Sasa njaa ya Micheweni na mende wa Mnazi Mmoja ni siasa. Mbaya zaidi ni kuwa kwake siasa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na ndiko kunakofanya ihojike ikiwa kweli serikali hii ina umakini wa kutosha kuiongoza Zanzibar kuelekea hayo yaitwayo “malengo ya milenia”.

Tukumbushane kidogo matukio haya yalivyogeuzwa kuwa siasa. La njaa ya Micheweni liliibuliwa na waandishi wa habari watatu, Salma Said kutoka Mwananchi Communications, Mwinyi Saadallah kutoka IPP Media na Munir Zakaria kutoka Channel 10. Ilikuwa ni baada ya waandishi hao kutembelea eneo hilo na kukuta tishio la njaa kutokana na ukosefu mkubwa wa chakula. Kama maadili ya kazi yao yalivyo, baada ya kukamilisha uchunguzi wao wakaitoa taarifa hiyo kwa umma kupitia vyombo vyao.

Mara baada ya kutoka kwa habari hiyo, mkuu wa mkoa wa Kaskazini Pemba, ilimo wilaya ya Micheweni, Dadi Faki Dadi, akakurupuka ‘kupiga siasa’ kwa kuikanusha. Ni bahati mbaya sana kwamba Dadi alipewa fursa ya kufanya hivyo na chombo kikubwa cha habari ulimwenguni, Shirika la Habari la Uingereza, BBC.

Dadi akaitumia BBC kuisiasisha njaa ya ‘watu wake’. Na hili la ‘watu wake’ linahitaji kutiliwa mkazo, maana licha ya kuwa kwake mkuu wa mkoa huo, Dadi ni mzaliwa na mwenyeji wa wilaya ya Micheweni na, hivyo, waliokumbwa na maafa hayo ni ndugu zake wa damu. Akatumia wasta wake kusema kwamba hakuna kitisho cha aina hiyo huko, bali ni hali ya kawaida kama zilivyo nchi nyengine za dunia ya tatu.

Siasa ya Dadi ikawanyima ndugu zake fursa ya kusaidiwa, maana hiyo ilikuwa ni kauli ya serikali. Hakuna taasisi yoyote ya kitaifa au kimataifa inayoweza kupeleka misaada katika eneo ambalo serikali imelitangaza kuwa halihitaji misaada hiyo. Msimamo wa Dadi kwa watu wa Micheweni ukawa hauna tafauti na wa Omar Bashir wa Sudan kwa maafa ya Darfur. Akaitumia BBC kuendelea kuwalaza ndugu zake na njaa na kuwashindisha kwa chochoni.

Lakini uongo huwa haudumu sana. Wanaozijuwa siasa za Zanzibar wamejenga imani kwamba, ukisikia jambo linakanushwa kwa nguvu na serikali, basi ujuwe kuwa jambo hilo ni la kweli. Walipofuatilia wakaona ukweli wake na wakakusanya misaada kuwapelekea ndugu zao wa Micheweni. Uongo wa Dadi ukashindwa!

Baada ya kuona kwamba sasa kila jambo liko hadharani, Dadi huyu huyu akajitokeza tena katika vyombo vya habari kukiri kwamba ni kweli kuna tatizo la njaa katika eneo hilo na kwamba misaada ya haraka inahitajika. Kulikuwa ni kujikosha tu, maana ni Dadi huyu huyu aliyekuwa amewahi hata kutumia mbinu zake zote kuhakikisha kuwa habari zilizokusanywa na wale waandishi watatu kuhusiana na njaa hiyo hazifiki kwa umma, lakini waandishi hao wakamzidi maarifa na ndipo akajitokeza kupitia BBC kujaribu kufuta ‘maandishi yaliyo ukutani’.

