Ikiwa maneno ya Marehemu Mwalimu Julius Nyerere: ”Nje ya Muungano, hakuna Wazanzibari”; yalikuwa ya kweli, basi pia ni kweli kuwa ”Nje ya Dola, hakuna CCM” Hapa, Rais Mkapa amebainisha wazi kwamba uthubutu ilionao CCM, jeuri yake na kiburi chake ni kwa kuwa pana vyombo vya dola vimesimama na mitutu ya bunduki dhidi ya yeyote anayekihatarashia uwepo wake madarakani.

NINAHOJI kwamba aina yetu wa mfumo wa utawala tuiiteni Mkapakrasia. Mkapakrasia ni aina ya utawala uliojitenga sana na raia unaowaongoza kwa imani kuwa nguvu ya kukaa na kuondoka madarakani imo mikononi mwa jeshi, usalama wa taifa na polisi; na wala sio mikononi mwa umma. Miongoni mwa tabia kuu za aina hii ya utawala ni kiburi, jeuri na utumiaji mbaya wa vyombo vya dola dhidi ya raia.

Huu ni muakisiko wa miaka kumi ya uraisi wa Rais Benjamin Mkapa, ambayo imeoanisha baina ya uwezo wake wa kujenga barabara na madaraja kwa umahiri wake wa kuzalisha mayatima, wajane, wakimbizi na walemavu wa maisha. Yote kwa jina la dola.

Rais Benjamin Mkapa aliyeiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka 1995 hadi 2005.
Rais Benjamin Mkapa aliyeiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka 1995 hadi 2005.

Kilichotarajiwa ni kuwa, Rais Mkapa angelijutia namna uraisi wake wa miaka kumi ulivyochangia kuiviza demokrasia na kukandamiza haki za binaadamu. Tulidhani, akiwa mtu anayependa sana kujisifia nafasi yake kimataifa, basi angelitamani kupata “husnulkatima”, mwisho mwema. Maana, bila ya mwisho huo, zile ndoto za kuja kufanya kazi za kimataifa, zinaweza kufutika, na badala yake kumalizikia alipoangukia Jenerali Augustino Pinochet wa Chile.

Narudia. Damu imemwagwa. Wakimbizi wamezalishwa. Mama, wake na dada zetu wamenajisiwa. Ndugu zetu wameuliwa na mbele yetu sasa ni mayatima na wajane tulioachiwa. Yote hayo yamefanyika kwa jila la dola. Yote katika wakati ambao yeye, Benjamin William Mkapa, ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama.

Basi, tukadhani kuwa baada ya yote hayo, Rais Mkapa alipaswa kutamani kuiwacha nchi hii ikiwa katika hali ya amani na mshikamano, angalau kwa maana nyepesi ya maneno hayo. Kufanya hivyo, kungelitufanya sisi raia tumkumbuke kwa mema, si kwa mabaya yake.

Kumbe hizo zilikuwa ni dhana tu, na uhalisia uko pengine kabisa. Nukta ya mjadala hapa ni hii kauli yake aliyoitoa hivi karibuni katika hoteli ya New Africa, Dar-es-Salaam, kwamba atatumia uwezo wake binafsi na wa dola kuhakikisha kuwa CCM inashinda.

Mimi ni Mzanzibari, na hapa nazungumzia kutokea angle hiyo. Ndugu zangu Wazanzibari, kuliko wengine wowote, wanaujuwa uzito wa kauli hii ya Rais Mkapa, maana Zanzibar imekuwa muhanga mkubwa wa matumizi ya nguvu za dola katika kuhakikisha ushindi wa CCM.

Kwa kusema hivi, Rais Mkapa ametukumbusha mengi sana, ambayo vyenginevyo tungelikuwa tayari kuyasamehe hata kama si kuyasahau. Ametukumbusha roho zilizotoka, damu iliyomwagwa na hishima iliyovunjwa wakati nguvu ya dola ilipotumika dhidi ya wale, ambao kwa njia moja ama nyengine, wamekuwa wakionekana kuhatarisha nafasi ya CCM kuendelea kushikilia madaraka hapa.

