kiongozi huyo anayatumia kwa ajili yao. Na, kwa hakika hasa, rejea nzuri ya kujenga hoja ya uhalali huu wa Wazanzibari kutumia nguvu ya umma ni kauli ya Rais Mkapa mwenyewe katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Mei 2003.

Ni bahati mbaya sana kwamba Rais Mkapa ana nyuso zaidi ya moja. Kuna wakati huzungumza hivi, kila mtu akashawishika na hoja zake, lakini mara hugeuka vile, kila mtu akachoka naye. Kumbukumbu ya karibuni zaidi ni yale aliyoyasema katika jarida la Prospect la Uingereza katika mahojiano yake na Jonathan Power, kwamba kuna kundi ndani ya CCM Zanzibar lililo tayari kuuwa kubakia madarakani, lakini wakati huo huo analiruhusu kuendesha vitendo vya kijanjawidi. Pia ni yale aliyoyasema Marekani juu ya kusikitishwa kwake na mauaji ya 2001, lakini wakati huo huo anaapa kutumia nguvu za dola kupambana na nguvu ya umma. Sisi Wazanzibari hujiuliza: “Hivi kuna Mkapa wangapi?”

Basi katika hotuba hiyo ya 2003, Rais Mkapa alisema hivi: “Hapana mahala bora pa kuhifadhi madaraka ya nchi zaidi ya kwa wananchi wenyewe”. Maana ya kauli hiyo ni kuwa madaraka ya nchi yanachimbukia mikononi mwa wananchi na ni jukumu la wanaoyatafuta, wayapatie kutoka huko.

Kwa taratibu za kistaarabu, ndio ikaamulika kuwa madaraka hayo yapatikane kupitia kura za wananchi. Na ili ridhaa hiyo ya kura ihalalike, basi ni lazima iwe inatokana na mfumo wa uchaguzi huru, wa haki, ulio wazi na wenye kukidhi vigezo vya kidemokrasia. Wakati ni jukumu la wananchi kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa na sifa hizo, ni jukumu lao pia kuona kuwa aliyepata ridhaa yao, ndiye huyo huyo anayeingia madarakani kuwaongoza. Huo ndio uhalali wa kuingia madarakani. Na hiyo ndiyo maana ya kauli ya Mkapa wa Mei 2003!

Mkapa huyo, kwa hivyo, aliwataka wananchi wasibweteke tu, bali wahakikishe kuwa anayeshikilia madaraka ayapate kutoka kwao. Inapotokezea kwamba ameyapata kwengineko kokote kusiko kwao, basi huyo hana uhalali wa kuwa kiongozi wao. Hawana jukumu la kumtii wala wajibu wa kumheshimu. Kinyume chake, wana haki ya kumzuia asichukuwe uongozi huo, maana uongozi halali lazima utolewe na wao.

Sasa inashangaza. Rais Mkapa anawataka Wazanzibari, ambao ni sehemu ya wananchi aliowahutubia Mei 2003, wapewe kiongozi wao na Tume ya Uchaguzi tu, hata ikiwa wana uhakika kuwa tume hiyo haikusema ukweli. Waingereza huiita hii kuwa ni paradox. Anakiharamisha kwa hoja ya nguvu kile alichokihalalisha kwa nguvu ya hoja!

Ni halali kwa Wazanzibari, kama ilivyo kwa wananchi wa nchi nyengine, kuhakikisha kuwa anayechukuwa madaraka ya kuwaongoza ni yule tu waliyemkabidhi dhamana hiyo kupitia uchaguzi ulio huru, wazi, wa haki na wenye kutimiza viwango vya kidemokrasia. Ni halali kutumia nguvu yao, kama umma, kujenga mustakabali wa nchi na kizazi chao.

Kinyume chake ni kuwa ni haramu kwa ‘mwengine yeyote’ kuingilia kati maamuzi hayo ya Wazanzibari hata awe ni Benjamin Mkapa (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu), George Waitara (Mkuu wa Majeshi), Epson (Mkuu wa Usalama wa Taifa), au Omar Mahita (Mkuu wa Polisi). Hakuna mwenye uhalali wa kuwaamulia Wazanzibari nani awe kiongozi wao. Ni haramu kwa vigezo vyote vya kistaarabu!