Hebu tujiulize, ingelikuwaje kama angelifanikiwa katika jitihada zake za mwanzo za kuzuia habari za njaa zisitolewe? Ni bahati nzuri kwa umma kwamba hapo alifeli, lakini vipi kama angelifanikiwa katika hatua yake ya pili ya kuitumia BBC kukanusha kuwepo kwa njaa na kutaka ‘uzushi’ ule upuuzwe na hivyo umma ukapuuza kweli? Majibu ya mswali yote ni kwamba, raia anaowatala wangeliendelea kuteseka kwa njaa. Sasa, siasa hii ya njaa inaidhalilisha SMZ.

Katika toleo lililopita, gazeti hili lilikuwa na mwito wa kiungwana kwa Dadi kwamba ajiuzulu nafasi yake ya ukuu wa mkoa, maana alikuwa ameshindwa kufanya kazi aliyopewa na Rais na hivyo kuwafelisha watu anaowaongoza. Katika kamusi la siasa za petu, hakuna msamiati “kujiuzulu kwa kushindwa kutekeleza majukumu” bali kuna “kung’ang’ania madaraka hata baada ya kushindwa kazi”.

Dadi analijuwa kamusi hilo kwa ghibu na hivyo hatarajiwi kuondoka alipo, maana haoni baya alilolitenda. Kuwalaza watu na njaa (sisemi kwamba alikuwa na jukumu la kuwalisha kama makinda ya ndege) halikuwa jambo kubwa kwake. Anavyojiona alikuwa akitekeleza ilani ya chama chake. Dadi hatajing’oa n’go!

Lakini Dadi hakujiweka, amewekwa. Ikiwa mwenyewe ameshindwa kuwajibika, basi aliyemuweka anaweza kumuwajibisha, akitaka. Ndipo hapa suala hili linapomgeukia bosi wake, Rais Amani Karume. Je, Rais kasimamia wapi? Ameridhika na utendaji kazi wa mwakilishi wake katika mkoa wa Kaskazini Pemba au hakuridhika nao? Je anamuona Dadi kama nini: mzigo au msaidizi? Maoni ya wengi wetu ni kwamba Dadi amefeli na hivyo anamfelisha bosi wake, kwa hivyo amuuzulu.

Dadi auzuliwe kwa kuwa hasaidii kuijenga taswira ya SMZ miongoni mwa jamii anayoiongoza, ambayo tangu hapo si nzuri. Anachofanya Dadi ni kuhalalisha tu kuchukiwa kwa SMZ Pemba na hivyo kuifanya iendelee kutokuungwa mkono. Kama serikali, SMZ ina jukumu la kujifanya ikubalike kwa watu wake, hata kama watu hao hawakuiweka madarakani. Wa kuijenga taswira mpya ya SMZ Pemba ni hao akina Dadi, wawakilishi wake. Na hiyo ni kazi iliyomshinda na, kwa hivyo, ni kwa maslahi ya ujenzi wa taswira ya SMZ Pemba kumvua Dadi ukuu wa mkoa. Hicho ndicho kitu chema pekee ambacho ‘siasa za njaa’ zinaweza kuisaidia SMZ Pemba.

Tuje kwenye ‘siasa za mende’ wa hospitali kuu ya Mnazi Mmoja, taswira nyengine ya SMZ. Siasa hizi zilianza kitambo kidogo, katika mwezi wa Agosti, pale kwa mara ya mwanzo picha za televisheni ya serikali, TvZ, zilipoonesha halaiki ya mende ikicheza foliti katika wodi ya watoto. Kwa kuwa mende huishi kwenye uchafu, basi tafsiri ya haraka haraka iliyopatikana ni kwamba wodi hiyo ni chafu na, kwa hivyo, si salama kwa afya za watoto wanaolazwa hapo.

Kuona picha zile, umma ukahamasika. Mmoja wa wasamaria, Mohammed Raza, akajitolea kuchangia ujenzi na vifaa kwa ajili ya wodi hiyo lakini SMZ ikapiga siasa zake kwa kuikataa ofa hiyo kwa madai kuwa eneo hilo lilikuwa tayari linashughulikiwa na jumuiya ya ZAYADESA inayoongozwa na Shadya Karume, mke wa Rais.

