NITANGULIE kusema kwa kuwa mawaziri ndio wawakilishi wa serikali, na kwa kuwa utumishi wao huitwa uwajibikaji wa pamoja, basi na majibu wanayoyatoa kwenye Baraza la Wawakilishi huwa ndio kauli ya pamoja ya serikali iliyo madarakani. Na, kwa hivyo, tunapozungumzia majibu haya mazuri, huwa ni majibu ya serikali kwa umma inauongoza.

Na kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyo, basi nataka niseme kuwa pamoja na majibu mazuri ya wahishimiwa mawaziri wanaohusika na Utalii na Habari yaliyotolewa hivi karibuni katika kikao kinachoendelea cha bajeti, nami nina jibu (sio swali) jingine la nyongeza!

Mawaziri hawa, katika nyakati tafauti lakini katika hamasa na muktadha unaofanana, walitekeleza wajibu wao wa kuitetea serikali wanayoitumikia kwa kujifakharisha kwa lisilo fakharishika! Ndiyo, si fakhari hata kidogo kwa serikali iliyopo madarakani kuzichukulia haki za raia wake kama ile ya kuandamana kuwa ni kisibu na kosa.

Kwa mfano, waziri anayehusika na utalii alipokuwa akijibu swali lililotaka kujuwa sababu zinazoweza kupunguza watalii hapa Zanzibar, alisema kuwa miongoni mwa sababu hizo ni ufanyaji wa maandamano bila ya kibali.

Naye Waziri anayehusika na Habari katika Afisi ya Waziri Kiongozi akijibu swali lililohusu vitendea kazi vya Televisheni Zanzibar huko Pemba, alitaja miongoni mwa vifaa hivyo ni kamera moja iliyovunjwa na waandamanaji wa Januari 27, 2001. La muhimu zaidi ni kuwa aliwanasihi wahishimiwa wawakilishi wa upande wa upinzani waisaidie serikali yake kuhakikisha kuwa mara nyengine mali zake hazihujumiwi katika hali kama hiyo ya maandamano.

Bila ya kuathiri chochote katika majibu hayo mazuri ya wahishimiwa mawaziri hawa, nakusudia kuliongeza suala la wizi wa kura katika majibu yote mawili. Nakusudia kusema kwamba kwa mfano, mara baada ya Waziri anayehusika na Utalii kutaja kuwa sababu mojawapo ya kupunguwa kwa watalii ni maandamano yasiyo na vibali, basi alikuwa amalizie kwa kusema kuwa maandamano hayo husababishwa na wizi wa kura.

Na, kwa hivyo, angeliuorodhesha wizi wa kura kuwa ni mongoni mwa sababu za msingi za kukimbiwa na watalii. Maana kura za wananchi zikiibiwa, waliobiwa hawatakubali. Nao huwa wana njia nyingi za kuonesha kutokukubaliana kwao na wizi huo, mojawapo ni hiyo ya kuingia mabarabarani kuandamana.

Hayo ndiyo yatakayoitwa maandamano haramu, yasiyo kibali. Na ni hapo anapoingia Waziri anayehusika na Habari katika nyongeza hii ya jawabu. Kwamba ikiwa watu wake watakwenda katika maandamano kama hayo (huku waandamanaji wakiwachukulia kuwa ni mamluki wa mwizi wa kura zao) basi hawatawastahmilia.

Hii ni kwa kuwa utendaji kazi wa TVZ unafanana zaidi na taasisi ya habari na uenezi ya chama tawala. Kwa hivyo, kwa kudhani kwamba wakiwavunjia vitendea kazi vyao ndio wanakikomoa chama tawala, ambacho ndio mtuhumiwa mkuu hapa, basi waandamanaji hawa wanaweza kuongozwa na hasira (na sio busara) kufanya kitendo kama hicho.

Ndio maana ikawa ni muhimu kwa waziri huyu, pamoja na jibu lake zuri la kuwanasihi wawakilishi wawaase watu wao kutoharibu mali za serikali, kuiasa pia serikali hiyo ihakikishe kuwa wizi wa kura za wananchi hautokei katika hali na hatua yoyote ile!

Na ni rahisi mno kuelewa mantiki ya kuweka nyongeza hii ya wizi wa kura katika majibu mazuri ya wahishimiwa mawaziri hawa. Kwamba kama kura hazitaibiwa, basi ni wazi kuwa hapatakuwa na maandamano yasiyo na vibali.

Serikali haitakuwa na sababu za kuyatangaza maandamano yoyote yale kuwa ni haramu kwa kuwa haitakuwa na la kukhofia kwayo. Maana maandamano huitwa haramu na serikali kwa kuwa ina kile kinachoitwa maandamano phobia, yaani woga wa maandamano. Woga huu hutokana na utoadilifu wa watawala, ambao hujitisha kwamba ile misururu ya waandamanaji inaweza kukosea njia na kuelekea ikulu kwenda kuwawajibisha kwa utoadilifu wao.

