Angalia huu mpishano hapa: karibuni kulisikika habari kwamba askari wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) huko Pemba walimfyatulia risasi na kumuua mtu mmoja kwa tuhuma za kusafirisha karafuu isivyo halali. Majuzi, alipokuwa ziarani katika mikoa ya Kusini, Rais Jakaya Kikwete aliwaamuru wanunuzi binafsi wa korosho watoe bei nzuri kwa wakulima. Picha unayoipata ni kwamba, wakati Zanzibar kuna ukiritimba wa bashara ya karafuu kufikia hadi askari wa serikali wanawaua raia kwa kusafirisha karafuu yao kuiuza watakako, serikali ya Bara imetoa uhuru wa kibiashara hadi inawataka wanunuzi binafsi wawe waadilifu.Karafuu(1)

Sasa kujuwa kwa nini kuna magendo ya karafuu Pemba, unapaswa kujuwa mazingira ambayo yamelizunguka suala lenyewe la magendo. Mojawapo ni Pemba yenyewe kwenye karafuu hizo na jengine ni la uhusiano baina ya Wapemba, wanaozimiliki karafuu zenyewe, na serikali zilizopo madarakani.

Tusaidiane kidogo. Hebu panda meli au ndege uelekee Pemba. Kwa meli, utashukia aidha Mkoani, kusini mwa kisiwa, au Wete, kaskazini yake. Kwa ndege, utatuwa Chake Chake, mji ulio katikati ya Pemba. Wapi utafikia, si muhimu sana, alimradi popote pawapo utakutana na sura moja tu ya umaskini uliopea!

Kwa mfano, kama utashukia Mkoani, utatua mguu wako juu ya ‘tuta’___ kama wenyewe wanavyoiita bandari hii. Hapa hutakutana na zile pirika pirika ulizozowea kukutana nazo bandarini Unguja au Dar-es-salaam. Hakuna msongo wa magari yanayoingia na kutoka bandarini kuchukuwa au kupeleka mizigo. Sana sana utakutana na gari mbili, tatu tu Hapa hapana meli kubwa za nje zinazopakuwa makontena wala zile boti ziendazo kwa kasi. Huenda meli uliyokuja nayo ikawa ndio pekee kwa siku hiyo nzima.

Mungu ajaalie ufikie katika eneo ambalo lina huduma ya maji na umeme na pia zamu za mgawo ziwe ni za hapo. Vyenginevyo, unaweza ukapindisha siku hiyo hiyo bila kutimiza azma ya ziara yako. Kwamba wewe umeshazowea mwangaza wa taa na maji ya mfereji, vitu ambavyo kwa watu wengi wa Pemba havipatikani. Giza na dhiki ya maji ni sehemu tu ya maisha ya huko. Na hiyo ndiyo Pemba!

Hata hivyo, kitu kimoja hutokijutia, nacho ni kuishi na watu wa Pemba. Hawa ni watu wakarimu sana licha ya umaskini wao. Ni nadra sana kumkuta ombaomba kule, badala yake watu watataka wakukirimu wewe, mgeni wao, kwa kila fadhila, kuanzia maneno mazuri hadi chakula.

Ikiwa utawaendekeza sana, basi kila siku utalala ukiwa umevimbiwa, maana kila nyumba utakayokwenda kusalimia utatafadhalishwa uwahi japo chai tu. Bora uwe unakula kwa mwenyeji wako tu, ambaye kwa siku zote utakazokuwa naye, atahakikisha kuwa ratiba yake ya chajio inabadilika, badala ya saa mbili usiku, itakuwa angalau saa kumi jioni. Hao ndio Wapemba!

Basi ikiwa wewe ni mtu uliyeyatumia maisha yako yote katika maeneo ya miji mikubwa tu ya nchi hii, utajikuta na maswali mengi ya mshangao badala ya udadisi. Hivi ni kweli nimo ndani ya Tanzania, au hata Zanzibar tu?

