TUNAKARIBIA kuadhimisha miaka 40 ya Mapinduzi ya Januari 1964 ya Zanzibar yaliyotanguliwa na uhuru wa Disemba 1963 uliodumu kwa mwezi mmoja. Kichwani mwangu nalikumbuka shairi The Beautiful Cesspool, ambalo, kama sikosei, liliandikwa na Dennis Brutus.
Ninalikumbuka kwa kuwa linaelezea mkanganyiko uliopo baina ya uhuru wa dhati na uhuru wa jina. Kwa kutumia picha ya taifa kubwa la Marekani, ambalo linajigamba kuwa liko huru na kwamba watu wake wanafaidi haki zote za kuwa kwao huru, Brutus anausasambura ukweli uliozikwa ndani ya uongo. Kwamba hata kama ni kweli kuwa Marekani kuna uhuru, basi wanaofaidika na uhuru huo ni wachache – na katika zama zake walikuwa ni wale Wamarekani weupe tu – wenye kauli, jiha na satwa!
Wao ndio wenye kuufaidi uhuru wa kuwa huru. Uhuru wa kuwa na elimu na wao wako ‘huru’ kwenda skuli kuichota elimu hiyo. Uhuru wa kumiliki mali na wao wako ‘huru’ kutumia vipawa vyao kuichuma mali hiyo. Uhuru wa maoni na wao wako ‘huru’ kuyapata na kuyatoa maoni hayo. Ni uhuru kwa maana ya uwezo wa kupata kile unachostahiki kukipata, kuwa nacho na kukimiliki katika wakati muwafaka!
Kwa wengine, wengi wao wakiwa Wamarekani weusi, uhuru huu ulikuwa ni kama mwezi tu ung’arao angani. Una rangi ya kupendeza na umbo la kutia matumaini. Wanatamani ushuke kutoka kule mbinguni uangukie viganjani mwao. Waushikeshike, wauvae, wauhisi mguso wake katika ngozi zao. Wanatamani uwe wao, waumiliki. Lakini kila siku mwezi unabakia kuwa kule kule tu, hauji viganjani mwao. Huo ni uhuru wa kujidhani, wa kutumai na kutaraji, lakini sio wa kupata!
Namna hiyo ndivyo ulivyo uhuru wetu. Uhuru wa kuishi katikati ya skuli na vyuo lakini ukashindwa kuipata elimu. Katikati ya hospitali lakini ukakosa matibabu. Mbele ya mifereji (Bara huitwa mabomba) lakini ukakosa tone la maji. Kandoni mwa duka la chakula na soko la kitoweo (Bara huitwa mboga) lakini ukashinda na njaa. Unatamani usome uondokane na ujinga, utibiwe uondokane na maradhi, na ule ili uondokane na njaa – na unaambiwa upo ‘uhuru’ wa kuyafanya hayo – lakini ukweli ni kwamba huko ‘huru’ kuweza kuyapata, kwa kuwa huna nyenzo wala uwezo nayo!
Kuwa huru ni kuwa na nyenzo na uwezo; na hicho hasa, naamini, ndicho kilichopiganiwa na wazee wetu katika hizo siku za mapambano ya kumkomboa mkulima na mkwezi wa nchi hii. Ikiwa walimwaga tone la damu yao kuikomboa nchi, basi tone hilo lilimwagika ili kumvua Mzanzibari kutoka minyororo ya dhiki na dhulma, ya unyonge na ulitima. Halikumwagika kwa nia ya kubadilisha sura zilizomo katika tabaka la watawala tu, bali lilimwagika ili kubadilisha staili yenyewe ya utawala.
Hapa utawala unakusudiwa kuwa ni ule utaratibu wa kuendesha nchi. Wakiamini kuwa nchi hii imo katika mikono ya watawala sio na wanaoiendesha sivyo, ndipo wazee wetu wakathubutu kuingia katika mapambano ya ukombozi. Walifanya hivyo kwa kuona kuwa ni watu wachache tu, waliokuwa na mahusiano na utawala, ndio waliokuwa wakizitumia fursa zote za kuufyonza na kuutumia utajiri wa nchi, huku kundi kubwa la watu likibakia kutumika kwa ajili yao tu. Akina akrabiina walikuwa wanafaidi kila jambo katika nchi – matibabu, elimu, makaazi ya fahari na maisha ya starehe – wakati makabwela wakiteseka kwa njaa, maradhi na ujinga.