Pasipokuwa na maandamano kama hayo, basi pia hapana upenyo wowote ule wa kuvunjwa kwa kamera za TVZ, kwa upande mmoja, na wala watalii kuikimbia nchi yetu, kwa upande mwengine. Ni kwa mantiki hiyo ya kuzuia maafa yanayoweza kufuatiwa na wizi wa kura, ndio maana wahishimiwa mawaziri hawa walipaswa kulitaja hili katika majibu yao mazuri ili kuonesha namna wanavyowajibika kwa nchi yao.

Kiongozi mwenye kuiwajibikia kweli nchi yake huweka maslahi ya umma mbele ya chochote kile, hata mbele ya cheo, jina na satwa yake. Maslahi ya umma ni pamoja na amani na usalama wao ukiachilia mbali ustawi na maisha yao.

Hapa petu uzoefu unatuthibitishia kuwa uchaguzi ndio fitna kubwa inayoyaondosha yote hayo. Kila tunapokaribia uchaguzi, ndipo amani inapozidi kutoweka, tunapokuwa katika uchaguzi, salama huharibika na hata tunapomaliza uchaguzi, huwa tayari ustawi wa maisha umeshadamirika.

Kwa hivyo ni uchaguzi tu, kuliko jambo jengine lolote lile, ndio unaoiweka nchi yetu katika hali ya kutotangamaa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Uongozi makini na unaoaminika ungelichelea hayo yasitokee. Nayo, kwa hakika, yanaweza kuepukwa kabisa ikiwa kitafanyika kitu kimoja tu, nacho ni kuuwacha uchaguzi kuwa huru, wa wazi na wa haki. Ni kuzuwia wizi wa kura za wananchi tu, basi!

Sote twajuwa kuwa ujambazi wa kura ni mbaya zaidi kuliko ujambazi wa kupora mali za watu. Nakusudia kusisitiza kwamba ujambazi wa kura una hatari zaidi kwa kuwa athari zake zinakwenda mbali mno, kwa kasi mno na kuwagusa watu wengi mno na kwa wakati mmoja. Kwamba hata huo ujambazi wa mali husababishwa na ujambazi wa kura, ni jambo linaloweza kuthibitishwa pasi na tone lolote la shaka. Kwa nini na kwa vipi?

Nichukulie mimi kuwa ni kiongozi niliyeingia madarakani kwa kuiba kura na ambaye kipindi changu cha uongozi ni miaka mitano tu. Ili kufika kwangu pale, ilinilazimu kuwekekeza mtaji mkubwa wa nguvu, ghilba na magube. Bila ya shaka, huo si mtaji ambao ningeliweza kuumudu peke yangu. Nilipaswa kuwa na timu kubwa na madhubuti ya kiufundi ikiwajumuisha watu wenye dhamana katika vyombo vya ulinzi na usalama, mahakama, mawizara na mwenginemo.

Hao wote, mwisho wa siku, wanatarajia (na kwa hakika wanastahiki) kufurahishwa. Furaha yao ni vyeo, mapesa na kudekezwa. Kwamba wao ndio walionisaidia kuiba, sasa napaswa kuwatunza ili nao wanitunzie wizi huo. Vyenginevyo, wanaweza kunigeuka.

Hii maana yake ni kuwa sitakuwa na muda wa kutosha kuijenga nchi, bali kulipa fadhila za kusaidiwa kuiba kura. Huko ndiko kusahau muawana na muamana wa nchi, ndiko kutupa majukumu ya msingi kapuni na, hivyo, ndiko kuporomoka kwa uchumi na kufujika kwa jamii.

Unapoporomoka mfumo wa kiuchumi, kwa upande mmoja, na ule wa kijamii, kwa upande mwengine, ndipo wimbi kubwa la wasio ajira, wasio maadili na wasio matumaini linapounganika kuunda muhimili wa uovu katika nchi. Matokeo yake ndiyo hayo ya wavuta unga, machangudoa, na, bila ya shaka, majambazi.

Hiyo ni njia moja tu ya kuithibitisha nadharia ya uwana wa ujambazi wa mali na ubaba wa ujambazi wa kura. Ni rahisi pia kuthibitisha tena kwa kutumia njia nyengine.

Chukulia tena kuwa mimi ni kiongozi nilyeiba kura kuingia madarakani. Niliowaibia kura zao hawanitambui na wanataka kila mtu afahamu hivyo. Ubinaadamu wangu lazima utanipa kibri cha kutaka kuuhalalisha uharamu wangu kwa njia yoyote ile, fa-amma fa-imma.

Matokeo ni kwamba natumia nguvu kubwa zaidi hivi sasa nikiwa madarakani kuliko zile nilizotumia wakati wa kuwaibia kura zao. Yaani katika kipindi changu cha miaka mitano hiyo, muda wangu mwingi unatumika kupambana na wale wanaoniona na kuniita kuwa ni mwizi wakura kuliko ule ninaoutumia kuleta maendeleo kwa watu wangu.

