KAULI ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Prof. Phelomon Sarungi, kwamba Jeshi la Wananchi wa Tanzania halitawavumilia wale wote wenye lengo la kuuvunja Muungano inatisha. Nasisitiza matumizi ya neno ‘kutisha’ maana ni neno hilo hasa ndilo ninalokusudia kulitumia katika makala hii.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi la tarehe 22 Agosti, 2004, Prof. Sarungi alisema kuwa Muungano na JWTZ ni watoto pacha, kwa hivyo Jeshi (ambalo hapa litakuwa ni Kurwa) halitavumilia kuona Muungano (Doto) unahatarishwa. Hiyo ilikuwa siku ya tarehe 20 Agosti 2004 huko Unguja Ukuu (na sio Zanzibar Mkuu kama baadhi ya vyombo vya habari vilivyoiita) katika shamrashamra za miaka 40 ya Jeshi hilo.

Uzoefu unatuonesha kuwa kila mara watawala wetu, hasa kutoka Tanzania Bara, wanapouzungumzia Muungano katika muktadha wa Uzanzibari, Wazanzibari na au Zanzibar, basi huamua kuijaza hadhira yao khofu za kuvunjika kwa Muungano huu na hatari inayoweza kutokea.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Phelomon Sarungi (kulia).
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Phelomon Sarungi (kulia).

Kwa uchache, hii ni mara ya pili katika mwaka huu kwa kauli kama hii kutolewa Zanzibar. Katika mwezi wa Aprili kwenye sherehe za miaka 40 ya Muungano zilizofanyika kitaifa katika uwanja wa Amaan, Zanzibar, Rais Benjamin Mkapa alisema maneno yanayopishana kidogo na hayo kisintaksia lakini yanayofanana sana kisemantiki.

Alionesha kuwa kuna watu wanaouangalia kwa jicho baya Muungano wetu na kwamba yeye, akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atahakikisha anayatumia madaraka aliyopewa kuulinda Muungano huu.

Wacha niseme tena na tena kwamba hapa pana upotoshaji wa makusudi wa hoja hii. Wanapojibu maswali, kwa mfano, ya nini maana ya kuvunja Muungano na nani anataka kuuvunja Muungano huo, watawala wetu huenda mbali kabisa na ukweli. Hufanya upotoshaji wa makusudi ili kuhalalisha vitisho vyao dhidi ya raia wanaohoji.

Kwa watawala, kuuvunja Muungano kunamaanisha kupinga muundo uliopo wa Muungano. Kwa sasa, muundo ‘unaoambiwa’ upo kwa miaka yote hii 40 ni wa serikali mbili. Nasema ‘unaoambiwa’ kwa kuwa akina mimi tunaushuku huo u-wili wa serikali hizo mbili hapa. Tunachokiona mbele yetu, kwa hakika kabisa, ni kiwango kimoja tu cha userikali – Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Tunapoiangalia Serikali ya Zanzibar na kuifasiri serikali kama chombo kikuu cha utawala kilichokabidhiwa khatma ya watawaliwa, basi hatuoni kuwa SMZ ndiyo inayoamua khatma ya Wazanzibari. Tunaamini, tena kwa ushahidi kabisa, kuwa khatma ya Wazanzibari, Uzanzibari na Zanzibar inaamuliwa Chimwaga.

Na mifano ya hilo iko mingi, inatosha kujaza kitabu cha kurasa alfu moja. Wa zamani kidogo ni ule wa kuondoshwa Mzee Abuod Jumbe Mwinyi katika nafasi ya urais wa Zanzibar na Mwalimu Nyerere, katika miaka ya ‘80. Hadi leo Wazanzibari wanajiuliza Mwalimu Nyerere alikuwa na mamlaka gani, kisheria, ya kumuondosha Rais waliyemuweka wenyewe!

Wa karibuni kidogo ni huu wa kupatikana mgombea Urais wa Zanzibar wa mwaka 2000. Hadi leo Wazanzibari wanajiuliza mipaka ya mamlaka na madaraka yao kwa nchi yao inaanzia wapi na kumalizikia wapi ikiwa hawathubutu hata kumuweka mgombea wanayemtaka wenyewe, sambe rais wao!

Lakini, kwa kutumia wasta wao walionao, nyenzo za kila aina za habari na uenezi, pamoja na nguvu kubwa waliyonayo kufanya mambo yawe vile wanavyoyataka, watawala wetu wamefanya ionekane kuwa kuukosoa muundo wao wa Muungano wa Serikali Mbili, ni kufanya hila za kuuvunja Muungano. Hawasemi kabisa kwamba watu wanapinga ‘muundo’ tu wa Muungano, bali husema wanapinga Muungano wenyewe.

Nauita huo kuwa ni upotoshaji wa makusudi wa hoja, nao ni miongoni mwa mambo yanayoufanya uhusiano huu baina ya Tanganyika na Zanzibar kuwa ni kizungumkuti. Ndio unaoonesha kuwa pana ‘siasa maalum ya Muungano kuelekea Zanzibar’ na ndio unaotilia shaka na shukuki dhamira ya watawala wetu.