Ametukumbusha ya Shumba Mjini, Micheweni-Pemba, mwanzoni mwa siasa za vyama vingi, 1992. Huko vyombo vya dola vilitumia nguvu zake kumpiga risasi na kumuua kijana Omar Ali Haji, aliyekuwa akipachika bendera ya Chama cha Wananchi (CUF). Huko kulikuwa ni katika kusimamia kauli ya Mkuu wa Wilaya hiyo wa wakati huo kwamba, asingeliruhusu bendera ya CUF kupepea katika wilaya yake. Ingawa baadaye bendera hiyo ilipepea, lakini ilipepea na roho ya mtu. Hili, hata kama lilitokea kabla ya yeye, Rais Mkapa, kuingia madarakani, lakini huo ukaanza kuwa mfano wa kuitumia dola kuhakikisha uwepo wa CCM madarakani.

Anatukumbusha ya Kilimahewa, katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2000. Kwa mara nyengine, nguvu za dola ziliuvamia umma uliokuwa hadhara ya CUF na kumimina risasi. Matokeo yake watu sita wakakatwa miguu kutokana na risasi hizo. Huo ni mwaka ambao tayari Rais Mkapa alishakuwa Amiri Jeshi Mkuu na akaleta hapa Zanzibar magari ya deraya na kuongeza vikosi vya polisi na jeshi vyenye silaha nzito nzito. Kwa kauli hii ya sasa, anatufanya tuunganishe kuwa, kumbe lengo lake la kuleta vikosi vile siku zile lilikuwa ni hili la kuhakikisha kuwa CCM inaendelea kubakia tena madarakani. Kwa gharama za damu ya Wazanzibari.

Hilo ndilo linalotupelekea kutukumbusha ya Januari 2001 ambayo, kwa hakika, hayana fahari yoyote kuyahadithia. Tusikumbushane ya kuuliwa Wazanzibari wenzetu 40, ya kunajisiwa mama na dada zetu, ya kuwekwa mayatima watoto wetu na kugeuzwa wajane mama zetu. Tusikumbushane haya, maana yanauma sana!

Lakini, kwa kutoa kauli aliyoitoa, kwa makusudi kabisa Rais Mkapa anatukumbusha hayo. Labda kutuonya kuwa yatajirejea. Silaha gani hii ya kisaikolojia! Anaturudisha nyuma kwenye kauli kama hii iliyotolewa na Waziri wake wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Profesa Philemoen Sarungi, akiwa Zanzibar Agosti 2004. Alichosema wakati huo Waziri Sarungi ni kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) halitavumilia watu wanaotaka kuuvunja Muungano wa Tanzania.

Wakati huo niliandika makala katika gazeti hili kufafanua maana ya kauli hiyo. Kwamba, kwanza, kwa watawala wetu, anayehatarisha Muungano ni yule anayezungumzia aina tafauti ya Muundo wa Muungano huo, kwa mfano, anayesema uwe wa serikali tatu badala ya huu wa mbili wa CCM. Pili, upande mmoja, tuna vyama vyengine visivyokuwa CCM na vyenye sera tafauti ya Muundo wa Muungano na, upande mwengine, tuna Wazanzibari walio wengi wasioridhika na muundo huu wa Muungano.

Katika uchaguzi unaokuja, kwa hivyo, Wazanzibari hawa kwa wingi wao wanaweza kukichagua chama kisichokuwa CCM ili kikidhi haja yao ya kuwa na aina tafauti ya Muungano. Sasa hapo, kwa mujibu wa kauli ile ya Waziri Sarungi na sasa hii ya Rais Mkapa, ni kuwa jeshi halitakubali hilo. Yaani jeshi halitakiruhusu chama kisichokuwa CCM kuingia na kuyashikilia madaraka.