Jibu ni ndiyo, na ndiyo maana ukazikuta bendera za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zikipepea katika milingoti mikongwe mbele ya majengo machakavu ya ofisi za serikali. Ndiyo ukaona magari yaliyoandikwa ZNZ au SMZ kukujulisha kuwa uko ndani ya Zanzibar. Pemba ni sehemu ya Tanzania na ni sehemu ya Zanzibar, lakini hii ni miongoni mwa sehemu zilizotupwa na kuachwa mkono kwa miaka mingi sana. Hiyo ndiyo Pemba!

Pemba inafahamika zaidi kwa karafuu yake na kwa watu wake. Kuna kipindi Zanzibar ilikuwa ikiongoza kwa uzalishaji wa karafuu ulimwenguni, na kwa kuwa karafuu yake nyingi hulimwa Pemba, basi hilo likakifanya kisiwa hiki kujulikana sana. Watoto wa Pemba, maarufu kama Wapemba, nao wameenea kila pembe ya Tanzania na dunia kwa jumla, na hivyo wanaitangaza Pemba. Lakini Pemba yao wanayoitangaza ni sehemu masikini sana.

Pengine kwa watu wasiowahi kufika Pemba itakuwa vigumu kuamini hivyo. Wanaweza wasiamini hilo kwa kuwa uelewa wao kuhusu Pemba umemezwa na vitu viwili___ yale wanayoyasikia kuhusu morali ya kisiasa ya Wapemba na ile picha wanayoipokea kutokana na maisha wanayoishi Wapemba walio nje ya Pemba, ambao wengi wao wana maisha mazuri kidogo katika sehemu walizo, kulinganisha na watu wengine.

Ukimuona kijana wa Kipemba anaendesha gari la bei mbaya katikati ya jiji la Dar-es-salaam au akiishi katika jumba la kifahari kule Arusha au Dodoma, unaweza kudhani kuwa watu hawa huzaliwa na vijiko vya dhahabu vinywani mwao. Kwamba kwao kuna visima vya fedha! Lakini ukweli ni kuwa Pemba na Wapemba walio huko ni masikini mno.

Basi ni hili la umasikini ndilo ambalo linaweza kuelezea kwa nini pana magendo ya karafuu pale. Kwamba tafauti na kisiwa chenzake cha Unguja, ambacho jaala imekifanya kiwe na chaneli nyingi za kutafutia riziki, Pemba ina karafuu tu.

Kwa mfano, kule hakuna bandari ya uhakika, kwa hivyo biashara ya kuingia na kutoka haina uhai wa kudumu. Kuna barabara mbovu, hata kwa zile zinazotoka au kuelekea katika miji yake muhimu, kwa hivyo ni shida kujenga mawasiliano ya kiuzalishaji baina ya wakulima wa mashamba na wafanyakazi wa mijini. Hakuna huduma za uhakika za umeme na maji, kwa hivyo watu hawawezi kujiajiri kwazo zikawa na tija kwao. Katika kilele cha makosefu na mapungufu hayo, hakuna muujiza wowote wa kuwaletea watu hawa maendeleo.

Kwa kudhoofika na ama kukosekana kabisa kwa hii iitwayo ‘miundo mbinu’, mzunguko wa fedha unakuwa mdogo sana Pemba, isipokuwa katika msimu wa karafuu tu. Hilo huwafanya watu kujikita katika shughuli yoyote duni iliyopo mbele yao, alimradi tu mkono uende kinywani, hadi hapo karafuu zizaliwe. Na, kwa bahati mbaya sana, karafuu huzaliwa mara mbili tu, Vuli na Mwaka. Ni katika vipindi hivi vya mavuno ya karafuu, ndio maisha ya Pemba hupata maana.

Watu wengi huwa wameshaekeza kila chao kwa kipindi chote cha mwaka kwa ajili ya kuivuna karafuu yao. Huwa wameshatumia nguvu zao zote, muda wao wote, pesa yao yote na, kubwa zaidi, matarajio yao yote kwa ajili ya siku hizi chache za neema. Siku zinapowadia, huwa wako tayari kuzitumia kwa kila namna iwaruhusuyo, alimradi tu msimu usiondoke na kuwaacha watupu.