Ndio maana, kwa kuwa watawala wamekuwa wakitaka ieleweke kuwa kuukosoa muundo wao wa Muungano ndiko kuuvunja Muungano, basi linapokuja swali la nani, kwa hivyo, anayetaka kuuvunja Muungano, jibu huwa ni yule anayeukosoa muundo wao.

Na kwa kuwa mtiririko wa matukio katika historia hii ya miaka 40 ya Muungano, unaonesha kuwa ni Wazanzibari ndio walioibuka kama wakosoaji wakubwa wa muundo huu, basi ni wao ndio wanaoonekana kutaka kuuvunja Muungano.

Ni kweli kuwa mifano ya harakati za Wazanzibari kuukosoa muundo huu iko mingi, kuanzia 1964 hadi sasa 2004. Nyuma, mwishoni mwa miaka ya ’60 na mwanzoni mwa miaka ya ’70, kulikuwa na Mzee Abeid Amani Karume mwenyewe. Yeye ndiye aliyekuwa mpinzani mkubwa wa muundo wa Muungano unaoigeuza Zanzibar kuwa koloni la Tanganyika. Kila siku alikuwa na shakashaka juu ya vile mwenzake, Mwalimu Nyerere, alivyokuwa anampelekesha.

Kisha ukaja wakati wa Mzee Abuod Jumbe. Upinzani wake wa muundo huu, ndio uliopelekea kulazimishwa kujiuzulu na Mwalimu Nyerere (kama nilivyotangulia kutaja hapo juu). Kisiasa, wakati huo uliitwa wa ‘Kuchafuka kwa Hali ya Kisiasa Zanzibar’.

Kuondoshwa kwa Mzee Jumbe kulifuatiwa na kipindi kifupi cha Mzee Ali Hassan. Yeye alikaa kwa muda mchache na, bila ya shaka, alikuwa amebanwa na woga kwa kile kilichomuondosha mtangulizi wake. Hata hivyo, Mwalimu Nyerere alikuwa amelegeza kamba yake kidogo kwa Zanzibar na, kwa hivyo, hapakuwa na mtikisiko mkubwa wa wazi wazi.

Lakini aliyemfuatia, yaani Mzee Idris Abdulwakil, alikuwa kama alivyokuwa Mzee Karume na Jumbe. Kuna matukio mingi yanayoripotiwa kuhusu namna alivyopingana waziwazi na wakuu wa Dodoma. Mara nyingi ilipotokezea kuizungumzia Zanzibar mbele ya Muungano, alikuwa akisema mwenyewe na sio kumtuma waziri wake.

Na hata ilipotokezea kuwa amedharurika na hivyo waziri wake kuchukuwa nafasi hiyo, yeye alithibitisha kwamba huo ndio uliokuwa msimamo wa serikali yake. Hakuwahi kuwa msaliti wala mwoga kwa hilo. Na kwa hakika hasa, ni sababu hiyo ndiyo iliyomfanya asisimame tena kugombea Urais kwa mara ya pili pale mwaka 1990, kama ulivyo utamaduni uliojengeka wa rais kukaa vipindi viwili.

Ni ndani ya wakati wake pia, aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake walipofukuzwa CCM na Mwalimu Nyerere kwa hilo hilo la kupingana na muundo wa Muungano.

Ya Awamu ya Tano, wakati wa Dk. Salmin ni ya karibuni zaidi na wengi tunayakumbuka. Jitihada za kujiunga na OIC, jaribio za kubadilisha katiba, mbali na mikwaruzano mingi kati yake na Dodoma zilikuwa ni katika harakati za kivitendo kupingana na aina ya muungano tuliyonayo.

Kwa hivyo, mtiririko huo unaonesha kuwa ni kweli kuwa Wazanzibari wamekuwa wakipingana na muundo uliopo wa Muungano kwa siku nyingi sana. Lakini, si kweli hata kidogo kuwa mtiririko huo unaonesha kuwa wamekuwa wakiupinga Muungano wenyewe. Wangelikuwa hawautaki, usingelikuwepo kitambo mno.

Turudi tena kule tulikoanzia, kwenye kitisho cha Profesa Phelomon Sarungi dhidi ya ‘wavunja Muungano’. Ninarudia tena kuwa Waziri huyu wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ametoa kitisho – kitisho cha kutumia jeshi kuhakikisha kuwa Muungano unadumu. Hiki ni kitisho sio tu kwa wakosoaji wa Muungano, bali pia kwa uhuru, demokrasia na udugu wetu. Kwa nini?

Kwanza ikumbukwe kuwa Profesa Sarungi ni Mbunge wa CCM na Waziri wa Ulinzi katika serikali ya CCM, chama ambacho Muundo wa Serikali Mbili ndiyo sera yake. Yeye, kwa chama chake hicho na nafasi yake hiyo, ni miongoni mwa wanaounda tabaka la watawala, ambao wameamua kuaminisha kuwa kuukosoa muundo wao wa muungano ndiko kuvunja muungano na ambako, kwa mujibu wa Profesa Sarungi, hakutavumiliwa na jeshi.

