NIMETUMIWA ujumbe katika simu ya mkononi usemao: “you can not eat your cake and have it, soma e-mail.” Nilipofungua akaunti yangu ya barua-pepe, nikakuta ufafanuzi wa ujumbe huo. Kumbe nilikuwa nasutwa kwa kuandika makala iliyopita katika safu hii.

Nikumbushe kuwa katika makala hiyo, nilikuwa nimempa heshima yake mkereketwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hapa Zanzibar, Mohammed Raza Dharamsi, kwa uthubutu wake wa kuitetea Zanzibar dhidi ya ukandamizwaji inayofanyiwa kwa jina la Muungano.

Nimesutwa kwamba nilikwenda mbali mno katika kuipa maana hatua ile ya Raza. Kwamba aidha nilikuwa ninamkuza sana asivyostahili au nimepotosha kile ‘hasa’ alichokikusudia. Nimehojiwa pia kwamba nahalalisha bendera ya Zanzibar hali nikijuwa vyema kwamba kuwepo kwake ni hatari kwa Muungano.

Picha maarufu inayoitwa "ya utiaji saini Hati za Muungano" baina ya Rais Abeid Karume (kulia) na Mwalimu Julius Nyerere (kushoto). Ni kweli Karume alisaini Makubaliano ya Muungano kama yanavyotekelezwa leo na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?
Picha maarufu inayoitwa “ya utiaji saini Hati za Muungano” baina ya Rais Abeid Karume (kulia) na Mwalimu Julius Nyerere (kushoto). Ni kweli Karume alisaini Makubaliano ya Muungano kama yanavyotekelezwa leo na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Nikaambiwa kuwa mimi na Raza hatuwezi kuizungumzia Zanzibar kama nchi baki, huku tukijuwa kuwa ilijiingiza kwa hiari yake kwenye Muungano. Kwamba hatuwezi kuzungumzia Zanzibar yenye nguvu zaidi – au kwa maneno yake “Zanzibar iliyo Zanzibar zaidi ya hivi ilivyo sasa” – halafu wakati huo huo tukasema tu waumini wa Muungano. Huko, mbali ya kuwa ni kwenda kinyume na katiba, bali pia ni utoto wa kuila keki yetu, kisha tukataka tubakie nayo!

Ukweli ni kuwa makala hiyo inayozungumziwa haikuwa imejikita hasa katika bendera ya Zanzibar wala kuonesha upinzani kwa Muungano. Nilichojaribu kufanya ni kuonesha mshikamano wangu na Mzanzibari mwenzangu kwa ajili ya Watani wetu, Mama yetu Zanzibar.

Lakini nachukulia ujumbe ule kama njia ya kunifanya niseme zaidi kuhusu kizungumkuti hiki cha uhusiano wa Tanganyika na Zanzibar kupitia Muungano tulionao. Nami hakuna jambo nisilolionea haya kulisema kama hilo. Sijawahi kujihisi vibaya kujitambulisha kwa Uzanzibari wangu popote pale na, kwa hivyo, sioni tabu kuutetea dhidi ya chochote na yeyote. Basi, ikiwa aliyenitumia ujumbe anasema kuwa mtu hawezi kuila keki yake na akabakia nayo, mimi nakusudia kuhoji kuwa Muungano wetu umeonesha uwezekano wa mtu mmoja kuila keki yake na kuendelea kuwa nayo, huku mwengine kutokuila kabisa lakini pia asiwe nayo!

Uwezekano huo, kwa mfano, ndio ulioipa uthubutu Tanganyika, kwa jina la Muungano, kuyaendea kinyume au kuyavunja Makubaliano ya Muungano (Articles of Union) kwa kisingizio cha kuimarisha Muungano huo. Makubaliano haya ya Muungano ndiyo msingi na sehemu muhimu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuyavunja haimaanishi tu kuvunja katiba, bali pia ni kuwatovukia adabu Watanganyika na Wazanzibari wote.

Mkataba wa makubaliano hayo ulisainiwa na waasisi wake ukiwa na vipengele kumi na moja tu, leo hii vipengele vya Muungano ni zaidi ya ishirini na mbili. Maana yake ni kwamba vimeongezeka kwa zaidi ya asilimia mia moja, na bahati mbaya ni kwamba vingi ya hivyo, kwa makusudi kabisa, vimewekwa kupoteza nguvu na hadhi ya Zanzibar.