Kule Pemba, karafuu ina maana kubwa katika maisha ya watu si kiuchumi tu, bali hata kijamii na kisaikolojia. Kwa mfano, ni katika msimu huu tu, ndipo wengi wa watu hudiriki angalau kununua nguo mpya, ama hata kula halua na pilau! Hata ule udume wa mwanamme huonekana wakati huu, ambapo angalau baba huweza kumnunulia mama kanga na vitambaa.

Kwa Wapemba, kumalizika msimu huu bila ya kunufaika nao, ni sawa kwa waumini wa Kiislam kumalizika mfungo wa Ramadhani bila ya kusamehewa madhambi yao. Huwa wamehasirika!

Siwezi kulitafsiri neno la Kiiengereza ‘belongingness’ kutokana na ufakiri wangu kwa lugha yangu mwenyewe, lakini zile hisia zipatikanazo na maana ya neno hili, ndizo walizonazo Wapemba kwa karafuu zao. Kwamba wanajihisi kuwa wao ni wa karafuu na karafuu ni ya wao tu! Kwamba sio tu wana karafuu, bali pia wanaimiliki karafuu___ na ni karafuu tu. Kwamba wao ni watu waliowachwa mkono na serikali zao na ndugu zao waliokwisha kubahatisha maisha nje ya Pemba. Wamekuwa kama wana wakiwa wasio na bega la kulilia kilio cha simanzi yao, ila karafuu yao tu.

Mfumo wa kidini wa watu hawa unawaruhusu kurithi mali za jamaa zao waliokufa. Kwa hiyo, mapenzi yao kwa mali hii, huwa sawa na mapenzi yao kwa yule waliyemrithi, kwa maana ya kuijali na kuithamini. Hivyo ndivyo Wapemba wanavyoyachukulia mashamba ya mikarafuu, ambayo mengi yao ni kuyarithiwa. Kila wanapoona kuwa pana njia nzuri zaidi ya kunufaika na karafuu yao, huifuata ili wapate thamani halisi ya nguvu yao na ya watu wao waliokwishatangulia mbele ya haki.

Hapa ndipo unapoweza kupata tafsiri ya hayo tuyaitayo ‘magendo ya karafuu’ katika maisha ya watu wa Pemba. Kwamba wengi wao wanajuwa kuwa wana uhuru na karafuu yao wenyewe na hawatambuwi ni wapi hapo panapotokea marufuku ya kuwazuia kuuza karafuu zao wanakotaka. Wanaamini, tena kwa haki kabisa, kuwa sheria ya kimaumbile inawapa wao umiliki wa karafuu zile. Na kwa kuwa hali zao za maisha ni duni mno, basi sasa hata wajibu wa kimaumbile unawapa uthubutu wa kuitumia karafuu hiyo kuinua hali zao, na si vyengineyo.

Ndio maana, licha ya kuwa sheria ya kudhibiti biashara ya karafuu ipo, kila uchao watu wanakamatwa na kuadhibiwa kwa kuivunja. Saidi Juma Hamadi, ambaye alishawahi kukamatwa na kushitakiwa kwa kosa hili, aliwahi kusema katika mahojiano yake na shirika la habari la Australia (ABC) mwaka 2002: “Kama inabidi kufanya tena (magendo haya ya karafuu), basi nitafanya. Ikiwa mahali pana ukandamizwaji, inakubidi upiganie haki yako. Tunajuwa kuwa tunayatia hatarini maisha yetu, lakini maisha ni magumu sana hapa. Inabidi tujitoe muhanga!”

Muhanga wenyewe ndio kama huu wa kupigwa risasi wakati wakitarazaki na maguni yao ya karafuu.

One thought on “Pemba, umasikini, magendo ya karafuu na risasi”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.