Kwa hivyo, wazee wetu wakapigania uhuru – walipoupata, wakaona hauwatoshi, wakafanya mapinduzi – kwa kusudi moja tu la kuwakomboa Wazanzibari. Kuwafanya wawe huru, kwa maana hiyo ya kupata haki zao, kuwa nazo na kuzimiliki, maana hizo ndizo nyenzo za kuyastawisha maisha. Jitihada zao zote zililenga kututoa kutoka Beautiful Cesspool, na kutufanya tuishi maisha ya kiutu, heshima na stahili ya kibinaadamu.
Lakini hivi sasa, ikiwa ni miaka 40 baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, ni humo humo kwenye Jaa Linalopendeza ndimo wengi wetu tunamoishi. Kwamba yale Mapinduzi yamesalitiwa! Yule mkwezi na mkulima aliyelengwa kukombolewa, bado hajakomboka. Bado anaendelea kudhalilika na kuteseka vile vile. Hadi sasa bado safari ya kuelekea kwenye uhuru wa kweli uliokusudiwa awe nao Mzanzibari ni refu sana na ngumu mno.
Baya zaidi ni kwamba safari hiyo sasa inakabiliwa na vigingi vingi zaidi kuliko huko nyuma kutokana na mabadiliko ya wakati na ongezeko la mahitaji. Kwa hivyo, Wazanzibari, kama raia, wanahitaji kwa haraka sana, harakati nyingine za ukombozi. Kwamba kilichobadilika Zanzibar ni sura za watawala tu, lakini sio staili ya utawala. Na ni kwa sababu ya hilo, ndio wengine tukaamini kuwa Zanzibar, kama nchi, bado haijawa huru. Kwamba bado haijawa na uwezo na nyenzo za kupata, kuwa nacho na kukimiliki!
Hoja ninayojaribu kuiwasilisha mbele yenu ni kwamba uhuru wa kweli uliopiganiwa na wazee wetu sio tulionao. Mapinduzi tunayoyasherehekea leo, tunayasherehekea tu kwa kuwa ni ada kufanya hivyo, lakini hayabebi tena ile azma yake yaliyolengwa.
Yale yale yaliyotakiwa yaondoke miaka 40 nyuma, ndiyo yaliyopo sasa. Tena, kutokana na hayo mabadiliko ya wakati na ongezeko la mahitaji, mambo hayo hivi sasa yapo kwa kiwango cha kutisha. Na ikiwa hivyo ndivyo, hakuna msamiati tutakaoutumia hapa kuhalalisha kujiita kwetu huru.
Nitapiga mifano mingi kadiri nitakavyoweza ili kuhalalisha msimamo wangu kwamba Zanzibar haijawa huru – si kiuchumi, si kisiasa, si kijamii. Wakati Zanzibar inapata uhuru wake mwaka 1963, thamani ya dola moja ya Kimarekani ikiwa ni shilingi saba tu za Kitanzania, ilikuwa inaingiza kiasi ya shilingi milioni mbili kwa mwaka kwa kusafirisha samaki wakavu Tanganyika. Kwa sasa, hiyo ingelikuwa ni zaidi ya shilingi bilioni tatu.
Mbali ya kuhakikisha kwake kuwepo kwa nafasi za kazi zisizopunguwa mia tano kwa mradi huo tu, pato hili pia lilihakikisha kujitanua kwa Zanzibar kiuchumi. Miaka 40 baada ya uhuru kupatikana, sio tu kwamba Zanzibar haina tena cha kukizalisha kuisafirishia Tanganyika, bali yenyewe ni tegemezi kwa yale yazalishwayo huko. Huko si kwenda mbele, bali ni kurudi nyuma. Na huo sio uhuru uliopiganiwa.