Siandiki kama mtaalamu wa masuala ya sheria, maana mimi siye. Wala siandiki kama mwanasiasa anayetetea maslahi yake, maana sinayo. Lakini mimi, kama walivyo Wazanzibari wengi, ni mtu ninayeziangalia siasa zilizouzunguka Muungano huu kwa mashaka. Nazishuku, na nitathibitisha shaka yangu, kwamba ni siasa zinazoitukuza Tanganyika kwa kuidhalilisha Zanzibar.

Naitaja Tanganyika kwa kuwa Tanganyika haikufa, bali ambayo imekuwa ikiendelea ‘kuuliwa’ katika Muungano huu ni Zanzibar. Ni Zanzibar ndiyo ambayo imeendelea kupoteza na kupoteza, kadiri Muungano huu ‘unavyoimarika’. Lakini hatupotezi kwa kuridhia. Nasisitiza tena kwamba hatujapata kuridhishwa hata kidogo na namna ambavyo Tanganyika imekuwa ikiutumia Muungano huu dhidi yetu, kama nchi na kama mshirika muhimu katika Muungano wenyewe. Tunalazimishwa tu.

Na, kwa hakika, mtu wa mwanzo kutufanya hayo, alikuwa ni Mwalimu Julius Nyerere mwenyewe, ambaye anachukuliwa kuwa ni mwasisi wa Muungano na, hivyo, kimsingi angelitarajiwa kuwa mtu wa mwanzo kuyaheshimu makubaliano baina yetu na sio kuyakengeuka. Nitatoa mifano. Kuna kitu kinaitwa Misingi Mikuu ya Muungano, kama ilivyoorodheshwa na Kamati Maalum iliyoteuliwa na Rais wa Zanzibar wa Awamu ya Tano kupendekeza Muundo Muafaka wa Muungano. Kwanza ni kuwepo kwa washirika wanaoonekana wazi katika utekelezaji wa shughuli za Muungano na, pili, washirika hao kuwa na uwezo sawa katika maamuzi.

Uwepo na uwezo huo hudhihirika kwa washirika hawa kuwa na kauli sawa wakati wa kufanya maamuzi, katika kutafuta suluhisho la matatizo na pia kuwa na fursa sawa ya kuzijadili, kuzitunga na kuzipitisha sheria zinazohusu mambo ya Muungano kitaifa na kimataifa. Nini alikifanya Mwalimu Nyerere? Chini ya mwezi mmoja tu, baada ya kutiwa saini kwa Makubaliano ya Muungano, alianza kuipopotowa Zanzibar kwa kutunga sheria ya kuzibatiza jina la Muungano shughuli zote za Tanganyika ambazo hazikuwa katika yale mambo 11 ya Muungano. Kati ya sheria hizi ni ile iliyoitwa The Transitional Provision Decree (N0. 1) ya mwaka 1964, ambayo iliwapa uhamisho wafanyakazi wote wa serikali ya Tangayika na kuwa wa serikali ya Muungano. Kwa sheria hii, ndio Mahkama kuu ya Tanganyika ikafanywa kuwa Mahkama Kuu ya Tanzania. Sheria hiyo ilichapishwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 01.05.1964. Bado Muungano mbichi!

Wiki mbili baada ya hapo, yaani tarehe 15.05.1964, akachapisha sheria nyengine iliyoitwa The Transitional Provision Decree (No. 2) ambayo ilielekeza kuwa kila pale penye neno au kumbukumbu inayosomeka Tanganyika sasa pasomeke Serikali ya Muungano wa Tanzania.

Ni vipi sheria hizi mbili ziliikosea Zanzibar? Ni kwamba yule mshirika wa Zanzibar katika Muungano (Tanganyika) sasa alikuwa ametoweka na hivyo Zanzibar haikuwa na upande wa kujadiliana nao panapohusika mambo ya Muungano. Kwa hivyo, hata lile agizo lililokuwemo katika Katiba ya Muda kwamba Tanganyika and Zanzibar are one United Sovereign State likabadilika na sasa ikawa Tanzania is one State and is a Sovereign United Republic, ambayo ndiyo iliyomo hadi sasa, na ndiyo inayotajwa na hao wanaodai kuwa Zanzibar kuwa na bendera yake ni kuvunja katiba. Kumbe tamko hili lenyewe liko kinyume na misingi ya Muungano, ambayo ni sehemu muhimu ya katiba yenyewe.