Nadhani, ni katikati ya kumbukumbu kama hizo, ndio maana gazeti la Tanzania Daima katika toleo lake la Jumatatu, 21 Machi, 2005, likashauri katika tahriri yake kuwa ni bora pasiwe na uchaguzi. Kwamba madhali Rais Mkapa ameshaamua kuwa atatumia nguvu za dola kuhakikisha kuwa CCM inashinda, basi kwa nini tupoteze mabilioni ya shilingi, nguvu na wakati wetu, ilhali matokeo yake tayari yameshajuilikana? Si ni afadhali tu, Rais Mkapa alihutubie Taifa na kututangazia madiwani, wawakilishi, wabunge na hata Maraisi wetu wa Zanzibar na Tanzania?

Nimesema kuwa kwa Zanzibar kauli kama hii ya Rais Mkapa ina maana kubwa sana kwa kuwa yetu ni nchi iliyoathirika sana na utumiaji mbaya wa nguvu za dola dhidi ya matakwa ya raia. Ni kauli inayotupa sababu ya kuamini kuwa hata hii Operesheni Dondola iliyoanzishwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Omar Idi Mahita, ni katika mikakati maalum ya kuhakikisha kuwa CCM inashinda Zanzibar. Kwamba hawa ni polisi wanaoletwa Zanzibar sasa kama vile vikosi vilivyotumwa mwaka 2000.

Hata kama IGP Mahita anajaribu kutoa maelezo tafauti ya Operesheni hiyo, lakini ni operesheni inayokuja katika wakati ambao Amiri Jeshi Mkuu wa nchi ametoa kauli ya kutumia nguvu za dola kuhakikisha ushindi wa CCM. Vivyo ni wakati ambao hata yule anayetumia kiwango cha chini kabisa cha akili, anaijuwa nafasi ya CCM Zanzibar. Kwamba kurudi madarakani kwa njia ya kura ni kile wanachokiita Waingereza ’next to impossible’, zaidi ya kutokuwezekana.

Sasa, kwa nini tusihitimishe kuwa pana uhusiano baina ya azma ya Rais Mkapa ya kutumia nguvu za dola kuibakisha CCM madarakani na ujio wa Operesheni Dondola? Maana, kimsingi Zanzibar haina tatizo la usalama wala la upungufu wa walinda usalama. Tatizo la Zanzibar ni la hao walinda usalama waliopo kujihalalishia kuwa watumishi wa CCM badala ya kuwa watumishi wa umma. Hakuna upenyo wowote wa kufikiri kuwa vijana wa Operesheni Dondola wanatoka mbinguni na hivyo hawajaathirika na ukereketwa wa CCM, ambao wakubwa wao wameukumbatia. Nasema hakuna uwezekano huo!

Sasa, tuhitimishe makala hii kwa nukta hizi tatu: kwanza, kwa kushuhudia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin William Mkapa, amethibitisha kuwa bila ya nguvu za dola, basi Chama chake Cha Mapinduzi hakiwezi kusalia madarakani. Kauli yake inaunga mkono ile hoja ya wapinzani kuwa dola yetu ni ya kipolisi (police state). Kwamba vyombo vya dola (Usalama wa Taifa, Jeshi la Wananchi na Polisi) ndivyo ambavyo hutoa madaraka na kisha vikamlinda viliyemuweka madarakani.

Ikiwa maneno ya Marehemu Mwalimu Julius Nyerere: ”Nje ya Muungano, hakuna Wazanzibari”; yalikuwa ya kweli, basi pia ni kweli kuwa ”Nje ya Dola, hakuna CCM” Hapa, Rais Mkapa amebainisha wazi kwamba uthubutu ilionao CCM, jeuri yake na kiburi chake ni kwa kuwa pana vyombo vya dola vimesimama na mitutu ya bunduki dhidi ya yeyote anayekihatarashia uwepo wake madarakani.

Pili, kauli hii itutosheleze kuwa Rais wetu si muumini wa demokrasia, bali wa hiyo Mkapakrasia. Ni Mkapacratic. Anachoamini yeye ni nguvu, jeuri na kiburi cha dola juu raia. Ndio maana si jambo la ajabu kwake kutumia lugha kali na za kuripuka dhidi ya raia anaowaongoza, maana haoni hata kidogo kuwa nguvu na madaraka aliyonayo yamechimbukia mikononi mwa raia hao.