Hadi mwaka 1964, wakati Mapinduzi yanafanyika, nchi pekee za Kiafrika zilizokuwa zikilingana na Zanzibar kwa pato kubwa la taifa zilikuwa ni Ghana na Afrika ya Kusini. Wakati huo Zanzibar ilikuwa inatowa misaada ya chakula na pesa kwa nchi nyingine ulimwenguni, zikiwemo nchi za Kiarabu kama vile Yemen. Leo Zanzibar, ikiwa chini ya kivuli cha Muungano, ni sehemu fukara kabisa duniani. Wazee wetu hawakupinduwa ili tuje tuwe omba omba!
Zanzibar haikuwa na uchache wa wataalamu katika nyanja zote za utawala na utekelezaji. Ni aibu kuwa miaka 40 baada ya Mapinduzi, tunaagizia wataalamu wa sheria, kodi na wengineo kutoka nje ya nchi, ambapo hadi mwanzoni mwa Mapinduzi ni nchi hii na Sudan tu, katika kusini nzima ya Jangwa la Sahara, ambazo zilikuwa na wataalamu wa kutosha, na wa ziada, wa kizalendo. Ikiwa tumerudi nyuma kiasi chote hiki badala ya kwenda mbele, ni fedheha kujiita kuwa sisi ni watu huru.
Katika huduma za kijamii, hali ni mbovu na ya kusikitisha hivyo hivyo. Miongoni mwa maazimio makubwa ya Mapinduzi yalikuwa ni kuwapatia wakulima na wakwezi wa nchi hii makazi bora, huduma nzuri kwa wazee wasiojiweza, elimu bora zaidi, chakula cha kutosha na matibabu yanayostahiki kupatiwa mwanaadamu. Kwamba huko nyuma, tunaambiwa, watu wengi walishindwa kuvipata vitu hivyo kwa kuwa, hata kama walikuwa na uhuru navyo, hawakuwa na uwezo wa kuvigharamikia. Maana vilimaanisha pesa, ambayo kwa wanyonge ilikuwa ni adimu mno kupatikana.
Matokeo yake, watoto wengi wa kimaskini wakaishia kuwa wajinga kwa kutokumudu kwenda skuli. Watu wengi wakawa wanalala na njaa, au kwa ‘kugongeana mwiko’, katika vibanda vyao vya makuti, na hata wengine wakawa wanakufa kwa kukosa matibabu kwa kuwa hawakuwa na pesa. Wachache waliokuwa na mkono wao katika tabaka la watawala, au wenye uwezo wa kifedha, ndio waliofaidi ladha ya kuwa huru.
Sasa leo, wakati tukisherehekea miaka hii 40 ya Mapinduzi, kuna yapi Zanzibar? Ni mfano wa yale tunayozungumziwa kwamba yalitokea nyuma ya miaka ya ’60. Wale wale watoto wa makabwela, waliozungukwa na skuli, wanakosa elimu bora kwa kuwa hawana uwezo wa kulipia.
Kwamba ni kweli kuwa skuli za serikali zipo, lakini kwa kuwa serikali haiko makini katika kuiboresha huduma hii, skuli zake zimefuiya na mfumo mzima wa elimu umeporomoka. Sasa kupata elimu nzuri inampasa mtoto alipie masomo ya ziada au mzazi amuandikishe mwanawe katika skuli za kulipia. Na kwa kuwa hayo yote yanamaanisha pesa, na pesa ni adimu kwa wakulima na wakwezi, basi elimu bora haipatikani kwao!
Badala yake ni watoto wa wakubwa na wenye pesa zao, ndio ambao wanaipata hiyo elimu bora. Wengi wao husomeshwa nje ya nchi na wachache wanaosoma ndani ya nchi ni katika zile zinazoitwa international schools, ambako malaki ya pesa za walipa kodi huyeyushwa kila mwezi.
Na kwa kuwa sasa tunaingia katika wakati ambapo kuipata kazi kunategemea kisomo mtu alichonacho, basi ni wazi kuwa watakaokuja kupata nafasi za kikazi (ikiwa zipo) watakuwa ni hao hao waliopata elimu bora. Mtoto wa mkulima na mkwezi atarudi kule kule kwenye pingu na jembe la mzazi wake.