Kuanza hapo haikuwa tena ajabu wala aibu kwa vikao vya chama na serikali kukaa Chimwaga kwa jina la Tanzania, kupitisha maamuzi yoyote wanayoyapendelea wakubwa wa Tanganyika, bila ya kuzingatia upande wa pili wa Muungano. Lakini ikawa ni dhambi kubwa kwa Wazanzibari kukaa na kuizungumzia khatima ya nchi yao ndani ya Muungano. Hata viongozi waliowekwa au kutumwa na Wazanzibari wenyewe walipothubutu kufanya jambo ambalo lingelimaanisha kuitutumua Zanzibar, basi kifimbo cha Mwalimu Nyerere kiliwachapa. Hicho ndicho kifimbo kilichowachapa akina Aboud Jumbe, Maalim Seif Sharif na Salmin Amour.

Hizi ndizo siasa za Muungano huu, za mkubwa kummeza mdogo, za mbinu na hila na vituko na vitimbi. Mambo haya, bila ya shaka, ndiyo ambayo yamekuwa yakiwatia khofu Wazanzibari kuhusiana na khatima ya nchi yao katika Muungano. Kuna kauli maarufu sana ya kumezwa kwa Zanzibar na kufutwa kabisa. Inasemwa kuwa hii ndiyo sera ya siri ya CCM, ingawa wenyewe wanalikanusha hilo. Lakini mtiririko kama huo wa matukio unaonesha kuwa muna angalau nusu ukweli katika kauli hii, kama si ukweli mtupu. Maana kila tukienda mbele, ndivyo Zanzibar inavyozidi kupoteza kwa kuutononesha Muungano. Kwa miaka yote 40 ya Muungano, kanuni inayouendesha Muungano huu imekuwa ni moja tu: kadiri Tanzania inavyozidi kupanda, Zanzibar izidi kuanguka. Gharama za kuimarika kwa Muungano zimekuwa ni kudhoofika kwa Zanzibar.

Huu ni ukweli wa kusikitisha na kuogofya na ndio unaotayarisha mazingira ya Wazanzibari kutaka bendera yao (na huko mbele kuja kudai mengine). Maana unapofikia pahala ukajikuta umeshapoteza mambo mengi kati ya yale uliyokuwa umeyamiliki na yaliyokufanya wewe kuwa wewe, huwa huna hakika tena kuwa hata hicho kilichomo mikononi mwako kitabakia. Huna uhakika wa utambulisho wako kuwa utaendelea kuwapo. Ikiwa kumi vimekwenda, kwa nini kimoja kibakie?

Miaka yote hiyo 40 ya Muungano huu imekuwa ikiishuhudia Zanzibar ikipoteza kila chake kinachoifanya kuwa Zanzibar. Wakati huo huo, kwa jina la Tanzania, Tanganyika imekuwa ikiingiza kila kinachoifanya kuwa Tanganyika, isipokuwa jina lake tu. Kwa maana nyengine ni kwamba gharama kubwa ya Tanganyika katika Muungano huu ni huko kupoteza jina lake la asili na faida kubwa ya Zanzibar ni huko kubakia na jina lake. Zanzibar kama nchi, dola na taifa huru haipo.

Nadhani walionihoji wanaamini kuwa haya ndiyo matokeo ya kawaida kwa nchi inapoingia katika muungano na nchi nyengine. Ndio maana ya kutumia huo msemo kwamba you can not eat your cake and have it. Ukitaka ubakie na keki yako, ili uufaidi ule uzuri wake kwa macho yako, basi usiile. Kama unataka uifaidi ile ladha yake katika kinywa chako na ulishibishe tumbo lako, basi ile. Lakini ukiila, ujuwe kuwa hutoiona tena milele. Hivyo ni kutuambia kuwa Zanzibar ilipoingia katika Muungano ilikuwa imechagua kuila keki yake na kwamba sasa haiwezi kuwa nayo tena milele na milele, vyenginevyo Muungano huu uvunjike. Haiwezi kutaka ibakie na uhuru, u-nchi, u-taifa na u-dola wake, kwa ufupi Uzanzibari wake, halafu wakati huo huo ikataka iwe katika Muungano. Maana kuwamo katika Muungano kunamaanisha kuyatoa muhanga mambo hayo. Muhanga ulioje huo (ama kwa maneno ya Raza: “Tumetoa sadaka kila kitu”)