Tupo tulioiona hiyo ni siasa kwa sababu mbili; ya kwanza ni kwamba hata kama Shadya Karume alikuwa anaishughulikia wodi hiyo, bado msaada wa Raza ungeliweza kupokelewa na kutumika katika eneo jengine maana si wodi hiyo tu yenye matatizo na, ya pili, ni kuwa msaada wa Raza ulikataliwa kwa kuwa ananasibishwa na utawala wa awamu iliyopita ambao hauivi na wa awamu hii.

Afadhali ‘siasa hizi za mende’ zingeliishia hapo, lakini wiki iliyopita SMZ ikaziendeleza. Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Shawana Buheti, akasema kwenye kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea sasa kwamba, mende hao huletwa na kinamama wanaolazwa katika hospitali hiyo. Siasa za kukwepa majukumu kwa kuhalalisha uovu!

Tuseme ni kweli kwamba, kutokana na kuishi kwetu katika mazingira machafu, basi bila kujijua mama zetu huenda na mende hao mikobani mwao pale hospitali na wakawaacha kuzaliana hadi tukawa na jeshi lile la mende wodini. Lakini ukweli huo pia unasema ukweli mwengine: kwamba mende huishi katika mazingira machafu, na kama hapana uchafu pale wodini, mende hao wasingeliamua ‘kujiripua’ na kuwa walowezi wa kudumu katika eneo ambalo wao na vizazi vyao wasingeliweza kuishi kwa kuandamwa na ‘operesheni usafi’ za mara tatu kwa siku.

Kwa hivyo, hospitali ni chafu kwa kuwa haisafishwi. Nani wa kuisafisha? Ni serikali, bila ya shaka, maana hii ni hospitali yake. Kama imeajiri wafanyakazi ambao hawaifanyi kazi hiyo, hilo si juu ya kinamama ‘wanaoleta mende’ kwa bahati mbaya. Ni juu ya wafanyakazi hao, kwa mintarafu ya kwamba ni juu ya serikali hiyo, kuhakikisha kuwa mende hao hawaingii wodini na hao wanaopenya kwa bahati mbaya wanaondolewa mara moja kabla kamera za TvZ hazijafika.

Kwa kuwa kuwapo kwa mende kunachafua taswira ya serikali inayoimiliki hospitali hii, hoja ya msingi kutoka kwa umma sio mende wale wamefikaje pale, bali ni kwa nini waendelee kubakia pale. Kwa serikali kulaumu kufika kwao lakini hapo hapo ikashindwa kupinga kubakia kwao ni kupiga siasa tu. Tatizo lipo pale pale.

Hapa napo, Rais Karume anapaswa kuingiza mkono wake kujijenga kabla ‘siasa za mende’ hazijazidi kumbomoa. Serikali haipaswi hata kidogo kukimbia majukumu yake kwa kuwasukumizia wananchi mzigo. Hiyo huitwa perplex complexity. Aina moja ya shakhsia ambapo mtu hujijengea mazingira ya kuukwepa ukweli unaomuandama na ambao ana dhamana nao. SMZ isiwe hivyo. Naibebe msalaba wake yenyewe. Na Rais Karume aongoze mbele katika ubebaji huo. Wananchi watamuelewa na watamsaidia.

Kwamba siasa za mende na njaa hazitaifikisha serikali yake mahala popote kimaendeleo. Ikiwa kila siku tutakaa tujadiliane, tushambuliane na tusutane juu ya watu wetu kukosa mlo mmoja tu kwa siku na juu ya usafi na usalama wa hospitali zetu tu, hatutakuwa na siku ya kukaa tukajadiliana na kupanga namna watu hao watakavyopata nyumba zao wenyewe, gari za kutembelea, na elimu nzuri kwa watoto wao. Tutaendelea kuwa hapa hapa tu penye njaa na mende na kufikia ‘malengo ya milenia’ itakuwa njozi ya kudumu kwetu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.