Wakati huu wa kusherehekea miaka hii 40 ya Mapinduzi, pita mitaani kwa makabwela ushuhudie hali ilivyo. Pita Miembeni, Jang’ombe, Sogea na kwengineko uone maandamano ya madumu ya maji. Pita vijijini kwetu ushuhudie hali ya watu walio ‘huru’. Pita Mtende, Kojani, Kiuyu na Marumbi usikie harufu ya njaa ikikunukia puani mwako.
Lakini, kejeli ilioje ni kuwa katika wakati huu huu, huko Mazizini na mwenginemo muchache, watu wanakula na kumwaga katika madebe ya taka. Huko kunasherehekewa miaka 40 ya Mapinduzi na uhuru wa mkulima na mkwezi. Huko ndiko uhuru na ukombozi ulikofika!
Wakati huu wa kufurahikia ukombozi wa mkulima na mkwezi, nenda katika jumba la wazee Sebleni, pale karibu na uwanja wa Amani, ukamuone huyo mkulima na mkwezi ‘alivyokombolewa’.
Mzee wa miaka 70, amechakaa na kuchafuka kama lilivyo hilo jengo lenyewe, anajikokota kwenda kutafuta makozi ya kupikia hadi karibu ya Mwera. Serikali iliyomuweka mule imeshindwa kumuekea mazingira ya kumtunza kikweli, na badala yake anadhalilika. Miaka 40 iliyopita, huyu alikuwa ni mtafutaji uhuru, alikuwa mpiganiaji ukombozi; na sasa nadhani ni dhambi kumuita yeye kuwa ni raia huru!
Wakati huu pia tembelea hospitali zetu, zile zilizoahidiwa na Mapinduzi kuwa zingelitowa huduma bora na bure. Mkwezi na mkulima hawawezi kupatiwa muda wa kuangaliwa sawasawa na madaktari kwa kuwa hawana pesa za kuwahonga. Hata wakishaangaliwa kwa hayo macho matupu, hospitali hiyo haina dawa. Wao, mkulima na mkwezi, wanatakiwa kununuwa dawa za elfu tano, pato lao la mwezi mzima. Huo ndio uhuru walioupigania?
Wakati huo huo, huku mkulima na mkwezi wakiteseka kwa maradhi bila ya dawa, fedha nyingi zinatumika kuwapeleka nje kwa matibabu watu walio na fursa katika utawala, hata kama maradhi hayo yangeliweza kutibiwa hapa hapa, tena kwa pesa kidogo tu au bure kabisa. Wao wanajuwa namna ya kuufaidi uhuru na wako huru kufanya hivyo. Kwamba wana nguvu, uwezo na nyenzo za kuutumia uhuru wao. Wao ndio ‘waliokombolewa’ na hayo Mapinduzi ya 1964.
Marehemu Jaramogi Oginga Odinga wa Kenya aliwahi kuandika kitabu na kukiita Not yet Uhuru, akimaanisha kuwa hata baada ya mkoloni wa Kiiengereza kuondoka nchini mwake, bado taifa la Kenya halikuwa huru.
Hiyo ni kwa kuwa wale waliochukuwa madaraka baada ya wakoloni hawa, walijigeuza kuwa wakoloni weusi na ambao walikuwa wabaya zaidi kuliko wakoloni weupe, maana hawa walikuwa wanakula nchi yao wenyewe. Walikuwa wanaitawala nchi kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha ya umma, ufisadi na utumizi mbaya wa madaraka. Walikuwa wanaifakamia keki ya uhuru kwa matonge. Nachelea sana kusema kwamba hali iko hivyo hivyo kwa Zanzibar. Waliochukuwa madaraka baada ya Uhuru na Mapinduzi wameigeuza nchi hii kuwa shamba lao, mali yao na vizazi vyao. Wao peke yao ndiyo waliojihalalishia kuila keki ya Mapinduzi kwa staili wanayoitaka wenyewe.

Wao peke yao ndio wanaopata makazi mazuri na ya kuridhisha, maji salama na safi, matibabu bure na bora, elimu ya juu na ya manufaa, chakula kizuri na cha kutosha, na mavazi ya kuvaa na kujipamba. Kwa sisi, watoto wa makabwela, bado tuko kule kule walikokuwa wazazi wetu miaka 40 nyuma. Kwetu, ni not yet uhuru!

An Nur, Na. 541, Disemba 26, 2003-Januari 1, 2004