Lakini namna mambo yanavyokwenda, yanakiuka busara za msemo huu. Zanzibar ni upande mmoja tu wa Muungano huu, upande wa pili ni Tanganyika. Kama ni kuila keki yake na kutokuwa nayo, Tanganyika nayo pia ingetakiwa isiwe nayo. Nakusudia kusema kuwa zile nguvu, ule uwezo, yale madaraka, yanayotafsiriwa kwa uhuru, utaifa na udola, nayo pia yasingelikuwa mikononi mwake (hapa usiniambie Tanganyika nayo imepoteza kila kitu, maana nimeshaonesha kuwa ilichokipoteza ni jina tu). Sasa kwa nini Tanganyika iendelee kuwa na keki yake hata baada ya kuila? Yumkini haikuila kabisa au kama iliila, basi ilimega kidogo tu!

Kwa Zanzibar hali ni tafauti. Nakusudia kusema kwamba ingawa ni kweli kuwa Zanzibar hainayo tena keki yake (imeshapoteza uhuru, utaifa na utambulisho wake) lakini haijapata kuila keki hiyo. Kwa nini? Kwamba busara ya msemo huo ni kwamba hata kama sasa utakuwa umeshaikosa keki yako, basi utakuwa umefaidika na mengine. Kwa mfano, tumbo litakuwa limeshiba na kiwiliwili kitakuwa kimepata virutubisho. Si tunajuwa kuwa keki hutengenezwa kwa mayai, unga wa ngano na siagi? Tunaambiwa kuwa kipande kimoja cha keki kina faida kubwa katika kiwiliwili kuliko hata sahani nzima ya wali! Basi ikiwa kweli Wazanzibari tumeila keki yetu, angalao si tungelikuwa tumejengeka kimwili?

Ninachokusudia kukihoji hapa ni kwamba kama kweli Zanzibar ilikubali kuutoa muhanga Uzanzibari wake na kuutumia muhanga huo, basi ingelikuwa imeshafaidika angalau kimaada. Yaani ingelikuwa hatuna Uzanzibari wetu, lakini angalau tungelikuwa na uchumi imara na mfumo madhubuti wa huduma za kijamii. Huko ndiko kujengeka kimwili kwa kuila keki yetu wenyewe. Lakini Zanzibar ya leo, ya miaka 40 baada ya Muungano, ni dhalilifu na kosefu zaidi katika uchumi na huduma za kijamii. Hili linamaanisha kuwa Wazanzibari hatukuila keki yetu. Tungeliila tungelikuwa na misuli imara. Tungelikuwa na uchumi madhubuti na hali nzuri za maisha.

Hapa swali ni kwamba kama hatukuila, keki hiyo iko wapi? Uko wapi uhuru wetu? Uko wapi utaifa wetu? Uko wapi utambulisho wetu? Ziko wapi nguvu na madaraka yetu? Jibu ni kwamba vyote hivyo havipo. Na kama ni hivyo, ni wazi kuwa keki imeliwa, ingawa walaji hatukuwa sisi. Ni Muungano ulioila keki yetu. Huo ndio uwezekano wa kutokuila keki yako bali pia usiwe nayo!

Basi jitihada hizi za kutaka kuwa na bendera, kujiunga na mashirika ya kimataifa na nyengine zozote za mfano wake, ni matokeo ya kuvizwa kwa Zanzibar katika Muungano. Ni radda ya siasa zilizouzunguka Muungano huu. Siasa ambazo zinamfanya mmoja aile keki yake na abakie nayo na mwengine asiile na asiwe nayo. Ni mchakato wa mabadiliko, ambapo Zanzibar inaitafuta keki yake. Hivi sasa, hata kama Mwalimu Nyerere angelikuwa hai, asingelilizuia hilo!

Kwa mara ya mwanzo makala hii ilichapishwa katika gazeti la Hali Halisi, Na. 8 la Juni 2005.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.