Pili, Wazanzibari walio wengi hawajapata kuridhika na muundo huu wa Muungano. Zanzibar, kama ilivyo kwa Tanzania nzima, kuna vyama vyengine vya siasa visivyokuwa CCM na vyenye sera tafauti ya muundo wa Muungano. Matarajio ni kwamba vyama hivi vitashiriki katika uchaguzi mkuu wa 2005 na inawezekana kwa kutumia uhuru na demokrasia yao, Wazanzibari kuamua kukiunga mkono chama kisichokuwa CCM ili kiwasaidie kubadili muundo huu wa Muungano.

Na kwa hivyo, ikiwa kwanza na pili hapo juu ni sahihi, basi mtiririko huo ukijumlishwa na kauli ya Profesa Sarungi unatupelekea katika hitimisho moja tu, nalo ni kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania halitakubali kuwaona Wazanzibari wakikiweka chama kisichokuwa CCM madarakani.

Kwa hitimisho hili, nikiwa kama Mzanzibari, siwezi kujizuwia kusikitika kwa ombwe na ombolezo kwamba Mama yangu Zanzibar anataka kuingizwa katika maafa mingine. Kwa mara nyingine tena, historia ya nchi yangu inataka kuchafuliwa kwa makusudi na, kama ilivyokuwa huko nyuma, mara hii pia si kwa maslahi ya Mzanzibari yeyote – si kwa aliye madarakani, wala aliye nje ya madaraka, wala kwa wa jana, wala kwa wa leo, na wala kwa kesho!

Siku zote khofu za Wazanzibari ni uingiliaji kati kutoka Bara. Na wana kumbukumbu nyingi za hayo, ya karibuni zaidi ikiwa ni mauaji ya Januari 2001. Si uzushi kwamba vikosi vingi vililetwa Zanzibar kutokea Bara na yale matukio yaliyoripotiwa ya ubakaji na udhalilishaji mwengine yalipata baraka zote kutoka huko.

Hakuna yeyote ambaye angelipenda picha zile zijirejee. Hakuna linalolitia uchungu kuliko kumuona mkeo au mwanao akinajisiwa mbele ya macho yako. Sote tunalaani yale yanayotokea Darfur hivi sasa, maana yanafanana sana na haya. Wazanzibari wasingelitaka kupelekewa Janjaweed.

Lakini je, kwa kutokutaka huko, ndio Wazanzibari walazimike kutokukiweka chama chengine chochote kisichokuwa CCM kushika madaraka ya nchi yao? Ikiwa ni hivyo, basi kuna tafauti gani baina ya kuwa nchi huru na kuwa koloni? U wapi uhuru hapo? I wapi demokrasia? U wapi utu na u wapi udugu?

Pengine nimekwenda mbali mno katika kuifafanua kauli hii ya Profesa Phelomon Sarungi. Lakini labda nawe ungelijiweka katika nafasi kama yangu, ya kuwa Mzanzibari, kisha ukaayangalia madonda yote ambayo historia imekutia katika kiwiliwili chako. Nina hakika ungeliuhisi ule mtonesheko wake. Ungeliuhisi uchungu wake. Ungeliumia kama ninavyoumia.

Nasisitiza kuwa utumiaji nguvu wowote ule hautaifaidisha chochote Zanzibar na kwamba hautasaidia kuuimarisha Muungano wa Tanzania. Muungano huu utadumu tu ikiwa utakuwa na nafasi katika nafsi za watu wenyewe, yaani ikiwa utazitosheleza nafsi zao na kujibu maswali yao. Jeshi, mizinga, risasi na vyenginevyo, haviwezi kuusimamisha ikiwa watu watakusudia kuuangusha.

Kwani historia iliwahi kushuhudia Muungano imara zaidi ya ule wa Kisovieti? Kuna Muungano gani uliokuwa ukilindwa na jeshi imara zaidi yake? Leo hii uko wapi? Na huko ambako bado Urusi inaendelea kung’ang’ania (kama Chechenya) kunatokea nini kila siku? Si maafa tu, misiba na vilio?

Hata hivyo, kama nilivyokwishaonesha kuwa kinachokosolewa na Wazanzibari sio Muungano wenyewe. Kama kuna yeyote anayeuthamini Muungano huu, basi ni Wazanzibari. Kinachokosolewa hapa ni muundo tu wa Muungano. Tungetaka kuwa na Muungano wa kiadilifu na ulio wazi zaidi na sio wa hila na kizungumkuti hiki.

Makala hii ilichapwa kwanza katika gazeti la Rai na kisha kurejewa katika An-Nur kwenye mwezi Septemba, 2004. Mwandishi hakumbuki namba za matoleo wala tarehe hasa ambazo makala hii ilipotoka.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.