Hilo lazima litaniingiza katika uvunjaji wa haki za binaadamu. Na kwa kuwa nchi hii ni tegemezi, na kwa kuwa wafadhili wameamua kuliweka suala la haki za binaadamu kuwa miongoni mwa vigezo vyao vya kutufadhili, na kwa kuwa niliowaibia kura zao ni mahodari mno wa kulitumia jukwaa la kimataifa, basi ni wazi kuwa watanipaka matope mno huko kwa wakubwa.

Kwamba hakuna mfadhili hata mmoja anayekubali kuzichukuwa pesa za kodi za watu wake na kumsaidia mwizi, vyenginevyo iwe mfadhili huyo ananufaika na wizi huo. Mfadhili asiyefaidika na wizi wa kura hana haja ya kumsaidia mwizi wake.

Hilo likitokea litakuwa na maana moja tu, nayo ni kususiwa na wafadhili. Nako ni kuuporomoa uchumi. Nako ni kuzidi kuichafua hali ya maisha. Nako ni kuongeza wimbi la uhalifu mitaani. Sasa, kwa kuwa nitataka kuwasuta wale wote wanaoniona mimi kuwa mwizi, basi nitafanya kila namna ya kulithibitisha suto langu. Kubwa zaidi ni kutaka kuiba tena katika uchaguzi ujao, na pengine mara hii kisayansi zaidi, ili kuwadhihirishia kuwa mimi ni mtu wa watu. Mduara wa wizi wa kura utaendelea, na zile athari zake zitajirejea.

Ndiyo. Vile alivyosema Mwl. Julius Nyerere kuwa mla nyama ya mtu hawezi kuacha, nami nasema kuwa mwizi wa kura za wananchi hakomi, bali huendelea na kuendelea tu. Akishaiba mara ya kwanza akafanikiwa, basi huutumia muda wa miaka mitano awapo madarakani kutayarisha sababu na mazingira ya wizi mwengine. Hujitengenezea fursa za kuiba tena. Na kuumba mazingira ya wizi wa kura ni kazi rahisi tu kwa kiongozi aliyepo madarakani. Anacholazimika kukifanya ni marejeo madogo tu katika somo lililotangulia kisha akapanga hisabati yake kiulaini. Ni kuzidisha kwa mbili au tatu, kutokugawa na chochote na kujumlisha matokeo ayapatayo.

Kwa mfano, kama mara ya mwanzo alitumia vikosi vitatu vya ulinzi kumsaidia wizi wake, basi mara hii sita. La kufanya ni kuongeza bajeti ya ulinzi na usalama katika nchi. Na ikiwa fedha za kufanya hivyo hapana, ni kupunguza kutoka wizara nyengine tu. Lengo ni ushindi tu. Kama mara iliyopita kuliikuwa na jimbo lililoleta upinzani mkali, mara hii ni kuamrisha Tume ya Uchaguzi wakalikata jimbo hilo au wakalichanganya na jimbo jengine lililo salama kwake. Kama katika uchaguzi uliopita kuna viongozi fulani wa upinzani walimchachafya, mara hii ni kuwasukia kesi na kuwasweka ndani kabla ya uchaguzi wenyewe.

Hata kama matokeo ya hayo yatakuwa ni ghasia, vurugu, uhalifu na kupotea kwa utangamano wa nchi, haitadhuru kitu kwake ikiwa lengo lake la kubakia kuwapo madarakani litafanikiwa. Wanasema katika kiwango kama hiki, kiongozi huwa anaamini moja tu: power, power by any means! Kwamba ni kawaida ya mwizi kutokuchelea matokeo mabaya yanayotokana na wizi wake, almuradi tu awe amekipata kile alichokitafuta. Lau ingelikuwa wizi wote wanajifunza kwa matokeo mabaya ya wizi wao, yakiwemo yale yanayowapata wenyewe binafsi, basi leo hii tusingelisikia tena hadithi za wizi kuchoimwa moto wala jela zetu zisingelifurika.

Na mwizi wa kura naye hawezi kujifunza kwa mifano mibaya kama ile ya akina Robert Guei wa Ivory Coast au Edward Schwerdnaze wa Georgia. Ikiwa kuna mfano wowote anaoweza kuuchukulia kuwa funzo kwake, basi ni ule wa George Bush wa Marekani au Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Sasa kwa kuwa uzoefu unaonesha kuwa wanaoweza kujifunza haraka kutoka na mifano mibaya kama hiyo ya wizi wa kura ni wapiga kura wenyewe, na kwa kuwa wapiga kura hawa wanaweza kufanya kile walichokifanya wenzao wa Georgia na Ivory Coast, basi ushauri pekee unaofaa kutolewa kwa wakati huu ni kuachana kabisa na azma ya kuiba kura.

Basi, pamoja na majibu yale mazuri ya wahishimiwa mawaziri hawa, wanapaswa kuanzia sasa kuwahamasisha wenzao katika serikali, katika Baraza na katika vyama vyote vitakavyoshiriki chaguzi zijazo, kuufuta kabisa msamiati wa kushinda kwa kuiba kura katika makamusi yao. Hilo likiwezekana, salama itapatikana na jibu litakifu swali!
______________________________________________________
Makala hii ilichapwa katika gazeti la Rai la mwaka 2004

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.