Mifano ni mingi sana. Mmojawapo ni kabla ya maafa ya Januari 2001, ambapo alitumia kila lugha ya kejeli kuzungumzia madai ya Upinzani Zanzibar, na hakuacha kufanya hivyo hadi pale vyombo vya dola vilipomtia aibu mbele ya jumuiya ya kistaarabu. Mfano mwengine ni vile alivyoviripukia vyombo vya habari mwaka jana, ambavyo kwa hakika vinabeba maoni ya umma, kuhusu suala la serikali yake kushindwa kupambana na rushwa. Huyo ndiye Rais Mkapa, na hiyo ndiyo Mkapakrasia!

Tatu, itudhihirikie sasa kwamba uchaguzi ’umeshachafuka’. Nasema ’umeshachafuka’, na sio ’utachafuka’, kwa kuwa kimahesabu tayari uchaguzi huu wa 2005 umeshafanyika. Kwamba uchaguzi haungaliwi kwa tukio moja tu la kutumbukiza vikaratasi vya kura kwenye kisanduku, bali mkufu mzima ambao una mambo mengi yanayotegemeana na kuathiriana. Hili la kauli ya Mkapa ni katika mambo hayo ambayo yanauhusu moja kwa moja uchaguzi huo na kwayo, wacha nithubutu kusema kuwa, Rais Mkapa ameshauchafua uchaguzi wenyewe.

Kwa nini? Kauli hii ya Rais Mkapa, akiwa kama kiongozi mkuu wa nchi na chama tawala, inavifanya vyama vyengine vilivyokuwa vimeshakusudia kushiriki katika uchaguzi huu kwa nia nzuri na imani kuwa maamuzi ya wapiga kura yatahishimiwa, ving’amue kuwa kumbe msamiati huo haumo kabisa kwenye kamusi la ushindi la CCM.

Inaufanya umma usiiamini tena kura yake. Kwamba hata baada ya kupiga kura, kauli hii inawatanabahisha wajuwe kuwa kuna nguvu za dola ambazo Rais wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu ameshaapa kuzitumia kuhakikisha kuwa Chama chake kinabakia madarakani. Tafsiri ya kauli hii ni kuwa Rais Mkapa anawataka wale wote watakaoingia kwenye uchaguzi huu wa 2005, watafaute njia nyengine za kuifanya kura yao iwe na maana, ikiwa kweli wanayataka madaraka – yaani wapambane na vyombo vya dola. Khalas!

Sote tunayajuwa matokeo ya mapambano kati ya nguvu za dola na nguvu za umma. Bila ya shaka, dola hushindwa, lakini ni kwa gharama kubwa sana ya kupotea kwa maisha, mali, utu na hishima. Hakuna mstaarabu yeyote anayelipendelea hilo. Na naamini kabisa, Rais Mkapa ni mstaarabu sana, hashindwi kulijuwa hilo.

Anajuwa kuwa, hasa kwa Zanzibar, nafasi ya kuuharibu uchaguzi huu kwa makusudi ya kutegemea kuja kusaini Muwafaka mwengine ni finyu sana. Ameshaelezwa hivyo si mara moja wala mbili. Kwa hivyo, kilichopo pekee ni ama kuuwachia umma kufanya maamuzi yake na kuyahishimu maamuzi hayo, au ni kuitumbukiza nchi hii katika maafa ambayo Tanzania na nchi zote za Maziwa Makuu zitapata athari yake.

Sasa, baada ya yote hayo, kwa nini Rais Mkapa anataka kuigonganisha tena dola na umma? Tuseme hakutosheka na wale wakimbizi waliozalishwa na serikali yake mwaka 2001, na sasa ana hamu ya kuzalisha wengine? Hakutosheka na damu iliyomwagwa na vikosi vyake vya ulinzi na usalama, na bado anataka damu nyengine? Hakutosheka na ile hishima ya mama na dada zetu iliyovunjwa kwa kunajisiwa, bado anataka ivunjwe zaidi? Hajatosheka na mayatima na wajane, bado anawataka wengine?

Kwa mara ya kwanza makala hii ilichapwa katika gazeti la Rai, Na. 599, la Machi 31-  Aprili 6 2005

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.