Hilo ni katika kuingia madarakani. Lakini utumiaji wa nguvu ya umma unahalalika pia ikiwa yule aliyekabidhiwa madaraka hakuyatumia kwa maslahi ya umma, maana uhalali wa kubakia madarakani unatokana na kuyatumia madaraka hayo kwa ajili ya wananchi waliokukabidhi na si vyenginevyo. Katika hotuba hiyo ya Mei 2003, Rais Mkapa waliwaambia hivi Watanzania: “Uhalali wa kuitwa mheshimiwa ni utumishi na uwakilishi wa wananchi wote. Kiongozi aliyechaguliwa na wananchi anapoanza kulewa wadhifa wake, anaposombwa na hisia za ukubwa na kuwadharau waliomchagua, huyo uhalali wake upo mashakani…”

Na uhalali wa kiongozi upokuwa mashakani, uhalali wa wananchi wenyewe kumuwajibisha unakuwa wazi. Ni haki yao kufanya hivyo. Uhalali wa uongozi wa sasa Zanzibar upo mashakani, kwa kuwa nao umesombwa na hisia za ukubwa na kuwadharau Wazanzibari.

Mifano ni mingi sana, tutaje michache. Wazanzibari wana haki ya kuishi maisha mazuri, angalao kwa kiwango cha kupata milo mitatu kwa siku, maji salama, afya na elimu bora. Chini ya CCM, Zanzibar imekuwa na maisha magumu sana. Kama kiwango cha mwisho cha dharau, Rais wa Zanzibar anajikusanyia shilingi milioni saba kwa mwezi, huku Wazanzibari walio wengi wakikosa hata milo miwili kwa siku.

Wakati rais na aila yake wanakimiwa kila kitu na serikali na hata kutibiwa nje kwa pesa za Wazanzibari, watoto wachanga wa Kizanzibari wanakufa kwa kasi ya ajabu kutokana na ukosefu wa huduma nzuri za kiafya.

Wakati Mazizini (eneo wanalokaa viongozi wa serikali) kila mtu kajichimbia kisima chake kwa pesa za Wazanzibari, Sogea na mwenginemo muna maelfu wa Wazanzibari wanaokosa hata maji ya kupikia futari zao (kama wanazipata).

Wakati inachukuwa siku arubaini kupata mshahara wa elfu hamsini kwa wafanyakazi wa serikali, serikali hiyo hiyo imeliachia dhamana yote ya biashara ya mafuta Shirika moja tu la GAPCO na hivyo kila uchao mafuta yanapandishwa bei Zanzibar. Kila siku kiwango cha pato kinashuka na kila siku, kwa hivyo, maisha ya wananchi yanazidi kuwa mabaya.

Rais Mkapa, Wazanzibari hawa wamedharauliwa vya kutosha na uongozi ambao wewe uliusaidia kuingia madarakani bila ya ridhaa yao. Wazanzibari hawa wana haki ya kuishi maisha mazuri. Wazanzibari hawa, kwa hivyo, wana uhalali wa kuiwajibisha serikali hii kwa kutokusimamia jukumu lake. Na wewe huna uhalali wa kutumia nguvu za dola dhidi yao pindi wakiamua hivyo.

Wazanzibari pia wana haki ya kuishi maisha salama na huru, yaliyoepukana na hofu na wasiwasi. Katika miaka mitano iliyopita, CCM imeifanya Zanzibar kuwa pahala pa khofu zaidi kupaishi. Mwaka 2001 iliwafanya Wazanzibari waikimbie nchi yao kufuatia mauaji na utesaji wa waandamanaji wasio na silaha. Kuanzia mwaka 2004 imekuwa ikisimamia na kuendesha vikundi vya wahuni (Janjaweed) ambao huvamia majumba na biashara, wakachoma moto mali na kuwakata Wazanzibari kwa mapanga. Sasa Janjaweed wameanza staili mpya ya kuwateka nyara Wazanzibari (rejea mkasa wa Mzanzibari Zahor Shaaban (45) 12/10/2005 Jang’ombe).

Kwa hivyo, sio tu kwamba CCM imeshindwa kulinda usalama wa Wazanzibari, bali pia inashiriki kuuvunja na kupandikiza khofu na machafuko ndani ya jamii. Hili linawapa uhalali Wazanzibari hawa kuinuka na kuiwajibisha CCM, maana imewavunjia haki yao ya msingi ya kuishi maisha ya salama na mali zao na watoto wao. Na katika vigezo vyovyote vile, visivyokuwa vya ukosefu wa heshima kwa maamuzi ya wananchi, Rais Mkapa hana uhalali wa kuwamiminia watu hawa risasi pindi wakiamua kuiondoa CCM madarakani.

Ni haki ya Wazanzibari pia kuishi nje ya mipaka ya ubaguzi na unyanyasaji. Wana haki ya umoja, ushirikiano na heshima, licha ya tafauti za kiuzawa, kidini na, au, za kisiasa. Na hiyo ndiyo fahari ya Zanzibar. CCM imeipora haki na fahari hiyo. Badala yake, kwa kutumia mawakala wake waliotapakaa kila mahala katika vyombo vya dola, vya habari na taasisi za kiserikali na za kiraia, imewagawa Wazanzibari baina ya Waafrika na wasio kuwa Waafrika, Wapemba na Waunguja, Wakaskazini na Wakusini, CUF na CCM, CCM A na CCM B, Awamu ya Tano (SAT) na Awamu ya Sita (SAS) na hata baina ya Ahalilbaiti (royal family) na Ajnabi (wasiotokana na nyumba kubwa).

Ni halali kwa Wazanzibari kuiunganisha tena Zanzibar yao kuwa moja. Ni halali yao kuirudisha heshima yao. Ni halali yao kushirikiana kwa ajili ya Mama yao mpendwa, Zanzibar. Na Rais Mkapa hana uhalali wowote wa kuwalazimisha Wazanzibari waendelee kugawanywa kwa misingi ya uzawa, itikadi na imani zao za kisiasa. Hana uhalali huo. Hana!

Wacha nimalize kwa kusisitiza tena na tena kuwa Wazanzibari wana nia, sababu na uwezo wa kutumia nguvu zao, kama umma, kuhakikisha kuwa anayeshikilia madaraka ya kuiongoza hatima ya nchi yao ni yule waliyemkabidhi wenyewe. Na watafanya hivyo kwa njia za amani kabisa. Hawana bunduki wala mzinga, lakini wana dhamira ya kweli na wataishi kusimamia dhamira hiyo.

Naye Rais Mkapa naazidi kuongeza vikosi na silaha nzito nzito Zanzibar, kana kwamba visiwa hivi sasa vimekuwa uwanja wa kivita, ili aje awamiminie risasi za moto Wazanzibari kwa kusudi la kuyapinda maamuzi yao. Ajuwe tu kuwa atawakuta wenyewe Wazanzibari wakiwa wameshikana mikono pamoja, wakiimba wimbo wa George Shea wa African National Congress ya Afrika Kusini:

Front line, I know it is bitter but I like it
I like it because it is where I belong
For out of bitterness comes equality, freedom and peace
I will be in front line when the roll is called
Front line valleys and plains of events and history

Na hata kama wimbo huu hautazama katika mtima mwa mtawala mhafidhina kama Rais Mkapa – hata kama hataiheshimu haki ya Wazanzibari kuamua hatima ya nchi yao – lakini daima dhamira itamsuta na historia itairikodi ari na ibra ya Wazanzibari kupigania haki yao kwa njia za amani mbele ya mtutu wa bunduki. Na kisha, huko mbeleni, Wazanzibari watakaobakia baada ya wenzao kwisha kuuliwa na vikosi vya Rais Mkapa, watainuka wampandishe Rais Mkapa kizimbani kwa mashtaka ya uhalifu dhidi ya binaadamu!

Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Hali Halisi, Septemba 2005, chini ya kichwa “Kuna Mkapa wangapi?”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.